Papa Benedikto XVI:Afrika ni pafu la kiroho la mwanadamu kwa shida ya imani na matumaini
Na Angella Rwezaula; – Vatican.
Wakati na baada ya kifo cha Papa Mstaafu Benedikto XVI, maoni mbali mbali kuhusu maisha yake na uzoefu wa huduma yake ya Kanisa lote la ulimwengu na upapa wake umeendelea kusikika kwa walio wengi. “Papa Mstaafu Benedikto XVI alilitendea sana Kanisa la Afrika kwa namna ya pekee akilibeba Bara letu moyoni mwake kwa ari, imani na ukarimu”, hivyo ndivyo alivyosema Kardinali Fridolin Besungu Ambongo, Cap., kwa niaba ya Maaskofu wa Afrika katika ujumbe wake wa kutoa salamu za rambirambi kufuatia na kifo cha Papa Mstaafu Benedikto XVI kilichotokea katika siku ya mwisho ya mwaka 2022 majira ya asubuhi katika nyumba ya Matre Ecclesiae, mjini Vatican.
Himizo la afrika kujiamini na kusimama kidete
Katika maoni yake, Kardinali Ambongo alisema kuwa daima Papa mstaafu alihimiza Afrika kujiamini ili kusimama kidete kwa heshima. Na aliona ndani ya Afrika kama pafu la kiroho kwa ubinadamu ambalo linaonekana kwa dhati kuwa katika mgogoro wa imani na matumaini”. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu katoliki la Kinshasa,(DRC)na makamu rais wa Mashirikisho ya Mabarza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar (SECAM), alibainisha kwamba “kwa muda wote wa huduma ya Upapa, kuanzia mwezi Aprili 2005 hadi alipojiuzulu mnamo Februari 2013, Papa mstaafu Benedikto XVI alitoa ushuhuda mkubwa wa uinjilishaji mpya kama mtumishi wa upendo katika ukweli”. Vile vile akiongeza kusema kuwa “ni yeye aliyeitisha Mkutano wa II wa Sinodi ya Afrika ili kulipatia Kanisa la Mungu katika Bara la Afrika ule msukumo mpya uliojaa matumaini na mapendo ya Kiinjili. Wakazi wote wa Afrika wanajua kwamba Papa Benedikto XVI aliwatendea sana kwa namna ya kipekee.”
Wosia wa Kitume Africae Munus utabaki kuwa wa thamani
Askofu mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Kinshasa (DRC) hata hivyo aliungwa mkono na maaskofu wengi wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki (AMECEA) ambao kwa mujibu wao walibainisha kuwa “kuitishwa kwa Sinodi ya Pili ya Afrika mnamo mwaka 2009, iliadhimishwa kwa dhati wakati ambao Makanisa mengi katika ukanda huo yalikuwa yakiadhimisha miaka 100 ya kusimikwa makanisa yao na Wosia wake wa Kitume Africae Munus wa baada ya Sinodi uliotiwa saini na Papa Msataafu Benedikto XVI mnamo mwaka 2011 utabaki kuwa nyakati za thamani kwa Kanisa Barani Afrika”.
Kukumbatia njia ya Kitaalimungu ili kuleta mabadiliko ya uinjilishaji
Katika hilo aidha “Msisitizo wa hayati Papa katika kukumbatia njia ya kitaalimungu inayoleta mabadiliko katika uinjilishaji ulileta mtazamo mpya wa utume wetu,” alitoa maoni Rais wa AMECEA, Askofu Charles Sampa Kasonde, Askofu wa Jimbo la Solwezi, nchini Zambia, kwa niaba ya maaskofu, mapadre, watawa wa kike na kiume, walei na vijana wa Afrika Mashariki. Naye Askofu Willybard Kitogho Lagho, wa jimbo la Malindi na Rais wa Tume ya Uekumene na Majadiliano ya Kidini katika Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Kenya (KCCB), alisema kuwa: “Papa Benedikto XVI alipendekeza mtindo mpya wa mazungumzo ya kidini ambayo yanapita zaidi ya kuvumiliana tu.”