Bara la Afrika lilimwombea Hayati Papa mstaafu Benedikto XVI
Na Angella Rwezaula; – Vatican.
Dominika tarehe 8 Januari 2023, katika uwanja wa Mtakatifu Petro majira ya saa sita kamili kulikuwa na watu zaidi ya 30 elfu wakimsikiliza Baba Mtakatifu Francisko tafakari yake na baadaye sala ya Malaika wa Bwana. Na wengi wa waamini na mahujaji hao walikuwa tayari wamekwenda kutembelea groto za Vatican yaani chini ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, zilizofunguliwa asubuhi saa 3.00 kamili katika kaburi la Hayari Papa mstaafu Benedikto XVI ili kusali kwa ajili yake.
Hata Bara la Afrika nzima liliungana na ulimwengu wote kumuombea hayati Papa msataafu Benedikito XVI aliyeanga dunia mnamo tarehe 31 Desemba 2022, majira ya saa 3.34 asubuhi na kuzikwa tarehe 5 Januari 2023. Sala ya Rosari iliongozwa katika Madhabahu ya Bikiria Maria huko Kibeho nchini Rwanda, kwa kuungana pamoja kupitia Radio Maria. Aliyeongoza Sala ya Rosari ni Msimamizi wa Madhabahu hiyo ya Bikira Maria, Kibeho, Padre Francoise Harelimana. Sala ya Rosari iliongozwa kwa lugha ya Kiingereza na kifaransa katika Kikanisa kidogo cha Tokeo la Bikira Maria huko Kibeho nchini Rwanda. Ushiriki wa Radio Maria Afrika ulifanyika manmoa tarehe 31 Desemba, majira ya jioni saa 12.00 kamili.
Kwa hakika ushiriki wa Radio Maria Afrika kwa lugha ya kifaransa zilikuwa ni: Burundi, Camerun katika stesheni ya Yaoundé, Guinea Conakry, nchini Madagascar, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na stesheni zake: Pointe Noire, Ouesso, Kinshasa, Bukavu, Goma, Kisangani, Lubumbashi, Mbandundu, na Matadi; nchini Rwanda; Togo katika stesheni zake Lomé, Dapaong, Kara, Atakpamé na Kpalimé
Kwa upande wa lugha ya kiingereza, walishiriki Radio Maria: KENYA katika steshi zake za Nairobi, Murang’a, Kisumu; Lesotho, Liberia, Malawi, Nigeria kwenye stesheni ya Abuja, Sierra Leone, Tanzania, Uganda katika stesheni zake: Kampala, Mbarara, Kabale, Hoima, Nebbi, Mbale, Gulu, na Moroto, huko Zambia, katika stesheni za Lusaka, Chipata na Livingstone. Lakini pia ziliunganishwa na Radio Maria Ulaya kama vile Radio Maria Ufaransa na Radio Maria Uswiss.
Hayati Papa mstaafu Benedikoto XVI ambayetangu mwanzo alikuwa amejifafanua kama "mfanyakazi mnyenyekevu katika shamba la Bwana", ni maneno ambayo yametufanya kwa hakika kuelewa umuhimu wa huduma yake aliyoifanya kama mfuasi wa Mtume Petro. Kwa maana hiyo ameacha urithi mkubwa wa tafakari ya kitaalimungu na kichungaji, na zaidi kwa mtazamo wa marejeo mengi. Inatosha kukumbuka nyaraka zake za kitume, lakini pia hata katekesi na mahubiri yake aliyotamka, ni maandiko yenye thamani kubwa sana za kimungu!
Hayati Papa Mstaafu Benedikto XVI ametuachia maelekezo muhimu ya kuendelea kuishi kwa roho na upendo mkubwa wa Mtaguso wa II wa Vatican ili Kanisa liwe daima lenye uwezo wa "kuzungumza kwa watu wa kila kizazi na daima lenye uwezo wa kuunganisha imani na sababu, upendo na ukweli." Hatutamsahau kamwe kwani Hayati Benedikto XVI alikuwa mfano mzuri wa upendo wa Injili na Kanisa. Maandiko yake, yamejaa upendo mkubwa na shauku kama ile ile aliyokuwa nayo Mtakatifu Agostino, Baba wa Kanisa ambaye alimuiga hata katika kazi yake ya mwisho kwenye masomo ya kitaalimungu (Thesisi) ilihusu yeye na akaweza kundika Waraka wake wa Kitume wa kwanza kuhusu upendo uitwao " 'Deus caritas est' mnamo tarehe 25 Desemba 2005.
Katika utangulizi wake aliandika kuwa: "Mungu ni upendo; yeye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake” (1 Yoh 4:16). Maneno haya kutoka katika Waraka wa Kwanza wa Yohane yanaeleza kwa uwazi wa pekee kiini cha imani ya Kikristo: sura ya Kikristo ya Mungu na pia taswira ya mwanadamu na safari yake. Zaidi ya hayo, katika mstari huohuo, Yohane anataka kama kusema kusema, mfumo wa kuwako wa Kikristo: “Tumetambua upendo alio nao Mungu kwetu na tumeuamini."