Dominika ya IV ya Mwaka A wa Kanisa: Heri za Mlimani, Muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Hii ni Katiba ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Dominika ya IV ya Mwaka A wa Kanisa: Heri za Mlimani, Muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Hii ni Katiba ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu.   (Suedtirol Marketing GmbH, Italy)

Dominika IV ya Mwaka A wa Kanisa: Heri za Mlimani Katiba na Mwongozo wa Maisha.

Mama Kanisa anatualika katika maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya IV ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa kutafakari kuhusu Heri za Mlimani, Muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Hii ni Katiba ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya IV ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa. Leo kwa namna ya pekee kabisa, Mama Kanisa anatualika kutafakari kuhusu Heri za Mlimani, Muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Hii ni Katiba ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Mama Kanisa anawakumbusha watoto wake kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani ufunuo wa Kristo Yesu. Yeye ni Bwana wa historia na viumbe vyote na hatima ya yote haya ni ufalme wa Kristo aliyedhalilishwa kwa kukamatwa, kuteswa na hatimaye kufa Msalabani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Heri za Mlimani ni dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo yanayopaswa kusimikwa katika utakatifu na uadilifu. Kiini cha tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya IV ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa ni sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mt. 5:1-12. Hii ni sehemu muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa ambalo limeitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Ufalme wa Mungu unawajumuisha wote: watakatifu waliotubu na kumwongokea Mungu; wadhambi wanaopambana na hali ya maisha yao, ili siku moja waweze kupata toba na maondoleo ya dhambi. Ni ufalme unaojengwa na maskini, wale “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi.” Hawa ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu, waliotafutwa na Kristo Yesu katika hali na mazingira yao; akawapenda upeo na kuwapatia kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake.

Heri za Mlimani ni muhtasari, katiba, dira na mwongozo wa maisha
Heri za Mlimani ni muhtasari, katiba, dira na mwongozo wa maisha

Ufalme wa Mungu unawaunganisha pia wagonjwa na waliopagawa na pepo wachafu; wenye kuhudhiwa kwa sababu ya haki. Maskini wana heri kwa sababu wao ni kiini cha Uinjilishaji unaoendelea kutekelezwa na Mama Kanisa kama sehemu ya mpango mkakati wa kazi ya ukombozi. Kristo Yesu katika Heri za Mlimani, anataka kuwafunulia waja wake Uso wa huruma na upendo wa Mungu na katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu, Mwenyezi Mungu ndiye mhusika mkuu anayejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, Neno wa uzima. Ni Mwenyezi Mungu anayewakirimia waja wake ufalme wa uzima na haki. Ndiye anayewafariji na kuwakirimia watu wake: wema, huruma na mapendo. Ni Mungu anayeganga, kuponya na kuokoa; kutakasa na kutakatifuza. Ni Mungu anayehukumu waja wake kwa haki na kuwakirimia amani inayosimikwa katika msingi wa: ukweli, haki, upendo na uhuru kamili; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja; sehemu muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Ni Mungu anayeonesha ukarimu na upendo dhidi ya tabia ya uchoyo, “Mkono wa birika” na ubinafsi, daima yote yakiwa ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Wimbo wa Katikati unaomwonesha Mwenyezi Mungu kuwa ndiye mhusika mkuu katika historia na maisha ya mwanadamu anayeshika kweli milele yote, huwafanyia watu hukumu kwa haki, huwapa wenye njaa chakula, huwafungua waliofungwa, huwafumbua macho vipofu na kuwainua wale walioinama na kuelemewa na mizigo ya maisha, huwahifadhi wageni na kuwategemeza wajane. Mwenyezi Mungu huwapenda wenye haki bali wasio na haki “watakiona cha mtema kuni.”

Heri za Mlimani ni utambulisho wa maisha na utume wa Wakristo
Heri za Mlimani ni utambulisho wa maisha na utume wa Wakristo

Nabii Sefania katika Somo la kwanza anakazia kuhusu: Unyenyekevu wa moyo; Umaskini na Uaminifu, ili kuweza kushiriki furaha na maisha ya uzima wa milele kama anavyofafanua kwa kina na mapana Kristo Yesu. Lengo kuu la Heri za Mlimani ni kukata na kuzima kiu ya furaha ya maisha ya uzima wa milele. Jambo la kushangaza katika ulimwengu mamboleo, kuna watu wanatafuta majibu ya mkato na mepesi mepesi katika maswali magumu ya maisha. Watu wanataka furaha ya chapu! Lakini kwa bahati mbaya mara nyingi inawaachia madonda makubwa, maafa na majuto ya muda mrefu. Mtume Paulo katika Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho 1Kor 1: 26-31 anatoa na kufafanua kwa muhtasari utambulisho wa Mama Kanisa; kwa kuonesha mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa: Upendeleo kwa maskini, jambo muhimu sana katika utambulisho wa Kanisa na kwamba, Kristo Yesu, ndiye kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Yote haya ni muhimu katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia kwani kwa njia ya Kristo Yesu, wamefanywa hekima itokayo kwa Mungu, na haki na utakatifu, na ukombozi, kusudi waweze kuona fahari juu ya Mungu.  Kristo Yesu anaendelea kutangaza na kushuhudia tunu msingi za ujenzi wa Ufalme wa Mungu, kwa kuwakaribisha wote hata wale watoto watukutu na wale wapotevu, ili awaonjeshe huruma na upendo wa Mungu Baba katika maisha yao. Heri za Mlimani ni Katiba ya maisha adili na matakatifu na utambulisho wa Kanisa unaosimikwa katika haki, huruma na mapendo.

Liturujia D 4

 

 

28 January 2023, 15:14