Dominika ya Neno la Mungu Mwaka A wa Kanisa: Ushuhuda wa Injili
Na Padre Gaston George Mkude, Roma.
Amani na Salama! “Cogitor, ergo sum” (Karl Barth): “Nipo kwa kuwa Mungu ananifikiria mimi – Ni sawa na kusema Mungu ananipenda, kila mmoja wetu ni tunda la upendo wa Mungu!” (Tafsiri yangu). Leo ni Dominika ya Neno la Mungu; Hivyo nawaalika kuzingatia katika tafakuri zetu za kila Dominika kuzama zaidi na zaidi katika hilo Neno. Tangu tarehe 30 Septemba 2019, Mama Kanisa ameitenga dominika ya tatu ya Mwaka kuwa ni dominika ya kuliadhimisha Neno la Mungu: kulitukuza, kulisherehekea, kulitangaza na kulishuhudia katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vya waamini. Hii ni kuzidi kulisimika Neno la Mungu katika mioyo ya waamini na kuonesha umuhimu wake katika maisha yao na katika maisha mazima ya Kanisa. Ni katika Maandiko Matakatifu tunakutana na Neno la Mungu, anayenena nasi lakini pia anayesubiri jibu kutoka kwa kila mmoja wetu. Neno la Mungu ni mdahalo wenye pande mbili, ni majadiliano kati ya marafiki wawili, yaani Mwenyezi Mungu na kila mmoja wetu. Na ndio tutaona pia katika tafakari yetu ya leo majadiliano na mdahalo huo wa kirafiki kati ya Yesu wa Nazareti na wafuasi wake wale wa kwanza. Ni kwa njia ya Maandiko Matakatifu Mungu ananena nasi, ni humo tunakutana na Neno wa Mungu, yaani Logos. Ni Mungu anayejifunua kwetu na hasa kuyajua mapenzi yake kwa njia ya Neno lake. Na ndio maana katika Liturujia zetu Neno la Mungu linapewa nafasi na umuhimu wa pekee kabisa. Mt. 4:12-23, mwaliko ni kwa kuzama katika kulitafakari Neno lake, tunapata kung’amua mapenzi ya Mungu katika maisha yak ila mmoja wetu.
Sehemu ya Injili ya Dominika Tatu ya Mwaka A wa Kanisa tunaweza kuigawa katika sehemu tatu, kutimia kwa unabii wa Isaya, kwa Yesu kuhamisha makazi yake kutoka Nazareti na kuhamia Kapernaumu-Galilaya (aya 12-17), wito wa wafuasi wale wa kwanza (aya 18-22) na misheni ya Yesu (aya 23). Baada ya kumaliza kazi Yohane Mbatizaji pale Yordani, ikiwa ni pamoja na kumbatiza Yesu, tunaona Yesu sasa anahamia Kapernaumu iliyopo Galilaya, mji au mahali ambapo anabaki kipindi chote cha kufanya misheni yake hadharani. Ni mkoa wa Kaskazini wa nchi ile ya Israeli/Palestina, ni mkoa wa mpakani. Labda yafaa japo kwa ufupi tujiulize ulikuwa ni mji wa namna gani na umuhimu wake kwa nyakati zile za Yesu. Yesu anatoka katika kijiji chake cha Nazareti, mahali alipolelewa na kukulia na pia alipofahamika na kujulikana vema na anaamua kuweka makazi yake katika mji wa pembeni mwa ziwa la Galilaya yaani Kapernaumu. Kapernaumu kilikuwa ni kijiji cha wavuvi na wakulima. Haukuwa mji mashuhuri sana nyakati za Yesu zaidi ya mji wa Tiberiade, au mji wa Magdala uliokuwa na viwanda vya samaki, ila pamoja na hayo bado Kapernaumu ulikuwa na faida moja ya pekee kuwa ulikuwa ni mji uliopo ufukweni mwa ziwa Galilaya, hivyo ilikuwa ni njia kuu kutoka Misri kupitia Damasko na kuelekea Mesopotamia au Iraki ya sasa. Ulikuwa pia ni mpaka kati ya Galilaya na milima ile ya Golani, ambao ndio ulikuwa mji wa Filipo (mwana mwingine wa Herode Mkuu). Hivyo Kapernaumu ilikuwa ni nchi ya mipakani.
Mwinjili Mathayo anapotueleza juu ya Yesu kubadili makazi yake anafanya nukuu pia Maandiko Matakatifu (Haggadah Midrashi). Kwa Wayahudi walioishi katika mkoa ule wa Galilaya, mkoa wa Kaskazini wa nchi ile Takatifu, walichukuliwa kama nusu wapagani, kwani wengi wao walikuwa wamechanganyika na watu wa mataifa mengine kwa tamaduni na hata maisha ya kijamii na kidini. Wayahudi waliokuwa wanaishi Yerusalemu, yaani katika Mkoa wa Yudea waliwadharau na kuwaona kama ni Wayahudi nusunusu na zaidi sana kama wapagani. Watu wa Galilaya walionekana kuwa wasiojua vema sheria au Torati, hivyo walionekana kuwa ni Wayahudi wasioshika vema mapokea ya kidini na mafundisho ya kirabi. Yesu anatushangaza katika somo la Injili ya leo, kwani anachagua kuanza kazi yake hadharani katika mji ule ulioonekana kuwa sio mji wa dini sana kama ilivyo Yerusalemu ya Yudea. Ni chaguo la Yesu kuanza utume na misheni yake kwa watu waliodharaulika na hata kutengwa, kwa watu wasiokuwa wa dini na imani sana, kwa watu wanaokuwa na tabia au hulka za kipagani. Yesu daima anachagua wanaohesabika wa mwisho au kusetwa na jamii zao, wanaokuwa wa mwisho kwa hali na vipimo vya kidini na kwa mantiki ya ulimwengu huu. Yesu ni nuru na mwanga anayekuja kuwaangazia wale wanaokuwa gizani, wanaokuwa katika uvuli wa mauti, wasiokuwa na maisha ya kweli. Kama tulivyosikia katika somo la Nabii Isaya; “Watu wale waliokaa katika giza wameona mwanga mkuu. Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti mwanga umewazukia.”
Akiwa Galilaya, Yesu anashangaa imani ya askari wa Kirumi na kusema hakuna mwenye imani kubwa kama huyo askari wa Kirumi katika nchi ile ya Israeli. (Mathayo 8:10-11) Hata anapokutana na makuhani na wazee bado anawakumbusha kuwa watoza ushuru na makahaba watakuwa wa kwanza kuingia katika ufalme wa Mungu. (Mathayo 21:31) Warumi kama wakoloni wao na makahaba walihesabika kuwa ni wapagani, ni watu waliotengwa na kusetwa na jamii ile ya Kidini ya Kiyahudi. Mwinjili Mathayo anatuonesha kuwa Yesu anabadili makazi yake ili litimie andiko la nabii Isaya. Yesu ni mwanga unaokuja ili kuwangazia wale wanaokuwa gizani, ni mwanga wa kutuangazia kila mmoja wetu ili tutembee katika mwanga na kutoka gizani. Ni nuru na mwanga kuu ili kutusaidia nasi tusitembee tena katika giza la dhambi na maovu. Ni kwa njia ya Neno lake sisi tunaongozwa kutembea katika nuru ya Mungu mwenyewe, ndio kuwa na maisha mapya yanayoakisi mapenzi ya Mungu. Yesu anatualika kutubu kwani ufalme wa mbinguni umekaribia. Toba anayotualika Yesu sio kuwa japo watu wema, au kusali vizuri zaidi kidogo, au kufanya jambo jema zaidi, hapana bali ni mabadiliko ya namna zetu za kufikiri na kutenda, ni kubadili vichwa vyetu, yaani wokovu wa fikra. Ni kuongozwa na Neno lake na si mantiki na akili zetu za kibinadamu, ni kukubali maisha yetu kuwa na mwelekeo kadiri ya Neno lake linalotufumbulia mapenzi yake. Tunapoadhimisha Dominika ya Neno la Mungu, hatuna budi kukumbuka daima kuwa Neno lake ni taa na mwongozo wa maisha ya kila mmoja wetu. Ni kujikabidhi na kuacha tuongozwe na hilo Neno la uzima.
Tunaona Yesu anawaita wanafunzi wake wale wanne wa mwanzo. Ni wazi mara nyingi tumetumia wito huu wa wanafunzi wa mwanzoni kabisa kumaanisha hasa miito ya upadre au utawa, ila sio nia wala lengo la Matayo mwinjili kuonesha juu ya wito wa mitume. Ni katekesi kwetu Wakristo Wabatizwa wote kuwa nini maana ya kukubali kumfuasa Yesu, ni wito kwa kila mmoja wetu na si tu kwa wale wachache wanaoitwa kuwa watumishi kwa daraja la upadre au maisha ya wakfu kama watawa wa kike na kiume. Hivyo leo mwinjiili Matayo anatualika kutafakari wito wa kila Mbatizwa, wito wa kila mfuasi wa Yesu Kristo. Kila mfuasi anayeitwa na Yesu hana budi kuitikia wito huo mara moja bila kusitasita wala kuweka masharti kwa upande wetu. Na ndio tunaona hapa vitenzi vinavyotumika vinaonesha hakuna nafasi ya kusimama na kupumzika bali daima kubaki katika mwendo. (Tunasoma katika aya za 18,21 na 23) Yesu anatualika kumfuata daima iwe mchana au usiku, iwe wakati wa furana au huzuni, wakati mzuri au mgumu, ni ufuasi wa daima, siku zote za maisha yetu. Hivyo nasi jibu letu kwa wito wake halinabudi kuwa kama lile la wale wanafunzi au wafuasi wanne wa kwanza, jibu la utayari na ukarimu wa upendo usio na kujibakisha kama Petro, Andrea, Yohane na Yakobo. (Rejea aya 20,22).
Waliacha nyavu, mtumbwi wao na hata baba yao. Kuwa wafuasi wa Yesu haimaanishi kuwa tunapaswa kuachana au kutokuwajali wazazi na ndugu na jamaa zetu kama wakati fulani tunavyofikiri na kutenda, kwa kweli hapana na wala sio mafundisho ya Yesu hayo. Kwa Wayahudi baba alikuwa ni ishara ya mshikamano na mapokeo ya mababu, ni kuendeleza yale walioishi na kuyashika walioishi kabla yao. Na ndio katekesi ya kiteolojia anayokusudia kutufundisha leo Mwinjili Mathayo ili kumfuasa Yesu hatuna budi kuachana na maisha ya kale, maisha ya mapokeo na yale yote yanayokuwa kinyume na Neno la Mungu. Ni kukubali kuwa na kichwa kipya, kubadili namna zetu za kufikiri na kutenda, sio kutenda kadiri ya mazoea na mapokeo bali sasa kuongozwa na Neno la Mungu na Mapokeo ya Kanisa. Ni Neno la Mungu kama tunavyofundishwa na Kanisa kwani Mama Kanisa daima anabaki kuwa mwalimu wetu, na ndio maana tafakuri zetu tunajitahidi ziendane na kile kinachofundishwa na Kanisa. Yesu anakutana na wafuasi wale wa kwanza katika mazingira ya majukumu yao ya kila siku, ndio mahali pakazi. Na ndio hata nasi leo tunapokuwa mahali petu pakazi kama Wabatizwa hatunabudi kuwa mashahidi wa kweli za Injili, waenezaji wa upendo na huruma ya Mungu kwa watu tunaowahudumia na kukutana nao. Ni kwa njia ya uwepo wetu hata katika mambo madogo tunayoyafanya siku kwa siku wengine waweze kukutana na Yesu Kristo. Mbatizwa anaalikwa kuwa shahidi wa Neno la Mungu katika nyakati na mahali pote.
Na mara baada ya kumfuasa Yesu, tunaona Yesu anatupa nasi misheni ya kufanya, ndio kuwa wavuvi wa watu. (Aya 19) Wafuasi wale wa mwanzo wa Yesu katika kazi yao ya awali ya uvuvi hawakuwa wanatumia ndoano bali wavu, ndio kusema walizamisha wavu majini na kisha kutega samaki na kuwavua, kuwaleta juu au kuwatoa majini. Katika Agano la kale, bahari iliaminika kuwa ni makazi ya shetani, magonjwa na kifo. Bahari ilionekana kutisha na kuogofya si tu kwa watu wa kawaida bali hata wale waliokuwa wataalamu wa kazi ya uvuvi, kwani daima ilikuwa ni ishara ya kifo na maangamizo. Hivyo kuwa wavuvi wa watu ndio kusema kuwatoa katika kina chenye giza na hatari na kuogofya, ni kuwaleta juu ili waweze kupata uzima. Ni wajibu wa kila mfuasi wa Yesu kutoka na kwenda kuwa mvuvi, kuwasaidia na wengine kutoka katika kina hatarishi ili waweze kutembea katika uzima. Na ndio wito aliotuchia Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuwa baada ya kukutana na Yesu Kristo hatuna budi kutoka na kuwashirikisha wengine furaha ya kufanyika rafiki na wafuasi wake Yesu Kristo! Imani ni tukio la kukutana na Yesu Kristo, hivyo kila mmoja wetu anayekubali kweli kuwa mfuasi anajawa na furaha ya kuwashirikisha wengine upendo na huruma ya Mungu! Hakika kila anayekutana na Yesu Kristo mfufuka anakuwa na mang’amuzi haya ya kujawa na furaha yenye tumaini la wokovu, furaha ya upendo ya kuwashirikisha wengine upendo na huruma ya Mungu.
Sehemu ya tatu na ya mwisho ndio ile inayooanisha na kuhitimisha kile ambacho Yesu anakifanya kwa kila mwanadamu, kufundisha, ndio kuwa mwanga kwa kila mwanadamu; kuhubiri Habari Njema, kutuhubiria Neno lenye faraja na matumaini, na ndio Habari Njema, kutuhakikishia kuwa upendo wa Mungu una nguvu kuzidi kila aina ya uovu na ubaya na pia kuponya magonjwa. Yesu anajaribu kuweka kwa ufupi kabisa misheni yake hapa ulimwenguni na kwa kweli ndio utume kwa kila aliye mwanafunzi na mfuasi wa Yesu Kristo. Naomba nimalizie tafakari yetu kwa kumnukuu mwanateolojia wa Kiprotestanti aitwaye Karl Barth ambaye naye amemnukuu mwanafalsafa Decartes. Wakati Decartes alisema “Cogito, ergo sum” (Nafikiri, kwa hiyo nipo) na badala yake anatualika mwanateolojia huyo kusema pamoja naye “Cogitor, ergo sum”, maana yake, “nipo kwa kuwa Mungu ananifikiria mimi”. Ni maneno yenye kuonesha na kukiri upendo wa Mungu usio na masharti kwa kila mmoja wetu. Ni Mungu anamtafuta na kutaka kumkomboa kila mmoja wetu, anakuja kwetu si kwa sababu sisi ni wema, bali kwa kuwa sisi ni wa thamani na hivyo anaotufikiria kila wakati na kila mara. Mimi nipo na ni wa thamani kwa kuwa Mungu ananifikiria na kunijali. Naomba niongeze pia maneno ya Carl Gustav Jung mwanasaikolojia aliyewahi kusema: “Vocatus atque non vocatus Deus aderit”, yaani, “iwe tumemuita au la, Mungu daima yupo pamoja nasi”, ndio asili ya Mungu kwani ni Upendo usio na masharti, daima anakuwa pamoja nasi hata kama hatuna muda wala kutaka aongoze maisha yetu. Wapendwa ni maneno yenye faraja kwa kila mmoja wetu hivyo hatuna budi kila mara kutenga muda na kukaa na kuongea naye na hasa kwa kuongozwa na Neno lake. Tafakari njema na Dominika takatifu kwenu nyote!