Dominika ya Neno la Mungu: Wito, Ushuhuda na Uekumene wa Sala na Huduma Makini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya Barua Binafsi, Motu Proprio “Aperuit illis” yaani: “Aliwafunulia akili zao” iliyochapishwa tarehe 30 Septemba 2019, kumbukumbu ya kiliturujia ya Mtakatifu Hieronimo, katika uzinduzi wa mwaka wa 1600 tangu alipofariki dunia, alianzisha maadhimisho ya Dominika ya Neno la Mungu inayoadhimishwa Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa na kwa Mwaka huu inaadhimishwa tarehe 22 Januari 2023 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo.” 1Yn 1:3. Baba Mtakatifu anasema hii ni Dominika kwa ajili ya kuliadhimisha, kulitafakari, kulieneza na kulishuhudia Neno la Mungu, dira na mwongozo wa maisha. Maadhimisho ya Dominika ya Neno la Mungu ni matunda ya Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu na pia yana mwelekeo wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Dominika hii inaadhimishwa wakati wa Juma la kuombea Umoja wa Wakristo na maadhimisho haya kwa mwaka 2023 yanaongozwa na kauli mbiu “Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki” Isa 1:17. Kristo Yesu kabla ya kupaa kwenda mbinguni “Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na Maandiko” Lk. 24:45.
Kwa ufupi Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Neno la Mungu inatualika kwa namna ya pekee, kutafakari kuhusu wito wa kila mmoja wetu na hatima yake, yaani kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, huku tukiwa tumeungana na kushikamana kama wafuasi wa Kristo Yesu na Yesu mwenyewe akiwa ni kiini na hatima ya Habari Njema ya Wokovu.Tunaongozwa na Neno la Mungu: Isa 9: 1-4; 1Kor 1: 10-13, 17 na Mt 4: 12-23. Yohane Mbatizaji baada ya kumtambulisha Kristo Yesu hadharani, alikamatwa, akafungwa na hatimaye atakuja kukatwa kichwa, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda kwa Mwanakondoo. Kristo Yesu anaanza utume wake huko Galilaya ya Mataifa, ili kuwatangazia na kuwashuhudia watu wa Mataifa uwepo wa Ufalme wa Mungu kati yao, kiini cha Fumbo la Umwilisho. Mwaliko ni kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Tunakumbushwa kwamba, wito ni zawadi kutoka kwa Mungu na ndiye anayechukua hatua ya kwanza kumtafuta na kumtuma mja wake. Wito wowote ule unadai sadaka na majitoleo, ili kuanzisha mahusiano na mafungamano mapya na Kristo Yesu. Tunaitwa kuwa ni watakatifu kama Baba yetu wa mbinguni alivyo Mtakatifu. Tunaitwa kuwa mitume na wafuasi wa Kristo Yesu ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.
Kauli mbiu inayoongoza Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2023 ni “Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki” Isa 1:17. Uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo unajikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini ili kujenga na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu Injili, ni kwa kadiri ile ile wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo na udugu kati yao. Uekumene wa damu unajikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.
Kwa ufupi kabisa, majadiliano ya kiekumene yawasaidie waamini kujenga na kudumisha umoja, ushiriki na utume wa Kanisa kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kwani majadiliano ya kiekumene na Sinodi ni sawa na chanda na pete, ni mambo yanayokamilishana na kutajirishana. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Hati ya “Dei verbum” yaani “Neno la Mungu”, wanafafanua: maumbile na maana ya ufunuo; urithishaji wa ufunuo wa Mungu; Uvuvio wa Kimungu na ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu, Agano la Kale na Agano Jipya. Neno la Mungu ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Umoja wa Wakristo upate chimbuko lake kwa kusikiliza Neno la Mungu, linalofafanuliwa na wachungaji, kiasi kwamba, hata Mahubiri yanachukuliwa kuwa kama “Kisakramenti” muda muafaka wa kufafanua uzuri wa Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya waamini. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika tafakari yao kuhusu Kanisa katika ulimwengu mamboleo wanakazia umuhimu wa Kanisa lililopo katika ulimwengu na linaloishi na kutenda kazi pamoja na walimwengu, ndiyo maana ya Kanisa kutoka kuwaendea watu wa Mataifa! Kwa upande wao, Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia walitilia mkazo pia umuhimu wa kutambua dhamana na utu wa wabatizwa wote ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume “Verbum Domini” alisema kwamba, Daraja dogo la Usomaji ni huduma ya waamini walei.
Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, pamoja na mabadiliko yote haya, lakini Mama Kanisa hana nia ya kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa wanawake, kama alivyowahi kutamka Mtakatifu Yohane Paulo II. Mama Kanisa anapenda kuendelea kuwa mwaminifu kwa Kristo Yesu pamoja na kuendelea kutia nia ya kuishi, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama ilivyotangazwa na Mitume pamoja na waandamizi wao, ili kweli, Kanisa liweze: kulisikiliza, kulihifadhi kitakatifu na kulitangaza kiaminifu. Mama Kanisa anataka kumtumikia Mungu na watu wake kwa uaminifu mkubwa. Mabadiliko haya yanapania pamoja na mambo mengine, kuwahamasisha wanawake kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya; kwa kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni na maamuzi muhimu katika maisha ya jamii wanamoishi. Ukuhani wa Ubatizo na Ukuhani wa Daraja ni muhimu kwa ajili ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, kwa muda wa miaka mingi wanawake wamekuwa wakitoa huduma ya usomaji wa Neno la Mungu na Utumishi Altareni kwani yote haya yanapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara, kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa sanjari na kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.
Makatekisita, ni sehemu muhimu sana kwa maisha na utume wa Kanisa, kumbe, wafundwe kikamilifu, ili wawasaidie waamini kukua katika imani kama ilivyokuwa kwa wale wafuasi wa Emmau, waliobahatika kufafanuliwa Maandiko Mtakatifu na Kristo Yesu alipokuwa anatembea pamoja nao njiani. Neno la Mungu lina utajiri mkubwa na amana ya kufundishia. Ni muhtasari wa maisha ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chemchemi ya imani na ukweli wa maisha na Fumbo la Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo. Neno la Mungu linafafanua historia ya wokovu, linabainisha maisha ya kiroho na kanuni ya Fumbo la Umwilisho. Baba Mtakatifu anawataka waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao! Neno la Mungu linatenda kazi ndani ya yule anayelisikiliza kwa makini, kiasi cha kumwajibisha kuwashirikisha wale wote anaokutana nao, ili kujenga na kudumisha umoja na mafungamano ya watoto wa Mungu.
Neno la Mungu ni chemchemi ya upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma kwa akina Lazaro wanaoendelea kuteseka sehemu mbalimbali za dunia hata katika ulimwengu mamboleo, changamoto na mwaliko wa “kufyekelea mbali ubinafsi na uchoyo”, ili kujenga na kudumisha umoja, ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, tukio la Yesu kugeuka sura mbele ya wafuasi wake, akaonekana akizungumza na Musa na Elia, ni ushuhuda wa utimilifu wa Sheria na Unabii. Maandalizi makini ya kupambana uso kwa uso na Kashfa ya Msalaba yaani: Mateso, Kifo na hatimaye, Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Katika mchakato mzima wa kusoma, kusikiliza, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya waamini, Bikira Maria anabaki kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kumwilisha Heri za Mlimani; muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu katika maisha yake.