Tafuta

2023.01.02 Papa Benedikto XVI wakati wa ziara yake ya kitume nchini Angola. 2023.01.02 Papa Benedikto XVI wakati wa ziara yake ya kitume nchini Angola. 

Kard.Kambanda,Africae Munus ya Papa Benedikto XVI:ni mpango wa maisha ya kichungaji

Askofu mkuu wa Kigali,Kardinali Kambanda akizungumzia juu ya Hayati Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI amesema anavyokumbukwa sana na Kanisa la Afrika kwa ziara zake za kichungaji barani humo na mawaidha ya Wosia wake wa Kitume wa 'Africae Munus' baada ya sinodiya Afrika."Bara la Afrika ni kama pafu la kiroho la mwanadamu."

Na Angella Rwezaula; – Vatican.

Katika mahojiano maalum na Vatican News na yaliyofanywa na Padre Fidele Mutabazi mjini Kigali, na Kardinali Antoine Kambanda, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Kigali, nchini Rwanda, alisema kuwa ziara za Papa Mstaafu Benedikto XVI, barani Afrika mnamo  mwaka 2009 na 2011 zilikuwa muhimu sana. Kardinali pia alikubali hata dokezo la Papa Mtaafu aliyefafanua kuhusu bara la Afrika kama pafu la kiroho la mwanadamu. “Ilikuwa taswira aliyoisifu Afrika kwa uchangamfu wake, mtazamo wa kidini wa watu wake na ustahimilivu wao wa kudumu”. Mahojiano nayo ni baada ya kifo cha Baba Mtaafu Benedikto XVI kilichotokea tarehe 31 Desemba 2022, akiwa katika makao yake aliyochagua kuishi katika nyumba ya Mater Ecclesiae mjini Vatican. kwa maana hiyo Kardinali  Kambanda alisema anavyokumbuka ziara zake za kichungaji barani Afrika ambapo mnamo Machi 2009, nchini Kamerun, aliwasilisha na kuanzisha Instrumentum Laboris yaani (hati ya kitendea kazi) kwa ajili ya  Sinodi Maalum ya Pili ya Maaskofu kwa Bara la  Afrika (inayojulikana pia kama Sinodi ya Pili ya Afrika). Aidha alikumbuka ziara yake ya kitume  nchini  Angola, nchi ambayo ilikuwa imekumbwa na vita na migogoro kwa miaka mingi. Ujumbe wake kwa ujumla ulikuwa wa amani na upatanisho. Na pia kuna ziara ya kukumbukwa nchini Benin.

Katika kujibu swali kuhusiania na nini maana ya Africae munus,  Kardinali Kambanda alisema, wakati wa ziara ya kitume ya siku tatu mnamo  2011 katika Jamhuri ya Afrika Magharibi ya Benin, Papa Mstaafu Benedikto XVI  aliwasilisha kwa Kanisa la Afrika Wosia wa Kitume wa Baada ya Sinodi, uitwao 'Africae Munus'. Kwa maana hiyo Hati iliyopewa jina, Africae Munus, ilikuwa matokeo ya kichungaji ya Sinodi ya Pili ya Afrika, iliyofanyika mjini Roma mwezi Oktoba 2009 kwa kuongozwa na kauli mbiu: "Kanisa Barani Afrika katika Huduma ya Upatanisho, Haki na Amani". Kwa  hiyo Africae Munus ni lugha ya Kilatini ikiwa na maana “Dhamana ya Afrika". Katika Wosia huo, Papa Benedikto XVI analikumbusha Kanisa Barani Afrika kuhusu umuhimu wa upatanisho, haki na amani kuwa ni maeneo muhimu ya kichungaji.

Na alipoulizwa na Vatican News,  iwapo Kanisa la Afrika limtelekeza Wosia wa Africae Munus, Kardinali Kambanda alieleza kuwa utekelezaji bado unaendelea. “Africae Munus” haijasahaulika kabisa. Ina ajenda ya maisha marefu na mpango wa utekelezaji. Ni ya muda mrefu kwa sababu inashughulikia baadhi ya changamoto muhimu zinazokabili Ukristo wa Kiafrika. Hizi ni pamoja na vurugu za kisiasa na migogoro inayochangiwa na tofauti za kikabila tofauti hizi zinaposimamiwa vibaya au kunyanyaswa …Tofauti zetu za kikabila na kitamaduni ni nyingi na zinaweza kutumiwa kujenga mataifa. Tofauti hizi ni nzuri, kama zinakuwa tu rangi tofauti za maua kwenye bustani,” alisisitiza Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Kigali.

Wosia wa Africae Munus unasisitizia umoja, upatanisho, haki, amani, na kuhakikisha kwamba maelewano yanakuwepo pale tofauti zinapotokea. “Ni changamoto kubwa kwa Ukristo wa Kiafrika kwa sababu Waafrika hupokea imani ya Kikristo kwa shauku, lakini linapokuja suala la tofauti za kikabila, na hasa wakati hizo zinapotumiwa kisiasa, changamoto ya jinsi ya kuishi imani ya Kikristo inakuwa shida.” Kardinali aliendelea, kwamba “Inapotumiwa vibaya kwa mawazo ya kisiasa yenye maono mafupi na itikadi mbovu za kisiasa zinazotaka kugawanya na kutawala, mkanganyiko huo unaweza kuharibu mataifa. Aidha  katika hili kuweza kuona sura ya Mungu katika kaka au dada ambaye ni tofauti na mimi, ambaye ni wa kabila tofauti na langu, inakuwa changamoto kwa imani yangu. Injili na imani yangu inatoa mwaliko niwapokee na kuwakaribisha wengine na kuwatumikia licha ya tofauti zetu.

Kwa hiyo, kardinali aliongeza kusema kuwa inaonekana wazi ni kwa jinsi gani dira ya Injili inaweza kuwa changamoto kubwa kwa Wakristo Barani Afrika katika kukabiliana na itikadi za mgawanyiko. Kwa upande wa Kardinali Kambanda, alisema kuwa Mkristo anaitwa kutazama maisha jinsi Mungu anavyoyaona ,  kwa mtazamo wa  upendo wa kaka na dada.  Kwa hiyo Wosiwa wa Africae Munus unagusa jeraha la Afrika ... Hata hivyo, licha ya haya yote, Afrika imejaa ushuhuda wa watu ambao walikufa kiimani kwa sababu waliishi kwa uaminifu maono haya ya Kikristo.  Na hatimaye, waliuawa kwa sababu ya imani yao,” alisema.

Kwa kutazama nchi yake, alisema kwa sasa nchini Rwanda wamekuwa na shuhuda nyingi sana, miongoni mwao wanayo familia ya Cyprien Rugamba na Daphrose Mukasanga, ambao waliuawa kwa sababu waliishi kwa uaminifu Injili ya upendo inayokinzana na migawanyiko ya kiitikadi kama vile itikadi ya mauaji ya kimbari, Kardinali wa  Kigali alifafanua. Cyprien na Daphrose Rugamba walikuwa wanandoa wacha Mungu walioanzisha Harakati ya  Upyaisho wa Karismatiki kikatoliki na Jumuiya ya Emmanuel nchini Rwanda mnamo mwaka 1990. Na mnamo tarehe 7 Aprili 1994, Cyprien na Daphrosa waliuawa pamoja na watoto wao katika kilele cha Mauaji ya Kimbari ya Rwanda dhidi ya Watutsi. Wanandoa hao walisimama kwa ujasiri kupinga migawanyiko ya kikabila. Mchakato wa kutangwazwa kwao kwao kuwa wenye heri ulifunguliwa na Vatican mnamo  mwaka wa 2015. “Kwa hiyo, hili ndilo ambalo Wosia wa Africae Munus anaendelea kutfundisha, kuimarishwa na kuungwa mkono na Papa Benedikto. Ni urithi tajiri ambao Papa Mstaafu Benedikto XVI ametuachia,” alisisitiza  Kardinali Kambanda.

Mahojiano kati ya Vatican News na Kard Kambanda wa Rwanda
10 January 2023, 15:25