Tafuta

Sherehe ya Bikira Maria, Mama wa Mungu sanjari na Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani kwa mwaka 2023. Sherehe ya Bikira Maria, Mama wa Mungu sanjari na Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani kwa mwaka 2023. 

Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, Theotokos, Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani 2023

Mama Kanisa anaaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, "Theotokos" sanjari na Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani inayonogeshwa na kauli mbiu “Hakuna mtu anayeweza kujiokoa Mwenyewe. Kupambana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na kwa pamoja kujielekeza kwenye njia ya amani. Leo Kanisa linakiri Ubinadamu na Umungu wa Kristo Yesu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika Liturujia ya Neno la Mungu, Mama Kanisa anapoadhimisha Sherehe ya Bikira Maria, Mama wa Mungu sanjari na Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani inayonogeshwa na kauli mbiu “Hakuna mtu anayeweza kujiokoa Mwenyewe. Kupambana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na kwa pamoja kujielekeza kwenye njia ya amani. Januari Mosi, 2023 ni siku maalum ya kumtolea Mwenyezi Mungu shukrani zetu kwa wema na ukarimu wake wote aliotutendea katika kipindi cha mwaka 2022 hata bila mastahili yetu, bali ni kwa huruma, wema na upendo wake wa daima, leo hii tumepewa tiketi ya kuuona Mwaka 2023. Dhamira kuu ya Kiliturujia ni kuadhimisha na kusherehekea sikukuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu na kujikabidhi chini ya ulinzi wake kwa mwaka unaoanza 2023. Itakumbukwa kuwa Januari Mosi, ni siku ya nane katika Oktava ya Noeli, hivyo ni siku ya kutahiriwa na kupewa jina kwa mtoto Yesu – kufuatana na mapokeo ya sheria ya Musa ya kutahiriwa mtoto wa kiume na kupewa jina siku ya nane baada ya kuzaliwa kwake. Januari 1, ni siku ya kuomba amani duniani. Januari Mosi ni siku ya kuuaga mwaka ulioisha na kuukaribisha mwaka mpya. Ni siku ya kufanya tathimini ya maisha yetu ya kiroho, kimwili, kifamilia, kijamii na kimahusiano na kuweka mipango mikakati kwa mwaka unaoanza. Januari 1, ni siku ya shukrani kwa Mungu kwa mema yote aliyotujalia mwaka ulioisha na kuwashukuru wote waliochangia kwa namna yoyote ile katika maisha yetu mwaka uliopita.

Mei Mosi, Januari 2023, Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, Theotokos
Mei Mosi, Januari 2023, Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, Theotokos

Baada ya dhambi ya asili aliyotenda Adamu na Eva, mwanadamu alipoteza urafiki na Mungu muumba wake na kujitenga naye (Mwanzo 3:23). Mungu kwa upendo na huruma yake kwa njia na namna mbalimbali, kupitia wafalme na manabii wake alianza taratibu kutufunulia mpango wake wa kumuumba upya mwanadamu. Kuzaliwa kwa Bikira Maria bila dhambi ya asili ni mpango wa Mungu katika harakati za kumkomboa mwanadamu. Kanisa Katoliki linaamini na kufundisha kuwa Bikira Maria kweli ni mama wa Mungu. Hii ni kwa sababu alimzaa mwana wa Mungu- Nafsi ya pili ya Mungu Mwana. Maandiko Matakatifu yanasema; “Mungu alimtuma Mwanaye ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao walikuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana (Gal 4:4-5)”. Kwa fumbo la umwilisho wa nafsi ya pili ya Mungu – Mungu Mwana, Bwana wetu Yesu Kristo mwilini mwa Mama Bikira Maria kulimfanya yeye kuwa Mama wa Mungu - daraja/nguzo kuu ya Mungu kujifanya mtu na kufungua ukurasa  mpya ndani ya historia ya wokovu wa mwanadamu. Kwa utii, alikubali  mapenzi ya Mungu yafanyike akisema; “Mimi ni mjakazi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema” (Luka 1:38). Kwa namna hii, Mungu aliye Mwenyezi, Mkuu kuliko vyote, akafanya makao yake katika tumbo la mama Bikira Maria, akazaliwa na kukaa kwetu  “Neno wa Mungu akatwaa mwili na akakaa kwetu” (Yn. 1:14). Kwa hivyo, mama Maria ni mama wa Mungu kwasababu yeye ni mama wa Kristo ambaye ni Mungu kweli na mtu kweli.

Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani 2023
Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani 2023

Katika lugha ya kawaida tunasema mama ya Padre au Sista, mama ya raisi au mbunge, haimaanishi kuwa aliuzaa upadre au usista, urais au ubunge isipokuwa, mtoto wake wa kuzaa ana hadhi ya upadre au usista, uraisi au ubunge. Katika Kanuni ya Imani tunasali; “Nasadiki kwa Bwana Mmoja Yesu Kristo, Mwana wa pekee wa Mungu. Aliyezaliwa kwa Baba, tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli”. Kwa maneno haya tunakiri kuwa Yesu ni mwana wa Mungu “aliyezaliwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria, akawa Mwanadamu”. Ikiwa Bikira Maria ni mama wa Mwana wa Mungu, aliye Mungu, kwahiyo Bikira Maria ni Mama wa Mungu Kwa hiyo Bikira Maria alimzaa Yesu ambaye ni Mungu kweli na mtu kweli (Rejea. Mt.1:18-25, Lk. 2:48, Yn.2:1, Gal.4:4, Lk. 1:42-43, Mt.2:1, Fil.2:6-7). Kumbe, Bikira Maria ni Mama kweli wa Yesu, kwakuwa hali ya ubinadamu wa Yesu ilichangiwa na Mama Bikira Maria kwa ukamilifu wote, kama ilivyo kwa mama zetu walivyochangia kikamilifu katika uundwaji wetu na kuitwa binadamu tuliokamilika. Bikira Maria ni kweli Mama wa Mungu, kwa kuwa alichukua mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na kuzaa nafsi ya Pili ya Mungu. Nasi twaamini hivyo na hatuna shaka.

Januari Mosi, Ni Siku ya Shukrani kwa Mungu
Januari Mosi, Ni Siku ya Shukrani kwa Mungu

Somo la kwanza la kitabu cha Hesabu (Hes. 6:22-27), ni sala ya baraka kuu ya Mungu kuwabariki wana wa Israeli  kupitia mkono wa Aaroni na wanawe makuhani. Kama ilivyokuwa katika kanuni ya baraka kwa waisraeli, Mungu anaahidi kuwaangazia nuru ya uso wake wale wote wanaopokea baraka yake. Mungu atakuwa nao daima. Basi nasi siku hii ya kwanza ya mwaka, tuombe neema na baraka za Mungu kupitia mikono ya Makuhani wake zikae na kudumu nasi kwa mwaka mzima tunaouanza ili uwe mwaka wa amani na neema tele. Somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia (Gal. 4:4-7), latuonyesha jinsi Mungu alivyomtuma Mwanae ambaye alizaliwa na Mama Bikira Maria, wakati ulipotimia, ili sisi sote tupate kupokea hali ya kuwa wana (Gal 4:5). Bikira Maria, kwa kumzaa Kristo  alihitimisha unabii wa manabii wa kale wa kuja kwake Masiha kuwakomboa watu kutoka dhambini. Umwilisho wa Yesu ni ukamilisho wa sheria ya Agano la Kale iliyokuwa matayarisho kwa ujio wake. Kufika kwa Kristo ulimwenguni kumetufanya huru na sheria hizo. Katika ubatizo tumefanywa ndugu wa Kristo na watoto wa Mungu. Hivyo basi, tukio nzima la umwilisho lilifungua milango ya wokovu kwa kila mmoja wetu. Lakini tukumbuke kuwa wokovu si jambo la kushurutiswa bali ni la hiari. Ili kuupokea lazima kila mmoja wetu kusema ndio yake ya hiari kama vile alivyofanya mama Bikira  Maria. Hatuna budi kuamua na kukusudia kwa dhati kumfuasa Yesu kwa moyo wa dhati huku tukiibeba misalaba yetu (Mt 16:24).

Waamini wanahamasishwa kuombea amani duniani
Waamini wanahamasishwa kuombea amani duniani

Injili ya Luka (Lk 2:16-21), inatupeka pembeni mwa Pango la Mtoto Yesu, ambapo tunawakuta wachungaji ambao baada ya tangazo kutoka mbinguni kusikika, walifunga safari kwenda Bethlehemu na huko walimwona Maria na Yosefu, na yule Mtoto mchanga aliyelazwa horini. Hawa ndio waliokuwa wanangojea kwa hamu ukombozi wa Israeli. Kumbuka hakuna chochote cha pekee wanachokutana nacho mbali na mtoto mchanga na wazazi wake. Lakini katika uchanga na unyonge wa yule mtoto walimtambua Mwokozi wa Wanadamu. Ili kuboresha na kuhuisha imani yetu, mara nyingi tunatafuta mambo yasiyo ya kawaida: tunatafuta ishara, miujiza, ushuhuda wa kimatokeo na ishara. Yesu anakuwa mkali kwao wanaotafuta uthibitisho na miujiza, tena anawaita “kizazi cha nyoka tena kiovu” (Lk 11:29). Kumbe tunaona kuwa Mungu anakuja kwetu kawa njia ya mtoto mchanga. Wachoraji wa pango na hori wanawaonesha wachungaji wakiwa wamepiga magoti mbele ya hori wakimpa mtoto heshima stahiki. Mamajusi nao walipofika wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia, walipiga magoti na kumpa mtoto Yesu heshima (Mt 2:11).

Waamini wawe ni wajenzi na madaraja ya haki, amani na maridhiano
Waamini wawe ni wajenzi na madaraja ya haki, amani na maridhiano

Luka katika sura ya kwanza ya Injili yake anasisitiza juu ya mshangao na furaha isiyo na kifani kwa yeyote anayefungamana na mpango wa Mungu. Elizabeti baada ya kutambua kuwa ana mimba kwa uwezo wa Mungu alishangilia: “Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana, katika siku zile alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu” (Lk 1:25). Simeoni na Nabii Hannah walimsifu Mungu kwa kuwaruhusu wauone wokovu uliondaliwa kwa ajili ya mataifa yote (Lk 2:28, 38). Maria na Yosefu walikuwa wakishangaa na kustaajabia mambo yaliyonenwa juu ya mtoto huyu (Lk 2:33, 48). Vivyo hivyo kwa wachungaji na Mamajusi. Siku ya kwanza ya mwaka mama Kanisa ameiweka iwe siku ya kuombea amani duniani. Historia inatufundisha na kutuonesha kuwa maadui wakuu wa amani ni tamaa ya mali, tamaa ya mwili na tamaa ya madaraka, cheo au mamlaka. Tamaa hizi zinafanya watu kudhulumiana haki zao na hata kuuana. Mang’amuzi ya kila siku yanatuonesha kwamba kwa asili moyo wa mwanadamu una maelekeo ya uovu na ubinafsi. Hata mtoto mchanga ana maelekeo ya ubinafsi, ndiyo maana akiona kitu kizuri anataka kiwe chake anaking’ang’ania na kulia mpaka apatiwe kitu hicho. Anataka kila kitu kizuri anachoona kiwe mali yake kwa namna yoyote ile.

UVIKO-19 imesababisha madhara makubwa, lakini pia kuna faida zake.
UVIKO-19 imesababisha madhara makubwa, lakini pia kuna faida zake.

Kila mmoja wetu ana maelekeo haya. Tusipofanyia kazi maelekeo haya kwa jitihada yetu na kwa neema ya Mungu tutakuwa na ubinafsi wa hali ya juu. Moyo ukiwa na maelekeo haya unataka kumiliki haki za wengine: mali, kazi, mke, mume, cheo. Mtu wa namna hii anatafuta mali siyo kwa ajili ya kuishi maisha yenye hadhi ya kibinadamu - kujipatia mahitaji msingi – chakula, mavazi, na makazi bali hupenda kujilimbikizia na kutosheleza tamaa zake kwa gharama yoyote ile bila kujali utu wa wengine. Mtu wa namna hii anaweza kutoa uhai wa mtu mwingine ili apate kile anachotamani kukipata. Mtu huyu anamwonea jirani yake wivu kwa kila anachofanya na kufanikiwa. Wivu huu unapokithiri ndipo tunaanza kutafuta namna ya kuwaangamiza waliofanikiwa. Tunadiriki kutafuta mbinu ya kuharibu ustawi wa wengine, tunapoelekea kushindwa tunawafitini kwa namna mbalimbali. Hali hii inawafanya majirani wasisaidiane kwa lolote, marafiki wanaishi kwa wasiwasi na kutoaminiana. Hili ni ashirio la kutokomea kwa amani siku baada ya siku. Hii ni kwa sababu Mungu hayumo kati ya watu hawa na hivyo hawatendi kwa haki na bila haki hakuna amani ya kweli. Basi siku ya kwanza ya mwaka ni vizuri kusali na kumwomba Mungu ashushe Baraka zake zitakazotusindikiza kwa mwaka mzima. Kama tukimsikiliza Roho wa Mungu aishiye ndani yetu tangu ubatizo, kama tukilisikiliza Neno la Mungu na kufuata mfano wa Kristo, kwa mwaka mzima tutakuwa chanzo cha amani. Hatutakuwa chanzo cha vita, mgawanyo, na mpasuko. Tutakuwa wapenda na wapigania amani. Nawakatieni Heri na Baraka za Mwaka mpya 2023 uwe Mwaka wa amani,upendo na neema tele.

 

02 January 2023, 14:24