Tafuta

Kwetu sisi Epifania ni sherehe ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani na kwa maajabu makubwa aliyoyafanya kwa namna alivyojidhihirisha kwetu. Kwetu sisi Epifania ni sherehe ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani na kwa maajabu makubwa aliyoyafanya kwa namna alivyojidhihirisha kwetu.   (Vatican Media)

Sherehe ya Tokeo la Bwana, Epifania: Ufunuo wa Kristo Yesu Kwa Watu wa Mataifa

Tokeo la Bwana ni ufunuo wa Kristo Yesu kama Masiha wa Israeli, Mwana wa Mungu na Mwokozi wa Ulimwengu. Mamajusi wanawakilisha dini za mazingira ya kipagani. Injili inaonesha matunda ya kwanza ya watu wa Mataifa wanaopokea Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Mamajusi wanaonesha ile kiu ya watu wa Mataifa kutafuta kwa Israeli mwanga wa Masiha.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, katika Sherehe ya tokeo la Bwana - Epifania. Sherehe hii huadhimishwa kila mwaka tarehe 06 Januari, lakini kwa sababu za kichungaji yaweza kuadhimishwa jumapili ya karibu ili waamini wengi waweze kushiriki na kutambua maana yake. Neno Epifania asili yake ni lugha ya Kigiriki, likimaanisha kutokea, kujionesha au kujifunua. Katika sherehe hii neno Epifania linatumika kumaanisha kujifunua kwa Mungu katika Nafsi yake ya pili Mungu mwana, katika umbo la mwanadamu kwa njia ya mtoto Yesu kwa kuzaliwa kwake na Bikira Maria huko Bethlehemu katika hori la kulishia wanyama chini ya ulinzi wa Yosefu mbele ya watu wa mataifa – wapagani- watu wasio wayahudi wakiwakilishwa na mamajusi - wataalamu wa elimu ya nyota waliotafuta ukweli wa mambo kupitia sayansi na elimu ya nyota. Kuna namna na matukio mengine ambayo kwayo Mungu alimtambulisha Mkombozi wetu, Masiha, Yesu Kristo. Yohane Mbatizaji alimtambua angali bado tumboni mwa mamaye Elizabeti kwa kuruka kwa furaha, Bikira Maria alipokwenda kumtembelea (Lk.1:44).

Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali waliongozwa na nyota kumwona Yesu
Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali waliongozwa na nyota kumwona Yesu

Wachungaji nao kwa kufuata maongozi ya Malaika walimtambua na kukiri kwamba Yeye ni Mkombozi wa wanadamu (Lk.2:1-20. Mamajusi wakiongozwa na nyota nao wakaja wakamsujudia na kumtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane (Mt.2:1-12). Mzee Simeoni na Anna walimtambua pale alipotolewa hekaluni (Lk.2:22-40). Wakati wa ubatizo Mtoni Yordani, Mungu alimtambulisha akisema: “Huyu ni Mwanangu mpendwa ninayependezwa naye, msikilieni yeye” (Mt.3:17). Na katika harusi ya Kana, alijita,bulisha kwa kugeuza maji kuwa divai (Yn 2:12). Matukio haya yote mwanzoni yaliadhimisha kwa pamoja katika sherehe ya Epifani – Tokeo la Bwana. Baadae yalitenganishwa na kila moja kuwekewa siku yake maalumu ya kuadhimishwa: Kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo kulianza kuadhimishwa tarehe 25 Desemba, kubatizwa kwake kuadhimishwa jumapili baada ya sikukuu ya Epifania – ambayo kawaida huadhimishwa 6 Januari. Hakuna tarehe maalum iliyowekwa kukumbuka tukio la muujiza wa Kana. Hivyo Yesu kujionesha kwa Mamajusi likawa tukio la msingi katika Sherehe ya Epifania hasa kwa wakristo wa mwanzo waliokuwa wapagani, kwasababu mamajusi walikuwa ni ishara ya Mungu kujifunua na kujidhihirisha kwa mara ya kwanza kwa watu wasio Wayahudi kwa Mataifa yote. Kwa hiyo sherehe ya Epifania ilikuwa kwa Wakristo wa mwanzo, sherehe ya watu wa Mataifa wapagani kupokea imani.

Sherehe ya Tokeo la Bwana: Ufunuo wa Kristo Yesu kwa Mataifa
Sherehe ya Tokeo la Bwana: Ufunuo wa Kristo Yesu kwa Mataifa

Kwetu sisi Epifania ni sherehe ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani na kwa maajabu makubwa aliyoyafanya kwa namna alivyojidhihirisha kwetu. Kwa matukio yote haya, Kristo ajionesha wazi kwamba Yeye ni Masiha. Epifania ni sherehe yetu kwani tunafahamu kuwa Yesu amejionesha kwa watu wa Mataifa – wapagani. Nao wamepokea Imani – wongofu – uzima. Tukumbuke kuwa Mamajusi hawakuwa Wayahudi, nasi pia ambao tumeipokea imani siyo Wayahudi lakini Kristo ametuzawadisha Imani na Upendo wa Kimungu. Katika masomo tunayosoma katika sherehe hii ya Epifania - Nabii Isaya, mtume Paulo na Mwinjili Mathayo wanaonyesha jinsi Mungu alivyojidhihirisha kwa watu “watu wa Mataifa.” Biblia haitaji majina ya mamajusi wala nchi walikotoka. Lakini wataalamu wa historia ya maandiko matakatifu wanataja majina yao na nchi walizotoka; Melkiori kutoka Uturuki, Baltazari kutoka Mongolia na Gaspari kutoka Ethiopia; kila mmoja peke yake akitokea katika nchi yake, walikutana njiani wakaamua kwa nia moja kuifuata ile nyota ili kumtafuta Masiha.

Epifania: Watu wa Mataifa kumpoea Mwana wa Mungu
Epifania: Watu wa Mataifa kumpoea Mwana wa Mungu

Hatari, uchovu na urefu wa njia havikuwakatisha tamaa, mpaka wakafike alikokuwa mtoto Yesu. Walipomwona na kumtambua mwana wa Mungu walipiga magoti wakamsujudia, wakafugua zawadi zao, wakampa: dhahabu ikiwa ni ishara ya ufalme wake, ubani alama ya ukuhani na umugu wake, na manemane - mafuta ya kupaka maiti kwa ajili ya maziko, ishara kuwa Yesu atajitoa sadaka, kuteswa na kufa kwa ajili ya dhambi zetu ili tupate kukombolewa. Hata wanawake walibeba manemane wakienda kaburini kumpaka Yesu kama asemavyo mwinjili Marko, “Maria Magdalena, Salome na Maria mama yake Yakobo walinunua manukato ya manemane ili wakaupake mwili wa Yesu” (Mk.16:1). Kumbe tunu au zawadi ambazo mamajusi walimtolea mtoto Yesu zilikuwa ni ishara ya kuanza kutimia kwa utabiri wa manabii wa yeye kumkomboa mwanadamu ndiyo maana katika sala ya kuombea dhabihu katika sherehe hii padre kwa niaba ya jamii ya waamini anasali; “Ee Bwana, tunakuomba utazame kwa wema dhabihu za Kanisa lako. Siyo dhahabu, ubani na manemane vinavyotolewa sasa, ila yule ambaye kwa dhabihu hizi tunamtangaza, tunamtoa sadaka na kumpokea, yaani Yesu Kristo."

Mamajusi waliongozwa na nyota kumwabudu Yesu
Mamajusi waliongozwa na nyota kumwabudu Yesu

Masimulizi yanasema kuwa Sherehe ya Epifania – tokeo la Bwana lilikuwa ni tukio ambalo Wakristo wa Kanisa la mwanzo waliliadhimisha kwa shauku kubwa. Hii ni kwa sababu ni kwa mara ya kwanza Mungu alimfunua mtoto Yesu kwa watu wa Mataifa – wapagani kwa njia ya mamajusi. Hii ilikuwa ni siku ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya masiha aliyekuja kuwakomboa watu wote hata wasio wayahudi. Nasi tuna kila sababu ya kuifurahia sherehe hii, tukimshukuru Mungu kujidhihirisha kwetu, kwa njia ya mwanae Bwana wetu Yesu Kristo nasi tukaamini na kumsadiki kuwa ndiye Bwana na mwokozi wa maisha yetu. Tunashukuru Mungu kwa zawadi ya imani ambayo ni fumbo kubwa kwetu kama mtume Paulo anavyowaambia wakristo wa Efeso katika somo la pili kwamba; kuitwa kwa watu wasio wayahudi kupokea imani ni kitu ambacho hakuna mtu aliyetegemea. Kwa kweli wayahudi waliamini kabisa kwamba ni wao tu wataokolewa na Masiya wakati watu wa mataifa mengine wangeangamia milele. Lakini ikawa kinyume, wengi wa waliomwamini Kristo ni wapagani – watu wa mataifa - wasio wayahudi. Hili ni fumbo kubwa – anasisitiza Paulo - fumbo ambalo hakuna mtu anayeweza kulieleza (Ef 3:4-6). Hivi ndivyo kuitwa kwetu katika imani kwa Kristo kulivyokuwa. Ni kwa neema tu tumeokolewa kwa njia ya imani siyo kwa mastahili yetu bali kwa zawadi ya Mungu (Ef 2:8).

Hata leo kuna watu wana kiu ya kutakana kuonana na Mungu
Hata leo kuna watu wana kiu ya kutakana kuonana na Mungu

Katika somo la kwanza Nabii Isaya (Isa. 60:1-6) anatabiri kushuka kwa mwanga mkuu utakaoiangaza Yerusalemu, nayo mataifa yote yatakayoiendea Yerusalemu yataangazwa kwa nuru yake. Mwanga huu ni Kristo. Nasi tulipomwendea na kumpokea kwa mara ya kwanza, ndani mwetu tulijaa furaha kwa kuwa giza la dhambi lilitokomezwa ndani ya mioyo yetu nasi tukawa kama taa ya mwanga wa furaha kwa wengine. “Ninyi mlikuwa gizani, lakini sasa ninyi ni mwanga katika Bwana” – anasisitiza Mtume Paulo (Ef 5:8). “Muwe kama watoto wa mwanga…katika wema, katika kuishi kwa haki na katika kweli” (Ef 5:9). “Neno la Mungu – liwe kwenu - kama taa ya kuangaza njia gizani, mpaka kutakapopambazuka na nyota ya asubuhi ichomoze mioyoni mwenu” – anatuasa mtume Petro (2Pet 1:19). Injili ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 2:1-12) inatuambia kilichotokea kwa mamajusi walipoondoka kwa Herode na kushika njia kuelekea Betlehemu: “ile nyota ilionekana tena na walipoiona walifurahi” (Mt 2:11). Imani katika Kristo ni chanzo cha furaha katika maisha yetu.  Mamajusi walijaa furaha kubwa tofauti na furaha ya kibinadamu, furaha ya roho iliyojaza mioyo yao.

Walipomwona Mtoto Yesu walijawa na furaha tele.
Walipomwona Mtoto Yesu walijawa na furaha tele.

Hii ndiyo furaha iliyoijaza mioyo yetu tulipobatizwa, tulipompokea Kristo kwa mara ya kwanza katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, na kuimarishwa na Roho Mtakatifu katika Sakramemti ya Kipaimara. Ndiyo furaha inayowajaa wawili wanapofunga ndoa kama Sakramenti, ndiyo furaha inawajaa wale wanaopekea sakramenti ya daraja takatifu na wale wanaojiweka wakfu kwa maisha ya kitawa. Furaha hii inaweza kutoweka pale Roho Mtakatifu anapoondolewa rohoni kwa dhambi, mwanga na furaha vinaondoka pamoja naye. Tunaalikwa kumrudisha katika sakramenti ya kitubio. Imani katika Kristo tuliyoipokea kwa kujifunua kwake kwetu kwa njia ya mamajusi inapaswa kuendelea kukua ndani yetu. Tukumbuke kuwa imani sio vazi la kulivaa na kulivua utakapo. Imani ni kama mbegu, ikishapandwa na kumea inapaswa kutunzwa ili iendelee kukua, la sivyo, inakufa. Kila siku tunapaswa kumpokea Kristo, kutimiza mapenzi yake kwa ukamilifu, kuweka matumaini yetu kwake zaidi na zaidi ili Mungu atupe nguvu kwa njia ya roho wake kwa ajili ya nafsi zetu {imani iliyo ndani yetu} ipate kuwa thabiti ili Kristo aishi ndani ya mioyo yetu kwa njia ya imani – anasisitiza Mtume Paulo (Ef 3:16-17). Tuombe neema na baraka zake Mungu, nasi tuweze kuisikia na kuifuata sauti yake ili ituangaze katika nuru ya kweli kama tunavyosali katika sala baada ya komunio tukisema; Ee Bwana, tunaomba ututangulie daima na popote kwa nuru yako ya mbinguni; na hili fumbo ulilolitaka kutushirikisha, tulitambue waziwazi na kulikubali kwa upendo.

04 January 2023, 15:39