Epifania ni sherehe ya wote wanaomtafuta Mungu. Neno la Mungu katika sherehe hii, linatuongoza kumtafakari Kristo Masiha wa Israeli, Mfalme na Mkombozi wa Ulimwengu. Epifania ni sherehe ya wote wanaomtafuta Mungu. Neno la Mungu katika sherehe hii, linatuongoza kumtafakari Kristo Masiha wa Israeli, Mfalme na Mkombozi wa Ulimwengu.   (Vatican Media)

Sherehe ya Tokeo la Bwana: Yesu Ni Nuru Halisi Inayoonesha Njia na Kufukuza Giza la Ulimwengu

Mamajusi kutoka Mashariki waliojitaabisha kumtafuta Mtoto Yesu na hatimaye walipomwona wakamzawadia: Ubani unaonesha Umungu wa Kristo; Manemane ni ushuhuda wa ubinadamu wa Kristo utakaokabiliwa na mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. Dhahabu ni kielelezo cha Ufalme wa Kristo Yesu, yaani; Ufalme wa kweli na uzima; Utakatifu na neema; haki, upendo na amani! Utu!

Na Padre Philemon Anthony Chacha, SDB, - Vatican.

Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 2013 alisema, Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali waliongozwa na nyota angavu hadi wakafanikiwa kumwona Mtoto Yesu, Nuru halisi amtiaye nuru kila mtu. Rej. Yn 1:9. Kama mahujaji wa imani, Mamajusi wamegeuka wenyewe na kuwa ni nuru inayong'ara angani na hivyo kuwaonesha watu dira na njia. Watakatifu nimwanga wa Mungu unaofukuzia mbali giza la usiku wa ulimwengu huu na kuwaongoza waamini katika Nuru ya kweli, Kristo Yesu, Bwana na Mkombozi. Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican Karibu katika tafakari ya Neno la Mungu ikiwa leo ni Sherehe ya Epifania, yaani sherehe ya Tokeo la Bwana, kuonekana kwa Yesu kama Masiha wa Israeli (rej. KKK 528). Neno Epifania linatokana na neno la Kigiriki epiphàneia yaani kujifunua, kujionesha. Hivyo tunashehereka leo ufunuo wa Mungu kupitia kwa Mwanae aliyejifanya mtu katika Yesu Kristo, ili aweze kumkomboa mwanadamu. Ni sherehe ya wote wanaomtafuta Mungu. Neno la Mungu katika sherehe hii, linatuongoza kumtafakari Kristo Masiha wa Israeli, Mfalme na Mkombozi wa Ulimwengu. Kristo hakuja kwa wana wa Israeli pekee yake, lakini hata kwa wapagani na familia nzima ya wanadamu. Ujio wa Mamajusi, wataalamu wa elimu ya nyota ni mwanzo wa muunganiko wa Mataifa yote, na kukamilika kwa utimilifu katika imani kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambapo watu wote watakuwa wana wa Baba mmoja na watajisikia ndugu kati yao.

Kristo Yesu ni nuru halisi inayofukuzia mbali giza ya Ulimwengu
Kristo Yesu ni nuru halisi inayofukuzia mbali giza ya Ulimwengu

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume: “Admirabile signum” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” anasema, inapokaribia Sherehe ya Tokeo la Bwana, au Epifania, sanamu za Mamajusi watatu kutoka Mashariki zinawekwa kwenye Pango la Noeli. Hawa ni wataalam wa nyota kutoka Mashariki waliojitaabisha kumtafuta Mtoto Yesu na hatimaye walipomwona wakamzawadia: Ubani unaonesha Umungu wa Kristo; Manemane ni ushuhuda wa ubinadamu wa Kristo utakaokabiliwa na mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. Dhahabu ni kielelezo cha Ufalme wa Kristo Yesu, yaani; Ufalme wa kweli na uzima; Utakatifu na neema; haki, upendo na amani. Kila mwamini anahimizwa kuwa kweli ni shuhuda na chombo cha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama chemchemi ya furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Mtoto Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali ni kielelezo cha watu kutoka katika medani mbali mbali za maisha, wenye kiu ya kutaka kukutana na Mfame wa amani, anayetuliza kiu yao ya ndani. Wanapomwona Mfalme katika hali ya Mtoto mchanga, kamwe hawashangazwi wala kuona kama hii ni kashfa ya mwaka, bali wanampigia magoti na kumwabudu kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ambaye ni chemchemi ya hekima yote ndiye aliyewaongoza kwa kutumia nyota angavu hadi kumfikia. Huyu ndiye yule Mungu anayewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi na kuwakweza wanyonge. Bila shaka, Mamajusi waliporejea makwao huko Mashariki ya mbali waliweza kuwashirikisha wengine matendo makuu ambayo Mwenyezi Mungu aliwatendea katika maisha yao.

Mamajusi hawakushangazwa na udogo wa Mtoto Yesu, wakamwabudu
Mamajusi hawakushangazwa na udogo wa Mtoto Yesu, wakamwabudu

Somo la kwanza kutoka kitabu cha Nabii Isaya, 60:1-6 tunakutana na utenzi, unabii ambao ni maono na utabiri wa muunganiko wa watu wote katika ile njia ya kuelekea Yerusalem (rej Jer 12,15-16; 16,19-21). Nabii anaona kundi kubwa la watu wakitembea kuelekea kwenye ule mji mtakatifu: Wote wanakusanyana; wanakujia wewe; Wana wako watakuja kutoka mbali (v. 4), kundi hili liligawanyika katika makundi mawili: moja liliundwa na wana wa Israeli wanaorudi kutoka utumwani, na kundi lingine liliundwa na mataifa yanayotoka mbali na Israeli yakivutiwa na mwanga na utukufu wa Mungu. Isaya anawaalika kusikiliza akisema: Ondoka, ee Yerusalemu, uangaze…Inua macho yako, utazame pande zote. (vv 1.4), kwa mwangaza huu mji wa Yerusalemu unawavuta kwake watu wote ili waweze kuwa kundi moja la waliokombolewa. Ipo haja ya kutoka katika ubinafsi wetu kuingia katika maisha mapya, yanayopatikana katika kuacha giza na kuelekea katika mji unaong’aa na kutoa nuru. Katika somo la pili, Mtume Paolo anagundua kuwa wito wake ambao ameitiwa ni kutangaza Injili kwa mataifa na anaeleza kuwa mpango wa Mungu ni kumkomboa kila mmoja ambae anataka kutembea katika ule mwanga wa Mungu pekee. Kumbe ni mwaliko wa kila mmoja ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili; (v. 6). Alama ya kweli ya maono haya ya ukombozi wa Mataifa yote ni Kanisa. Kanisa lina jukumu la kuunganisha watu wote, kuwapeleka wote katika ile Imani ya Kristo katika kutangaza Injili. Kumbe, katika ulimwengu huu uliogawanyika ni vyema kutangaza kwa furaha na kwa imani; na kupitia kwa Kristo, ambae ni mwanga wa mataifa (Lumen gentium), anayeng’aa juu ya uso wa Kanisa (rej Lumen gentium 1), inakuwa ni rahisi muunganiko wa kweli wa kila kiumbe.

Kristo Yesu ni Nuru Halisi ya Ulimwengu
Kristo Yesu ni Nuru Halisi ya Ulimwengu

Na katika Injili Takatifu kama ilivyoandikwa na Mwinjili Mathayo anatueleza jinsi Mamajusi ambao ni wageni wanakuja kutoka Mashariki, wanatoka mbali kuja kutafuta ule mwanga waliouona unang’ara katika nyota ili waweze kumwabudu mfalme aliyezaliwa. Ndugu msikilizaji wa Radio Vatikani, Swali tunalopaswa kujiuliza leo ni kwanini mamajusi hawa wametembea umbali mrefu kufika Bethlehemu waweze kumsujudia Kristo kwa Imani wakati wale wa karibu hawakufanya hivyo? Jibu tunaloweza kupata ni kwasababu walikuwa na ile hamu ya kukutana na yule Mfalme-Masiha aliyezaliwa na kumwabudu. Hawakuridhika kufahamu tu kuwa amezaliwa. Mara walipogundua ile nyota, wakaifuata na kuuliza watu waliokuwa wanafahamu zaidi yao, na kusema: Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia (v. 2).  Mamajusi waliendelea kushika njia, huku ile nyote waliyoiona ikawatangulia mpaka sehemu alipozaliwa mtoto Yesu. Hamu yao ya kusujudu na kuabudu ilikuwa kubwa sana, hata zawadi walizobeba zilikuwa hazionekani kuwa ni nzito. Kwao kila kitu kilikuwa na maana kama kiliwasaidia kumuona Mungu. Walitembea umbali mrefu kwa ajili ya kukutana na Mkombozi Tujiulize kidogo, Ni umbali gani, ni kilometa ngapi tunatembea, ni muda gani tunautoa kwa ajili ya Kristo, ni bidii gani tunafanya kumtafuta Kristo? Kama mamajusi walivyojitoa kutembea umbali mrefu, ambao hawakuchoka kumtafuta Mtoto aliyezaliwa; nasi pia tunaalikwa leo kujitoa wenyewe katika kumtafuta Kristo, kutia bidii katika kufanya mapenzi ya Mungu katika maisha yetu.

Kristo Yesu ni Nuru na Mwanga wa Mataifa
Kristo Yesu ni Nuru na Mwanga wa Mataifa

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, wengi wetu tunashindwa kwenda Kanisani kushiriki Ibada ya Misa Takatifu kwa kisingizio kuwa kanisa lipo mbali. Tunashindwa kusali katika familia zetu kwa kuwa eti hatuna muda, tumetingwa na mambo mengi. Mbele ya Kristo ambae leo anajionyesha kama mwanga wa mataifa, tunaitwa kufanya maamuzi na kutafakari kama tunataka kuwa wana wa nuru, kama tunataka kuongozwa na mwanga wa kweli au tunapenda kufuata zile nyota zingine ambazo zinatufanya kujifikiria wenyewe na ubinafsi wetu, zinatufanya kuwa na chuki na majivuno. Haitoshi tu kujua wapi Kristo amezaliwa, kama walimu wa sheria na makuhani, bali kwenda kujua wapi alipozaliwa. Hatupaswi kubaki kuangalia tu, tunapaswa kwenda na kuingia katika nyumba ya Yesu nasi tuweze kusema kama mamajusi “nasi tumekuja kumsujudia” (Mt 2,2). Mamajusi walijiachia ili waweze kuongozwa na nyota, na ndipo wakatambua kuwa Kristo ni nani na wapi anaishi. Kumbe ishara ya nyota iliwaongoza katika kuujua Ukweli. Nasi pia katika maisha ya yetu ya Kikristu tunaweza kuongozwa na ishara mbalimbali zinazojitokeza kwa namna mbalimbali. Ishara hizi zinaweza kuwa: ni Neno la Mungu, Mafundisho ya Kanisa, Sakramenti, lakini hata ushuhuda wa wengi wanojikita katika kuifuata Injili. Tufuate ishara hizi ili kuweza kuutambua ule ukweli katika maisha yetu ya Imani. Tumuombe Kristo leo atusaidie kujikita katika kumpenda Yeye, ili azidi kung’ara zaidi ya kitu chochote ndani ya mioyo yetu, na mwanga uwe ni nuru kwa watu wote tunaokutana nao, kwa namna ya pekee kabisa katika familia zetu. Nawatakia Sikukuu njema ya Epifania yaani Tokeo la Bwana.

Epifania 2023

 

06 January 2023, 15:45