Tafuta

Tokeo la Bwana ni Mungu anayejifunua katika mazingira duni na dhaifu! Leo tarehe 6 Januari ni sherehe ya Epifania, ni sherehe ya, Tokeo la Bwana ni Sherehe ya mwanga. Tokeo la Bwana ni Mungu anayejifunua katika mazingira duni na dhaifu! Leo tarehe 6 Januari ni sherehe ya Epifania, ni sherehe ya, Tokeo la Bwana ni Sherehe ya mwanga.   (losw - Fotolia)

Sherehe ya Tokeo la Bwana: Mungu Anajifunua Katika Mazingira Duni na Dhaifu

Tarehe 6 Januari ni sherehe ya Epifania, ni sherehe ya, Tokeo la Bwana ni Sherehe ya mwanga. Ni Yesu anayejifunua na kujidhihirisha kwa watu wa mataifa yote, maana yeye ni Mkombozi wa ulimwengu mzima. Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali, tunaposoma Biblia hatusikii sana juu ya habari zao kuwa walitoka taifa gani na walikuwa watu wa namna gani, walikuwa wangapi!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na salama! Epifania, Tokeo la Bwana ni Mungu anayejifunua katika mazingira duni na dhaifu! Leo tarehe 6 Januari ni sherehe ya Epifania, ni sherehe ya, Tokeo la Bwana ni Sherehe ya mwanga. Ni Yesu anayejifunua na kujidhihirisha kwa watu wa mataifa yote, maana yeye ni Mkombozi wa ulimwengu mzima. Epifania linatokana na neno la lugha ya Kigiriki επιφαινω (epifaino) maana yake ni kitendo cha kujidhihirisha au kujifunua. Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali, tunaposoma Maandiko Matakatifu hatusikii sana juu ya habari zao kuwa walitoka taifa gani na walikuwa watu wa namna gani, walikuwa wangapi, na hata baada ya kumwona mtoto Yesu na kurejea makwao walifanya nini baada ya hapo. Haya yalikuwa ni maswali yaliyosumbua sana pia zile jumuiya za waamini za Kanisa la mwanzo na labda hata sasa tunaposoma sehemu hii ya Injili tunabaki na maswali kadha wa kadha. Ni kutokana na maswali hayo basi mapokeo yanasema walikuwa Wafalme watatu kutokana na zile zawadi tatu, na majina yao ni Gaspari aliyekuwa kijana, Melkiori (mzee kiumri) na Baltasari (mtu wa makamu). Injili haisemi kuwa walikuwa wangapi au walikuwa wafalme ila wanatambulishwa kama wataalamu wa nyota au mamajusi. Hawa wataalamu wa nyota au mamajusi, kwa nyakati zile za kuzaliwa Yesu walikuwa ni watu wenye hekima na uwezo wa kutafsiri njozi ili kujua mambo yajayo na kusoma mapenzi ya Mungu katika matukio ya kawaida na yasiyo ya kawaida katika maisha. Mwinjili Mathayo anatuonesha kuwa hawa mamajusi ni wawakilishi wa watu wa mataifa mengine zaidi ya wana wa Israeli waliopata kumwona Mtoto Yesu.  Mwinjili anaandikia jumuiya ya wanakanisa ambayo tayari imekuwa na waamini hata watu kutoka mataifa mengine nje ya Wayahudi.  Ni lengo la Mwinjili Mathayo kutuonesha kuwa Yesu Kristo tangu mwanzoni amezaliwa kama Mwokozi na Mkombozi wa mataifa yote. Rej. Mt. 2:1-12.

Ni kwa njia ya Kristo Yesu watu wameiona nuru ya ulimwengu
Ni kwa njia ya Kristo Yesu watu wameiona nuru ya ulimwengu

Zaidi sana Mamajusi wanawakilisha wale wote wenye njaa na kiu ya kukutana na Mungu. Ndio wale wote wanaotaka kufanya urafiki wa ndani na wa pekee kabisa na Mungu. Ni wenye njaa na kiu ya kweli na ya haki ya kuingia katika mahusiano ya daima na Mungu. Kama vile mamajusi walivyokutana na vikwazo mbali mbali katika safari yao ya kukutana na Mtoto Yesu, ni mwaliko kwetu kutambua kuwa safari yetu ya hija hapa duniani ya kuchuchumilia utakatifu kwa kuingia katika mahusiano na Mungu hakika tutakutana na vikwazo na hata magumu mengi kama waliyokutana nayo wale wataalamu wa anga na nyota. Nyota anayozungumzia Mwinjili Mathayo ni zaidi ya ile ya angani, anatualika kuitafuta pia katika Maandiko Matakatifu, maana hadhira yake ilikuwa inaelewa vema Agano la Kale na kuhusiana na unabii wa nyota itakayowaangazia kutoka gizani.  Na ndio maana Herode pia aliwaalika wakuu wa makuhani na waandishi ili wamweleze Maandiko Matakatifu yanasemaje. (Kitabu cha Hesabu 22-24), Balaamu anatabiri juu ya nyota itakayochipuka kutoka uzao wa Yakobo, anaagua miaka 1200 kabla ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo. (Hesabu 24:17,19) Nyota hii ni Yesu Kristo anayeangaza kila mwanadamu. Hivyo simulizi hili la mamajusi ni mfano anaotumia mwinjili Matayo kwa Kanisa lile la Karne ya kwanza ambapo watu wa mataifa mengine nao walimwongokea Kristo na kupokea imani na kuwa wafuasi wake Yesu Kristo.

Mwenyezi Mungu amejifunua katika hali ya uduni na unyonge
Mwenyezi Mungu amejifunua katika hali ya uduni na unyonge

Ni kupitia Taifa la Israeli, watu wa Mataifa nao wameweza kuifikia hii Nyota iliyotabiliwa na manabii miaka mingi kabla ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo. Mwinjili Mathayo anawaandikia wale Wakristo wa kwanza waliojua vema kabisa Maandiko Matakatifu hasa Agano la Kale, hivyo adhira yake ilimwelewa vema kabisa kuwa nyota anayoiongelea ni Masiha au Kristo anayekuja kutuangazia kutoka katika maisha ya giza. Kila mara tunaposoma Injili ya Matayo hatuna budi kukumbuka alitumia mtindo ule wa Haggadah Midrashi, ndio ule wa kufanya rejea katika Maandiko Matakatifu ndio Agano la Kale. Na ndio mwaliko daima kila tunaposoma Maandiko Matakatifu hatuna budi kutambua kuwa ni Yesu Kristo anapaswa kubaki kuwa muhusika wetu mkuu ili tuweze kupata ujumbe kusudiwa kwani ni kwa njia yake sisi tunakutana na sura halisi ya Mungu! Mamajusi ni wawakilishi wa watu wa mataifa mengine, waliokuwa wapagani ila nao nyota ile imewaangaza na kuwaalika kufika kumsujudia huyu mtoto aliyezaliwa. Na ndio wanamtambua huyu mtoto kama Mfalme na Mungu kweli na ndio wanamsujudia na kumtolea zawadi za dhahabu, ubani na manemane. Mamajusi wanasafiri kutoka katika nchi zao na wananyanyua macho yao juu wakiongozwa na nyota ile ya haki, wakati Herode na waandishi na wakuu wa makuhani wanabaki katika hali zao za awali, maana hawapo tayari kuongozwa na Mungu mwenyewe katika maisha yao. Mamajusi kwa bahati mbaya wanafika Yerusalemu na kwenda kwenye jumba la mfalme Herode ili huko waweze kukutana na Mungu.

Mamajusi wanawawakilisha wote wenye kiu ya kuonana na Mungu
Mamajusi wanawawakilisha wote wenye kiu ya kuonana na Mungu

Ni kukosea mahali sahihi kwani huko katika jumba la kifahari la kifalme hawakutani na Mungu. Na ndio mara nyingi hata nasi tunabaki na sura ya Mungu isiyokuwa sahihi sana ya kutumaini kukutana na Mungu mwenye nguvu na kuogofya ya dunia hii, mwenye mamlaka na majeshi ya kuamrisha maaskari na watumishi wake. Kinyume chake wanakutana na Mungu katika mazingira duni na dhaifu kabisa kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu, ndio kule horini wanakutana na Mungu katika nafsi ya huyu mtoto mchanga akiwa amevikwa mavazi ya kitoto na akiwa mikononi mwa binti yule mdogo Mariamu. Mfalme Herode alibaki akisumbuliwa na habari hizo. Neno la Kigiriki linalotumika ni ταρασειν (tarasein) likimaanisha ile hali ya kuchafuka kwa bahari, ndio hali ya chuki kali na mbaya aliyojaa nayo Herode, na kinyume chake ni mamajusi waliojawa furaha na shauku kubwa walipomwona Mtoto Yesu akiwa na Mama yake Maria pale Bethlehemu. Mamajusi ni kinyume na Herode, Mamajusi wanakubali kuongozwa na mantiki siyo tena ya duniani bali ile ya Mungu mwenyewe, wakati Herodi alibaki kuongozwa na mantiki ya dunia hii, mantiki ya kutawala na kuwa mkubwa hata kwa gharama ya maisha ya wengine. Hali ya Herodi ndio ya wivu mkali ambayo tunaweza hata kuwa nayo sisi pale tunaposikia mema au mazuri au mafanikio ya wengine, ni hali inayokuwa kinyume na imani yetu kama Wakristo.

Walimkuta Mtoto Yesu kwenye Pango lakulia wanyama
Walimkuta Mtoto Yesu kwenye Pango lakulia wanyama

Ni hali ya kubaki katika upagani, hali ya kutokufurahi kuona mafanikio ya wengine, hali ya kuchafua majina ya wengine na hata kutamani kuwaangamiza na kuwaondoa katika sura ya dunia hii. Ni vema tukajiuliza ni mara ngapi ndani mwangu nimejawa na wivu na hivyo kuwa kama Herode? Ni swali la kutafakari kila mmoja wetu katika Dominika hii ya Epifania, Sherehe ya Ufunuo wa Bwana. Somo la kwanza: Isa 60:1-6 linatueleza kuwa mwanga ule ulioiangaza Yerusalemu, uliwaongoza watu wote kwenda katika mji ule mtakatifu na zawadi zao. Na ndio unabii huu unakamilika katika somo la Injili ya leo ambapo mamajusi ndio watu wa mataifa wanaokuja na zawadi zao kwa Mtoto Yesu aliye nyota ile ya haki. Wakiongozwa na mwanga au nyota ile ya Masiha, Mamajusi wanakuja Yerusalemu na dhahabu, ubani na manemane. Zawadi hizi baadaye zinaelezwa kuwa na maana pia ya kitaalimungu kadiri ya mapokeo ya waamini wa Kanisa la mwanzo; Dhahabu ikimtambua kuwa Yesu ni Mfalme, ubani ukionesha Umungu wake na Ukuhani wake wa milele na manemane ikionesha Ubinadamu wake na hasa fumbo lile la kifo chake. (Mk15:23; Yoh 19:39) Ni Taifa la Israeli pia lilijulikana kama Taifa lenye Mungu kama Mfalme wao, Taifa la kikuhani na pia mchumba mwaminifu wa Mungu. Ni dhahabu inayoashiria Ufalme wa Israeli, ubani kuwa ni Taifa la Mungu na manukato ya manemane yenye harufu nzuri kama harufi nzuri ya bibi harusi au mchumba mwaminifu wa Mungu.

Hata watu wa Mataifa wameuona wokovu wa Mungu wetu
Hata watu wa Mataifa wameuona wokovu wa Mungu wetu

Watu wa mataifa wanamsujudia mtoto Yesu na hivyo kumtambua kama Mungu wao na Mfalme wao. Mamajusi wanabaki kuwa ni ishara ya Kanisa zima kama jumuiya ya waamini kutoka watu wa rangi zote, kabila zote, lugha zote na mataifa yote. Kuwa mwanakanisa haimaanishi kukataa utambulisho wetu wenye kuonesha tofauti zetu mbali mbali, bali ni utajiri wa Kanisa kwani ni moja, takatifu, katoliki na la mitume na lenye watu kutoka mataifa yote bila kubagua. Kila mwanakanisa anaalikwa kubaki na utambulisho wake uwe wa lugha au utamaduni na hivyo kila mmoja wetu kuwa mchango na msaada katika kulijenga Kanisa la Kristo, kila mmoja wetu akialikwa kuwa jiwe hai la kuujenga mwili fumbo wa Kristo, yaani Kanisa lake. Mamajusi ni kielelezo na mfano wa maisha ya kila mwanakanisa, ndio maisha ya kutoka na kuanza safari ya kuifuata nyota ile ya ukweli, ndio Kristo Mwenyewe. Ni kama mwaliko wa Kristo mwenyewe kwetu, kama alivyowaalika wanafunzi wake pembeni mwa ziwa la Galilaya, njoo unifuate. (Mt. 4:18-22). Ni mwaliko wa kuachana na yote yanayokuwa kinyume iwe ni vitu au tabia zetu zisizoakisi ufuasi wetu. Kinyume chake ni kuwa sawa na makuhani wa Yerusalemu waliodhani kuwa wao wana ukweli wote na hivyo kukosa kujishusha na kutoka na kwenda Betlehemu kumsujudia mtoto Yesu, aliye Kristo wa Bwana.

Twendeni kukamwabudu na kumsujudu Kristo Yesu
Twendeni kukamwabudu na kumsujudu Kristo Yesu

Somo la kwanza kutoka Kitabu cha Nabii Isaya 60:1-6 ni mwaliko wa kuvaa nuru, maana utukufu wa Bwana utakuwa juu ya watu wale waliokata tamaa na kuwa katika giza la utumwa kwa miaka mingi kwani saa yao ya wokovu sasa imefika.  Na ndio siri anayozungumzia Paulo Mtume katika waraka wake kwa Waefeso na siri hiyo ndio ukombozi wa watu wote. Katika Kristo na kwa njia ya damu yake, Mwenyezi Mungu anatufanya watu wa mataifa yote, kuwa warithi pamoja na Mwanae wa pekee. Ndugu zangu, Mamajusi mara baada ya kumuona mtoto Yesu walirejea nyumbani kwako kwa njia nyingine. Ni mwaliko kwetu nasi pia mara baada ya kukutana na Yesu Kristo hatuna budi kubadili njia na kuanza njia mpya nayo ndio ile ya Yesu Kristo mwenyewe, njia ya uzima na ukombozi. Epifania ni mwaliko wa kuanza kuishi maisha ya mwanga, maana nuru yake mtoto Yesu imetufikia na hivyo hatuna budi kutembea katika nuru na mwanga wa kimungu. Ni mwaliko wa kuyabadili maisha yetu na kutembea katika mwanga. Ni kuacha yale yote ambayo yanatuweka mbali na Mungu na wengine, ndio kuacha maisha ya dhambi. Kinyume chake ni Herode anayesema anataka kumwabudu mtoto Yesu ila akiwa na nia ovu ndani mwake. Wapendwa tumwombe Mungu atukinge na roho ile ya wivu na kisasi katika maisha yetu ili daima tuwe wajumbe wa Upendo wa Kimungu kwa watu wote. Ninawatakia nyote Dominika takatifu ya Epifania au Tokeo la Bwana na mwaka mpya 2023 wenye kila neema na baraka zake Mwenyezi Mungu na hasa tuzidi kujaliwa neema ya kuwa na njaa na kiu ya kumtafuta Mungu katika maisha ya siku kwa siku. Hakika ni Mungu anayetutafuta sisi kwanza lakini nasi hatuna budi kujaliwa kiu na njaa ya kukutana naye hata katika madogo ya maisha yetu.

06 January 2023, 14:57