Dominika ya Ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristo. Popote alipo Kristo, hapo kuna Yordani! (Mt. Ambrosi). Dominika ya Ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristo. Popote alipo Kristo, hapo kuna Yordani! (Mt. Ambrosi).  

Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana: Msingi wa Maisha ya Kikristo, Lango la Uzima Katika Roho

Ni katika Ubatizo wetu sisi nasi tumefanyika kuwa wana na warithi pamoja na Mwana pekee wa Mungu, ni upendo wa ajabu tuliojaliwa na Muumba wetu hivyo hatuna budi nasi kuilinda na kuitunza heshima hiyo kubwa. Sisi ni watoto Mungu kwa Ubatizo wetu! Ubatizo ni msingi wa maisha ya Kikristo na lango la kuingilia uzima katika roho, lango la Sakramenti za Kanisa

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Dominika ya Ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristo. Popote alipo Kristo, hapo kuna Yordani! (Mt. Ambrosi). Ni katika Ubatizo wetu katika Roho Mtakatifu sisi nasi tumefanyika kuwa wana na warithi pamoja na Mwana pekee wa Mungu, ni upendo wa ajabu tuliojaliwa na Muumba wetu hivyo hatuna budi nasi kuilinda na kuitunza heshima hiyo kubwa. Sisi ni wana wa Mungu kwa Ubatizo wetu! Ni kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo tunajaliwa kushiriki maisha ya Kimungu, maisha ya neema na utakatifu. Hivyo hatuna budi kuienzi zawadi hiyo kubwa kwa ushuhuda wa maisha yetu ya siku kwa siku. Katika Maandiko Matakatifu sehemu za kijiografia daima zinabeba ujumbe wa kitaalimungu; mathalani bahari, mlima, jangwa, Galilaya, Samaria, Mto Yordani na kadhalika na kadhalika. Mwinjili Luka hataji mahali alipobatizwa Yesu, ila Mwinjili Yohane anatuonesha kuwa ni Yohane Mbatizaji alikuwa akibatiza ng’ambo ya Mto Yordani. (Yohane 1:28). Mapokeo yanatuambia kuwa Yesu alibatizwa na Yohane Mbatizaji katika ng’ambo ya Mto Yordani na sehemu iliyojulikana kama Betabàra, na ndio sehemu ambapo Yoshua aliwaongoza wana wa Israeli wakati wanaingia katika nchi ile ya ahadi. Hivyo hapa pia leo tunaona ujumbe wa kwanza Mto Yordani ndio kusema ni njia ya kivuko, inayoashiria kutoka maisha ya utumwani na kuingia katika nachi huru. Ni safari kama ile waliyoifanya wana wa Israeli nasi kwa ubatizo wetu tunaifanya kwa kuachana na maisha ya utumwa wa dhambi na kuanza maisha mapya, ndio maisha ya kuwa wana wa Mungu, warithi pamoja na Mwana pekee wa Mungu, yaani Yesu Kristo.

Ubatizo: Kufa na Kufufuka na Kristo Yesu
Ubatizo: Kufa na Kufufuka na Kristo Yesu

Betabàra mahali alipobatizwa Yesu tunaambiwa na watalaamu wa Jiografia kuwa ndio sehemu ya chini zaidi kutoka usawa wa bahari kwa mita 400.  Hivyo Yesu anaanza utume wake hadharani kutokea pale, na hapa pia kuna ujumbe wa kitaalimungu. Yesu kutoka juu mbinguni anashuka mpaka sehemu ya chini kabisa ya dunia ni kutaka kutuonyesha kuwa amekuja kwa ajili ya wokovu wa kila mwanadamu, wa kila mmoja wetu aweze kunyanyuliwa na kupata wokovu (Kenosis). Mungu hawezi kumsahau hata mmoja wetu hata yule anayekuwa mbali naye kiasi gani, hivyo amekuja na daima anamtafuta kila mwanadamu ili apate wokovu. Fumbo la Umwilisho wa Mungu kuja na kukaa kati yetu ili nasi tuweze kushiriki Umungu wake, na ndio utakatifu wake. Nyakati zile za Yesu, Ubatizo ulitumika kama ishara ya nje ya kuonesha mtu anayeanza maisha mapya. Hivyo kama neno Ubatizo linavyomaanisha kuzamishwa. Kwa kuzama inaashiria kifo, na kuibuka tena ni kuzaliwa upya, hivyo katika madhehebu ya Ubatizo mmoja alizamishwa kudhihirisha kifo na ndio kuachana na yale yote ya zamani na kwa kuibuka ndio kusema kuzaliwa upya, kuwa kiumbe kipya kwa maji na Roho Mtakatifu.

Sakramenti ya Ubatizo: Kuzaliwa Upya katika Neno na Roho Mtakatifu
Sakramenti ya Ubatizo: Kuzaliwa Upya katika Neno na Roho Mtakatifu

Yohane Mbatizaji pia aliwaalika watu wabatizwe, akiwa na lengo moja kubwa la kuwaalika wafuasi wake kufanya toba na wongofu wa ndani kama maandalizi ya kumpokea Masiha.  Hivyo waliobatizwa walitambua kwanza hali yao ya dhambi na hivyo kuhitaji kuanza maisha mapya. Na ndio maana mafarisayo na masadukayo hawakwenda kubatizwa kwani wao walijiona kuwa ni watu wema na wenye haki, wasio na dhambi, hivyo hawahitaji Ubatizo ule aliohubiri Yohane Mbatizaji. (Luka 7:30). Kama hiyo ndio maana kusudiwa ya Ubatizo ule wa Yohane, swali ni je kwa nini Yesu alibatizwa hali hakuwa na dhambi?  Swali hili si tu linatusumbua sisi leo na labda hata wanataalimungu wa leo bali liliwasumbua hasa waamini wale wa jumuiya za kwanza za Wakristo. Na ndio Mwinjili Mathayo anajaribu kutuonesha sababu za kwa nini Ubatizo kwa Yesu. Mwinjili anatuonesha majibizano baina ya Yohane Mbatizaji na Yesu pale Mto  Yordani.  Yohane Mbatizaji naye alitatizwa na hilo na ndio maana alimkatalia Yesu, kwani alijua kuwa hana dhambi na hivyo hahitaji Ubatizo ule wa toba. Yesu anasisitiza ili litimie neno la kukamilisha kila haki.  Yohane Mbatizaji anatambua mara moja kuwa hana budi kukubali mapenzi na mipango ya Mungu hata kama anakosa sababu ya moja kwa moja kwa muono na mtazamo wake wa kibinadamu. Na ndio tunaona pia hata Mtume Petro alipomwona Yesu anataka kumuosha miguu naye alikataa mwanzoni, ni mara baada ya kutambua kuwa hana budi kutii na kukubali mapenzi na mipango ya Mungu katika maisha yake.

Ubatizo ni mlango wa wokovu
Ubatizo ni mlango wa wokovu

Nasi mara kadhaa tukibaki na mantiki zetu za kibinadamu tunajikutana tunashindwa kutii na kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu. Haki ya Mungu ni ile inayotaka na kualika wokovu wa watu wote, hata mmoja asipotee. (1Timoteo 2:4) Mwandishi wa (Waraka kwa Waebrania 2:11), anatuonesha kuwa Yesu hakuona aibu kutuita sisi ndugu zake, sisi tulio wadhambi na wakosefu. Ni mwaliko hata kwetu leo kutambua upendo na wema wa Mungu kwa kila mwanadamu bila kujali ni mdhambi au ni mkosefu kiasi gani, ni mapenzi ya Mungu kuwa kila mmoja awe mwana na mrithi pamoja na Kristo, ndio wokovu na uzima wa milele. Ni kutuonesha tangu awali kuwa anabeba madhambi na makosa yetu na hivyo kutufia pale juu msalabani na siku ya tatu kufufuka. Ubatizo wake pale Yordani unaonesha fumbo lile la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wake. Hivyo Ubatizo wake ni kiashiria cha Fumbo la Pasaka: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, kiini cha wokovu wetu. Baada ya huo utangulizi hapo tunaona hata Mwinjili Mathayo kama Wainjili Luka na Marko anaelezea tukio la Ubatizo wa Yesu kwa kutumia ishara kuu tatu, kufunguka kwa mbingu. Njiwa na Sauti kutoka juu. Kwa kweli Wainjili hapa wanatumia ishara hizi ambazo ilikuwa ni rahisi kueleweka kwa Jumuiya zile za waamini lakini pia hata nasi kwetu leo. Kufunguka kwa Mbingu. Kwa kweli Mwinjili hapa hataki kuonesha kitendo cha muujiza cha mbingu kufunguka kama tunavyoweza kufikiri hapana. Mwinjili Mathayo hapa kwa kusema mbingu zilifunguka anarejea Unabii wa Nabii (Isaya 64.7-8 na 63:19). 

Ubatizo wa Bwana: Mshikamano wa Kristo Yesu na Wadhambi
Ubatizo wa Bwana: Mshikamano wa Kristo Yesu na Wadhambi

Kabla ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo, wana wa Israeli waliamini kuwa Mungu amefunga mbingu, kwa maana ya kutokutuma tena manabii na wajumbe wake kwa kuwa walikosa kuwa waaminifu kwa Agano na pia kwa kutenda dhambi.  Hivyo waliendelea kujiuliza ni mpaka lini Mungu atabaki kuwa mbali nao? Mbingu kufunguka ni ishara ya kupokea mjumbe na ujumbe wa Mungu kwa watu wake. Mwinjili Mathayo anaonesha leo kuwa ni kwa kuanza kazi kwake hadharani Yesu Kristo, Mungu anafungua tena mbingu, Mungu anashuka na kukaa na watu wake. Ni Habari Njema, ni Injili kwetu sote. Mungu sasa amesikia kilio chao na hivyo kufungua tena mbingu, kutuma tena na sasa anamtuma Mwana wake wa Pekee ili kunena na kutufunulia mapenzi na zaidi zaidi sana sura halisi ya Mungu kwetu. Ishara ya pili ndio ya Njiwa.  Yesu anaona Roho wa Mungu akishuka kama njiwa, kwa kweli hata hapa pia Mwinjili Matayo hataki kutuonesha kuwa katika tukio la Ubatizo wa Yesu alishuka kweli njiwa kwa maana ya kiumbe ndege, hapana. Yohane Mbatizaji anatambua kuwa kutoka mbinguni haishuki au kudondoka tu mana bali hata maji ya kuangamiza kama wakati wa gharika kuu. (Mwanzo 7:12) Moto pia ulishuka na ulioangamiza watu kule Sodoma na Gomora (Mwanzo 19:24). Labda na hapa pia alikuwa anatarajia Roho wa Mungu ashuke katika umbo la moto au maji ili kuangamiza na kutetekeza wale wote walio wadhambi na wasiokuwa tayari kufanya toba na kumpokea Masiha.

Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, mwanzo wa maisha mapya
Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, mwanzo wa maisha mapya

Tunakumbuka hata wale wanafunzi wa Yesu baada ya kuona watu walikataa kumpokea Yesu katika miji na vijiji vyao, walimshauri Yesu aamuru moto ushuke kutoka juu na kuwaangamiza watu wale. Badala yake Roho wa Mungu anashuka katika umbo la njiwa, ndio kusema katika umbo la wema na upole.  Ni kuonesha kuwa Mungu hashuki kuja kuangamiza na kulaani na kuharibu bali kuokoa. Njiwa pia ilikuwa ni ishara ya kujishikimanisha na kiota chake.  Hivyo Mwinjili Mathayo anatuonesha kuwa Roho wa Mungu daima anajishikamanisha na Yesu Kristo kama njiwa anavyojishikamanisha na kiota chake. Yesu ni Hekalu la Roho wa Mungu, ni makazi ya kudumu ya Roho wa Mungu, Roho wa Upendo, Msamaha na Huruma. Ishara ya tatu ndio sauti kutoka juu. Sauti ilikuwa ni ishara inayotumiwa na marabi kutaka kuonesha Mungu anayenena na kuwasiliana na watu wake.  Na hapa nia kuu ni kutaka kumtambulisha Yesu, ni Mungu mwenyewe anamtambulisha Yesu kwetu. Napenda kukumbusha kuwa Injili iliandikwa baada ya mateso, kifo na ufufuko wake Bwana wetu Yesu. Wanafunzi na wafuasi walibaki na maswali mengi na hasa juu ya kifo chake cha aibu na mateso makali. Katika macho ya kibinadamu, Yesu alionekana kushindwa kwa kifo chake, aliyeacha na kutelekezwa na Baba yake.

Wazazi na walezi wazingatie malezi bora kwa watoto wao.
Wazazi na walezi wazingatie malezi bora kwa watoto wao.

Ni katika muktadha huo tunaona leo Mwinjili Mathayo anatoa jibu la maana ya kifo na mateso yake Bwana wetu Yesu Kristo kwa nukuu tatu kutoka Agano la Kale. Ndio mtindo ule wa Hagaddah Midrashi, kufanya rejea katika Agano la Kale. “Huyu ni mwanangu. (Zaburi 2:7) Katika mila za Kiyahudi neno mwana alimaanishi tu mzaliwa wa kibailojia, bali zaidi sana ni kutaka kusema mfanano. Hivyo kwa kutambulishwa kuwa ni Mwana wa Mungu, ni sawa na kusema Mungu. Ni sura halisi ya Mungu tunakutana nayo katika huyu Mwana. Mpendwa; Itakumbukwa kuwa Abrahamu alialikwa na Mungu kumtolea sadaka Isaka mwanaye mpendwa. (Mwanzo 22:2, 12, 16) Hivyo Yesu anatofautishwa na manabii na wajumbe wengine wa Mungu kwani Yeye ni Mwana Mpendwa kama Isaka kwa Abrahamu. Niliyependezwa naye. Nukuu hii tumeiona pia katika somo letu la kwanza la leo. (Isaya 42:1) Mungu anamtambulisha Yesu kuwa ni mtumishi wake, anayekuja ulimwengu ili kila mmoja wetu aweze kuhesabiwa haki. Ndio kusema utambulisho huu unatupa majawabu ya maswali juu ya Masiha kwani tofauti na mantiki na matarajio ya kibinadamu.

Tunzeni neema ya utakaso katika maisha yenu ya kila siku
Tunzeni neema ya utakaso katika maisha yenu ya kila siku

Ni kama Petro akiwa katika nyumba ya kuhani mkuu alimkana Yesu kwa kusema simjui mtu huyu, ndio kusema alikuwa anasema ukweli, kwani alikuwa bado hajaelewa mantiki ya Kimungu ndani ya Masiha wake. Kwake Masiha hakupaswa kuonekana mnyonge na mtumishi bali alikuwa amebaki na mantiki ile ya kibinadamu, labda hata nasi leo hatuna budi kutambua kama kweli tunataka kuwa wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo hatuna budi kuachana na kubweteka kwa kuongozwa na mntiki zetu za kibinadamu. Naomba nimalizie tafakuri yetu na maneno ya Mtakatifu Ambrosi wa Milano: “Ubique nunc Christus, ubique Iordan est” Kwa Kiswahili “Popote alipo Kristo sasa, hapo kuna Yordani” (Tafsiri yangu) Ndio kusema Yordani kwa maana ya Ubatizo wetu ni mto wa uzima wa milele, ni mto wa ukombozi wetu. Ni kwa Njia ya Ubatizo nasi tumefanyika wana wa Mungu na warithi pamoja na Mwana Pekee wa Mungu, Yesu Kristo. Ni katika sakramenti ya Ubatizo nasi tunashiriki fumbo lile la Pasaka, la mateso, kifo na ufufuko. Kisima cha Ubatizo ni chemu chemu ya uzima wa KIMUNGU, ni humo tunajaliwa neema ya kufanyika kuwa wana wa Mungu. Nawatakia tafakari njema na Dominika takatifu ya Ubatizo wa Bwana!

07 January 2023, 11:44