Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya nne ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Ufafanuzi wa kina wa Heri za Mlimani. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya nne ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Ufafanuzi wa kina wa Heri za Mlimani. 

Tafakari Dominika ya Nne ya Mwaka A: Heri za Mlimani: Ufafanuzi wa Kina

Ili tupate furaha na heri ya kweli hatuna budi kupanda mlimani na kulisikiliza Neno la Yesu Kristo, ndio hotuba ile ya Heri nane za mlimani. Ndio mwaliko wa kuachana na mantiki zile za kidunia na kuivaa ile ya Mungu mwenyewe, tukikubali kwa msaada wa Roho Mtakatifu kuongozwa na Neno la Mungu, ili kuweza kupata furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika maongozi ya Mungu.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Heri na Furaha ya kweli ni katika kukubali kuongozwa na mantiki ya mbinguni, yaani ya Mungu mwenyewe! Mwanadamu daima anatafuta furaha ya kweli, ndio maisha ya heri, maisha ya amani ya ndani kabisa kwanza na Muumba wake, na nafsi yake na wote wanaomzunguka. Furaha ya kweli sio burudani au mihemuko ya vionjo vya kihisia kwani hivyo ni vya muda mfupi na vya kupita, na hudanganya. Furaha ya kweli ni ya ndani na inadumu, haitegemei nyakati wala hali za muda za kupita, ndio kusema heri na furaha ya kweli ni kuonja mbingu tungali bado hapo duniani! Furaha na heri ya kweli haipatakani kwa kuongozwa na mantiki ya hapa duniani bali kwa kukubali kuongozwa na mantiki ya mbinguni, yaani ya Mungu mwenyewe. Ndani ya mwanadamu kuna kiu na njaa kubwa ya kukutana na Mungu, ya kufanya mahojiano naye lakini zaidi sana ya kupata kitulizo cha nafsi kwani ndani mwetu tuna maswali mengi na hata shida nyingi zinazotusonga na kutuandama. Ni wapi tunaweza kukutana na Mungu na kuongea naye kwa njia ya majadiliano? Kwa Wayahudi sehemu ya kukutana na Mungu waliamini ni juu mlimani na ndio mang’amuzi waliyofanya Abrahamu, Musa na Eliya.  Ni juu mlimani huko Wayahudi waliamini katika kukutana na Mungu. Mwinjili Mathayo anatuonesha kuwa hotuba ya kwanza ya Yesu kwa wafuasi wake inafanyika juu mlimani. Hata hivyo Mwinjili Matayo anataka kutupa mafundisho yenye Katekesi ya Kitaalimungu, kwani sio lengo lake kuishia kutuonesha juu ya mlima kama mahali pa kijiografia. Ni mwaliko kwetu kusaka nafasi ya kukutana na Mungu hasa katika Neno lake linalopatikana katika Maandiko Matakatifu.

Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu
Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu

Dominika iliyopita ya Neno la Mungu ilitualika kutambua kuwa ni katika Neno lake humo tunakutana na Mungu, humo tunapata nafasi ya kujadiliana naye na zaidi sana kujifunza mapenzi yake katika maisha yetu kwani kwa njia ya Maandiko Matakatifu, Mungu Mwenyezi anajifunua kwetu. “Yesu…alipanda mlimani”; Ndio kusema Yesu anatoka na pia anawaalika wafuasi wake kutoka katika sehemu ya tambarare, kutoka katika mantiki ya ulimwengu huu na kuanza kuongozwa na ile ya Mungu mwenyewe. Ni kupanda mlimani ili tuongozwe na Mungu mwenyewe kwa msaada wa Neno lake na kuachana na namna za kufikiri na kutenda kadiri ya mantiki ya chini, ndio ile ya ulimwengu na kidunia. Na ndio tunaona mafundisho ya Yesu katika somo la Injili ya Dominika ya Nne ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa Mt 5:1-12 inatutaka kuvaa kichwa kipya, kupata wokovu wa fikra, wa kubadili vichwa na kuvaa kile kinachoongozwa na mantiki ya mbinguni. Ili tupate furaha na heri ya kweli hatuna budi kupanda mlimani na kulisikiliza Neno la Yesu Kristo, ndio hotuba ile ya Heri nane za mlimani. Ndio mwaliko wa kuachana na mantiki zile za kidunia na kuivaa ile ya Mungu mwenyewe, tukikubali kwa msaada wa Mungu Roho Mtakatifu kuongozwa na Neno la Mungu. Kuna heri gani katika kuwa maskini wa roho, au mwenye huzuni, au mpole, au mwenye njaa na kiu ya haki, au mwenye huruma, au mwenye moyo safi, au mpatanishi, au mwenye kuudhiwa kwa ajili ya haki? Hakika kwa mantiki ya dunia hii hakuna heri katika yote ambayo Yesu leo anatufundisha na kutuhubiria, vinginevyo lazima kuangalia maisha kwa jicho lingine, ndilo lile la kuongozwa na mantiki ya mbinguni.

Heri Maskini wa Roho Maana Ufalme wa Mbinguni ni wao
Heri Maskini wa Roho Maana Ufalme wa Mbinguni ni wao

“Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.” Umaskini anaouzungumzia Yesu sio ule wa kuwa hohehahe au ufukara wa kukosa mali na vitu kama ambavyo wengi tunashawishika kuitafsiri hivyo. Jumuiya zile za mwanzo kabisa za Wakristo hazikuishi katika umaskini wa mali na vitu bali kati yao hakuna hata mmoja aliyetindikiwa na kitu, ndio kusema waliishi kwa upendo kiasi kwamba hakuna aliyebaki katika hali duni ya kukosa hata mahitaji yake ya msingi. (Matendo 4:34). Yesu anaongeza kwa kusema heri maskini wa roho, ndio kusema hasifu umaskini kama umaskini bali ni ile hali ya kutokujishikamanisha na mali, na badala yake kutumia yote tunayojaliwa kwa upendo na hasa kwa kuwajali na kuwasaidia wengine wanaokuwa na uhitaji.  Maskini wa roho ndio wale wanaotambua kuwa yale yote walio nayo sio kwa ajili yao peke yao, bali wao wamewekwa kuwa walinzi na waangalizi na hivyo hawana budi kutumia yote kwa upendo. Ndio wale wasioweka hazina yao katika mali na vitu. Maskini wa roho sio yule asiye na kitu bali ni yule anayempa Mungu nafasi ya kwanza na kutumia mali zake kwa upendo kwa Mungu na jirani. Maskini wa mali anaweza kukosa umaskini wa roho, ikiwa atajichukia mwenyewe hata kujilaani, na mbaya zaidi kuwachukia wengine wanaomzidi mali au uwezo, na hata kutamani mali za wengine na kutaka kujitajirisha kwa njia ovu. Hivyo kilicho cha muhimu ni wokovu wa fikra, wa kuwa na moyo wa kumtegemea Mungu daima iwe tuna mali au la, tunaodumu wenye upendo kwa Mungu na kwa jirani. Tunaalikwa kufanana na Mungu mwenyewe ambaye pamoja na kumiliki vyote vya ulimwengu mzima bado anabaki maskini kwani ametukabidhi vyote tuvitumie kwa sifa na utukufu wake. Ni upendo usio na masharti wala kujibakisha ambao tunaalikwa kuuishi na hapo kweli tunakuwa maskini wa roho, na tutapata heri au furaha ya kweli sio kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu bali ya Mungu mwenyewe.

Heri wenye huzuni maana hao watafarikika
Heri wenye huzuni maana hao watafarikika

“Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika.” Huzuni na mateso sio jambo jema au chanya. Hata Mungu hafurahii kutuona tukiwa wenye huzuni au tunapopitia mateso na magumu ya maisha, pamoja na kwamba anaruhusu nyakati hizo ngumu, ili kwazo tuweze kupata neema zisizoonekana kwa macho ya nyama kwa wakati huo. Kwa wasikilizaji wa Yesu wa nyakati zile walielewa mara moja pale aliposema heri wenye huzuni kwani anafanya rejea Kitabu cha Nabii Isaya. (Haggadah Midrashi) Wenye huzuni ndio wale wasio na makazi ya kuishi, wasio na mashamba ya kulima kwani urithi wa baba zao ulichukuliwa na wageni na wao kugeuzwa kuwa watumwa, na kupatwa na mateso ya kila namna. (Isaya 61:7) Kwa hawa wenye huzuni ambao walikuwa na mioyo iliyopondeka, na walivaa magunia kama vazi la maombolezo na kujipaka majivu, kwao Nabii Isaya anawaletea ujumbe wa matumaini na faraja ya kweli. Ni Mungu anakuja kugeuza yote kwa kuwatoa katika hali hizo za huzuni na mateso. (Isaya 61:3) Na ndio ujio wa Yesu ulimwenguni unakuja ili kutupa faraja na matumaini ya kweli. Yesu akiwa kwenye Sinagogi la Nazareti anaonesha kuwa unabii wa ahadi ile umetimia kwa ujio wake. Ni kwa ujio wake anakuja kuwa faraja na matumaini kwa wale wote waliopondeka mioyo, waliosetwa na wanaokuwa katika hali duni na mateso makubwa. (Luka 4:21).

Heri wenye upole maana watairithi nchi
Heri wenye upole maana watairithi nchi

“Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi.” Wanyenyekevu anaozungumzia Yesu ndio wale tunaokutana nao pia katika Agano la Kale. (Haggadah Midrashi) (Zaburi 37) Wanyenyekevu ndio wale wanaopitia madhulumu ya haki zao, uhuru wao na hata wa mali zao. Ni maskini kwani wenye nguvu wamewapora mashamba yao, nyumba zao, na hata mali kidogo waliyobaki nayo nayo imeporwa na wakati mwingine hata watoto wao. Ndio wale ambao hawachagui njia ile ya kutumia mabavu au nguvu, au kisasi katika kutetea haki zao. Ndio wale ambao hawaruhusu kuongozwa na roho ya chuki na kisasi. Wanyenyekevu ni wale ambao wanakubali kuongozwa na mantiki ya Mungu mwenyewe kwa kumtegemea Mungu katika hali na nyakati zote. Yesu anatambulishwa kama mnyenyekevu (Mathayo 11:29 na 21:5), sio kwa maana ya kuwa dhaifu au muoga, bali kwa maana ile ya kuongozwa na mantiki ya Mungu mwenyewe. Pamoja na kukutana na upinzani na kutendewa vibaya bado Yesu hakuchagua njia ile ya kulipiza kisasi au kutumia nguvu na mabavu kwani hiyo sio mantiki ya Mungu bali ya ulimwengu huu. Hivyo wenye heri ni wale ambao hata kama wanapitia madhulumu na mateso, wanachagua njia ya Yesu mwenyewe ya kubaki wanyenyekevu. Na ndio mwaliko wa Yesu kwetu sisi tunaokuwa wafuasi wake, kubaki wanyenyekevu kama Bwana na Mwalimu wetu alivyo mnyenyekevu. Ni vema kukumbuka daima kuwa nchi mpya watairithi sio wale wenye kutumia maguvu na kulipiza kisasi bali kwa wale wanaotembea katika njia ya unyenyekevu.

Heri wanyenyekevu wa moyo!
Heri wanyenyekevu wa moyo!

“Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.” Njaa na kiu ni hali ambazo tunakutana nazo kila siku katika maisha ya mwanadamu. Hivyo, wafuasi wa Yesu tunaalikwa kuwa na njaa na kiu sio ya chakula na kinywaji, kama ambavyo tunakuwa nayo kila siku bali leo tunaalikwa kuwa na ile ya haki.  Haki anayoizungumzia Yesu leo ndio ile ya Mungu mwenyewe. Mungu ni mwenye haki, sio kwa sababu anawapatia mema wale wanaokuwa wema kama sehemu ya malipo na mastahili yao, bali kwa kuwapatia na kuwatendea mema hata na wale wanaokuwa wadhambi na wakosefu. Kwa upendo wake usio na mipaka anawajalia mema hata wale walio waovu. Ni mwenye haki kwa kuwa anataka wanadamu wote tupate wokovu kwa njia ya kuujua ukweli wote. (1Timoteo 2:4). Kwetu haki ni pale muovu au mkosefu anapoadhibiwa kwa makosa au madhambi yake. Bali kwa Mungu haki inatendeka kwa kusukumwa na upendo wake wa Kimungu pale ambapo mkosefu na mdhambi anapofanya toba na kuongoka, ndio kumwelekea Mungu.  Haki yake daima ni wokovu, ndio kumrejesha na kumstahilisha haki yule anayetembea katika njia ya uovu na uasi. Hivyo anayekuwa na kiu na njaa ya haki kwa kila mkosefu na mdhambi, huyo hakika atashibishwa. Ndio yule anayefurahi kama Mungu pale anapomwona mwingine naye anapata wokovu, mwingine anakuwa rafiki wa Mungu na wanadamu. Sio yule anayefurahi kuangamia na kupotea kwa mwingine. (Yohane 6:39 na Ezekieli 18:23).

“Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.” Badala ya kuongozwa na roho ile ya kuwaadhibu wakosefu au kulipa kisasi tunaalikwa kuwa wenye huruma na msamaha. Ndio kutimiza mwaliko wa Yesu Kristo kuwa wenye huruma na wenye kusamehe wengine wanaotukosea katika maisha. (Luka 6:36-37) Ni mwaliko wa kuwa na huruma kama Baba yetu wa mbinguni alivyo na huruma. Kuwa wenye huruma na rehema ni zaidi ya kusamehe kwani tunaalikwa pia kuwa na roho ya kuwajali wengine wanaohitaji upendo wetu. Ndio kuwa na roho kama ya yule Msamaria aliyemwonea huruma msafiri aliyejeruhiwa na kuachwa njiani nusu mfu. (Luka 10:37). Marabi wa nyakati za Yesu walifundisha kuwa Mungu ni mwenye huruma kwani anawavisha nguo walio uchi. Na daima walirejea tukio la Mungu kuwavisha nguo wazazi wetu wale wa kwanza Adamu na Hawa baada ya anguko lile la kwanza mle bustanini. (Mwanzo 3:21).

Heri wenye rehema maana hao watapata rehema
Heri wenye rehema maana hao watapata rehema

“Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu.” Usafi ni moja ya masharti makubwa na muhimu katika ibada za dini ya Kiyahudi. Na ndio utaona dini ya Kiyahudi iliwataka waamini wake kutawadha kila mara wanaposhika kitu najisi. (Marko 7:3-4). Pamoja na hayo kwa Yesu mkazo haupo katika usafi wa nje bali ule wa ndani, ndio ule wa moyo na roho ya mtu. Yesu anatufundisha sio kile kimwingiacho mtu kutoka nje kinacho mfanya mtu kuwa najisi bali kile kinachotoka ndani mwake, yaani kitokacho moyoni mwake. (Mathayo 15:17-20). Wenye moyo safi ndio wale wanaokuwa na mioyo isiyogawanyika kwani wanaishi kwa kuenenda kadiri ya mapenzi ya Mungu na si kinyume chake. Ndio wale wanaolinganisha maisha yao na Neno la Mungu na sio kwa mantiki na vionjo vyao vya dunia hii. Sio wale wenye mioyo iliyogawanyika, wanaotumikia mali na Mungu. Ndio wale wenye kumpenda Mungu na jirani katika hali na nyakati zote za maisha. (Mahtayo 5:28)

“Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu.” Katika mafundisho ya Marabi daima walisisitiza umuhimu wa kuleta amani kati ya watu waliokosana na kuhitilafiana. Neno amani (shalom) katika Maandiko Matakatifu halimaanishi tu kutokuwepo kwa vita au magomvi au kutokuelewana bali linajumuisha pia mafanikio katika mapana na ujumla wake, mahusiano mema na Mungu na wengine, amani ndani ya nafsi ya mtu mwenyewe, afya na siha njema, haki na furaha. Hivyo wapatanishi ndio wale wanaohakikisha kila mmoja anayemzunguka anaishi kwa kuwa na hii shalom ya kweli, ndio mafanikio ya kweli katika nyanja mbali mbali.

Heri wapatanishi maana wataitwa wana wa Mungu
Heri wapatanishi maana wataitwa wana wa Mungu

“Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.” Maisha ya ufuasi sio lelemama, sio rahisi na hivi tangu mwanzoni Yesu anatutahadharisha wanafunzi na rafiki zake. Madhulumu na mateso ni sehemu ya maisha ya kila mfuasi wake Yesu Kristo, hivyo tutashutumiwa na hata kuudhiwa kwa uongo kwa ajili ya Kristo Mfufuka na Injili, lakini sisi tunahakikishiwa na Yesu kuwa tubaki na hakika ya kuwa na heri na furaha ya kweli. (Zaburi 7:2 na 119:84, 86). Heri za mlimani ndio katiba na mwongozo wa maisha ya kila mfuasi wake Kristo Yesu. Ili kuziishi hatuna budi kuruhusu wokovu wa fikra, kuvua kichwa cha kale na kuvaa kichwa kipya, ndio mantiki ile ya Mungu mwenyewe. Ni mwaliko wa kufanya metanoia, ndio kubadili kichwa au wokovu wa fikra. Nawatakia tafakuri njema na Dominika takatifu!

27 January 2023, 16:22