Injili zote nne zinakazia kutuonesha Umungu wa Kristo na zote zinahitimishwa kwa kutuonesha Fumbo la maisha ya Yesu Kristo, yaani mateso, kifo na ufufuko wake uletao maisha na uzima wa milele. Injili zote nne zinakazia kutuonesha Umungu wa Kristo na zote zinahitimishwa kwa kutuonesha Fumbo la maisha ya Yesu Kristo, yaani mateso, kifo na ufufuko wake uletao maisha na uzima wa milele.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Pili Mwaka A wa Kanisa: Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu

Yesu wa Nazareti aliye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu: Dhambi ya kutoamini, ya majivuno, chuki, kiburi na mengine mengi yasiyopendeza mbele ya Mungu, ndiye anayekuwepo kabla ya vitu vyote kwani Yeye ni wa milele, ni Mungu, na juu yake kuna Roho wa Mungu, ni Mwana wa Mungu. Ni utambulisho wenye ujumbe mzito na kitaalimungu kwa wote.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Kristo Yesu kwa kushuka mtoni Yordani, anayatakasa maji yale ya ubatizo kutuondolea dhambi zetu na hivyo kufanyika wana wa Mungu na Kanisa! Baada ya maadhimisho ya sherehe za fumbo la Umwilisho, yaani Noeli, Mama Kanisa anatupatia nafasi ya kuendelea kumtambua huyu mtoto aliyezaliwa na kukaa kati yetu. Noeli ni nafasi ya kuutafakari upendo wa Mungu unaokuja kwetu ili tupate uzima wa milele. Ni Mungu anayechagua njia ile nyonge na duni kabisa ya kujifunua kwetu, kwa njia ya huyu mtoto anayezaliwa na binti mdogo wa Kiyahudi yaani, Mama Bikira Maria pangoni katika mji ule wa Daudi wa Betlehemu. Ikiwa dhambi kubwa ikiwa ni majivuno, iliyomweka mwanadamu mbali na Mungu na wengine, ni kwa njia ya unyenyekevu kabisa Mungu anaingia tena katika historia ya wokovu wetu. Wakati Injili pacha yaani za Marko, Mathayo na Luka zinaonesha mwanzo wa misheni ya Yesu hadharani kwa tukio la Ubatizo wake, Mwinjili Yohane hatuoneshi tukio hilo na badala yake anatoa nafasi kwa Yohane Mbatizaji anayemtambulisha Yesu kama Mwanakondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Wakati Injili ya Matayo ililengwa zaidi kwa Wayahudi Wakristo, Injili ya Marko ililengwa kwa Wakristo wa Kanisa la Roma au Warumi wa nyakati zile, Injili ya Luka iliwalenga zaidi Wakristo wenye asili ya Kigiriki na Injili ya Yohane ndiyo ilibaki kuwa ya watu wote. Lakini Injili zote nne zinakazia kutuonesha Umungu wa Kristo na zote zinahitimishwa kwa kutuonesha Fumbo la maisha ya Yesu Kristo, yaani mateso, kifo na ufufuko wake uletao maisha na uzima wa milele.

Kristo Yesu ni mwanakondoo wa Mungu
Kristo Yesu ni mwanakondoo wa Mungu

Mwinjili Yohane anatuonesha kuwa Yohane Mbatizaji si tu mtangulizi wa Masiha bali zaidi sana ni mtambulishaji wa Masiha kwetu. Ni kwa kupitia Yohane Mbatizaji anamtambulisha Masiha wa Mungu kwa watu wote. (Yohane 1:6-8) Ujumbe kutoka kwa makuhani na walawi wanakwenda Mtoni Yordani ili kumuuliza kama Yohane Mbatizaji ndiye Masiha au la. Na hapo tunaona anawajibu kwa kuwaambia kuwa yeye siye Kristo…yeye anabatiza kwa maji, ila kati yao amesimama mmoja ambaye wao hawakumtambua, anayekuja baada yake, ambaye hawezi hata kulegeza gidani za viatu vyake. (Yohane 1:19-28). Ni katika muktadha huo ndio tunaona Yesu akiingia katika simulizi la Injili yetu ya leo. Dakika chache kabla tunaona macho na masikio yote yalikuwa kwa Yohane Mbatizaji, hata kutuma wajumbe kuja kumuuliza kama ndiye Masiha au la. Ni katika mazingira haya tunaona mara moja anafika Yesu na Yohane Mbatizaji anamtambulisha; “Tazama Mwanakondoo wa Mungu, yeye anayeondoa dhambi ya ulimwengu!” (Yohane 1:29) Ni Yohane Mbatizaji anayemtambua na hivyo kuwatambulisha si tu wasikilizaji wake bali hata nasi leo kuwa ni Yesu wa Nazareti aliye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu. Ndiye anayeondoa dhambi ya kutoamini, ya majivuno, chuki, kiburi na mengine mengi yasiyopendeza mbele ya Mungu, ndiye anayekuwepo kabla ya vitu vyote kwani Yeye ni wa milele, ni Mungu, na juu yake kuna Roho wa Mungu, ni Mwana wa Mungu. Ni utambulisho wenye ujumbe mzito na mkubwa wa kiteolojia kwani Yohane Mbatizaji hafanyi utambulisho wa jina au mahali atokapo Yesu bali ni juu ya wasifu wake unaoakisi pia misheni na asili yake ya Kimungu.

Kwa Sakramenti ya Ubatizo, mwamini anaondolewa dhambi ya asili
Kwa Sakramenti ya Ubatizo, mwamini anaondolewa dhambi ya asili

Yohane Mbatizaji anakiri na kuonesha kuwa hata naye hakumtambua wala kumjua Yesu kuwa ndiye Masiha wa Mungu, hivyo anafikia kumtambua baada ya kukiri na kukubali kutokumjua na kumtambua Masiha, na kukubali kuongozwa na Roho wa Mungu wenyewe.  (Yohane 1:31 na 33) Hivyo hata nasi kama kweli tunataka kumtambua Yesu kama Masiha hatuna budi kukubali kutokumtambua na hivyo kuanza kufanya safari ya kiimani kama aliyoifanya Yohane Mbatizaji huku tukiongozwa na Roho wa Mungu. Ni safari ya kila siku katika maisha yetu, ni safari ya mang’amuzi ya kuitambua sura halisi ya Mungu kati yetu. Mungu anayejifunua katika maisha ya kawaida kabisa, na hivyo tunabaki na mshangao wa daima! Nawaalika katika tafakuri yetu ya leo kuchukua ishara mbili za msingi ili kwazo zitusindikize na kutusaidia katika kumtambua Yesu, nazo ndizo MWANAKONDOO NA HUA au NJIWA. Mwinjili Yohane kwa sehemu hii ya Injili ya leo anaitumia kama katekesi si tu kwa Kanisa au jumuiya zile za mwanzo bali hata kwetu leo. “Tazama, Mwanakondoo wa Mungu”, ni maneno anayotamka Yohane Mbatizaji na huku akimkazia macho Yesu, nawaalika ili kupata ujumbe na maana ya katekesi hii hatuna budi tangu mwanzo kuwa huru na tafsiri rahisi kama vile kwa kuangalia hulka na tabia za mwanakondoo kama upole na unyenyekevu. Katika Maandiko kuna maana nyingi na hata yawezekana kuwa kidogo ngumu ila zikilenga kutusaidia kupata maana kusudiwa katika Injili ya leo.

Wokovu wa mwanadamu umetundikwa Msalabani.
Wokovu wa mwanadamu umetundikwa Msalabani.

Yohane Mbatizaji yawezekana alilelewa kati ya wamonaki wa Kumrani, hivyo alielewa vyema maisha ya kiroho ya Wayahudi, kama Myahudi aliyeelewa kuwa wasikilizaji wake waliweza kumuelewa mara moja na kwa urahisi anapomtambulisha Yesu kama Mwanakondoo. Kwa Myahudi, picha ya mwanakondoo inamrejesha kwa mwanakondoo wa Pasaka, ambaye damu yake ilipakwa katika miimo ya milango, hivyo kwa kupakwa kwake iliweza kuwaokoa kutoka kwa mjumbe yule wa kifo. Hivyo ni katika nafsi ya Yesu, kwa damu yake haswa kama ile ya mwanakondoo, wote wanapata wokovu.  Na ndio utaona kuwa Yesu alihukumiwa kifo mchana ule uliotangulia Pasaka, kwani kwa desturi pia wanakondoo wa Pasaka walichinjwa na makuhani mchana uliotangulia Pasaka pale hekaluni kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka ya Wayahudi. (Yohane 19:14) Na pili utaona pia Yohane Mwinjili anatuonesha kuwa Yesu pale msalabani hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa kama ilivyokuwa desturi kwa mwanakondoo wa Pasaka. (Yohane 19:36) Maana ya pili ya Mwanakondoo wa Mungu tunaiona pia katika Maandiko Matakatifu katika unabii wa Isaya anapozungumzia juu ya Mtumishi wa Mungu anayeteseka, yaani Anawim wa Mungu.  (Isaya 53:7,12) Ni Mtumishi wa Mungu anayeongelewa na kufananishwa na mwanakondoo anayeongozwa kwenda machinjioni, mpole na anayebeba dhambi za watu mabegani mwake. Na hata wataalamu wa Maandiko wanatuonesha kuwa Yohane Mbatizaji alitumia neno la Kiaramayo “talyà” likiwa na maana mbili, yaani mwanakondoo na mtumishi, hivyo hapo ingesomeka na kubeba maana zote mbili katika Kitabu cha Nabii Isaya. Hivyo Kristo ndiye anayebeba dhambi zetu zote, hivyo anakubali kwa hiari yake kumwaga damu yake kwa ajili ya kuwakomboa ndugu zake, yaani mimi na wewe. Hakika Yesu Kristo ni mwanakondoo na mtumishi wa Mungu anayeteseka, Anawim!

Kristo Yesu anaendelea kujitoa sadaka wakati wa Misa Takatifu
Kristo Yesu anaendelea kujitoa sadaka wakati wa Misa Takatifu

Zaidi sana tunaona pia Yohane Mbatizaji kwa utambulisho wa Mwanakondoo wa Mungu anatukumbusha sadaka ile ya Abrahamu. Isaka akiwa njiani na baba yake kwenda mlima Moria anamuuliza baba yake, kuwa wana moto na kuni, lakini yu wapi mwanakondoo wa sadaka? Na ndipo Abrahamu anamwambia ni Mungu mwenyewe atawapa mwanakondoo wa sadaka. (Mwanzo 22:7-8). Ndio leo Yohane Mbatizaji anajibu na kusema, tazameni mwanakondoo wa Mungu, ni Yesu anayetolewa na Mungu kwa ajili ya ulimwengu mzima ili awe sadaka kwa yetu sisi tulio wadhambi na wakosefu. Ni yeye anayebeba dhambi zetu na kuutoa Mwili na Damu yake ili iwe fidia ya madhambi yetu. Kama alivyo Isaka, mwanapekee wa Abrahamu tunaona Yohane Mbatizaji anamfananisha na Yesu kama Mwana pekee wa Mungu aliyependezwa naye, kama Isaka aliyebeba kuni ndivyo na Yesu anabeba mti wa msalaba kuelekea pale Kalvario, mpole na mnyenyekevu katika kutimiza mapenzi ya Baba yake. Kama tunavyosoma katika Midrashi za Kiyahudi kuwa Isaka alikubali kutolewa sadaka na hata kumwambia baba yake amfunge sawa sawa ili awe sadaka inayokubalika mbele ya Mungu, ndivyo na Yesu anavyokubali na kupokea kikombe kile cha kutolea Mwili na Damu yake pale juu msalabani ili alipie dhambi ya ulimwengu mzima. Mwanakondoo pia anazungumziwa katika Kitabu cha Ufunuo. Kwa Wayahudi waliamini kuwa mwisho wa ulimwengu mwanakondoo atashinda kwa kuharibu nguvu zote za yule mwovu, dhambi na dhuluma. Kristo ndiye anayetukomboa kutoka katika kila uovu na anayetusamehe dhambi zetu.

Ushiriki mkamilifu wa Sadaka takatifu ya Yesu ni muhimu sana
Ushiriki mkamilifu wa Sadaka takatifu ya Yesu ni muhimu sana

Na ndio katika kila Adhimisho la Ekaristi Takatifu tunaalikwa kumtazama Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu mzima. Ndiye anayetoa Mwili wake kwa ajili ya wengi, na kutualika kunywa Damu yake kwa ajili ya wokovu wetu. Tazameni Mwanakondoo wa Mungu, ndio mwaliko wa kukubali kuingia katika mahusiano ya kweli na ya ndani pamoja naye. Ni mwaliko wa kumkaribisha katika maisha yangu ili afanye makao yake ndani mwangu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha wokovu wetu kwani kwayo tunampokea huyu Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu. Labda mpaka hapa tunaweza kujiuliza kama Yohane Mbatizaji alielewa kuwa Yesu ndiye anayezungumziwa katika Maandiko Matakatifu kama tulivyofanya rejea hapa juu.  Na hasa tukizingatia kuwa Yohane Mbatizaji mara mbili anakiri na kusema kuwa hakumtambua kuwa ndiye Masiha. (Yohane 1:29, 36) Kwa hakika tunaweza kusema hapana hakuweza kuwa na uelewa huo mkubwa na mpana tangu pale mwanzoni mwa kazi ya Yesu hadharani, itoshe kueleweka kuwa ni nia na lengo la Yohane Mwinjili kwani alikuwa anatoa katekesi kwa Wakristo wale wa jumuiya za kwanza na kwetu leo. Na ndio tunaona Yohane Mwinjili anatumia tukio la leo kumtambulisha Yesu katika mapana na hasa kwa kuoanisha na misheni yake ulimwengu kama Mwanakondoo wa Mungu, anayekuja ili ulimwengu upate wokovu wa kweli.

Kristo Yesu Mwanakondoo wa Mungu
Kristo Yesu Mwanakondoo wa Mungu

Ishara ya pili zaidi ya MWANAKONDOO ndiyo HUA au NJIWA. Tofauti na Injili ndugu tunaona Yohane Mbatizaji akimuonesha njiwa si tu akishuka bali alibaki juu ya Yesu. Katika Agano la Kale, Roho wa Mungu aliwashukia na kubaki juu ya wale aliowateua na kuwatuma na kubaki nao kwa kipindi kile tu cha misheni kusudiwa. Ila leo tunaona Roho wa Mungu anabaki juu ya Yesu, ndio kusema Yesu ni Mungu kwani daima ndani mwake ndio makao ya kudumu ya Roho wa Mungu. Ni kwa kupitia Yesu basi tunaona Roho wa Mungu anaingia ulimwenguni. Na ndio Ubatizo katika Roho. Ubatizo wa Yohane ulikuwa ni wa nje kwa maana ya maji bali Ubatizo wa Yesu ni katika Roho Mtakatifu, hivyo sio wa nje bali wa ndani kabisa mwa kila anayeupokea. Ni kuungana na Roho wa Mungu, ni kufanyika wana wa Mungu, warithi pamoja na Yesu Kristo. Ubatizo ni kuzamishwa katika ushirika wa Kimungu, yaani Utatu Mtakatifu, ndio kupokea maisha ya neema, maisha ya muungano na Mungu! Yesu Kristo alipoingia katika maji yale ya mto Yordani na kubatizwa na Yohane, hakika maji yake hayakufanya kitu kwa Yesu na badala yake Yesu Kristo ndio anayapa uwezo maji yale ili kutuondolea dhambi zetu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Kama alivyosema Mt. Ambrosi; “Alipo Kristo hapo kuna Yordani”, na ndio kwa njia ya Ubatizo nasi tunapokea neema juu ya neema, ya kuzaliwa upya na kufanyika kweli wana wa Mungu, warithi pamoja na Mwana pekee wa Mungu yaani Kristo Yesu. Na ndio Habari Njema ya furaha tunayotangaziwa leo kwa kila mbatizwa kuwa kwa Ubatizo wetu tunashiriki na kupata kuwa viumbe wapya. (1Yohane 1:3-4) Ubatizo ni mlango wa lazima unaotujalia kuwa wana wa Mungu, na ndio pia kufanyika wanakanisa. Tafakari njema na Dominika takatifu!

13 January 2023, 11:09