Tafakari Dominika ya Pili ya Mwaka A wa Kanisa: Kristo Yesu Ndiye Mwanakondoo wa Mungu
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli (Napoli) Italia.
Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Yohane Mbatizaji wakati alipokuwa anawabatiza watu ubatizo wa toba iletayo maondoleo ya dhambi, alimwona Kristo Yesu akimwijia akamtambulisha kwa watu kuwa ni Mwana kondoo wa Mungu anayezichukua dhambi za ulimwengu. Wengi walimfananisha Yohane Mbatizaji na Nabii Elia aliyewatakasa Waisraeli kutoka katika ibada ya kuabudu miungu na kuwarejesha tena katika imani ya kweli iliyojikita kwa Mwenyezi Mungu aliye hai, yaani Mungu wa Abramu, Isaka na Yakobo. Kristo Yesu ni nuru ya ulimwengu. SOMO LA KWANZA: Isa. 49:3, 5-6: Katika somo letu la kwanza tunasikia juu ya “mtumishi wa Bwana” ambaye Mungu amemteua tangu tumboni kwa ajili ya kufanya utume kwa makundi mawili: kwanza, atafanya utume kwa watu wake mwenyewe (yaani watu wa taifa la Israeli): “… ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena…”; Pili, atafanya utume wa kuleta wokovu hata miisho ya dunia: “upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia.” Kwa Wayahudi, “neno miisho ya dunia” lilimaanisha “mataifa yote ya ulimwengu.” Kwa maneno mengine, mtumishi wa Bwana atafanya utume wa kuwarudisha watu wake (Waisraeli/Wayahudi wenzake) mbele za Bwana na pia kuleta wokovu kwa watu wa mataifa yote. Mtumishi wa Bwana atashughulikia wokovu wa watu wote, siyo wa Wayahudi tu. Kwa kuwa Agano la Kale linatabiri yatakayotukia katika Agano Jipya, basi ni dhahiri kuwa “mtumishi wa Bwana” anayezungumziwa leo ni Bwana Wetu Yesu Kristo ambaye utume wake wa kwanza ulikuwa kuwavuta Wayahudi wenzake kumrudia Mungu na kadhalika utume wake ulikuwa kuwaletea wokovu watu wa mataifa yote. Ingawa mtumishi anayezungumziwa ni Bwana Wetu Yesu Kristo, sisi nasi tunapaswa kushiriki utume huo wa Kristo. Tangu tumboni mwa mama zetu tumeteuliwa kuhubiri habari njema ili watu wavutwe kwa Mungu na pia tunapaswa kuwa nuru kwa wengine ili nao wapate wokovu. Kila mmoja wetu ajiulize kama anatimiza wajibu huo. Je, sisi tunatangaza habari njema kwa maneno na maisha yetu? Je, matendo na maisha yetu kwa ujumla yanatoa nuru kwa wengine?
SOMO LA PILI: 1 Kor. 1:1-3: Somo letu la pili ni utangulizi wa barua ambayo Paulo anawaandikia Wakristo wa Kanisa la Korintho, kabla ya kuingia ndani zaidi na kugusia mambo muhimu yaliyokuwa yakiendelea katika kanisa la Korintho, hasa majivuno, dhambi za zinaa, migawanyiko miongoni mwa Wakristo iliyotokana na tofauti za machimbuko, hali ya kifedha, uwezo wa kuzungumza au hadhi yake (social status). Leo katika utangulizi wa barua yake Paulo anawakumbusha Wakorintho mambo muhimu yafuatayo: (i) Wakristo wa Korintho ni “Kanisa la Mungu.” Paulo anawaita Wakristo wa Korintho kuwa ni “… Kanisa la Mungu lililoko Korintho.” Kanisa siyo jengo bali ni kusanyiko (ekklesia) la watu waliobatizwa na kumwamini Kristo. Hivyo, “wabatizwa wa Korintho” ni mali ya Mungu- kanisa la Mungu na wala siyo mali ya mtu fulani kama wao wenyewe Wakorintho walivyojipambanua kadiri ya mtu aliyewahubiria Injili wakisema, “Mimi ni wa Paulo,” na wengine “Mimi ni wa Apolo” na wengine “Mimi ni wa Kefa.” Hivyo Paulo anaposema, “kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho” anawakumbusha kuwa wao wote wanamilikiwa na Mungu- wameitwa na Mungu. (ii) Wakristo wa Korintho “wametakaswa”. Neno la Kigiriki lililotumika kumaanisha “kutakaswa” lina maana ya “kutengwa kwa shughuli maalum” au “kutengwa na uozo/upotovu.” Hivyo, Paulo anawakumbusha kuwa kwa kubatizwa na kumpokea Kristo, Wakristo wa Korintho wanapaswa kujitenga na uozo/uharibifu unaoendelea katika jamii yao kwani wao wenyewe wametengwa kwa shughuli maalum- yaani kutangaza na kuishi Injili.
Hivyo, Wakorintho wanapaswa kujibandua na malimwengu na kujiambatanisha ya mambo yamhusuyo Mungu. (iii) Wakristo wa Korintho “wameitwa kuwa watakatifu”. Hapa Paulo anawakumbusha kuwa, licha ya madhaifu yao, Wakristo wa Korintho wanapaswa daima kupania utakatifu ambao kimsingi unatokana na mkristo kuwa katika mahusiano mazuri na Mungu kwa kujitenga na dhambi (iv) Mungu Baba na Mungu Mwana ni chanzo cha neema na amani kwa Wakristo. Paulo anaposema, “Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo” analenga kuwakumbusha kuwa Mungu ndiye chanzo cha neema na amani ya kweli. Hivyo, Paulo anawakumbusha kuwa neema na amani havitoki kwa mwanadamu bali vyatoka kwa Mungu. Sehemu hii ya barua ya Mtume Paulo kwa Wakorintho inatulenga sisi pia. Mosi, tutambue kwamba “Kanisa ni mali ya Mungu”. Kwa bahati mbaya wapo wanaofikiri kanisa ni mali yao binafsi. Watu wa namna hii utawasikia wakisema, “kanisa langu” au wakisema, “bila mimi kanisa hili lisingekuwa hivi lilivyo”. Daima tukumbuke kuwa ustawi wa waamini (kanisa) ni kazi ya Mungu na Yeye ndiye mmiliki. Pili, tutatumbue kuwa kwa ubatizo wetu “tumetakaswa”, yaani tumetengwa na uozo unaosababishwa na kukumbatia malimwengu. Kwa bahati mbaya sisi wabatizwa “tumejishikamanisha na upotovu wa ulimwenguni” kwa kujiambatanisha na dhambi na kushabikia malimwengu. Yaani wakati mwingine ni vigumu kutofautisha kati ya mkristo na mpagani- wote tunaonekana kuwa sawa.
Na malimwengu yametuzingira kila pande na hivyo tumejikuta tunahangaikia zaidi malimwengu: anasa, mali, biashara, wanawake/wanaume na vivutio vingine vya ulimwengu huu. Tatu, tumeitwa kuwa watakatifu. Tunapaswa kutambua kuwa “mwito wetu ni kuwa watakatifu”. Hata hivyo tusisahau kuwa safari ya kuutafuta utakatifu si lelemama. Tutapataje utakatifu? kwa kuishi amri na maagizo ya Mungu, kwa kutimiza wajibu wetu kwa Mungu na kwa jirani zetu na kwa kujitenga na malimwengu. Nne, tutambue kuwa Mungu (Mungu Mmoja, Nafsi Tatu) ndiye chanzo cha neema na amani. Paulo anathibitisha hili kwa kusema, “Neema na … amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.” Kwa bahati mbaya watu wengi tunadhani neema tunazopokea (afya, nguvu, uwezo wa akili, utajiri, imani na karama nyingine) ni kazi ya juhudu zetu wenyewe. Kadhalika tunafikiri kuwa amani inaletwa na wingi wa mali tulizonazo, vyeo tulivyonavyo au ustawi wa biashara zetu. Tunajidanganya! Amani ya kweli inatoka kwa Mungu. Na tunaipata amani hii tunapomtumikia Mungu na tunapowatumikia wenzetu.
SOMO LA INJILI: Yn. 1:29-34: Leo katika Injili Yohane Mbatizaji anamtambulisha Yesu kwa wanafunzi wake akisema ya kuwa Yesu ni “Mwanakondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu.” Ni maneno haya haya ya Yohane Mbatizaji yanarudiwa na Padre katika kila adhimisho la Misa anapoinua juu hostia takatifu akisema, “Tazama, Mwanakondoo wa Mungu, tazama, aondoaye dhambi za ulimwengu…” Yohane Mbatizaji anamfunua Yesu kama Mwanakondoo. Kwa nini Yohane anamwita Yesu kuwa ni Mwanakondoo? Tukitaka kuelewa vizuri alichomaanisha Yohane Mbatizaji ni vizuri kurudi kwenye matukio muhimu katika historia ya wokovu wa Wayahudi: (i) Tukio la Pasaka ya kwanza ya Wayahudi kule utumwani Misri (Kut. 12:21-28). Katika tukio hili Mungu aliagiza Waisraeli wachinje mwanakondoo na kisha damu yake iwekwe kwenye birika kisha wachukue majani ya husopo na kuchovya ndani ya damu na kupaka katika vizingiti na miimo yote miwili ya milango ya nyumba za Waisraeli. Damu hiyo itakuwa ni ishara kwa malaika wa kifo kuwa nyumba hiyo ni ya Waisraeli na hivyo atairuka wakati anapita kuangamiza wazaliwa wa kwanza wa Wamisri. Wazaliwa wa kwanza wa Wayahudi wataepuka kifo kwa sababu ya damu ya mwanakondoo itakayomfanya malaika wa kifo aruke nyumba zao. Ni katika mwanga wa tendo hilo lililotukia Misri, Yohane Mbatizaji anamtambulisha Yesu kuwa ni Mwanakondoo wa Mungu kwani kwa damu ya Kristo itakayomwagika msalabani sisi sote tunaepushwa na mauti ya milele. Kwa hiyo Yesu Kristo ni mwanakondoo wa Pasaka aliyetolewa sadaka kwa ajili yetu. Mtume Petro anasisitiza hili akisema, “Lakini hamkukombolewa kwa vitu vyenye kuharibika: kwa fedha au dhahabu; bali kwa damu ya thamani ya Kristo, ambaye alikuwa kama mwanakondoo asiye na dosari wala doa” (1 Pt. 1:19). (ii) Ibada za Waisraeli za kutoa sadaka za wanyama (hasa kondoo).
Hata baada ya kufika Israeli wakitokea Misri, Waisraeli waliendelea kutoa sadaka za wanyama kama njia ya kujipatanisha na Mungu baada ya kutenda dhambi kama mtu mmoja mmoja au kama taifa. Mnyama maarufu aliyetolewa kama sadaka ya dhambi (mnyama anachinjwa kwa niaba ya watu waliotenda dhambi) ni mwanakondoo. Mtu aliyekiri mbele ya Mungu kuwa ametenda dhambi alifika hekaluni akiwa na mwanakondoo (au mbuzi), kisha aliweka mikono yake juu ya mwanakondoo (ishara ya kuhamishia dhambi zake kwa kondoo) na kisha kondoo alichinjwa na damu yake alinyunyuziwa yule mtu mdhambi (mtoa sadaka). Namna hii ya utoaji wa sadaka ilionesha kuwa “mnyama anachukua nafasi ya mwanadamu,” yaani “mwanadamu kwa sababu ya kutenda dhambi alistahili kufa, lakini mnyama [mwanakondoo] anakufa kwa niaba yake ili mwanadamu apate msamaha wa dhambi zake.” Ni tendo lililoashiria kuwa “mwanadamu anaomba msamaha wa dhambi ili apatanishwe na Mungu.” Hivyo, Yohane Mbatizaji anapomtambulisha Yesu kama Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu anamaanisha kuwa Kristo ndiye Mwanakondoo halisi ambaye atachukua dhambi zetu na kuuawa kwa niaba yetu ili sisi tupate msamaha wa dhambi na kupatanishwa na Mungu. Kwa Yohane Mbatizaji, Yesu Kristo ni Mwanakondoo halisi anayetolewa sadaka ili kuondoa dhambi za ulimwengu kwani kondoo waliotolewa sadaka na Wayahudi kwa uhalisia wake hawakuondoa dhambi (rejea Ebr. 10:4) bali walikuwa ni kivuli tu cha “mwanakondoo wa kweli- Bwana Wetu Yesu Kristo” ambaye atakufa kwa niaba yetu ili tupate kweli msamaha wa dhambi na kupatanishwa na Mungu.
Kutokana na somo letu la Injili ya leo tunafunuliwa kuwa: (1) Kristo ndiye anayeondoa dhambi zetu. Ingawa tunafahamu kuwa Kristo kwa kujitoa sadaka pale msalabani aliondoa dhambi zetu na kutuondoa katika minyororo ya dhambi na mauti, bado anaendelea kutuondolea dhambi zetu kila siku kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho. Je, ni Wakatoliki wangapi tunamwendea mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu kwenye Sakramenti ya Kitubio? Leo hii kwa sababu ya changamoto za Wapentekoste/Waprotestanti au kwa kupuuzia tu, Wakatoliki wengi tumeacha kuijongea Sakramenti ya Kitubio ambayo kwayo “Mwanakondoo halisi- Bwana Wetu Yesu Kristo, anatuondolea dhambi zetu.” (2) Yesu ni Mwana wa Mungu. Yohane anaendelea kufunua kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu. Yeye mwenyewe alijua ukweli huo alipokuwa anambatiza Yesu. Je, mimi na wewe tunatambua ukweli huo. Je, Yesu ambaye ni Mwana wa Mungu ana nafasi gani katika maisha yako? Tafakari, chukua hatua na kufanya mabadiliko.