Tafakari Dominika ya Pili Ya Mwaka A wa Kanisa: Yesu: Nuru na Mwanakondoo wa Mungu
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya pili ya Mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Kwa Sherehe ya ubatizo wa Bwana tulihimisha kipindi cha noeli na kuanza kipindi cha kawaida cha mwaka. Tunaweza kusema kuwa Jumapili ya kwanza ya kipindi cha kawaida tuliadhimisha Ubatizo wa Bwana ambapo Mungu katika nafsi Tatu za Utatu Mtakatifu alijidhihirisha: Mungu Roho Mtakatifu katika alama na ishara ya njia, Mungu Baba kwa sauti yake iliyosikika ikimtambulisha Mungu Mwana kwetu sisi ikisema: Huyu ni Mwanangu Mpendwa, Msikilizeni yeye. Ujumbe wa masomo ya dominika ya pili ya Mwaka A wa Kanisa ni kuwa Yesu ni Nuru ya ulimwengu na Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu. Nasi kwa ubatizo tumeondolewa dhambi ya asili na adhabu zake zote pamoja na dhambi zingine na tumewekwa kuwa nuru kwa Mataifa kwa maneno na matendo yetu ili kwayo watu wengine wamjue, wampende na kumtumikia Mungu na mwisho sote kwa pamoja tuweze kufika kwake mbinguni. Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa 49:3, 5-6). Ni sehemu ya utenzi wa pili katika zile tenzi nne za Mtumishi wa Mungu; 1. Isa 42, 1-9, 2. Isa 49, 1-6, 3. Isa 50, 4-11, na 4. Isa 52, 13 – 53, 12. Somo hili linatufundisha kuwa Mungu alimchagua mtumishi wake tangu mwanzo kuwa nuru ya Mataifa yote. Haya yametimia katika Yesu Kristo ambaye Mungu amemweka awe nuru kwa mataifa ili apate kuwa wokovu wa watu wake hata miisho ya dunia.
Yesu Kristo ni mwanga halisi kwa watu wa mataifa yote. Yeye ni utimilifu wa utabiri huu wa Nabii Isaya. Naye alikuja kuyafanya mapenzi ya Mungu Baba kama Mzaburi anavyoimba katika wimbo wa katikati akisema; “Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, kuyafanya mapenzi yako” (Zab. 1, 3, 6-9, (K) 7, 8). Katika Misa ya Usiku wa Noeli Nabii Isaya alituambia: “Watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu. Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti. Nuru kuu imewaangaza” (Isa 9:2). Yesu ndiye Nuru ya kweli. Naye anajishuhudia akisema: “Mimi ndimi Nuru ya ulimwengu; yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe bali atakuwa na nuru ya uzima wa milele” (Yn 8:12). Nasi twajua ushuhuda huu ni wa kweli maana wanaomfuata yeye wanakuwa mwanga; “Ninyi ni mwanga wa ulimwengu” (Mt 5:14). Na mataifa yote yanashuhudia hili kama mzaburi anavyoimba katika wimbo wa mwanzo; “Ee Mungu, nchi yote itakusujudia na kukuimbia, naam, italiimbia jina lako, wewe Mtukufu” (Zab. 66:4).
Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho (1Kor 1:1-3), anajishuhudia wazi bila kusita kuwa ameitwa kuwa Mtume wa Mungu. Katika somo hili, Mtume Paulo anawaita Wakorintho watakatifu kwa sababu Mungu aliwaweka wakfu kwa njia ya Ubatizo. Hivyo anawatakia neema na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Bwana Yesu Kristo zikae nao daima. Tena anawaonya wasiuchafue utakatifu huo kwa mambo ya kiulimwengu, yaani wasijiingize katika dhambi. Mtume Paulo anawatakia wakristo Neema na Amani ya rohoni vitokanavyo na Roho wa Mungu. Ndiyo kusema anawaombea kwa Mungu ili waepukane na dhambi na wawe na uhuru wa kweli. Haya ni mausia kwa wakristo wa nyakati zote. Nasi tukishika hilo tutaleta Umoja na Mshikamano kati yetu sisi na kuufikia wito wa kuwa watakatifu kwa kuepuka nafasi za dhambi na kuyaishi mausia ya Kiinjili. Injili tunayoisoma ni ya Mwinjili Yohane (Yn. 1:29-34). Katika mzunguko wa mwaka wa Kiliturujia mwaka A tunatafakari Injili ya Mathayo, mwaka B Injili ya Marko na mwaka C Injili ya Luka. Lakini, domenika ya pili tunasoma Injili ya Yohani. Katika mwaka A, sehemu ya Injili ya Yohane tunayoisoma (Yn. 1:29-34), inasimulia jinsi Yohane Mbatizaji alivyoshuhudia mambo matatu juu ya Yesu: 1. Yesu ni Mwana Kondoo wa Mungu azichukuaye dhambi za ulimwengu. 2. Naye alishukiwa na Roho Mtakatifu. 3. Tena yeye ni Mwana wa Mungu naye alikuwapo tangu milele yote. Ndiyo kusema utabiri wa Nabii Isaya unatimia katika Yesu Kristo, nuru halisi aliyetumwa na Mungu Baba kuja kututoa katika giza la dhambi na mauti.
Yohane Mbatizaji ameyafahamu haya yote si kwa uwezo wake bali kwa ufunuo wa Roho Mtakatifu. Nasi tukimruhusu Roho Mtakatifu atuongoze, hakika tutayatambua makuu ya Mungu katika maisha yetu. Yohane Mbatizaji anamtambulisha Yesu akisema: Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za dunia." Swali la kujiuliza kwanini Yohane Mbatizaji anamlinganisha Yesu na Mwanakondoo wa Mungu. Itakumbukwa kuwa nyakati hizo kila asubuhi na mchana mwanakondoo alitolewa sadaka katika Hekalu la Yerusalemu kwa ajili ya dhambi za watu wa Israeli, wakifuata maelekezo ya Mungu kupitia kiongozi wao Musa kuwa: “Basi sadaka utakazotoa juu ya madhabahu ni hizi, mwanakondoo wa mwaka mmoja wawili siku baada ya siku. Mwanakondoo mmoja utamchinja asubuhi na wa pili utamchinja jioni…itakuwa ni sadaka ya kuteketezwa milele katika vizazi vyenu vyote mlangoni pa ile hema ya kukutania mbele ya Bwana, hapo nitakapokutana nanyi, ili ninene na wewe hapo” (Kut 29:38-42). Tena, katika kila sherehe ya Pasaka, mwanakondoo alichinjwa katika kila familia ya Myahudi, na nyama yake kuliwa wakati wa mlo wa Pasaka. Tendo hili lililenga kuwakumbusha watu wa Israeli kwamba waliwekwa huru kutoka utumwa wa Wamisri, kutokana na damu iliyopakwa katika kila miimo ya milango ya Waisraeli pale malaika alipopita kuwaadhibu wa Misri kwa kuwaua wazaliwa wa kwanza (Kut 12: 1-14).
Katika mazingira haya Yohane Mbatizaji alipomtambulisha Kristo kama mwanakondoo wa Mungu aondoae dhambi, wanafunzi wake waliweza kuelewa kwamba Yesu Kristo ni yule anayetolewa na kuchinjwa kama mwanakondoo kwa ajili ya maondoleo ya dhambi za ulimwengu mzima. Damu ya wanakondoo ambayo Wayahudi walitolea kama sadaka haikuwa na uwezo wa kuwaondolea watu dhambi zao, bali ni Mungu ambaye aliona toba ya watu, na kuwasamehe dhambi zao. Kondoo waliotolewa sadaka kwa karne nyingi mpaka Kristo alipofika zilikuwa zinamwelekea Kristo, mkombozi anayekuja. Yeye ndiye ambaye kwa damu yake dhambi za ulimwengu zinasamehewa, mwanadamu anapatanishwa na Mungu. Ndiyo maana Kristo alitolea maisha yake kama sadaka siku ile ya Pasaka ya Kiyahudi, wakati ambapo Makuhani wa Kiyahudi walikuwa wanalielekea Hekalu la Yerusalemu wakati wa mchana ili kutolea dhabihu kwa ajili ya dhambi za watu wao. Yesu sasa ni Kuhani Mkuu kwa mfano wa Melkisedeki. Kwa damu yake sisi tunapata msamaha wa dhambi na uhuru kamili kama Mtupe Petro anavyosema; “Mlikombolewa si kwa vitu vinavyoharibika kama vile dhahabu na fedha, bali kwa damu ya thamani kubwa ya mwanakondoo asiye na ila wala waa, yaani Yesu Kristo (1Pet 1:18-19).
Kazi hii ya ukombozi inaendelezwa na Kanisa kwa njia ya utangazaji wa Neno la Mungu, Sala, na Maadhimisho ya Sakramenti hasa Ubatizo, Upatanisho na Ekaristi Takatifu. Msamaha huu ni kwa wote ambao wako tayari kuupokea. Kila mkristo kwa njia ya ubatizo amepokea wajibu wa kuwa nuru kwa mataifa kwa kuendelea kuuambia ulimwnegu na wale waliolemewa na dhambi kuwa; “Yesu ndiye mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu”. Ili tufanikiwe katika hili lazima tuwe watu wakweli na kuwaonyesha watu ukweli. Tunaishi katika ulimwengu ambao utamaduni wa taarifa za uongo ndizo zinazosambaa na kuenea kwa haraka kuliko ukweli. Ili tuwe kweli nuru kwa ulimwengu, tunapaswa kuwaonyesha watu ukweli ni upi katika mambo ya Imani na katika maadili. Tunaitwa na kutumwa kuwafundisha watu ukweli na kuusimamia ukweli. Gharama ya kuwa Nuru ni kuishi maisha ya mfano ili watu wayaone matendo yetu mema. Matendo yetu yawe mfano kwa wengine ili yawavutie kwa Kristo. Ili tuwe mfano lazima kiwango cha utakatifu wetu kiwe juu zaidi. “Utakatifu wenu usipozidi ule wa Mafarisayo na Waaandishi hamwezi kuingia katika ufalme wa Mungu” (Mt 5:20). Utakatifu wetu lazima uwe wa juu tuweze kuwa kweli Nuru ya ulimwengu.
Ndivyo maana Yesu anasema; “watu hawawashi taa na kuiweka ndani ya pishi bali juu ya kiango ili iwaangazie wote waliomo ndani” (Mt 5:15). Kwa ubatizo tumewekwa juu ya kiango. Watu wakituambia; “Shuka chini nasi tutakuamini” (Mt. 15:32), usishuke maana Mungu anasema; “Nimekuweka uwe Nuru kwa Mataifa”. Nuru yetu inatoka kwa Kristo aliye juu ya yote. Hivyo tunapaswa kuwa watii kwa sauti yake kuwa wasikivu kama Mzaburi katika wimbo wa katikati anavyosema; “Maskio yangu umeyazibua katika gombo la chuo nimeandikiwa kuyafanya mapenzi yako. Sheria yako imo moyoni mwangu. Ndipo niliposema, Tazama nimekuja kuyafanya mapenzi yako” (Zab. 1, 3, 6-9, (K) 7, 8). Katika kumshuhudia Kristo na kuwa mwanga lazima tutapata upinzani. “Nuru imekuja ulimwenguni lakini watu wamependa giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao yalikuwa maovu. Kila atenaye maovu huogopa mwanga ili matendo yake maovu yasije yakaonekana wazi” (Yn 3:19). Tukumbuke maneno ya wahenga kuwa kama watu wanakubaliana na sisi kwa kila kitu tujue kuwa ama wamekuwa watakatifu kama sisi au sisi tumefanana nao. Basi tumwombe Mungu Mkuu na Mtukufu aangaze giza la mioyo yetu. Atujalie Imani sahihi, Matumaini thabiti, Mapendo kamili, Busara na Ufahamu, ili tutimize agizo lake takatifu na la kweli ili tuupate wokovu wa milele kama anavyosali Padre katika Sala ya kuombea dhabihu akisema; “Ee Bwana, tunakuomba utujalie kuadhimisha vema mafumbo haya, kwa maana kila tunapoadhimisha ukumbusho wa sadaka hii, kazi ya ukombozi wetu inatendeka."