Tafakari Dominika ya Pili Kipindi cha Mwaka A: Wito wa Utakatifu wa Maisha ni Kwa Wote
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican popote pale ulipo, wakati huu tunapotafakari kwa pamoja Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Pili ya Kipindi cha mwaka AQ wa Kanisa. Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana ni tukio ambalo lilifunua haki ya Mungu inayokita mizizi yake katika huruma, upendo na wokovu wa watu wote. Kwa njia ya Ubatizo, Kristo Yesu anafunua utume wake unaowahamasisha watu wa Mungu kuwa ni vyombo vya huruma, upendo na haki. Mwinjili Mathayo 3: 1-17 anaelezea Ubatizo uletao toba na maondoleo ya dhambi. Hili ni tukio ambalo limetufungulia lango la safari ya maadhimisho ya Dominika 34 za Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, fursa ya kumfahamu taratibu Kristo Yesu kama Mwanakondoo wa Mungu, Kanisa linaloundwa na watakatifu wa Mungu na wadhambi wanaopaswa kutubu na kumwongokea Mungu. Ni fursa ya kung’amua utambulisho wetu kama Kanisa la Kisinodi linalohamasishwa kujenga utamaduni wa kusikiliza na kufanya mang’amuzi kwa pamoja, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, tukitambua kwamba, utume na umisionari wetu unapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo, ambamo tunashirikishwa: Ufalme, Ukuhani na Unabii wa Kristo.
Mama Kanisa katika busara yake, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa anatuwekea mbele ya macho yetu ya imani Yohane Mbatizaji kama anavyosimuliwa na Mwinjili Yn 1: 29-34 anaye mtambulisha Kristo Yesu kuwa ni “Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu. Kristo Yesu ndiye aliyeshuhudiwa na Roho Mtakatifu akishuka kama Hua na kukaa juu yake. Huyu ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu. Itakumbukwa kwamba, Yohane Mwinjili, ni yule mwanafunzi aliyependwa na Kristo Yesu, mwenye kumbukumbu hai ya wito na utume wake, anakaza kusema ameona tena anashuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu. Kristo Yesu ndiye aliyekamilisha utabiri wa Mpango wa Ukombozi ambao Mwenyezi Mungu aliupanga tangu milele yote, kama anavyosimulia Nabii Isaya 49: 3; 5-6. Mzaburi anakaza kusema, “Tazama nimekuja, kufanya mapenzi yako. Kristo Yesu ndiye yule Mtumishi wa Mungu anayesimuliwa kwenye Agano la Kale na kwa namna ya pekee na Nabii Isaya 49: 3, 5-6. Ndiye Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake uletao wokovu. Kristo Yesu alikuja kufunua wokovu wa Mungu kwa watu wa Mataifa kwa njia ya: unyenyekevu na roho ya kujihinisha “Abnegationem.”
Huyu ndiye yule Mtumishi aliyetumwa na Baba Milele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kuwaganga na kuwaponya wale waliovuka na kupondeka moyo. Yote haya yanafumbatwa katika Fumbo la Msalaba, kama sehemu ya utekelezaji wa mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wake. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kwa njia ya Ubatizo, wanashiriki pia katika utume wa Kristo Yesu, yaani wanashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu. Mwinjili Yohane anamshuhudia Kristo Yesu kuwa ndiye yule Mtumishi Mwaminifu na Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu. Mama Kanisa amemtambua Kristo Yesu kuwa ndiye Mtumishi wa Mwaminifu wa Mungu, Masiha na Mkombozi wa Ulimwengu; Fukara, mtii na mwaminifu; mwingi wa huruma na mapendo, kiasi hata cha kukubali, kuteswa, kufa na hatimaye kufufuka kwa wafu. Kwa ufupi kabisa, Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa inatupatia muhtsari wa imani ya Kanisa na utimilifu wa unabii katika Kristo yesu, Mtumishi wa Mungu na Mwanakondoo wa Mungu.
Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa katika Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho 1: 1-3, anawakumbusha Wakristo kwamba, kwa njia mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, wametakaswa, wanaitwa wawe watakatifu pamoja na waamini wenzao. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, waamini wote ndani ya Kanisa wanapaswa kuwa ni Watakatifu, kwa sababu Kristo Yesu ndiye chanzo na hatima ya utakatifu wote. Rej. Mt 5: 48; LG 40. Imani, matumaini na mapendo ni nyenzo muhimu katika kuambata utakatifu wa maisha. Wakristo ni matunda ya upendo wa Mungu na kwa kulipokea pendo lake, wamepewa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu. Wakristo wametakatifuzwa kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kumbe, huu ni wito na utume wa wafuasi wote wa Kristo Yesu. Ushirika wa Watakatifu “Sanctorum communio” ni sehemu ya kiri ya imani ya Kanisa kwa kutambua ushirika wa mema ndani ya Kanisa kunakofanyika kwa njia ya Sakramenti za Kanisa pamoja na kuchota katika hazina ya pamoja. Huu ni ushirika wa mambo matakatifu na ushirika kati ya watakatifu. Ni ushirika wa imani, Sakramenti za Kanisa, Karama katika mchakato wa ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Ni ushirika wa upendo unaosimikwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Ibada ya Kanisa kwa watakatifu wa Mungu, au visakramenti na hasa zaidi kwa Bikira Maria, ni kwamba, imani ya Kanisa inawaelekeza waamini kujenga na kudumisha uhusiano mwema na Kristo Yesu unaofumbatwa katika kiungo cha ushirika wa watakatifu. KKK 946-962.
Huu pia ni mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni kiini cha historia nzima ya wokovu. Kanisa linawafundisha watoto wake kutambua uwepo wa dhambi na umuhimu wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha. Kanisa linakumbatia wakosefu ndani mwake, lakini linahitaji pia kutubu, kutakaswa na kuendelea na mchakato wa kujipyaisha, tayari kutangaza na kushuhudia Ukuu wa Fumbo la Msalaba, utambulisho wa Mtumishi wa Mungu, Masiha na Mkombozi wa Ulimwengu. Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, ni fursa ya kumfahamu taratibu Kristo Yesu kama Mwanakondoo wa Mungu, Kanisa linaloundwa na watakatifu wa Mungu na wadhambi wanaopaswa kutubu na kumwongokea Mungu. Kumbe, Kipindi cha Mwaka wa Kanisa ni fursa ya kung’amua utambulisho wetu kama Kanisa la Kisinodi linalohamasishwa kujenga utamaduni wa kusikiliza na kufanya mang’amuzi kwa pamoja, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, tukitambua kwamba, utume na umisionari wetu unapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo.