Tafuta

Watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Musoma katika kipindi hiki cha Kwaresima wekezeni zaidi katika toba na wongofu wa ndani ili mpate neema, baraka na utakatifu wa maisha. Watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Musoma katika kipindi hiki cha Kwaresima wekezeni zaidi katika toba na wongofu wa ndani ili mpate neema, baraka na utakatifu wa maisha.  (Vatican Media)

Askofu Msonganzila: Wekezeni Katika Toba Ili Mvune Neema, Baraka na Utakatifu

Askofu Msonganzila: kipindi hiki cha Kwaresima wekezeni zaidi katika toba na wongofu wa ndani, ili kuvuna neema, baraka na utakatifu. Askofu Msonganzila amewahimiza waamini kuwekeza katika: Sala binafsi na zile za kijumuiya; toba na wongofu wa ndani; kujisadaka bila ya kujibakiza katika kumwilisha Injili ya upendo na huduma kwa jirani, hasa wale wenye mahitaji maalum.

Na Daniel Benno Msangya, - Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Toba ya Kwaresima na Mchakato wa Sinodi.” Ni ujumbe unaochota amana na utajiri wake kutoka katika tukio la Kristo Yesu kugeuka sura mbele ya wanafunzi wake Petro, Yakobo na Yohane nduguye, baada ya kuwa ametangaza Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, jambo ambalo lilionekana kuwa ni kashfa kwa Mtume Petro, kiasi cha kuambiwa na Kristo Yesu, alikuwa ni Shetani, kikwazo kwake kwani alikuwa hawazi yaliyo ya Mungu bali ya wanadamu. Rej Mt 16:23. Kipindi hiki cha Kwaresima, anasema Baba Mtakatifu ni mwaliko wa kupanda juu Mlimani ili kupata mang’amuzi ya maisha ya kiroho, ili kuzama zaidi katika Fumbo la maisha ya Kristo Yesu kama utimilifu wa Sheria na Unabii. Ni mwaliko wa kumsikiliza Kristo Yesu kwa umakini mkubwa kama mtindo wa maisha ya Kanisa la Kisinodi. Waamini wapambane na changamoto za maisha na utume wao kwa ari, ujasiri na moyo mkuu, ili kwamba, Fumbo la Msalaba liwasaidie kukuza imani, matumaini na mapendo, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa Kanisa la Kisinodi.

Waamini wekezeni katika sala mpate neema na baraka
Waamini wekezeni katika sala mpate neema na baraka

Itakumbukwa kwamba, kauli mbiu inayonogesha ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2023 ni "Tunawaombea Mjaliwe Kufanywa Imara Katika Utu..." Efe 3: 16. Ujumbe unachota utajiri kutoka katika Neno la Mungu, Mafundisho ya Kanisa juu ya Utu, Uundwaji wake, Kufanywa imara katika utu; Na jinsi ya kuuvua utu wa kale: Neno la Mungu, Sala na Toba. Ni katika muktadha huu, Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania, katika maadhimisho ya Jumatano ya Majivu kwa Mwaka 2023, yaliyoadhimishwa kwenye Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mungu, Kanisa kuu amewaalika watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Musoma katika kipindi hiki cha Kwaresima kuwekeza zaidi katika toba na wongofu wa ndani, ili hatimaye, waweze kuvuna neema, baraka na utakatifu wa maisha. Askofu Msonganzila amewahimiza waamini kuwekeza katika: Sala binafsi na zile za kijumuiya; toba na wongofu wa ndani; kujisadaka bila ya kujibakiza katika kumwilisha Injili ya upendo na huduma kwa jirani, hasa wale wenye mahitaji maalum yaani: watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; wagonjwa na walemavu; wazee na wajane, bila kusahau wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Wekezeni katika matendo ya huruma,chemchemi ya utakatifu
Wekezeni katika matendo ya huruma,chemchemi ya utakatifu

Huu ndio wakati uliokubalika, ni wakati wa wokovu. Waamini wahakikishe kwamba, wanaongeza ubora na tija katika maisha na vipaumbele vyao, ili kweli Kipindi cha Siku 40 cha Mfungo wa Kwaresima kiweze kuwaletea baraka, neema na utakatifu wa maisha. Askofu Michael George Mabuga Msonganzila ametumia fursa hii, kukemea chachu ya ubaya wa moyo na maovu inayoongezeka siku kwa siku. Matukio ya ujambazi, uporaji kwa kutumia nguvu, ubakaji na mauaji, ni ishara ya kuongezeka kwa utamaduni wa kifo unaopekenya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Haya ni matukio ambayo kamwe hayawezi kufumbiwa macho, yanapaswa kushughulikiwa kikamilifu ili haki iweze kutendeka na amani kutamalaki katika maisha ya watu. Inasikitika kuona kwamba, jamii bado inaendekeza mfume dume, ukatili na nyanyaso dhidi ya wanawake na watoto. Umefika wakati kwa jamii kuwekeza kikamilifu katika Injili ya upendo ndani ya familia. Kwaresima ni muda muafaka wa kujipatanisha na Mungu, jirani pamoja na mazingira kwa njia ya toba ya kiikolojia, sala, matendo ya huruma: kimwili na kiroho, ili mwisho wa safari ya kiroho jangwani katika nyoyo zao, Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia: neema, baraka na utakatifu wa maisha.

Jimbo la Musoma
24 February 2023, 16:14