Jumatano ya Majivu Mwaka A wa Kanisa: Tubuni na Kuiamini Injili
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Lliturujia ya Neno la Mungu, Jumatano ya Majivu, siku ya kwanza ya kipidi cha kwaresma. Ni kipindi cha siku arobaini za vita vya kiroho inayosimikwa katika sala, kufunga, kutafakari Neno la Mungu na kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa upendo kwa matendo ya huruma kama inavyoashiria sala ya Koleta ikisema; «Ee Bwana, utujalie sisi waamini wako tuanze vita vya roho kwa mfungo mtakatifu. Nasi tulio tayari kupigana na pepo wabaya tujipatie nguvu kwa sababu ya kufunga». Ni kipindi cha toba kama wimbo wa mwanzo unavyotualika ukisema; «Ee Bwana, wewe wavipenda vitu vyote vilivyopo, wala hukichukii kitu cho chote ulichokiumba. Unawasamehe watu dhambi zao kwa ajili ya kufanya kitubio na kuwahurumia kwa kuwa ndiwe Bwana Mungu wetu» (Hek. 11:24-25, 27). Ni safari ya kiroho ambayo kilele chake ni adhimisho la fumbo la ukombozi wetu - mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo – Pasaka kama inavyoashiria sala ya kubariki majivu tunayopakwa kama alama na ishara ya kukubali kuwa tu wadhambi wanaofanya toba inavyosema; «Ee Mungu, unayependezwa na unyenyekevu na kutulizwa na kitubio chetu, usikilize kwa wema sala zetu. Uwashushie kwa rehema baraka yako watumishi wako watakaopakwa majivu haya; ili baada ya kutimiza wajibu wa Kwaresima waje waliadhimishe fumbo la Pasaka la Mwanao, wakiwa wametakata rohoni».
Nayo sala ya kuombea dhabihu inasema; «Ee Bwana, tunatoa sadaka hii ya kuanzia Kwaresima, na kukuomba tuzishinde tamaa mbaya kwa matendo ya kitubio na mapendo. Nasi tukisha takaswa dhambi, tuwe na ibada ya kuadhimisha mateso yake Mwanao». Kabla ya kuzama katika tafakari ya masomo ni vyema kuchukua tahadhani. Kuna uwezekano wa kufikiri na kudhani kuwa hakuna jipya katika kipindi hiki na kipindi cha mwaka wa kiliturujia uliopita. Tukumbuke kuwa kila adhimisho la tukio lolote la kiliturujia katika historia ya wokovu wa mwanadamu linapoadhimishwa katika mzunguko wa mwaka wa liturujia wa Kanisa lina hali mbili kwanza : kutukumbusha yaliyotokea katika historia ya ukombozi wetu na pili kuhuisha na kupyaisha maisha yetu ya kiroho katika kumfusa Kristo. Kumbe kila mwaka wa kiliturujia ni mpya na wa pekee na hakuna unaofanana na mwingine, maana kila mwaka unapyaisha na kuhuisha maisha yetu ya kiroho na hivyo kutuleta karibu zaidi kwa Mungu. Daima tukumbuke kuwa matukio yote ya kiliturujia tunayoadhimisha zaidi ya kutukumbusha yaliyotokea zamani, yanafanya sehemu ya maisha yetu na yanatufanya tuonje upendo wa Mungu katika mafumbo yanayoadhimishwa katika kila hatua ya maisha yetu hapa duniani tunapoelekea maisha ya umilele huko mbinguni.
Kumbe tusikianze kipindi hiki kwa mazoea kana kwamba hakuna jipya lolote bali kwa moyo wa usikivu tufungue macho na masikio ya mioyo yetu tuweze kujichotea neema na baraka zitokanazo na kipindi hiki kwa njia ya Yesu Kristo Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Yoeli (2:12-18). Katika somo hili Mungu kwa kinywa cha Nabii Yoeli anatuita tumrudie Yeye kwa mioyo yetu yote, kwa kufunga na kwa kulia na kwa kuomboleza. Tunaambiwa tuirarue mioyo yetu, na siyo mavazi yetu. Katika siku za Agano la Kale, watu walikuwa na desturi ya kurarua mavazi yao kama ishara ya kufanya toba. Hata hivyo, walikuwepo wengine walioyararua mavazi yao kama ishara tu ya nje, lakini ndani ya mioyo yao hawakuwa na toba ya kweli. Mioyo yao ya “jiwe” haikubadilika, walibaki kama walivyokuwa tangu awali. Nabii Yoeli, anatuita kumrudia Mungu sio kama mtu mmoja mmoja tu, bali ni wito pia kwa watu wote, wazee vijana na watoto. Ni mwaliko wetu sote kufanya toba ya kweli na kumrudia Mungu. Somo la pili ni la Waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (2Kor 5:20-6:2). Katika somo hili Mtume Paulo anatusihi tupatanishwe na Mungu kwa njia ya Kristo Mwana pekee wa Mungu ambaye Mungu mwenyewe alimtuma aje kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi. Mungu asiyejua dhambi alimfanya Yesu kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye (2Kor 5:21). Yesu Kristo hakujua dhambi, lakini alifanywa kuwa dhambi ili sisi tusio haki tufanywe kuwa haki katika Yeye. Sisi wadhambi tulistahili kifo hiki cha kutisha, kifo alichokufa Yesu kutokana na Upendo wa Mungu ili sisi tusamehewe.
Injili ni ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 6:1-6;16-18). Katika Injili hii tunapata mafundisho ya Yesu ya namna tunavyopaswa kukiishi kipindi hiki cha Kwaresima. Yesu anatuonya tusiwe wanafiki, tusifanye matendo mema ili tuonekane machoni pa watu wengine, kwani kwa kufanya hivyo tunakuwa tumepokea thawabu yetu kwa njia ya watu wanaotutazama, kutustaajabia, na kutusifia. Kumbe, matendo yetu mema yasilenge kujionesha kwa watu wengine, bali yawe ni mawasiliano binafsi kati yetu na Mungu yaani kujenga muungano na Mungu wetu aliyemtakatifu kwa sala, sadaka na kufunga. Siku ya kwanza ya Kwaresima inapambwa na tendo la kiroho la kupakwa majivu katika paji la uso. Tendo hili ni ishara ya kukubali kuwa tu wa dhambi tunahitaji kufanya toba ili tusamehewe. Ndiyo sala ya kubariki majivu ya matawi yaliyobarikiwa mwaka uliotangulia katika dominika ya matawi na nyimbo zinazoimbwa wakati wa kupakwa majivu, vyote vinatualika kufanya toba. Moja ya sala inasema; “Ee Mungu, wewe hupendi wakosefu wapotee bali wageuke. Usikilize sala zetu, upende kuyabariki kwa rehema yako, majivu haya tunayotaka kupakwa kichwani. Kwa hiyo sisi tujuao kwamba tumetoka mavumbini, tufanye bidii ya kufunga Kwaresima, tujaliwe kupata maondoleo ya dhambi zetu na uzima mpya, tuweze kufanana na Mwanao aliyefufuka.
Na baadhi ya antifona za nyimbo zinasema; “Tugeuze mwenendo wetu kwa majivu na gunia, tufunge na kulia mbele ya Bwana kwa maana Mungu wetu ni mwingi wa rehema, naye hutusamehe dhambi zetu” (Yoe. 2:13). Ee Bwana, unitakase dhambi zangu. Ee Mungu, unirehemu (Zab 51:2). “Tugeuze mwendo wetu, tufanye vema zaidi mambo tuliyokosa kwa ujinga, isije ikawa tunapotafuta nafasi ya kutubu tusiweze kuipata, tukafikiwa ghafla na siku ya kufa. Sikia, ee Bwana, uturehemu sisi kwa kuwa tumetenda dhambi mbele yako” (Bar. 3:2). Tendo hili la kupakwa majivu katika paji la uso linaambatana na ujumbe unaosema; “Tubuni na kuiamini Injili” (Mk. 1:15) au “Mwanadamu kumbuka kuwa wewe u mavumbi na mavumbini utarudi” (Mw. 3:19). Majivu hutukumbusha kwamba sisi ni viumbe duni na dhaifu kimwili na kwamba maisha yetu ni mafupi. Majivu yanatukumbusha kuwa kila binadamu atakufa na kusahaulika katika uso wa dunia. Mbele ya kifo sote tuko sawa; wafalme, wasomi na matajiri, maskini, vilema na punguani, mbele ya mauti, wote ni sawa. Mungu ndiye mwenye mamlaka juu pumzi ya wote. Mifupa ya watu wote ndani ya kaburi ni sawa.
Majivu hutukumbusha udhaifu wetu kiroho. Hakuna binadamu asiye mdhambi. “Tukisema kwamba hatuna dhambi twajidanganya wenyewe na wala kweli haimo ndani mwetu. Lakini tukiziungama dhambi zetu, Mungu ni mwaminifu, tena mwadilifu na wa haki, hata atatusamehe dhambi na kututakasa na kutusafisha na udhalimu wote” (1Yn 1:8-10). Kumbe, sote tunahitaji kufanya toba. Ndiyo maana mwanzoni mwa kipindi hiki cha Kwaresma, Mama Kanisa anatuhimiza kuchunguza dhamiri zetu ili tujue hali yetu ya kiroho ikoje. Hili ni sharti muhimu la uponywaji wa ndani. Ndiyo maana majivu tunayopwakwa ni ishara ya matumaini na mwaliko wa kuanza maisha mapya yanayompeza Mungu. Kanisa haliishii katika maneno - “mwanadamu kumbuka kwamba u-mavumbi na mavumbini utarudi” (Mw. 3:19) bali linaendelea kutukumbusha kwamba - “Tubuni na kuiamini Injili” (Mk. 1:15). Ni mwaliko wa kuachana na maisha ya kale – maisha ya dhambi na kuanza maisha mapya ya kiroho yenye furaha, amani na utulivu.
Kumbe, ili tuweze kukiishi vyema kipindi hiki na kupata matunda yake, hatuna budi kutenga muda wa sala, kufanya toba na malipizi, kujikatalia furaha za kimwili, kuwasaidia na kuwatendea kwa ukarimu na upendo watu walio wahitaji. Matendo haya ni dawa za kutuponya na ugonjwa wa ukiro –ukosefu wa kinga ya rohoni – dhambi. Tunapaswa kuonyana na kusaidiana kidugu. Ukimwona ndugu yako anaanguka dhambini msaidie aikwepe dhambi. Tuishinde dhambi kwa wema. Basi, kipindi hiki cha kwaresma kiwe ni kipindi cha kurekebisha mahusiano yaliyojeruhiwa: Mahusiano yetu na Mungu, mahusiano na nafsi zetu, na jirani yetu na viumbe viumbe vingine pia. Tumwombe Mwenyezi Mungu, ili kwa neema zake, mfungo wetu uweze kutusaidia zaidi kushindana na kila hali inayotuzuia kutekeleza mapenzi Yake kwa kuzaa matunda mema kwa wakati kama wimbo wa Komunio unavyosema; “Mwenye kuitafakari sheria ya Bwana mchana na usiku, atazaa matunda yake kwa majira yake” (Zab. 1:2-3). Na Sala baada ya Komunyo inahitimisha ikisema; “Ee Bwana, sakramenti tulizopokea zituletee shime yako, ili kufunga kwetu kukupendeze, kutupatie nasi dawa ya kutuponya”. Nawatakieni nyote mwanzo mwema wa kipindi cha Kwaresima. Tumsifu Yesu Kristo.