Kard.Hollerich ameomba kuachiliwa kwa Askofu Rolando na wafungwa wengine huko Nicaragua
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Rais wa Baraza la Maaskofu barani Ulaya (COMECE), Kadinali Jean-Claude Hollerich sj., anaonesha mshikamano wa Maaskofu wa Umoja wa Ulaya kwa Kanisa Katoliki la Nicaragua ambalo linakabiliwa na dhiki kubwa kutokana na mateso ya Serikali. Kardinali Hollerich ameomba aachiliwe Askofu Rolando Álvarez na wafungwa wengine”. Katika barua iliyotumwa kwa Askofu Carlos Enrique Herrera Gutiérrez, OFM, Rais wa Baraza la Maaskofu wa Nicaragua, Jumatatu tarehe 6 Februari 2023, Kardinali Jean-Claude Hollerich anaelezea ukaribu na mshikamano wa Maaskofu wa Umoja wa Ulaya kwa ajili ya wakatihuo mgumu unaokabili Kanisa Katoliki mahalia kwa sababu ya mateso ya kimfumo yanayofanywa na mamlaka za umma.
Askofu, makuhani na waamini walioshitakiwa kwa uongo
Tangu mnamo mwezi Agosti 2022, Askofu Rolando Álvarez na baadhi ya makasisi na waamini nchini Nicaragua wako kizuizini na kwa sasa wako chini ya mashtaka ya jinai. Kwa maana hiyo Kardinali Hollerich alitoa wito kwa mamlaka ya kitaifa ya Nicaragua kumwachilia mara moja Askofu Rolando Álvarez na wafungwa wengine, walioshtakiwa kwa uwongo kuwa walikula njama dhidi ya uadilifu wa kitaifa na kusambaza habari za uongo.
Kujitola kwa COMECE kuhusu uhuru,demokrasia na haki,Nicaragua
“Tunafuatilia kwa ukaribu maendeleo ya hali ya Nicaragua, inayooneshwa na mnyanyaso wa Kanisa Katoliki na waamini wake. Katika barua yao imebainisha “Maaskofu wa COMECE tunajitolea kukuza uhuru, demokrasia na haki nchini Nicaragua kupitia mazungumzo yetu ya kawaida na wawakilishi wa taasisi za Umoja wa Ulaya (EU)”. Mnamo 2022, serikali ya kitaifa ilimfukuza Balozi wa Kitume Askofu Mkuu Waldemar Stanislaw Sommertag na watawa 18 wa Shirika la Wamisionari wa Upendo. Pia iliwafunga makasisi saba na washirika wawili katika jimbo la Matagalpa, na vile vile ilifunga vituo tisa vya radio katoliki, ikaondoa chaneli tatu za Kikatoliki kutoka katika vipindi vya televisheni vya kujiandikisha na kuzuia maandamano na mahujaji.