Kwaresima Ni Kipindi cha Kupanda Mlimani Tabor, Mchakato wa Kisinodi
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Jumatano ya majivu ni mwanzo wa kipindi cha neema, ni safari ya kupanda mlima Tabor pamoja na Yesu, ndio Kwaresima ya Kisinodi. Tunaalikwa kufunga siku hii ambapo kila mmoja anapakwa majivu kwenye paji la uso na kukumbushwa kufanya toba, pia kuwa tu mavumbi na mavumbini tutarudi, ni kukumbushwa juu ya kifo chetu na hivyo mwaliko wa kufanya toba ya kweli na kubadili maisha yetu kwa dhati. Ibada ya Jumatano ya majivu ni mwaliko wa kufanya toba ya kweli, si tu leo bali siku zote za maisha yetu. Ibada ya Jumatano ya majivu katika Kanisa la karne za mwanzo ilitumika kuwa ndio Ibada ya kujipatanisha na Mungu. Hivyo waamini tofauti na sasa waliungama dhambi zao hadharani kwa kupakwa majivu, na walisafiri na roho ya toba mpaka Alhamisi Kuu asubuhi ambapo ndio walipokea msamaha wa dhambi na adhabu zitokanazo. Hivyo, katika karne za baadaye Ibada hii ikabadilika mtindo wake na kubaki kuwa wazi kwa Kanisa zima kupakwa majivu na ndio mwanzo wa safari ya siku zile arobaini za toba na kujipatanisha na Mungu. Majivu katika Maandiko Matakatifu yana maana kuu mbili, kwanza kuonesha udhaifu na uduni wetu. Na pili ndio ishara ya nje ya kuonesha moyo wa toba na wongofu wa ndani na kutaka kubadili maisha yetu kwa kumwelekea Mungu. Na ndio utaona hata leo Jumatano ya Majivu imebaki kutunza maana zote mbili, kutukumbusha kuwa sisi ni mavumbi, na pia kutualika kutubu na kuamini Injili.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Kwaresima mwaka huu wa 2023, anatualika kutafakari tukio lile la Yesu kupanda juu mlimani Tabor na kung’ara sura akiwa pamoja na Mitume wale watatu, Simon Petro, Yakobo na Yohane. Ni tukio tunalokutana nalo katika Injili zote pacha, yaani Mathayo, Marko na Luka. Kwaresima anatukumbusha Baba Mtakatifu kuwa ni tukio la kupanda mlimani, na pia ni tukio la Kisinodi. Yesu anapanda mlimani pamoja na wafuasi au mitume wale watatu. Ndio kusema ni kipindi cha kupanda mlimani, ndio kuachana na kujitenga na mantiki za dunia hii. Ni kusafiri pamoja na Yesu, ni kipindi cha Kisinodi, na mwaliko ni kupanda na kusafiri sio peke yetu bali pamoja na Yeye aliye Njia (Odos), ambaye ndiye Yesu Kristo mwenyewe. Kusafiri na kupanda mlimani ni jukumu zito na lenye madai, hivyo daima tunahitaji neema za msaada katika kulitekeleza hilo. Safari ya kisinodi inahitaji daima neema za Mungu mwenyewe ili kwazo sote tuweze kutoka na kujitenga na mantiki ile ya dunia ili kwa pamoja tupande juu mlimani pamoja na Yesu Kristo na huko tuweze kuivaa mantiki ile ya Mungu. Yesu anajitenga na kupanda mlimani pamoja na wanafunzi wale watatu, baada ya Simon Petro kukiri kuwa ni Kristo lakini kushindwa kupokea fundisho juu ya mateso na kifo chake Yesu Kristo.
Hivyo ni mwaliko si tu kwa Simon Petro bali hata nasi kwetu leo. Kupanda mlimani ni kukubali kupokea katekesi juu ya fumbo la mateso, kifo na ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Ni fumbo ambalo kulikubali na kulipokea hatuna budi kuachana na mantiki za dunia hii na hivyo kusafiri na kupanda mlimani pamoja na Yesu kwa siku hizi arobaini. Kubaki chini ni kuendelea kama Simon Petro kuwaza na kuenenda kadiri ya mantiki ya dunia hii, ambayo ni kinyume na mapenzi ya Mungu. (Mathayo 17:1) Sehemu hii ya Injili ya Kugeuka sura Yesu tunaitafakari kila Dominika ya pili ya Kwaresima. Ndio kusema Yesu anatualika nasi kujitenga na kupanda mlimani pamoja naye. Pamoja na kuwa mtindo na ratiba za maisha yetu yanaendelea kama kawaida, lakini Kwaresma ni mwaliko wa kujitenga na kupanda mlimani pamoja na Yesu Kristo. Ni kipindi cha neema, cha kupanda mlimani pamoja na Taifa zima la Mungu na huko tuweze kwa pamoja kujifunza mapenzi ya Mungu katika maisha yetu. Yesu ndiye Njia, hivyo kupanda mlimani ni kufanya mang’amuzi ya pamoja, ndio safari ile ya Kisinodi. Hivyo, safari ya Kisinodi si nyingine bali ni ile ya kupanda mlimani pamoja naye aliye Njia yetu, yaani Yesu Kristo, na huko kupata nafasi ya kumtafakari na kumjifunza zaidi Yeye aliye kichwa cha Kanisa. Ni mwaliko kama mitume kupanda pamoja naye juu mlimani ili huko tuweze kulitafakari pamoja naye fumbo Kristo, yaani mateso, kifo na ufufuko wake.
Pamoja na madai na ugumu wa kupanda mlimani, tunaona wanapofika kileleni wanafurahi kuonja na kuuona utukufu wa Mwana wa Mungu alipogeuka sura yake mbele yao. Ni sawa na safari ngumu na yenye madai ya kupanda mlima, daima tunapofika kileleni tunajawa na furaha ya kuweza kuona uwanda mpana na mzuri. (Panorama) Hivyo hivyo anasema Baba Mtakatifu Francisko kuwa safari ya Kisinodi ni sawa na kupanda mlima, hivyo ni safari ngumu na yenye kututaka kufanya sadaka kubwa, lakini furaha yetu ni pale tutakapofika kileleni kwa pamoja kuuona uzuri wa uwanda mpana zaidi. Safari ya Kisinodi inahitimishwa na kufika kileleni, ambako tutajawa na furaha yenye mshangao wa kuuona na kuuonja utukufu wa Mungu. Ni pale juu kileleni, hapo tunaweza kuona uwanda mpanda zaidi ambao sio rahisi kuuona tukiwa chini kwenye nchi ya tambarare. Kuonja mantiki ya Mungu lazima nasi tukubali kufanya safari ile ya Kisinodi ya kupanda mlimani si peke yetu bali pembeni yetu akiwepo Yesu Kristo mwenyewe. Safari ya Kwaresima ina malengo makuu mawili kama safari ile ya kupanda mlima Tabor, ndio kufanya mageuzi mawili, yaani ya mtu binafsi na pia kama Kanisa. Hilo linawezekana tu kwa njia ya Yesu Kristo mwenyewe, ndio njia ya kushiriki na kulitafakari fumbo Kristo, la mateso, kifo na ufufuko wake Yesu. Ili nasi tuweze kugeuka sura, yaani kubadili namna zetu za kufikiri na kutenda, Baba Mtakatifu anatualika kutafakari mambo makuu mawili katika safari hii ya kupanda mlimani, yaani safari ya Kwaresima ya Kisinodi. Katika tukio lile la Yesu kugeuka sura mlimani, tunaona Mungu anatoa maagizo mawili.
Mosi, huyu ndiye Mwana wangu msikilizeni Yeye. (Mathayo 17:5) Hivyo, ili nasi tuweze kufanya mabadiliko ya kweli kwa mtu binafsi na pia kama Kanisa hatuna budi kumsikiliza Mwana wa Mungu. Na hasa kwa kusikiliza Neno la Mungu. Kulisoma, kulitafakari na kuliweka katika maisha yetu Neno la Mungu. Baba Mtakatifu anatusisitiza pamoja na kumsikiliza Mungu hatuna budi kujenga utamaduni mzuri wa kusikilizana sisi kwa sisi. Hata baada ya tukio lile mitume wanajawa na hofu na woga kiasi cha kuanguka kifudifudi na kufunika sura zao. Yesu anawasogelea, anawagusa na kuwaalika wasimame na wasiogope. (Mathayo 17:6-8) Hata baada ya mang’amuzi haya makubwa, wanaalikwa kushuka kutoka juu mlimani na kwenda kuwa mashuhuda wa fumbo Kristo. Na ndivyo safari ile ya Kisinodi, kama ya Kwaresma mwishoni tunaalikwa kurudi katika maisha yetu ya siku kwa siku na huko tuweze kuwa mashahidi wa utukufu na ukuu wa Mungu kwa watu wake. Lengo sio kubaki pale juu mlimani, bali kurejea katika maisha ya kawaida tukiwa tayari na zana na tunu zile za kuweza kuishi vema imani yetu. Thawabu tunaona ni “motif”, au wazo linalojirudiarudia mara 7 katika Injili ya leo. Wazo la thawabu lilikuwa ni wazo la msingi kabisa katika imani ya Mafarisayo. Mtu mchamungu aliyeenenda kadiri ya amri na maagizo ya Mungu, basi huyo alijiwekea thawabu zake mbele ya Mungu na hivyo kubarikiwa na kinyume chake basi alipokea laana na kila aina ya ubaya iwe hapa duniani na maisha ya baadaye. Naomba nirudie kusema hili fundisho la Mungu anayelaani ni kufuru kabisa na hivyo halipaswi kuwepo kati yetu waamini Wakristo.
Thawabu anayotuambia Yesu leo katika Injili sio malipo bali ni katika kujaliwa uwezo wa kusafiri na kupanda naye mlimani na huko kujaliwa kugeuza namna zetu za kufikiri na kuenenda. Hivyo zawadi yetu, ni furaha katika kupenda kama Mungu anavyotupenda, kushiriki katika hali yake ya Kimungu na ndio kushirika au kuujenga ufalme wa Mungu hapa duniani. Kwaresima tunaalikwa kufanya mambo makuu matatu lakini katika mwono tofauti na ule wa Mafarisayo yaani: Kusaidia maskini/matendo ya huruma, kusali na kufunga. Kusaidia maskini au matendo ya huruma hakuna budi kusukumwa na upendo wa kweli na haki ndani mwetu na sio kujitafuta na kumdhalilisha au kumshusha muhitaji anayefika kwetu au tunaokutana nao siku kwa siku. Na ndio sadaka ya kweli kama tunavyoona katika lugha ya Kiebrania “tzedakàh” ambayo maana yake sisisi ni iliyo ya haki. Na ndio hata Mtakatifu Ambrosi anaelezea sadaka kwa muhitaji ni kumpa iliyo haki yake. Vyote tulivyo navyo katika ziada hatuna budi kutambua kuwa ni kuwadhulumu wengine wasiokuwa na kitu kabisa. Vyote tulivyonavyo si mali yetu, bali ni mali ya Bwana. (Zaburi 24) Hivyo tunaalikwa kutenda haki na ndio kuwapa wengine mastahili yao. Hivyo katika kusaidia wahitaji sio kwamba nawafanyia upendeleo bali ni kuwashirikisha yale mema ya Mungu tuliyokabidhiwa kuwa waangalizi tu. Yafaa kufanya matendo ya huruma kwa unyenyekevu mkubwa, maana ni kuwashirikisha wengine mema ya Mungu na kamwe si mema yetu!
Kwaresima pia tunaalikwa kuwa ni kipindi cha sala. Ulimwengu wa leo yafaa tukiri kuwa wengi wetu hatujui tena maana ya sala na jinsi ya kusali vizuri. Yesu anatuonya kutopayukapayuka maneno kama wafanyavyo wapagani. Lakini pia tunajiuliza kwa nini tusali wakati Mungu anajua kabla hali yetu na hata mahitaji yetu ya ndani? (Matayo 6:8) Katika nyakati za Yesu kama leo kulikuwa na aina kuu mbili za sala nazo ni sala za jumuiya na zile za binafsi. Sala za jumuiya ndizo zilifanyika hekaluni, katika masinagogi na hata sehemu za wazi na zilifanyika mara mbili kwa siku, yaani saa 3 asubuhi na saa 9 alasiri na mara moja kwa mwaka walitolea sadaka hekaluni kule Yerusalemu kwa kila Myahudi mchamungu. Yesu hapingi taratibu hizi za kusali maana hata naye alisali na alienda Hekaluni ila anawaonya juu ya namna wanavyosali mintarafu thawabu. Wasifanye kwa ajili ya kujionesha au kusifiwa bali ni kujaribu kufanana na Mungu tunayeongea naye katika sala zetu. Nasi lazima kuwa makini na namna yetu na sababu ya kusali, je ni ili nionekane na kusifiwa kuwa mimi ni mtu wa sala au ni muda wa kuwa na Mungu ili niweze kufanana naye zaidi siku kwa siku? Kusali ni kuingia katika mahusiano na Mungu, ni tendo la upendo kwani tunataka kuungana naye! Na upande wa sala binafsi, Yesu anatualika kuingia chumbani, kwa maana katika hali ya kubaki mimi na Mungu wangu tu. Ni kuingia katika mdahalo na huyu anayenijua mimi undani wangu, ni kubaki naye katika mdahalo, si tu wa mimi kuzungumza bali zaidi kumsikiliza. Ni mazungumzo ya masikilizano kwa pande zote mbili yaani Mungu na sisi tulio wanae, ni mdahalo wa upendo na kirafiki, ni moyo unaoongea na moyo mwingine.
Kusali ni mazungumzo yanayojengeka katika mahusiano ya upendo na imani, tunasali kwa kuwa tunakutana na Mungu anayetupenda bila masharti nasi tunasali kwa imani na matumaini. Ni mdahalo na Mungu sio ili kumshawishi ili afanye kadiri ya matakwa yangu mimi na matamanio yangu, bali kukubali mipango ya Mungu katika maisha yangu. Ni kujikabidhi ili neema yake itutie nguvu ya kuenenda kadiri ya mpango wake katika maisha yetu. Ni kujinyenyekeza kwake mzima mzima bila kujibakiza, na hapo inakuwa ni sala ya kweli na sio kutaka yafanyike kadiri yetu na matamanio yetu katika maisha. Ni kukubali kushiriki fumbo la ukombozi yaani mateso, kifo na ufufuko. Na daima tunapokuwa katika safari ya kipindi cha Kwaresma hatuna budi kukumbuka ni kuadhimisha fumbo la Pasaka, ni kubaki na tumaini na faraja ile ya Pasaka. Hivyo sala ni kujiweka wazi mbele ya Mungu, ni kumsikiliza Mungu ili kuweza kujua ni nini mpango wake katika maisha yangu. Na ndio tunaalikwa kuangalia pia mahali ambapo tunaweza kujikusanya kweli na kuweza kuingia katika mazungumzo ya kina na Muumba wetu. Yesu alijua jinsi ya kusali na hata kuchagua mahali ambapo alijitenga na ulimwengu ili aweze kubaki na Baba yake wa Mbinguni. (Marko 1:35; 6:46; Luka 5:16 na 6:12) Sala ya kweli thawabu yake ni kutuunganisha na Mungu ili nasi tuweze kuenenda kadiri ya mpango wake kwetu. Kumbe sala pia inatusaidia kufanana na Mungu. Kusali ni kukubali kupanda mlimani pamoja na Yesu, ni safari ya Kisinodi, pamoja na jumuiya ya Kanisa na tukisafiri pamoja na Yesu mwenyewe.
Kwaresima pia ni kipindi cha kufunga. Kufunga katika dini nyingi inachukuliwa kama aina ya kujitesa na kujinyima na hata wengine kipindi hiki utasikia wakisema wanalala chini bila godoro au wanazima simu zao au mitandao ya kijamii au wanajikatalia kula nyama au kunywa bia au mvinyo au hata soda, na mambo mengi mengine watu wanajikatalia katika kipindi cha Kwaresma. Mazoezi ya namna hii hayana budi kuongozwa na Yesu Kristo mwenyewe, najinyima na kujikatalia ili mwingine anayekuwa muhitaji zaidi yangu aweze kuneemeka. Kufunga chakula kati ya Wayahudi ilikuwa ni kitu cha kawaida na hivyo wachamungu walifunga mara mbili kwa wiki bila kula wala kunywa kuanzia waawio ya jua mpaka machweo yake, ilikuwa ni kila Jumatatu na Alhamisi. Na hata marabi waliwasisitiza wanafunzi wao kushika amri hii ya kufunga kila wiki. (Luka 18:12) Katika Agano Jipya mkazo juu ya umuhimu wa kufunga tunaona ni kidogo sana maana Mtume Paulo katika nyaraka zake hataji hata mara moja na Yesu anazungumzia mara mbili tu juu ya kufunga, yaani pale alipoulizwa kwa nini wanafunzi wake hawafungi na katika Injili ya leo. Ni katika Injili ya leo anatuonesha lengo na shabaha ya kufunga sio kujitesa au kubaki na njaa bali kuwashirikisha wengine furaha na tumaini lile lililopo ndani mwetu.
Hivyo tusifunge kama wafanyavyo wanafiki kwa kukunja sura zao bali kuosha uso na kuupaka mafuta. Ni kuwa na uso wa matumaini na furaha na kuwashirikisha wengine furaha na matumaini yetu. Mfungo ni mwaliko wa kufurahi kwani tunaalikwa kuwa na furaha kwa kujikatalia kwetu ili ndugu yetu muhitaji abaki na furaha kwa kushirikishwa mema aliyotujalia Mwenyezi Mungu. Furaha ya kweli hupatikana katika kupenda! Mfungo wetu hauna budi kukubaliwa na Mungu kwa kumuiga Mungu mwenyewe, kufungua mioyo yetu kwa upendo na kumwelekea kila muhitaji anayetuzunguka katika mitaa yetu, majirani zetu, na popote pale wanapokuwepo wahitaji. Naomba kusisitiza hili kila ninachojinyima naalikwa kumshirikisha mwingine aliyemuhitaji zaidi. Vinginevyo mfungo wetu unakuwa sawa na kufanya diet kwani kunabaki ni kwa masilahi binafsi. Baba Mtakatifu Francisko katika mojawapo za homilia yake anatualika pia kufunga ndimi zetu kwa kuzing’ata ili zivimbe ili kuepuka kusengenya na kuwasema vibaya wengine, labda ni mfano wa kichekesho ila tukumbuke Kwaresma inakuwa na maana tu kama tunajaribu kufanana zaidi na Mungu kwa kuwapenda wengine na hivyo wakati mwingine tunaweza kusali au kutoa sadaka na kufunga ila kama hatuna upendo kwa mwingine ni kazi bure. Tumuombe Mungu mfungo wetu utusaidie kufanana zaidi na Mungu. Kupanda milimani ni mwaliko wa kugeuka na kuwa wapya, kuwa na namna ile ya Mungu mwenyewe na hiyo ndio metanoia ya kweli. Safari njema ya kupanda mlima ya siku arobaini pamoja na Yesu mwenyewe. Kwaresima yetu ikawe kweli tendo la Kisinodi, ndio kusafiri pamoja na Kristo Yesu aliye Njia, Kweli na Uzima.