Maandalizi ya Sinodi kwa awamu ya kibara:Kuanzia tarehe 1-6 Machi, inafanyika awamu ya pili kwa bara la Afrika huko Ethiopia Maandalizi ya Sinodi kwa awamu ya kibara:Kuanzia tarehe 1-6 Machi, inafanyika awamu ya pili kwa bara la Afrika huko Ethiopia 

Sonodi:Kanisa nchini Ethiopia ni mwenyeji wa awamu ya kibara,kuanzia 1-6 Machi 2023

Katika awamu ya kibara ya Sinodi ambayo inaendelea ulimwenguni kote,Bara la Afrika linajiandalia awamu hiyo itakayofanyika Ethiopia,kuanzia 1-6 Machi 2023 katika kutafakari kwa kina namna ya kufanya mang’amuzi wakiongozwa na Hati ya Kitendea Kazi ya kibara iliyotokana na awamu ya I ya mashauriano ya makanisa mahalia.

Na Angella Rwezaula; - Vatican.

Katika miezi hii, tumeona mikutano mingi katika mabara mbali mbali ya awamu ya kibara, kama ile ya Bara la Ulaya, Bara la Amerika Kusini, Kati na Kaskazini, Australia na Visiwa vyake, Nchi za Mashariki ya Kati na Asia na kwa mara nyingine tena ni Sinodi ya kibara kwa ajili ya Afrika ambayo inatarajiwa  kufunguliwa kuanzia tarehe 1-6 Machi 2023 huko jijini Addis Ababa, nchini Ethiopia. Mkutano huo unatazamiwa kuwa na washiriki ambao watatafakari kwa kina ndani ya mazingira ya Afrika kuhusu Hati  ya Kitendea Kazi ya Tume ya awamu ya  Kibara (DCS) ambayo ilitolewa na Kamati ya Sinodi mjini Vatican mnamo 2022, mara baada ya awamu ya kwanza ya mashauriano ya makanisa mahalia. Mkutano huo utajumuisha washiriki 108 ambao miongoni mwake watawakilishwa na waamini walei 44, vijana 36, wanovisi watano na waseminari watano. Pia kutakuwa na mapadre 32, watawa wa kike 10, watawa wa kiume 6, maaskofu 13 na makadinali 10.Zaidi ya hayo, wafanyakazi wa kiufundi watawakilishwa na wanachama wanne kutoka Mpango wa Sinodi Afrika (ASI) na waandishi wa habari 11 kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya Kikatoliki na mashirika ya mawasiliano hata mwakilishi kutoka Vatican News.

Kanisa barani afrika kukutana na kutafakari maoni ya Kanisa la Afrika

Katika mahojiano ya hivi karibuni, wa mujibu wa taarifa kutoka AMECEA, na mwandishi Sr. Jecinter Antoinette Okoth, (FSSA), alibainisha kuwa Padre Anthony Makunde Katibu Mkuu Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki (AMECEA) kuhusiana na tukio hilo alisema kwamba kuna masuala mengi ambayo yameibuliwa na makanisa mahalia. Kwa njia hiyo wanapaswa kutafakari pamoja kama mabara yao kwa kile kilichotoka katika majimbo yote  ulimwenguni  ambacho kilikusanywa pamoja ili kutoa Hati ya Kitendea Kazi ya  Hatua ya Bara. Kwa njia fulani, Kanisa la mahalia  litakuwa likitafakari maoni kutoka katika Kanisa la Ulimwengu wote. “Hii ina maana Kanisa Barani Afrika litakutana ili kusali na kupambanua kwa pamoja juu ya Hati hiyo lakini kwa kuzingatia mazingira yetu ya ndani, baada ya kusoma hati hiyo, kutafakari na kuomba maongozo ya Roho Mtakatifu tunakwenda kutazama maeneo ambayo tunadhani yametugusa zaidi katika muktadha wetu wa Kiafrika”. Kwa mujibu wa Karibu Mkuu wa AMECEA alifafanua  kuwa mabaraza nane ya kikanda ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ambayo yanaunda Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar (SECAM), kila moja yametengewa nafasi ya kutuma uwakilishi katika mkutano huo wa Juma  moja.

Baada ya vikao viwili  ni fursa kutafakari katika Hati ya kitendea kazi

Katibu Mkuu wa AMECEA alisisitiza zaidi kwamba, mkutano huo unawaleta pamoja wajumbe kutoka bara zima la Afrika na Visiwani na kwamba utatumia njia iliyopendekezwa na Baba Mtakatifu, yaani, mazungumzo ya kiroho na kusikiliza kile ambacho Roho Mtakatifu analiambia Kanisa Barani Afrika kupitia wawakilishi. Padre Makunde aliendelea kuweka wazi kuwa baada ya vikao viwili vya kazi vya wataalam kutoka bara hilo, Kikundi hicho  kilitoa mapendekezo kama hoja za kutumia fursa ya mkutano wa bara, na hivyo haja ya wajumbe wa Addis Ababa kuelewa mbinu hiyo kwa sababu ni tofauti na ile inayotumiwa mara nyingi katika mikutano mingine. “Kabla ya mkutano ujao, mabaraza ya kanda yanatarajiwa kutoa utambulisho kwa wajumbe wao ili waelewe vizuri waraka utakaotumika wakati wa kusanyiko na muhimu zaidi mbinu ya utambuzi. Kwa hiyo wajumbe wanatakiwa kusoma na kusoma tena (waraka huo),” Padre Makunde alieleza. “Njia hii iko katika mfumo wa maombi ili kuruhusu mwanadamu kamili kujihusisha, kiakili na kiroho. Sio jambo ambalo linahitaji mjumbe kupata kanuni katika kitabu lakini badala yake kuruhusu ujumbe katika hati na kuzama ndani ya mioyo na akili zetu, na kuruhusu Roho Mtakatifu kuwavuvia. Kwa hivyo, wakati wa mkutano miitikio kutoka kwa wajumbe inatarajiwa kuongozwa na Roho Mtakatifu,” alisisitiza Padre Makunde.

Kuitikia wito wa Bwana Yesu wa kupendana

Padre Makunde alitaja baadhi ya maeneo yanayotia wasiwasi ambayo Kanisa Barani Afrika halipaswi kushindwa kuyatafakari kwa kina ni pamoja na masuala kama vile “Ulinzi na ulinzi wa taasisi ya kifamilia kwani hii imejitokeza sana katika taarifa za kikanda kuwa ni changamoto ya kichungaji kwa familia katka Kanisa barani Afrika.” Kwa hiyo "masuala kadhaa yaliyotajwa kuwa changamoto zinazokabili Afrika yanaweza kushughulikiwa kwa kukuza maadili ya familia. Kanisa lenyewe linategemea jinsi familia zilivyo na nguvu, hivyo kuharibu familia ni kuliangamiza Kanisa". Katibu Mkuu wa AMECEA pia alipendekeza kuwa wajumbe wanapaswa kujadili jinsi Kanisa Barani Afrika linapaswa kuishi imani wanayokiri. Ripoti zinataja masuala kama vile vita na ukosefu wa haki wa kijamii ambao ni kinyume na Imani ya Kikristo. Ikiwa tutaitikia wito wa Bwana wetu Yesu Kristo wa kupendana, masuala haya yasiwe changamoto za kila siku katika mazingira ya Kikristo,” alisisitza Padre Anthony. Kwa kuongezea alisema “Kwa hivyo, tunahitaji kutafuta njia za kuimarisha ukweli kwamba tunapaswa kuishi kile tunachodai katika imani yetu ya Kikristo. Eneo lingine linalolitia wasiwasi Kanisa Barani Afrika, Padre Makunde alisema ni, kukumbuka wito wa Bwana wetu Yesu Kristo wa kwenda sehemu zote za dunia na kufanya wanafunzi kwa vile Kanisa Barani Afrika ambalo bado ni changa na linahitaji uinjilishaji zaidi. Wakati tunawafikiria wale ambao tayari ni Wakristo na hawako katika ushirika kamili, tunawafikiria pia wale ambao hawana fursa ya kusikia Neno la Mungu”, Padre  Makunde alisema.

Kwenda zaidi ya dini zetu katika mchakato wa kiekumene

Mbali na Wakatoliki watakaohudhuria mkutano huo wa bara, Katibu Mkuu wa AMECEA alisisitiza kuwa kutakuwa na washiriki wa dini nyingine ambao watajiunga na mkutano huo. Hawa ni pamoja na wajumbe kutoka Dini za Jadi za Kiafrika, kutoka jumuiya ya Waislamu na kutoka Kanisa la Kiorthodox la Ethiopia. Ingawa sisi ni Wakatoliki, tunaishi katika jamii yenye mchanganyiko wa kidini. Kwa hivyo, mtazamo wa kiekumene unaoneshwa katika mchakato wa safari hii ya sinodi. Sisi (Wakatoliki) tunahitaji kwenda zaidi ya dini yetu ili kufikia hata madhehebu mengine ya Kikristo na kwa dini zisizo za Kikristo”. Alibainisha Padre  Makunde. Tuko katika jamii ambayo bila kujali itikadi zetu za Kikristo sisi ni wanadamu na wengi wa dini hizi tunazohusiana nazo ni za Mungu mmoja, kwa hiyo, tunaamini katika Mungu mmoja na hiki ni kiungo cha kuunganisha.  Kila Mkatoliki ajue kwamba Sinodi bado haijaisha na roho ambayo imewashwa na safari hii ya sinodi bado haijaisha. Hebu tusaidie uwepo wa Roho Mtakatifu katika shughuli zozote, iwe shughuli za Kanisa au shughuli za kijamii, tukijua kwamba sisi sote ni wana na binti wa Muumba mmoja, na tumeitwa kutembea kwa pamoja,” alihitimisha, Padre Makunde, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki (AMECEA) wakati wa kuwakilisha kwa kirefu juu ya Mkutano huo wa awamu ya kibara kwa Afrika inayofanyika kuanzia tarehe 1-6 Machi 2023 jijini Adis Ababa, Ethiopia.

Awamu ya II ya Sinodi barani Afrika kuanzia 1-6 Februari 2023
28 February 2023, 09:19