Tafuta

Masomo ya dominika ya VI Mwaka A wa Kanisa yanatukumbusha uhusiano uliopo kati ya Amri za Mungu, uhuru wa mwanadamu na ufalme wa Mungu. Masomo ya dominika ya VI Mwaka A wa Kanisa yanatukumbusha uhusiano uliopo kati ya Amri za Mungu, uhuru wa mwanadamu na ufalme wa Mungu.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika 6 ya Kipindi Mwaka A wa Kanisa: Amri za Mungu na Uhuru wa Mwanadamu

Masomo ya dominika hii yanatukumbusha uhusiano uliopo kati ya Amri za Mungu, uhuru na ufalme wa Mungu. Hakuna ufalme bila sheria. Ufalme wa Mungu nao una sheria, kanuni, taratibu na miiko yake ambazo zimewekwa kwa upendo na zinapaswa kufuatwa kwa upendo pasipo shuruti bali kwa uhuru kamili ili kila mmoja awajibike katika maneno na matendo yake mwenyewe .

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 6 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatukumbusha uhusiano uliopo kati ya Amri za Mungu, uhuru wa mwanadamu na ufalme wa Mungu. Hakuna ufalme bila sheria. Ufalme wa Mungu nao una sheria, kanuni, taratibu na miiko yake ambazo zimewekwa kwa upendo na zinapaswa kufuatwa kwa upendo pasipo shuruti bali kwa uhuru kamili ili kila mmoja awajibike katika maneno na matendo yake mwenyewe katika maisha yake ya hapa duniani ambayo kwayo tunastahilishwa kuingia katika ufalme wa Mungu kwenye maisha ya umilele yote mbinguni. Somo la kwanza ni la kitabu cha Yoshua bin Sira (YbS 15:15-20). Katika somo hili Yoshua Bin Sira anatueleza juu ya ukuu wa Mungu kwa kumpatia kila mtu uhuru na utashi. Kila mtu ana uhuru wa kuchagua kati ya mema na mabaya. Mungu anapendelea mtu achague mema; lakini hamshukurutishi kwani anachagua kwa ufahamu na kwa uhuru kamili. Hivyo kila mtu yuko huru kuchagua kati ya uzima au mauti na hakuna anayelazimishwa. Lakini mwisho wa yote kutakuwa na hukumu ya haki kwa yale tunayoyachagua. Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 2:6-10).  Katika somo hili Mtume Paulo anatueleza kuwa Hekima ya Mungu ni mpango wake wa kutukomboa sisi kwa msalaba wa Yesu Kristo.

Amri za Mungu na uhuru wa mwanadamu: Dhamiri nyofu
Amri za Mungu na uhuru wa mwanadamu: Dhamiri nyofu

Hekima hii imefunuliwa kwa wanyofu kwa njia ya Roho, maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Hekima hii, wenye kuitawala dunia hawaijui; maana kama wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa utukufu. Nasi tumwombe Mungu Roho Mtakatifu kila wakati katika maisha yetu ili aweze kutuongoza katika kuijua hekima hii ya Mungu ambayo ndiyo inayotuwezesha kuishi vyema maisha ya hapa duninia tukifuata amri na maagizo ya Mungu ambayo kwayo tutastahilishwa kuingia katika ufalme wa milele huko mbinguni. Somo la Injili ni ilivyoandikwa na Matayo (Mt 5:17-37). Katika somo hili Yesu anatufundisha kuwa Torati na Manabii ni jumla ya mapenzi ya Mungu ambayo aliyafunua katika Agano la Kale. Yesu mwenyewe hakuja kutangua hiyo sheria, bali kuitimiliza kwa kukazia kwamba kila wazo, neno na tendo liwe na lengo moja tu: kutimiza mapenzi ya Mungu. Yesu anasisitiza kuwa amri zote zinapaswa kufundishwa na kufuatwa kwa ukamilifu wake. Hakuna amri ambayo ni ndogo ya kupuuzwa na kutofuatwa, zote lazima zifuatwe. Kumbe kuua, kumwonea mwingine hasira au kummfyolea au kuapiza, kuzini au kutamani zote ni dhambi. Ili kuonyesha ubaya wa dhambi Yesu anatumia lugha ngumu na ya kuogofya kama vile kung’oa jicho au kuukata mkono na kuvitupilia mbali pale viungo hivi vinapotukosesha. Katika somo hili, Yesu anasisitiza umuhimu wa kusameheana na kusuluhishana maana hicho ndicho kipimo cha sisi kusamehewa na sadaka zetu kukubaliwa mbele za Mungu.

Dhambi ya asili na uhuru wa mwanadamu
Dhambi ya asili na uhuru wa mwanadamu

Uwezo wetu wa kutambua lipi ni jema na lipi ni baya ambao Yoshua Bin Sira anatueleza katika somo la kwanza, umeathiriwa na dhambi ya asili. Tangu Adamu na Eva walipomkaidi Mungu kwa kula tunda la mti wa ujuzi wa mema na mabaya, kizazi chao chote kimeathirika na kuwekewa amri ambazo lazima tuzifuate. Kumbe amri za Mungu zinamsaidia binadamu awe huru. Uhuru ni uwezo wa kuchagua mema bila kizuio chochote. Jambo ni jema iwapo linaendana na maumbile ya binadamu. Hilo jema linamsaidia mtu kuwa kama alivyokusudiwa kuwa na Mungu mwenyewe. Mungu ndiye aliyemuumba binadamu akaweka lipi liwe zuri kwake na lipi ni jema kwa mwanadamu litakalomsadia kufikia ukamilifu. Amri za Mungu zinatuonyesha lipi ni jema kwetu. Hivyo, amri za Mungu zinatusaidia kuwa huru maana zinatusaidia kujua kipi ni kizuri. Mungu akishatuonyesha lipi ni jema lipi ni baya anatuacha tuchague wenyewe. Anaheshimu uhuru wetu. Lakini kwa sababu ya kiburi bado pia hizi amri hatuzifuati tunavyopaswa. Wakati mwingine, tunakataa makusudi kujifunza ili tujue lipi ni jema. Nafasi za kujua zipo lakini hatuweki juhudi. Kwasababu ya kiburi, wakati mwingine tunajua lililo jema lakini tunakataa kulitenda. Tunafuata hisia zetu ambazo zinalegeza uwezo wa utashi wetu kuchagua lilo jema.

Umuhimu wa kuunda dhamiri nyofu na hofu ya Mungu
Umuhimu wa kuunda dhamiri nyofu na hofu ya Mungu

Kwa sababu ya mazoea ya kibinadamu, amri za Mungu zinaonekana kuwa kinyume cha matazamio yetu na mazoea yetu na hivyo kuonekana zinatesa na kudai sana. Injili inaeleza vizuri: mmezoea kufanya hivi, mimi na waambia fanyeni hivi. Yesu anatukumbusha kila mara kuweka juhudi kufahamu ukweli ni upi. Wimbo wa katikati umetuambia; “Bwana nifungue macho niyatazame maajabu ya sheria yako.” Ili tuweza kufanikiwa katika maisha yetu ya kiroho yatupasa kufanye mazoezi na kuwa na mazoea ya kutenda mema ili kujijengea fadhila. Maana bila kufanya hivyo inawezekana kufahamu kabisa kuwa jambo fulani ni baya lakini tukashindwa kuliepuka na kujizuia kulitenda kwa sababu hatujajingea mazoea ya kutenda mema na kuacha mabaya. Fadhila zinajengwa kwa kutenda mema kwa kurudiarudia mpaka kuyafanya mazoea na hivyo inakuwa ni vyepesi kuchagua lililo jema na kuacha lililo baya. Basi tumwombe Mungu Baba aliyetuumba atujalie neema na baraka zake tuweze kuutumia vyema uhuru na utashi aliotujalia katika kutimiza mapenzi yake ili mwisho wa yote tuweze kupokea taji ya utukufu huku mbinguni aliko yeye tukafurahi na watakatifu wake milele yote. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari D6
10 February 2023, 17:20