Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya VI ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Yesu Kristo ni utimilifu wa Torati! Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya VI ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Yesu Kristo ni utimilifu wa Torati!   (Vatican Media)

Tafakari Dominika 6 ya Mwaka A: Yesu Ni Utimilifu wa Torati!

Baadhi wanadhani Yesu amekuja na mafundisho mapya, na hata kushawishika kudhani kuwa amekuja na mafundisho yanayokinzana na Torati. Ujio wa Yesu ni utimilifu wa kile ambacho Mungu ameanza kukifunua katika Agano la Kale. Ni Yesu anakuja kutoa maana ya maagizo na amri za Mungu; kuwafunulia watu sura ya Mung, kutupa maana ya kila agizo la Mungu kwa mwanadamu.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Yesu Kristo ni utimilifu wa Torati! Sehemu ya Injili ya Dominika ya 6 ya Mwaka A wa Kanisa Mt 5: 17-37 kama ya Dominika mbili zilizopita ni mwendelezo wa hotuba na mafundisho ya Yesu akiwa juu mlimani pamoja na wafuasi wake; Ni mwendelezo wa maisha kanuni au katiba anayoitoa pale juu mlimani kama vile Musa alivyopokea amri za Mungu juu ya mlima Sinai, Yesu naye anachagua mlimani kuwapatia maagizo na kanuni za maisha kwa kila mfuasi wake. Mlimani katika muktadha wa Kiyahudi ni mahali pakukutana na Mungu. Hivyo, amri na maagizo ya Yesu ni amri na maagizo ya Mungu kwa watu wake. Ni katika muktadha huo wa hotuba ya Yesu pale juu mlimani, maarufu kama “Heri za Mlimani” alipoanza kuwaalika wanafunzi wake kubadili vichwa vyao, kwa maana ya kuongozwa na mantiki si ya ulimwengu huu bali ile mpya ya Yesu Kristo Mwenyewe. Baadhi wanadhani Yesu amekuja na mafundisho mapya, na hata kushawishika kudhani kuwa amekuja na mafundisho yanayokinzana na Torati. Ujio wa Yesu ni ukamilifu wa kile ambacho Mungu ameanza kukifunua katika Agano la Kale. Ni Yesu anakuja kutupa sasa maana ya maagizo na amri za Mungu, ndiye anayekuja kutufunulia sura ya Mungu katika ukamilifu wake. Ndiye anayekuja kutupa maana yak ila agizo la Mungu kwa mwanadamu.

Kristo Yesu ni utimilifu wa Sheria
Kristo Yesu ni utimilifu wa Sheria

Yesu alishika sheria, ila tofauti na wengi wa wasikilizaji wake ni jinsi alivyoanza kuwaalika kwa kuwafundisha kuwa sheria zimewekwa sio kwa kumkandamiza mwanadamu bali ni kwa kumtumikia mwanadamu. Yesu anazipta tafsiri sahihi sheria au Maandiko Matakatifu. Yesu aliye Neno la Mungu, sasa anatoa maana ya Neno la Mungu. Kwa kusukumwa na upendo kwa mtu, Yesu alivunja hata sheria ya Shabbàt yaani Sabato, na ndio katika mazingira ya namna hii tunaona baadhi ya wasikilizaji wake wanakuwa na mashaka kuwa ni mvunjaji wa sheria na hivyo ujio wake ni kuja kuharibu Torati. Yesu akiwa pale juu mlimani anatoa Torati mpya, anawafundisha Sheria mpya ambayo kwa kweli ndio tunaona inatualika kubadili vichwa vyetu kwa maana ya kubadili namna zetu za kufikiri na kutenda. Ni mwaliko wa ukombozi wa fikra. Musa (Kitabu cha Kumbukumbu la Torati 28:10-13) tunaona anawahakikishia wana wa Isreali kuwa ikiwa watakuwa waaminifu na hofu ya Mungu basi Mungu atawajalia mema mengi na hasa utajiri wa hapa duniani. Leo Yesu akiwa pale mlimani anawahubiria heri walio maskini, heri wanaoteseka, unaona kabisa Yesu anafundisha kinyume au kupinga kile alichofundisha Musa.

Na hata nasi leo tu mashahidi wa utitiri wa makanisa hasa nchini kwetu Tanzania na Barani Afrika, na wahubiri wengi na wanaofuatwa na wengi ni wale wanaohubiri Injili ya mafanikio na utajiri na mali, Injili ya vitu vya ulimwengu huu. Leo hii katika makanisa hatusikii tena heri ya kuwa maskini, ya kuteseka na kuudhiwa bali utajiri, uponyaji, mafanikio na mambo ya namna hiyo. Tunaona leo Yesu anatualika sisi tulio wafuasi wake kuongozwa na mantiki mpya. Yesu anajifunua leo kwa kutuonesha msimamo wake. Yesu anatuonesha kuwa hakuja kuiharibu au kuitengua Torati bali kuikamilisha, kuipa maana ile kudusiwa na Mungu kwani Yeye ndiye Neno wa Mungu, ni Mwana wa Mungu anayekuja kumfunua na kumdhihirisha Mungu katika ukamilifu wake.  Yesu anamaliza sehemu ya kwanza ya Injili ya leo kutualika nasi kuwa Sheria ya Mungu iliyo hai, si tu kwa maneno yetu bali kuliishi Neno lake katika ukamilifu wake. Si kwa kuchagua yale tu tunayoona tunayaweza na kutupendeza, bali kuishi Neno katika ukamilifu wake na hivyo kuwa mashahidi wa imani kwa wale wanaotuzunguka. Kama tulivyoona Dominika iliyopita mwaliko wa Mwanafalsafa wa Kijerumani ambaye hakuamini katika uwepo wa Mungu akitutaka tuwe Biblia (Friedrich Nietzsche). “Wakristo, iweni Biblia!”

Kristo Yesu Ni Ufunuo wa Huruma na Upendo wa Mungu
Kristo Yesu Ni Ufunuo wa Huruma na Upendo wa Mungu

Sehemu ya pili ya Injili yetu ya leo, tunaona sasa Yesu akirejelea baadhi ya amri zile alizopokea Musa na kuwakabidhi wana wa Israeli bali sasa anazipa maana pana na ya kina zaidi. Yesu leo anatoa katekesi ya kina juu ya amri za Mungu, na hasa tutaona zote zikionesha roho ya sheria ni upendo daima na kamwe hakuna sheria au amri za Mungu isiyoakisi ukweli huo. Tunaona Mwinjili Mathayo anatumia kanuni ile ya uandishi mmoja kwa mifano yote sita, ingawa leo tutaisikia minne na mingine miwili iliyobaki tutaitafakari Dominika ijayo. Hapa utaona baadhi ya tafsiri zinaonesha kana kwamba kuna kupingana kile kilichopo katika Agano la Kale na kila anachosema Yesu mlimani akiwa na wanafunzi wake. Kwa kweli hapana na badala yake Yesu anawasisitiza kuwa imeandikwa hivi na sasa Mimi nasema…anasema kama nilivyotangulia kusema hapo juu kuwa anaingia kwa mapana na kina kila amri. Yeye aliye Neno la Mungu (Logos kwa Kigiriki au Parashà kwa Kiebrania) Imeandikwa usiue, na Yesu sasa anatupa kila aina au tafsiri mbalimbali zinazomaanisha kuua. Yesu anatualika si tu kuishia kuwa hatujaua mwingine kimwili, kwani pia ni kuua, kwa mfano kumsema mwingine maneno ya kujeruhi au yasiyofaa, kuchukia mwingine, na mambo kama hayo. Kuua kunaanzia mioyoni mwetu, huwezi kumchukia mtu mwingine na ukabaki na amani ya ndani. Chuki ni sawa na kuua kwani ni sawa kutokuona thamani au nisema kujifunga macho na hivyo kukosa kuona kuwa mwingine naye ni sura na mfano wa Mungu. Ni kumwona na kumtendea kama kitu kwani hauoni tena thamani na utu wake. Hivyo ndio kudiriki kusema mpumbavu, mjinga, yote ni sawa na kusema mtu asiye na thamani yake, ni kushindwa kuiona sura na mfano wa Mungu ndani mwake.  

Yesu anafafanua maana ya Neno na Sheria za Mungu katika utimilifu wake
Yesu anafafanua maana ya Neno na Sheria za Mungu katika utimilifu wake

Kuua ni kukosa kumpenda mwingine, kukosa kumtakia mema mwingine kama anavyotufundisha Mt. Thoma wa Akwino. Yesu anatukumbusha leo tena kwa kurudiarudia mara tatu kuwa huyo mwingine ni ndugu yako. Neno ndugu linatumika mara kadhaa ili kutukumbusha kila mwanadamu hapa ulimwenguni ni ndugu yangu na yako. Ni kwa kuwa na matazamo huo ndipo nasi tunaweza kuona thamani ya kila mwanadamu tunayekutana naye. Ndipo Yesu leo anatukumbusha kuwa kinachopaswa kuwa safi sio mwili bali ni roho zetu. Hivyo kupatana na ndugu yangu na yako ndio kiini cha usafi wa kweli. Kwa Wayahudi wanaposali sala ile ya “Shemàh Israeli”, yaani, Sikia Israeli, kadiri ya Talmudi, na mara tu wanapoanza kuisali hawawezi kuikatisha, na kwa kuweka msisitizo wanasema hata nyoka akiwa anapita miguuni mwako hupaswi kuikatisha sala hiyo. Yesu leo anatualika kubadili vichwa vyetu, kuwa si tu kuikatisha sala ya Shemàh Israeli, bali hata sala ya kutolea sadaka hekaluni kila unapotambua kuwa hujapatana na ndugu yako. Sala sio tu kanuni ya kuitekeleza bali ni kitendo kinachoonesha mahusiano yetu ya ndani kabisa na ya upendo kwa Mungu na hivyo kututaka kuwa na mahusiano mema na wengine pia. Anayesali anampenda kweli Mungu, na hivyo anampenda pia jirani! Kusali ni kuingia katika mahusiano na Mungu na wengine.

Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha
Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha

Na ndio tunaona waamini wale wa Kanisa la Mwanzo tayari wanatambua umuhimu na ukubwa wa swala la kupatana na ndugu. (Waefeso 4:26) Paulo anatukumbusha kuwa jua lisitue tukiwa bado na hasira. Na hata katika Maandiko ya mapokeo na mafundisho ya Mitume (Didache 14:1-2) tunasoma Wakristo wakisisitizwa kuwa wasijumuike katika mijumuiko ya Siku ya Bwana yaani Dominika ikiwa bado hawajapatana na ndugu. Na ndio mafundisho ya mitume sehemu ile ya kwanza inatukumbusha umuhimu wa kuchagua njia ile ya uzima, ndio ile ya kumpenda Mungu na jirani. Yesu pia leo anafundisha juu ya amri ile ya sita ya usizini kwa undani zaidi. Yesu kama kawaida yake haishii tu juujuu bali anaingia ndani na kuonesha nini chanzo cha ubaya huo. Yesu anakwenda mbali zaidi hata kutualika kukata au kuondoa aidha macho na mikono yetu kama inatupelekea kutenda dhambi, ndio kusema kuingia ndani mwetu na kujichunguza na hivyo kujua nini hasa chanzo cha yote maovu tunayoyatenda katika maisha yetu. Ni kwenda na kung’oa mzizi wa kila anguko katika maisha yetu. Wongofu wa kweli unatutaka kuingia kwanza ndani mwetu, kuondoa magugu na yote mabaya yanayotuweka mbali na Mungu na wengine.

Kristo Yesu alifafanua kwa kina Amri na Maagizo ya Mungu
Kristo Yesu alifafanua kwa kina Amri na Maagizo ya Mungu

Anasema ni heri kutupwa jehenamu kiungo kile kinachotupekelea kuanguka. Jehenamu mara nyingi tunashawishika kufikiri mara moja juu ya moto wa milele, hapana bali ni vema tukajua leo asili yake ni nini. Ni jalala lililokuwa kusini Magharibi mwa mji ule wa Yerusalemu.  Ilikuwa pia sehemu iliyolaaniwa kwani pia ilitumika kuwateketeza sadaka watoto wadogo kwa mungu Moloki, hivyo wengi waliichukua kuwa sehemu ile ni mlango wa ulimwengu wa mashetani na mapepo wabaya. Hivyo dhambi ni sawa na kukubali mwenyewe kwa hiari na utashi wetu kujiingiza na kujiteketeza katika moto wa jalala lile la Jehanamu. Kuishi katika dhambi yoyote ile ni sawa na kuishi jalalani ambako daima kuna moto na funza. Ni kukaa mbali na Mungu. Yesu pia anaongea kwa mapana juu ya talaka. Yesu anaonesha waziwazi mapenzi ya Mungu tangu pale mwanzo aliopoasisi Taasisi ile ya familia kuwa wawili wale wanakuwa mwili mmoja, kwani Mungu ndiye anayewaunganisha na hivyo hakuna sababu yeyote ile ya kuwatenganisha isipokuwa ni zinaa. Zinaa inayosema hapa ni muunganiko ule usiokuwa halali tu ila kinyume na hapo hakuna sababu yeyote inayoweza kuhalalisha talaka. Yafaa sana hasa kwetu wanafunzi na wafuasi wa Yesu kuwa makini na mantiki za ulimwengu wa leo kuhusu taasisi hii ya Ndoa.

Kristo Yesu ni utilimifu wa Torati ya Musa.
Kristo Yesu ni utilimifu wa Torati ya Musa.

Tupo mashuhuda wa ulimwengu wetu wa leo ambapo kuna makundi ya watu mbalimbali na hata ndani ya Kanisa wanaotaka Kanisa lianze kufundisha kinyume na mapenzi ya Mungu kama tunavyosoma katika Maandiko Matakatifu. Lakini pia Kanisa linabaki kuwaonesha huruma ya Mungu na kuwasindikiza hata wale wanaokuwa wameshindwa au kupatwa na shida katika maagano yao ya ndoa. Kanisa tunaalikwa sio kuwatenga na kuwanyanyapaa bali daima kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu kwao. Mfano wa nne ndio ule wa kuapa. Wakati wa uhamisho wa Babeli wana wa Israeli walianza kuiga mitindo ya watu wengine, yaani ya kipagani na mojawapo ilikuwa ni hii tabia ya kuapa. Kila wanapozungumza au kuongea ili kuonesha kuwa kitu anachosema ni kweli basi walijiapisha. Na ili kukwepa kulitaja bure Jina la Mungu waliapa kwa mbingu, hekalu, nchi, wazazi na hata vichwa vyao. Yesu leo anatukumbusha kuwa tuachane na tabia na mazoea ya namna hiyo. Kwa nini Yesu anatualika kuepuka tabia hiyo si tu kwa sababu tunataja jina la Mungu bali zaidi sana ni kuepuka sura au taswira potofu ya Mungu. Mungu wetu haenendi au kutenda kwa kulipa kisasi kama baadhi yetu tunavyoweza kudhani na kufikiri. Mungu hatendi kama sisi wanadamu (Anthropomorphic). Jumuiya ya waamini ni jumuiya ya wana wa Mungu, hivyo ndiyo yetu na iwe ndiyo, na hapana yetu iwe hapana, ndio kusema mwanafunzi wa Yesu ni yule anayeishi bila kuwa na sura mbili. Ni mwaliko wa kuwa wakweli daima. Nawatakia tafakari njema na Dominika takatifu.

09 February 2023, 17:35