Tafuta

Tafakari ya Dominika VII Mwaka A wa Kanisa: Upendo kwa Mungu na jirani ni dira na mwongozo wa maisha ya Wakristo. Tafakari ya Dominika VII Mwaka A wa Kanisa: Upendo kwa Mungu na jirani ni dira na mwongozo wa maisha ya Wakristo.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika 7 ya Mwaka A wa Kanisa: Upendo Kwa Mungu na Jirani Ni Muhimu Sana

Hii ni katekesi juu ya Torati, "Neno" katiba ya maisha ya kila mfuasi wa Yesu, hivyo ni masharti ya lazima kama nasi tunataka kuwa kweli wanafunzi wake Yesu Kristo kuweka katika maisha yetu ya siku kwa siku. Ndio utambulisho na amana yetu. Katika jamii zile za watu wa kale kwa kuwa hakukuwa na serikali au vyombo vya dola vya kusimamia haki msingi za binadamu, utu na heshima.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! “Kama ningepaswa kuandika kitabu cha Maadili chenye kurasa mia, basi kurasa tisini na tisa ningeziacha wazi bila maandishi. Ile kurasa ya mwisho ya mia ningeliandika:wajibu pekee nilio nao ni kupenda!” (Albert Camus- Mwanafalsafa kutoka Ufaransa.) Sehemu ya Injili ya Dominika ya Saba ya Mwaka A wa Kanisa, Mt 5: 38-48 ni mwendelezo wa hotuba yenye mafundisho au maisha kanuni ya Yesu anayoyatoa kwa wafuasi wake akiwa pale juu mlimani. Ni katekesi juu ya Torati, ni katiba ya maisha ya kila mfuasi wa Bwana wetu Yesu Kristo, hivyo ni masharti ya lazima kama nasi tunataka kuwa kweli wanafunzi na wafuasi wake Yesu Kristo kuweka katika maisha yetu ya siku kwa siku. Ndio utambulisho wetu na amana yetu. Katika jamii zile za watu wa kale kwa kuwa hakukuwa na serikali au vyombo vya dola vya kusimamia haki na usawa katika jamii, hivyo mara nyingi jamii ziliwaadhibu wakosaji hata kwa namna iliyopitiliza na hata kutishia uhai wa mkosaji kwa lengo moja tu, ili liwe fundisho na hasa tishio kwa wengine wasijekufanya kitendo au jambo lisilokubalika na jamii. (Mwanzo 4:23-24) “Lameki akawaambia wake zake, Ada na Sila sikieni sauti yangu! Sikilizeni nisemayo enyi wake za Lameki. Mimi niliua mtu kwa kunijeruhi, naam, nilimuua kijana kwa kuniumiza. Ikiwa Kaini atalipizwa mara saba, kweli Lameki atalipizwa mara sabini na saba.”

Upendo kwa Mungu na jirani ujenge ari na moyo wa Kanisa la Kisinodi.
Upendo kwa Mungu na jirani ujenge ari na moyo wa Kanisa la Kisinodi.

Ni kutokana na muktadha huo wa adhabu za kupitiliza tunaona katika kitabu cha (Kutoka 21:23-25) tunasikia “Lakini kama yatakuwapo madhara mengine, basi, lazima amlipe uhai kwa uhai, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu, kuchomwa moto kwa kuchomwa moto, jeraha kwa jeraha, na pigo kwa pigo” Ni maagizo ili kuepuka ukatili uliopitiliza ili mkosaji alipe tu kadiri ya kosa lake alilolifanya na si kinyume chake. Na ndio tunaona leo kuna sheria ijulikanayo kama “ius talionis” (The Law of retaliation), sheria ya kulipiza kisasi, jino kwa jino na jicho kwa jicho. Na ndio mantiki inayoongoza ulimwengu wetu wa leo kuwa kila mkosaji hana budi kulipa sawa na kosa alilolitenda. Lakini tunaona leo Yesu anatualika wanafunzi wake kubadili vichwa kwa maana ya kubadili namna zetu za kufikiri na kutenda, ni kuongozwa na mantiki mpya. (Mathayo 5:38-42) Mwasisi wa Taifa la India, Gandhi aliwahi kusema: “Kama tutatumia sheria ya kale, ya jicho kwa jicho, basi ulimwengu mzima sote tungekuwa vipofu.” Ndio kusema kila mmoja wetu ni mkosefu na mkosaji, hivyo dawa pekee ni upendo na msamaha.

Watu wanahitaji kujipatanisha na Mungu katika maisha
Watu wanahitaji kujipatanisha na Mungu katika maisha

Hata marabi au walimu wa Kiyahudi wakati wa Yesu walifundisha katika Talmudi kuwa ikiwa mtu anataka kukuua, basi hata usichukue muda kutafakari bali muwahi kwa kumuua yeye. Mafundisho ya namna hii kwa kweli hayakupata ukinzani wowote kwani yanaendana na mantiki ya kufikiri na kutenda ya dunia hii. Sasa leo tunaona Yesu anatuambia wanafunzi wake: “…Msishindane na mtu mwovu” ni kinyume na ius talionis, ile sheria ya kulipiza kisasi kila tunapokosewa au kutendewa jambo baya. Yesu analiweka hili fundisho lake kinagaubaga kwa kutoa mifano minne katika maisha yetu ya kila siku. Ndio kusema ni fundisho lenye uzito na umuhimu mkubwa. Mfano wa kwanza, Yesu anasema anayekupiga shavu la kulia basi umgeuzie na la kushoto. Kwa kweli yafaa kuelewa vema fundisho hili la Yesu kwani kwa Wayahudi kofi kwa shavu la kulia, ni sawa na kusema kutendewa ubaya mkubwa au shambulio la mwili. Hivyo adhabu yake ilipaswa kuwa malipo ya karibu mshahara wa mwezi mzima. Yesu anatualika wanafunzi na wafuasi wake si tu kuwa wema zaidi au wapole bali kugeuza na shavu la kushoto.  Si kwamba Yesu anatutaka kuishi na kuenenda kama wajinga, la hasha bali kuwa watu wa msamaha na kamwe kutolipiza kisasi. Uovu hauondolewi kwa uovu mwingine bali daima kwa msamaha. Kuondoa uovu kwa kulipiza uovu ni kuongeza uovu na maovu duniani, hivyo ni kwa njia ya msahama na upendo uovu unaondolewa duniani.

Jamii ijikite katika misingi ya haki, amani na maridhiano
Jamii ijikite katika misingi ya haki, amani na maridhiano

Yesu haishii hapo bali pia anatoa mfano mwingine unaogusa upande wa uchumi. Kwa desturi nyakati za Yesu, Wayahudi walivaa mavazi mawili, yaani kanzu ndefu la mikono mifupi au mirefu na juu yake walitupia pia joho. Joho lilivaliwa hasa nyakati za baridi lakini pia lilivuliwa wakati mmoja anapofanyakazi. Kwa watu maskini si tu joho lilivaliwa nyakati za mchana bali pia lilitumika kama blanketi hata nyakati za kulala usiku. (Kutoka 22:25-26). Ndio kusema kuwa mfuasi wa Yesu anayeenda kushitaki kwa kutorudishiwa kanzu lake, kama vile kanzu ilivyokuwa vazi la kwanza au vazi la ndani lililomstiri mtu, huyu anakuwa amenyang’anywa au ameondolewa vyote alivyokuwa navyo na kuachwa bila kitu. Ni mtu anayebaki uchi, kwa maana bila mali, bila kitu kingine chochote. Anabaki vile alivyozaliwa kwa kuporwa na kunyang’anywa mali zake zote. Mfuasi wa Yesu anaalikwa si tu kukubali kuporwa kanzu bali atoe na joho pia, abaki uchi kama vile Bwana na Mwalimu wetu alivyobaki pale juu msalabani.  Bado Yesu anatualika kuwa watu wa msamaha na kuenenda sio kwa mantiki ya ulimwengu huu bali daima kuongozwa na mantiki ya Injili.

Kanisa liwe ni chombo cha upatanisho
Kanisa liwe ni chombo cha upatanisho

Yesu bado anatupa mfano wa tatu ndio matumizi mabaya ya madaraka. Nyakati za Yesu ilikuwa desturi kwa watawala na hasa maaskari wa Kirumi na hata baadhi ya wakubwa wa Kiyahudi walilazimisha watu kubeba mizigo yao. Hapa tutakumbuka Simoni wa Kirene alipolazimishwa kuubeba msalaba wa Yesu katika masimulizi ya Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo.  (Mathayo 27:31) Ikiwa Wazeloti waliwafundisha watu kupinga unyanyasaji wa aina hii, kwa upande mwingine Yesu anawaalika wafuasi wake kuongozwa na mantiki ya msamaha na upendo hata kwa watesi wetu. Mfano wa nne ndio ule wa mtu anayekuja kwa kukopa. Na hapa yafaa tuelewe si tu pesa bali anayekuja kwangu na kwako kwa shida yeyote ile. Ndio Yesu anatualika kutokumgeuzia uso, kwa maana kutokuwa tayari kumsaidia au kwa kuangalia je ninanufaika nini binafsi? Mfuasi wa Yesu daima anaalikwa kutenda wema bila kusubiri au kungojea faida binafsi. Ni kupenda bila kuweka masharti, ni kupenda kama Mungu anavyopenda kama ambavyo tutaona mwaliko wa Yesu kwetu kuwa tuwe wakamilifu na watakatifu kama Baba yetu wa Mbinguni. Na mfano wa mwisho ndio juu ya amri ya upendo yenye pande mbili, kumpenda jirani na kumchukia adui.

Kanisa liwe ni chombo cha huruma ya Mungu
Kanisa liwe ni chombo cha huruma ya Mungu

Tunaposoma Maandiko ile ya kwanza kumpenda jirani tunaiona katika (Mambo ya Walawi 19:18) bali ya kumchukia adui kwa kweli haipo bali hapo Yesu anafanya rejea kwa mantiki iliyekuwepo nyakati zile na kwa kweli si tu nyakati zile bali hata zetu leo. (Zaburi 137:7 – 9) “…Ee Babiloni, mharibifu wee! Heri yule atakayekulipiza mabaya uliyotenda! Heri yule atakayewatwaa watoto wako na kuwapondaponda mwambani.” (Zaburi 139:12- 22 na hasa aya ile ya 19) “…Laiti, ee Mungu, ungewaua watu waovu! Laiti watu waovu wangeondoka kwangu! Wanasema vibaya juu yako, wanasema maovu juu ya jina lako. Ee Mwenyezi Mungu nawachukia wanaokuchukia; nawadharau sana wale wanaokuasi! Adui zako ni adui zangu; ninawachukia kabisa kabisa”.  Hivyo Yesu anarejea mtindo wa kufikiri kama tuliousoma kutoka kitabu cha Mzaburi na kwa kweli hatuna budi kukiri hata baadhi yetu leo bado tunafikiri tuna haki ya kumchukia adui yetu au adui wa Mungu. Lakini tunasoma pia hata katika Agano la Kale mwito wa kutolipiza kisasi au kulipa uovu kwa uovu. (Kitabu cha Methali 24:29) “Usiseme ‘Nitamtenda kama alivyonitenda! Ni lazima nilipize kisasi!” (Kutoka 23:5) “Ukimwona punda wa mtu anayekuchukia ameanguka na mzigo wake, msaidie mtu huyo kumsimamisha punda wake, wala usimwache na kwenda zako”.

Huruma ya Mungu isaidie kuondokana na kulipiza kisasi.
Huruma ya Mungu isaidie kuondokana na kulipiza kisasi.

Kama Mungu alivyo na maadui nasi hakika tutakuwa na maadui, watakuwepo wanatuchukia na hata kututakia mabaya iwe katika familia zetu, jumuiya zetu, mahali pa kazi na kadhalika na kadhalika, lakini sisi tunaalikwa kufafa na Baba yetu wa mbinguni. Kama vile Mungu hamchukii yeyote, basi nasi tunaalikwa kuwapenda hata wale wanaotuchukia na kutunenea na kututakia mabaya katika maisha yetu. Ni ngumu ni kweli lakini tunaweza kuliishi fundisho hili kwa msaada wa neema za Mungu mwenyewe. Yesu anakwenda mbali zaidi si tu kuwapenda maadui zetu bali pia kuwaombea maadui.  Ndio kusema hapa Yesu anatualika nasi kufanana na Mungu mwenyewe aliye upendo kwa asili. Kupenda kama Mungu anavyopenda, ndio kupenda bila masharti. Mungu anapenda hata adui zake, hata waovu, hata wanaompinga na kukataa uwepo na uweza wake, ndivyo nasi tunaalikwa kupenda bila kuweka sharti lolote lile, si kwa sababu ni ndugu au jamaa au rafiki au wanaotunenea mema bali kupenda kama Mungu anavyotupenda wote. Amri hii na maagizo haya ya Yesu si tu magumu kwetu leo na hasa hili la kupenda na kuwaombea maadui, bali hata kwa waamini wa karne za mwanzoni kila mara walitafsiri kwa namna zao ila yafaa ieleweke kuwa hakuna tafsiri nyingine bali ni mwaliko wa kupenda kama Mungu anavyotupenda bila kuangalia hali zetu za ndani au nje, bila kuangalia mahusiano yetu na Yeye aliye muumba wetu.

Jifunzeni kusamehe na kusahau
Jifunzeni kusamehe na kusahau

Kumwombea adui, kuomba ni kunyanyua mioyo yetu kumwelekea Mungu, ni kukubali mapenzi ya Mungu katika maisha yetu, ni kutaka kunena lugha moja na Mungu, kama ndivyo basi ni kwa njia hiyo pekee nasi tunaweza kupenda kama Mungu, kufikiri na kutenda kwa kuongozwa na mantiki ile itokayo juu. Anayesali au kuomba ananyanyua macho yake juu, anataka naye kufikiri na kutenda kwa kuongozwa na mantiki ile ya Mungu na ni kwa njia hiyo pekee nasi tunaweza kuwapenda hata walio adui zetu. Hata adui yule asiyekutakia kabisa lolote jema katika maisha, aliyekuachia kidonda na jeraha lisilopona katika maisha yako, yule ambaye hata sasa bado anataka hata kuondoa maisha na uhai wako, adui tunaalikwa kumpenda na kumsamehe na zaidi sana linawezekana tu kwa kuwaweka katika sala na maombi yetu, ni kwa msaada wa neema za Mungu tu nasi tunaweza kufikiri na kutenda kama Mungu. Si kwa akili zetu wala nguvu zetu tunaalikwa kuishi tunu za Injili bali hatuna budi kujitegemeza katika neema za Mungu mwenyewe. Iweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu kama nilivyotangulia kusema hapo juu, ni mwaliko wa kupenda kama Mungu anavyotupenda sote bila kuweka masharti fulani fulani.  Ukamilifu wetu si kwamba hatuna dhambi au hatutendi uovu bali ni katika kupenda kama Mungu anavyopenda, ni katika kuongozwa na mantiki ile ya kimungu katika maisha yetu. Nawatakia tafakari njema na Dominika takatifu. Shavua tov!

14 February 2023, 11:48