Tafuta

Tafakari Neno la Mungu Domikina ya 7 ya Mwaka A wa Kanisa Tema kuu: Amri kuu ya mapendo na maisha ya utakatifu Tafakari Neno la Mungu Domikina ya 7 ya Mwaka A wa Kanisa Tema kuu: Amri kuu ya mapendo na maisha ya utakatifu 

Tafakari Dominika ya 7 ya Mwaka A wa Kanisa: Upendo na Maisha ya Utakatifu

Tukitaka kuupata ufalme wa Mungu sharti tuwe watakatifu. Viashiria vya kuwa watakatifu ni kuishika na kuiishi vyema amri kuu ya mapendo: Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa nguvu zako zote na kwa akili zako zote (Kumb 6:5) na Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe (Wal 19:18). Amri hii inatutaka tuwe na moyo wa unyenyekevu ili tuweze kuishi.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 7 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Katika mpangilio wa kiliturujia mwaka huu, dominika hii ya 7 Mwaka A, 2023 inafunga sehemu ya kwanza ya kipindi cha kawaida tutakachoendelea nacho baada ya Pasaka kwa dominika ya 11. Kumbe Jumatano ijayo baada ya dominika ya 7, itakuwa ni Jumatano ya Majivu inayofungua kipindi cha Kwaresima kwa maandalizi ya Pasaka. Kwa minajili hiyo, masomo ya dominika ya 8, 9 na 10 Mwaka A kipindi cha kawaida hatutayatafari kwasababu dominika ya 8 tutaadhimisha Sherehe ya Pentekoste, ya 9 tutaadhimisha Utatu Mtakatifu na ya 10 tutaadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu. Masomo ya dominika tano zilizopita kipindi cha kawaida yaani dominika ya 2, 3, 4, 5 na 6 mwaka A yalitukumbusha mambo muhimu katika maisha yetu ya kikristo na ufalme wa Mungu ambayo ni vyema kujikumbusha ili kujiandaa vyema kuanza kipindi cha Kwaresima. Dominika ya 2 tulifundishwa kuwa Yesu ni Nuru ya ulimwengu na Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu. Nasi kwa ubatizo tumeondolewa dhambi ya asili na adhabu zake zote pamoja na dhambi zingine na tumewekwa kuwa nuru kwa mataifa kwa maneno na matendo yetu ili kwayo watu wengine wamjue, wampende na kumtumikia Mungu na mwisho sote kwa pamoja tupate kustahilishwa kuurithi ufalme wa mbinguni. Dominika ya 3, tulikumbushwa kuepuka nafasi za dhambi na kujiweka chini ya utawala wa upendo wa Mungu.

Uwepo wa dhambi, toba na wongofu wa ndani
Uwepo wa dhambi, toba na wongofu wa ndani

Dominika ya 4, iliweka mbele yetu heri nane ambazo ni mhutasari wa katiba ya maisha ya kikristo inayotudai kuwa maskini wa roho, wapole, wanyenyekevu, wenye huruma, watu wa amani, wenye upendo, walio tayari kuteseka kwa ajili ya Kristo. Dominika ya 5, tulifundishwa kuwa kama ilivyo kazi ya chumvi kwa chakula na mwanga kwa maisha ndivyo tunavyopaswa kuwa sisi wakristo kwa watu wengine duniani ili nao waujue ufalme wa Mungu. Dominika ya 6 tukafundishwa juu ya uhuru wetu binadamu katika kuzishika na kuziishi Amri na sheria za Mungu katika maisha yetu kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Masomo ya dominika hii ya 7 Mwaka A wa Kanisa yanasisitiza kuwa tukitaka kuupata ufalme wa Mungu sharti tufanane na Mungu, tuwe watakatifu kama yeye Mungu Baba yetu wa mbinguni alivyo mtakatifu. Viashiria vya kuwa watakatifu ni kuishika na kuiishi vyema amri kuu ya mapendo: Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa nguvu zako zote na kwa akili zako zote (Kumb 6:5) na Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe (Wal 19:18). Amri hii inatutaka tuwe na moyo wa unyenyekevu ili tuweze kuishi vizuri na watu wa aina zote hata maadui zetu: “Nawaambieni; wapendeni maadui zenu na waombeeni wale wanaowadhulumu” (Mt 5:44). Na hii amri kuu ya mapendo inaambatana na fadhila za huruma na msamaha. Kipimo cha amri hii ni upendo wa Mungu kwetu sisi aliyetuumba kwa sura na mfano wake na kutufunulia upendo wake kwa njia ya Yesu Kristo. Yeye ndiye kioo cha namna ya kupendana; “Pendaneni kama mimi nilivyowapenda ninyi” (Yoh 13:34).

Amri kuu: Upendo kwa Mungu na jirani.
Amri kuu: Upendo kwa Mungu na jirani.

Somo la kwanza ni la katika Kitabu cha Mambo ya Walawi (Wal 19:1-2, 17-18). Katika somo hili Mungu kwa kinywa cha Musa anawataka Waisraeli, taifa lake teule, waishi kitakatifu, wawe watakatifu kama yeye Mungu wao alivyo Mtakatifu, wadumishe uhusiano wao kati yao na yeye Mungu wao kwa kuishika sheria/amri kuu ya mapendo, wasichukiane wao kwa wao, kila mmoja asimchukie mwenzake kwa dhambi zake, wala asilipize kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wao, bali kila mmoja ampende jirani yake kama nafsi yake. Hivi ndivyo tunavyopaswa kuishi sisi Wakristo. Somo la pili ni la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 3:16-23). Somo hili ni mwendelezo wa maonyo na mashauri ya Mtume Paulo kwa wakristo wa Korintho kutokana na mafarakano yaliyokuwepo katika jumuiya yao. Mtume Paulo anawasihi wawe na umoja kwa vile Roho Mtakatifu anakaa ndani yao. Nasi tukizusha mafarakano kati yetu tunaharibu hekalu la Mungu. Paulo anasema; Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo sisi tuliobatizwa kwa maji na roho mtakatifu. Kama mzaburi anavyotuambia kumjua Mungu ni mwanzo wa hekima ndivyo anavyosisitiza mtume Paulo kuwa tusijione wenye hekima bali tujinyenyekeshe mbele za Mungu tupate kuhekimishwa kwa hekima yake maana hekima ya dunia hii ni upuuzi mbele za Mungu.

Lipeni uovu kwa kutenda mema
Lipeni uovu kwa kutenda mema

Injili ni ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 5:38-48). Katika sehemu hii ya Injili, Yesu anatoa mafundisho mazito ambayo yanabadilisha kabisa mtazamo wa maisha ya kale yaliyoongozwa na sheria kandamizi na za ubaguzi za kulipiza kisasi katika agano la kale. Somo hili ni mwendelezo wa maendeleo ya amri ya mapendo katika somo la kwanza la kitabu cha mambo ya walawi. Yesu anakazia kupendana bila kubaguana kiasi cha kumpenda hata adui zetu ndiyo amri kuu ya mapendo. Hivyo tusishindane na mtu mwovu, tusilipe ovu kwa ovu, bali tuushinde uovu kwa wema. Yesu anasisitiza maisha ya kusaidiana na kusameheana akisema; “Na mtu atakayekushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili. Akuombaye, mpe; naye atakayekukopa kwako, usimpe kisogo, waombeeni wanaowaudhi; ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru; Je! nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, Je! nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.”

Heri Maskini wa Roho Maana Ufalme wa Mbinguni ni wao
Heri Maskini wa Roho Maana Ufalme wa Mbinguni ni wao

Ili kuelewa vizuri mafundisho haya ya Yesu ni vizuri kurejea katika sheria za Agano la kale hasa zile zilizowahusu maadui wa wana wa Israeli. Itakumbukwa kuwa Waisraeli walipokuwa wakisafiri kutoka Misri kwenda nchi ya ahadi walikutana na mataifa mbali mbali yaliyoishi jangwani kama wayebusi, waamaleki, wakanaani, wahiti, wafilisti na kadhalika. Mataifa haya yalikuwa na sheria, desturi na tamaduni zao. Waisraeli waliiga baadhi ya sheria na tamaduni zao. Moja ya sheria ni ya familia kulipiza kisasi. Hii ilitokea wakati mwanafamilia alipouawa kwa kuonewa, ndugu mwanamume wa karibu katika ukoo wa aliyeuawa alipaswa kulipiza kisasi kwa kumwua yule aliyesababisha kifo cha ndugu yake. Sheria hii ilisema hivi; “Mlipiza kisasi cha damu atamwua mwuaji, wakati akikutana naye, atamwua” (Hes 35:19). Jambo baya zaidi katika sheria hii ya familia ya kulipiza kisasi, ni kwamba siyo mwuaji tu bali pia familia yake yote ingeweza kuuawa kama yule ndugu wa damu alikuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Sheria hii iliingizwa katika maandiko matakatifu kwa sababu maisha ya wakati huo yalikuwa ya kikatili na ndugu katika familia walipaswa kulindwa kwa kila njia. Musa alichukua sheria hii katika mazingira yale na kuiingiza katika Torati kama onyo kwa waisraeli wasije wakajiingiza katika vitendo vya uhalifu na mauaji. Licha ya kuwa kosa hili walishalifanya wana wa Yakobo baada ya dada yao Dina kubakwa kule shekemu ambapo waliwaua wanaume wote na kuwachukua wake na watoto wao kama mateka (Mwanzo 34). Na kama ilitokea mwisraeli alifanya kosa hilo la kuua, kulikuwa na miji iliyotengwa kwa aliyeua kuweza kukimbilia ili asije akauawa (Hes 35: 9-33).

Iweni watakatifu kama Baba Yenu wa Mbinguni
Iweni watakatifu kama Baba Yenu wa Mbinguni

Baadae sheria hii ya familia kulipiza kisasi ilifanyiwa marekebisho, badala ya kumuua mwuaji, adhabu nyingine ziliwekwa na fidia ilidaiwa kutoka kwa aliyetenda kosa lile au kutoka kwa familia yake. Mabadiliko yaliifuata sheria ya zamani ya Talioni iliyoanzishwa na Mfalme Hammurabi. Sheria hii ilisema kuwa kulipiza kisasi hakupaswi kuzidi uzito wa kosa alilotenda mhalifu. Musa aliichukua sheria hii ya Hammurabi iwe mwongozo kwa waisraeli katika swala la kulipiza kisasi na hivyo kusema; “Msionyeshe huruma, uhai kwa uhai, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu” (Kumb 19:21). Kwa hiyo katika kulipiza kisasi, usiende zaidi ukalipa zaidi ya dhara lililokupata. Baadaye sheria ya kulipiza kisasi ilionekana haina maana miongoni mwa waisraeli. Kwa hiyo Musa aliifanyia marekebisho tena kwa maelezo ya somo la kwanza la dominika hii ya 7 mwaka A akisema; usimchukie ndugu yako, wala usimlipize kisasi, umpende kama unavyojipenda mwenyewe (Wal. 19:17-18). Lakini maelekezo haya yalilenga kuwalinda waisraeli na watu walikaa kati yao na kukubali kuifuata dini ya kiyahudi na utamaduni wao. Ndiyo maana sharia nyine ilisema; “Kama mgeni akiishi nanyi katika nchi yenu, msimdhuru, mnapaswa kumchukulia kama mmoja wenu na kumpenda kama ninyi wenyewe” (Wal 19:34). Kwa upande mwingine sheria ya kisasi iliendelea kutumika kwa watu wasio waisraeli au wapagani. Pale mpagani alipomkosea mwisraeli, sheria ya kisasi ilitumika. Kumbe wapagani hawakuchukuliwa kama jirani zao.

Tujitahidi kutenda yale yanayo mpendeza Mungu
Tujitahidi kutenda yale yanayo mpendeza Mungu

Sisi tuliobatizwa, tukamkataa shetani na fahari zake zote, na tukaahidi kumfuata Yesu Kristo aliyetoa maisha yake ili sisi tukombolewe kutoka utumwa wa dhambi tunapaswa kuiishi amri kuu ya mapendo bila ubaguzi wowote kwa maneno na matendo. Ndiyo maana katika sala ya koleta Padre anasali kwa niaba ya waamini akisema; “Ee Mungu Mwenyezi, tunakuomba utujalie kuwaza daima mambo yanayofaa, na kutimiza kwa maneno na matendo yanayokupendeza”. Basi tujitahidi kuishi ahadi zetu za ubatizo katika ukamilifu wake bila kuongeza wala kupunguza lolote katika maongozi ya Yesu ili tupate wokovu katika yeye kama mzaburi anavyoimba katika wimbo wa mwanzo akisema; “Nami nimezitumaini fadhili zako; moyo wangu na uufurahie wokovu wako. Naam, nimwimbie Bwana, kwa kuwa amenitendea kwa ukarimu” (Zab. 13:5-6). Pale tunapokosea na kuanguka katika dhambi tusibaki dhambini bali tuwe wepesi wa kusimama na kuomba msamaha kwa tuliowakosea na kuungama dhambi zetu mara moja maana Mungu wetu ni mwenye huruma atatusamehe kama tunavyoimba katika zaburi ya wimbo wa katika tukisema; “Bwana amejaa huruma na neema, haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhila, hakututendea sawasawa na hatia zetu, wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote, aukomboa uhai wako na kaburi, akutia taji ya fadhili na rehema” (Zab. 102:8, 10). Tumuombe Mungu Roho mtakatifu atuangazie tuweze kuyaishi haya mafundisho vyema ili siku moja tukayaishi katika ukamilifu wake huko mbinguni aliko Mungu Baba yetu. Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika 7 A
15 February 2023, 15:08