Tafuta

Kwaresima ni kipindi cha majiundo ya kiroho kwa kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kukuza fadhila mbalimbali hasa fadhila za haki, kiasi, huruma na kujiimarisha zaidi kiimani Kwaresima ni kipindi cha majiundo ya kiroho kwa kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kukuza fadhila mbalimbali hasa fadhila za haki, kiasi, huruma na kujiimarisha zaidi kiimani  (©SirioCarnevalino - stock.adobe.com)

Tafakari Dominika ya Kwanza ya Kwaresima Mwaka A: Majaribu ya Imani!

Kwaresima ni kipindi muafaka cha majiundo ya kiroho kwa kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kukuza fadhila mbalimbali hasa fadhila za haki, kiasi, huruma na kujiimarisha zaidi kiimani sanjari na kujenga mafungamano na muunganiko na Mungu wetu mtakatifu kwa kuwatumikia waliodhaifu na wahitaji ili tuweze kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa upendo na haki.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima mwaka A wa Kanisa, siku ya 5 ya majiundo ya kiroho kwa kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kukuza fadhila mbalimbali hasa fadhila za haki, kiasi, huruma na kujiimarisha zaidi kiimani na kujenga mafungamano na muunganiko na Mungu wetu mtakatifu kwa kuwatumikia waliodhaifu na wahitaji ili tuweze kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa upendo. Kipindi hiki tulikianza siku ya Jumatano ya Majivu tulipopakwa majivu katika paji la uso. Tendo hili takatifu la kiroho ni ishara ya toba ya kweli. Ndivyo unavyotualika wimbo wa mwanzo ukisema; “Ataniita nami nitamwitikia; nitamwokoa na kumtukuza; kwa siku nyingi nitamshibisha” (Zab. 91:15-16). Masomo ya dominika ya kwanza ya Kwaresima yanatueleza juu ya uwepo wa vishawishi na majaribu katika maisha yetu ya kila siku tukiwa safarini kuelekea mbinguni. Hivyo hatuna budi kujiandaa kikamilifu ili tuweze kuvitambua na kukabiliana navyo. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Mwanzo (Mwa   2:7-9, 3:1-7.) Somo hili linahusu simulizi la anguko la kwanza la mwanadamu. Nyoka amewekwa kama mfano wa kishawishi na majaribu.  Katika somo hili tunapata ufahamu wa chanzo na asili ya magonjwa, mateso na kifo katika maisha ya mwanadamu ni matokeo ya dhambi ya asili. Hii ni dhambi ya kutotii amri na maagizo ya Mungu iliyotendwa na Adamu na Eva – wakiwakilisha binadamu wote.

Jangwani ni mahali pa mapambano ya maisha, sala na kufunga
Jangwani ni mahali pa mapambano ya maisha, sala na kufunga

Hii ni dhambi ya kujiamulia lipi ni jema na lipi na baya. Ni dhambi ya kuchukua nafasi ya Mungu. Mungu alimuumba mtu mzima, mwili na roho, akampa maisha ya heri na amani bila kufa. Hali hii ingedumu tu iwapo mtu angejinyenyekea chini ya mapenzi ya Mungu. Walakini mtu alimwasi Mungu. Kilichotokea kwa Adamu na Eva baada ya kumwasi Mungu kwa kukosa utii ndicho kilichotokea kwetu kwani asili yetu ilikuwa ndani mwao; biblia inasema; baada ya kutenda dhambi, Adamu na Eva walitambua kuwa walikuwa uchi (Mw 3:7). Uchi unawakilisha hali ya udhaifu, hali ya kutojiweza, hali ya kupoteza neema na kuwa mbali na Mungu. Kwaresma ni kipindi cha kijiweka karibu zaidi na Mungu. Kilichotokea kwa Adamu na Eva baada ya kukosa utii ndio kilichotokea kwetu; biblia inasema; baada ya kutenda dhambi Adamu na Eva walitambua kuwa walikuwa uchi (Mw. 3:7). Uchi unawakilisha hali ya udhaifu, hali ya kutojiweza, hali ya kupoteza neema. Uchi unaoongelewa hapa sio aibu aipatayo mtu anapoonekana bila nguo hadharani, bali ni hali ya kutojiweza kabisa, hali ya udhaifu ya Adamu na Eva walioipata baada ya kukosa utii kwa Mungu. Walipojitenga na Mungu walijisikia hawana uwezo wa kumrudia Mungu walikuwa dhaifu kabisa. Hata sisi pia tunakuwa hivyo; kwa kujitenga na Mungu, dhambi inatufanya dhaifu kabisa tusio na uwezo wa kumwona Mungu kati yetu, tusio na uwezo wa kumrudia Mungu na kuongea naye.

Yesu aliongozwa jangwani na Roho Mt. kwa siku 40
Yesu aliongozwa jangwani na Roho Mt. kwa siku 40

Somo la pili ni Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum 5:12-19.) Katika somo hili Mtume Paulo anatueleza jinsi Mungu katika hekima yake na upendo wake alivyogeuza ubaya wa mwanadamu kuwa wema na alivyobadili laana ya mwanadamu kuwa baraka ya thamani kwa njia ya mateso na kifo cha mwanae Yesu Kristu. Kumbe, Adamu wa kwanza aliingiza hali ya dhambi na mauti katika dunia hii na Adamu wa pili, yaani Yesu Kristo, alileta neema inayoshinda dhambi na mauti. Ndiyo maana katika sala ya koleta Padre anasali; “Ee Mungu Mwenyezi, utujalie tuzidi kuifahamu siri ya Kristo na kupata manufaa yake katika mwenendo wetu mwema kwa mfungo wa Kwaresima wa kila mwaka.” Injili niile  ilivyoandikwa na Mwinjili Mathayo (Mt 4:1-11). Kila jumapili ya kwanza ya Kwaresima, Injili husimulia jinsi Yesu alivyojaribiwa na Shetani na kuvishinda vishawishi vyake. Hii ni kutuambia kwamba kwaresma ni kipindi cha kupambana na majaribu na vishawishi vya shetani katika maisha yetu ya kikristo. Silaha za kupambana na shetani na kumshinda ni sala, mafungo na toba ya kweli. Ndiyo maana utangulizi wa dominika hii ya kwanza ya kwaresma unasema; “Yeye alifunga chakula siku arobaini, akaonyesha ubora wa namna hiyo ya kufanya kitubio. Amewaepusha watu wote na hila za nyoka wa kale na kutufundisha kushinda chachu ya uovu”. Adamu alishindwa na kishawishi; Waisraeli jangwani walishindwa pia na kishawishi. Lakini Yesu alikishinda kishawishi kwa kupinga wazo la kujitakia enzi ya kibinadamu na kumdharau Mungu; alijiweka chini ya Mungu na akatimiza mapenzi yake. Ndivyo nasi tunavyopaswa kufanya katika maisha yetu.

Yesu kwa Siku 40 alifunga na kusali
Yesu kwa Siku 40 alifunga na kusali

Yesu baada ya ubatizo wake mtoni Yordani aliongozwa na Roho Mtakatifu kwa muda wa siku arobaini nyikani akifunga na kusali. Itakumbukwa kuwa namba 40 kibiblia inamaanisha mda wa kutosha wa maandalizi. Gharika ilichukua siku 40 (Mw. 7:17-20), Noa alimtoa Kunguru ndani ya safina siku ya arobani (Mw. 8:6). Kwaresima ni kipindi che kukumbuka ahadi za ubatizo wetu tulipokufa kuhusu dhambi na kuzaliwa upya katika roho. Musa alikaa mlimani siku 40 kupokea amri kumi za Mungu (Kut. 24:16-18). Kwaresma ni kipindi cha kuzipokea, kuzitafakari na kuziishi amri za Mungu. Waisraeli walikaa jangwani miaka 40 wakiongozwa na Mungu katika maisha mapya ya watu huru (Mw. 40:36-38; Kumb. 2:7). Kwaresima kipindi cha kukubali kuongozwa na Mungu katika maisha mapya. Nabii Elia alitembea siku 40 kufika mlima Horebu baada ya kula na kunywa chakula alicholetewa na malaika wa Mungu (1Waf. 19:3-8). Kwaresima ni kipindi cha kilishwa chakula cha kiroho ili tupate nguvu za safari ya kuelekea mbinguni. Waninawi walifunga siku 40 na kubadili maisha yao hata Mungu akaghairi adhabu aliyotaka kuwatenda (Yona 31:1-4). Kwaresima ni kipindi cha mabadiliko ya maisha ya kiroho. Ni kipindi cha toba na wongofu. Wafalme wakuu wa Israeli waliongoza miaka 40: Saul aliongoza miaka 40 (Mdo 13:21); Daudi miaka 40 (1Waf. 2:11), Solomoni miaka 40 (1Waf.11:41), Esau alioa akiwa na miaka 40 (Mwa. 25:20). Kwaresima ni kipindi cha kukubali kuongozwa na Mungu.

Kwaresima ni kipindi cha kukubali kuongozwa na Mungu.
Kwaresima ni kipindi cha kukubali kuongozwa na Mungu.

Namba arobaini inaendelea. Maisha ya Musa yamegawanyika katika sehemu kuu tatu kila moja ikichukua miaka 40 ambapo alipokimbia kutoka Misri alikuwa na miaka 40, alikuwa na miaka 80 alipowatoa waisraeli Misri (Kut. 7:7), na alikufa akiwa na miaka 120 (Kumb. 34:7), wapelelezi wa Israeli katika nchi ya Kaanani walichukua siku 40 (Hesabu 13:25), na waisraeli walikaa miaka 40 ya amani chini ya waamuzi (Waamuzi 3:11, 30). Na Yesu alikaa jangwani siku 40 akifunga na kusali (Mt. 4:2) na baada ya kufufuka aliwatokea wanafunzi wake kwa siku 40 akiwaimarisha kabla ya kupaa mbinguni (Mdo 1:3.) Katika mazingira hayo ya upweke, kufunga na kusali kwa muda wa siku 40, shetani anamjaribu na kumshawishi Yesu. Kishawishi ni nini? Kishawishi ni mvuto au msukumo kutoka ndani au nje ya mtu, unaomvuta au kumsukuma kutenda jambo zuri au baya. Vishawishi, mara nyingi hutujia katika namna mbili: Kwanza, tunasukumwa na vionjo vya miili yetu. Miili yetu inawaka tamaa mbalimbali kama vile kula au kunywa, kupenda au kupendwa, au kufanya chochote kile ambacho mwili unadai ufanye na kukusukuma kutoa uamuzi. Pili, tunashawishiwa na kuvutwa na watu wengine kutenda jambo fulani. Ushauri huo unaweza kuwa mzuri au mbaya.

Kishawishi cha kutaka kujimbafai
Kishawishi cha kutaka kujimbafai

Kishawishi cha kwanza ni kuonyesha mamlaka na uwezo, kwa kuamuru jiwe liwe mkate. Katika jaribu hili, shetani anamshawishi Yesu abadili mwelekeo wa kazi yake ya kumkomboa mwandamu kutoka utumwa wa dhambi, kuelekea zaidi katika utumwa wa mahitaji ya kimwili kwa kumwambia afanye muujiza wa kubadili jiwe kuwa mkate ambao ndio mahitaji ya kila siku. Ndivyo alivyomjaribu Eva na kumwambia; “Ati!  Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani?” Ni wazi hakuna maisha bila chakula cha kimwili. Lakini Yesu anatufahamisha kuwa binadamu sio mwili tu ana roho ndani mwake na roho ndiyo itiayo uzima. Hivyo hatuishi kwa mkate tu, yaani mahitaji yetu ya kimwili peke yake bali tunahitaji pia chakula cha kiroho tunachokipata kwa kufanya mapenzi ya Mungu. Ndiyo maana Yesu anasema; “chakula changu ni kuyafanya mapezi ya Mungu”. Jaribu hili la miujiza limetushika kwelikweli wakristo wa sasa. Kizazi chetu cha sasa kinalilia miujiza, ya uponyaji wa magonjwa, kuondokana na balaa na mikosi, kupata mume au mke, kupata kazi na mafanikio au kupanda vyeo. Kizazi chetu kinatafuta miujiza kwa kila kitu tunachofanya. Kwaresima hii tufanye mabadiliko, tumrudie Mungu, tufanye toba ya kweli, tutapata Baraka na kibali machoni pake na tutafanikiwa katika maisha yetu.

Msalaba ni kielelezo cha hekima ya Mungu
Msalaba ni kielelezo cha hekima ya Mungu

Kishawishi cha pili ni kutafuta ukuu au utawala kwa kupewa mali kwa kumwabudu shetani. Hili ni jaribu la kutafuta mamlaka, kupenda vitu kuliko kumpenda Mungu. Adamu na Eva waliamua kutokumtii Mungu kwa kula tunda la mti waliokatazwa na Mungu ili wawe sawa na Mungu, wawe na mamlaka juu yao wenyewe. Yesu hakudhubutu kumjaribu Mungu, yeye hakufikiri kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kung’ang’ania (Wafilipi 2:6-11). Yesu hakutaka mamlaka ya kisiasa au utajiri na mali alizoahidiwa na shetani. Yeye alibaki mwaminifu kwa Mungu Baba, akiwa mpole, mnyenyekevu, mvumilivu na mtiifu kwa Mungu, rafiki wa watoto, maskini na wanyonge. Kizazi cha sasa kinatafuta mamlaka, ufahari, na nguvu kwa kila namna hata kwa nguvu za giza na mauaji ya watu wasio na hatia. Kwaresima hii tufanye mabadiliko, tumrudie Mungu, tufanye toba ya kweli, tutapata Baraka na kibali machoni pake na tutafanikiwa katika maisha yetu. Kwaresima hii tusali na tufunge kwa ajili ya dhambi za mauaji ya kinyama kwa binadamu hasa wasio na hatia kwa ajili ya kulinda maslahi na mamlaka yao. Tusali na kufunga kwa ajili ya wanaojitenga na Kanisa kwa kudai wanakarama hasa za kunena kwa lugha na uponyaji. Tusali na kufunga kwa ajili ya wanaotafuta mali kwa njia zisizo halali, wanaojikusanyia mali ambazo wao wenyewe hawawezi kuzimaliza, tulie na kuomboleza, tumrudie Mungu kwa mioyo yetu yote. Hii ndiyo kwaresma yenyewe ambayo Jumatano ya majivu nabii Yoeli alituasa tuifanye toba ya kweli kwa kurarua mioyo yetu wala si mavazi yetu kwa kufunga na kuomboleza.

Neno la Mungu ni dira na mwongozo wa maisha
Neno la Mungu ni dira na mwongozo wa maisha

Majaribu ya Yesu ni kielelezo cha majaribu yetu tunayokutana nayo kila siku katika maisha. Hakuna hata mmoja atakayemaliza maisha ya hapa duniani bila magumu au majaribu yoyote. Udhaifu wetu wa kimwili kama njaa, kiu, uchovu, wivu au tamaa ni majaribu ambayo yanatupatia mahangaiko, huzuni na ugomvi wa kila aina. Vipawa tulivyo navyo kama elimu, uwezo wa kuongea, cheo, au kuponya hutufanya tuwe na majivuno na kusababisha masengenyo, utengano na mauaji makubwa. Kutokana na uwezo au nafasi tulizonazo katika maisha wengine tunajiona ni wa maana sana kuliko wengine na hivyo tunawanyanyasa na kuwakatilia mbali. Hayo yote hutokana na vishawishi vya mali, heshima na mamlaka. Hivyo tutambue kuwa tunakabiliwa na vishawishi vingi vya kila aina. Tunaalikwa kuvitambua vishawishi hivyo na tuwe tayari kukabiliana navyo. Kiongozi wetu Kristo aliyashinda majaribu yote. Nasi tukimtegemea Mungu tutashinda. Tunaweza kuepuka vishawishi kwa kufunga, kutenda matendo ya huruma, kutenga muda wa kuongea na Mungu katika sala binafsi, kushiriki Misa Takatifu na kupokea sakramenti hasa kitubio na Ekaristi pasipo unafiki na kufuru. Basi tuendelee kujiweka chini ya maongozi ya Mungu tukiomba neema na msaada wake ili tudumu katika imani yetu ili Kristo atakapofufuka tufufuke naye tutoke katika makaburi ya dhambi zetu tuuridhi ufalme wa mbinguni tuliotayarishiwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 

Dominika ya 1 Kwaresima
24 February 2023, 16:00