Kwaresima ni safari ya toba na wongofu wa ndani kwenda jangwani huku tukiruhusu tuongozwe na Mungu Roho Mtakatifu! Kwaresima ni safari ya toba na wongofu wa ndani kwenda jangwani huku tukiruhusu tuongozwe na Mungu Roho Mtakatifu!  

Tafakari Dominika ya Kwanza ya Kwaresima: Majaribu ya Yesu Jangwani: Mahusiano!

Kwaresima ni safari ya toba na wongofu kwenda jangwani huku tukiruhusu tuongozwe na Roho Mtakatifu! Dominika ya kwanza ya Kwaresima, Somo la Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 4:1-11 ni juu ya majaribu ya Yesu. Namba 40 katika Biblia ni namba kamilifu, kwa maana si tu kwa kipindi fulani bali siku zote za maisha yake akiwa hapa duniani alijaribiwa na yule mwovu, Shetani.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Kwaresima ni safari ya toba na wongofu wa ndani kwenda jangwani huku tukiruhusu tuongozwe na Mungu Roho Mtakatifu! Dominika ya kwanza ya Kwaresima, Somo la Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 4:1-11 ni juu ya majaribu ya Yesu jangwani kwa siku 40 mchana na usiku. Namba 40 katika Biblia ni namba kamilifu, kwa maana si tu kwa kipindi fulani bali siku zote za maisha yake akiwa hapa duniani alijaribiwa na yule mwovu, na ndio nasi tunaalikwa safari ya siku hizi 40, ni kipindi cha neema tunapoalikwa nasi kusali, kufunga na kutenda matendo ya huruma. Kwa kweli maisha ya kila mfuasi ni safari ya jangwani kama walivyosafiri wana wa Israeli miaka 40 jangwani, Yesu anajaribiwa jangwani kwa siku 40 nasi sasa tunatenga siku hizi 40 za mfungo wa Kwaresima, lakini daima hatuna budi kuongozwa na Roho Mtakatifu kama alivyomuongoza Yesu. Ni kipindi cha neema hivyo hatuna budi kumruhusu Roho wa Mungu atuongeze nasi katika safari hii ya kuwa jangwani kwa siku 40. Mfungo ni kipindi cha kujipa nidhamu ya kiroho dhidi ya uovu na yule mwovu. Somo la Injili ya leo, linatupa maswali mengi, mmoja aliwahi kuuliza swali, wakati Yesu akiongozwa na yule Ibilisi mpaka mnara wa Hekalu la Yerusalemu; ni nani alitangulia mbele ni Yesu au yule mshawishi? Na labda swali hili linafungua maswali mengi mengine; mfano ni mlima gani mkubwa kiasi cha kuwa juu na kuona milki zote za ulimwengu? Iliwezekana vipi au tuna maelezo gani leo ya kisayansi kwa mwanadamu kuweza kufunga bila kula na kunywa kwa siku 40 mchana na usiku? Na je, huyo mshawishi alikuwa katika umbo gani? Na labda ni nani alimsimulia Mwinjili Mathayo masimulizi haya kwa usahihi wake? Na kwa kweli maswali yanaweza kuwa mengi juu ya sehemu ya Injili tuliyoisikia leo. Yafaa kama tulivyotafakari siku nyingine kujua tangu awali aina ya uandishi na nia ya mwandishi.

Yesu kwa Siku 40 alijaribiwa jangwani usiku na mchana
Yesu kwa Siku 40 alijaribiwa jangwani usiku na mchana

Mwinjili Marko simulizi juu ya majaribu ya Yesu analiweka kwa ufupi kabisa katika aya 2 tu, ni kuwa Yesu aliongozwa na Roho Mtakatifu jangwani kwa siku 40 na huko akajaribiwa na Ibilisi. (Marko 1:12-13) Ndio kusema namba 40 haina budi kueleweka kuwa si tu kwa siku hizo tunazoweza kuzihesabu bali siku zote za maisha yake.  Namba 40 ni namba kamilifu inayoonesha siku zote za maisha yake. Hivyo tangu mwanzo yafaa tutambue ni mwaliko wa kuingia jangwani sio kwa kipindi hiki cha Kwaresima tu, yaani cha mfungo wa siku zile 40 ambazo tunaweza kuzihesabu, bali ni mwaliko wa kutambua kuwa maisha yetu yote ni mapambano dhidi ya uovu na yule mwovu. Jumuiya zile za mwanzo za Wakristo walikiri juu ya nyakati ngumu na za majaribu kwa Yesu Kristo.  Na hasa wakati ule akiwa pale juu msalabani: “Saa tisa alasiri Yesu akalia kwa sauti kubwa, akasema, Eloi, Eloi, lema sabakthani? Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” (Marko 15:34) Yawezekana baadhi yetu maneno haya ya Yesu yakawa magumu kueleweka ila yafaa tukumbuke kuwa Yesu hapa alikuwa ananukuu sala ya kutoka Mzaburi kama alivyokuwa akifanya kila mara katika maisha yake (Zaburi 22). Maisha yake na kila wakati yalikuwa ni sala, na hivyo yaliongozwa na Neno la Mungu.

Jangwani ni mahali pa mapambano ya maisha
Jangwani ni mahali pa mapambano ya maisha

Ndio kusema Wakristo wale wa Kanisa la Mwanzo daima walilielewa Agano Jipya kwa kufanya rejea na kuongozwa na Agano la Kale. Na ndiyo aina ya uandishi anayotumia Mwinjili Matayo. Daima kuelewa ujumbe wake hatuna budi kuusoma sehemu nyingi kwa kuhusianisha na Agano la Kale. Kama vile Israeli ilivyokuwa Taifa teule lililoitwa kutoka katika nchi ya utumwa Misri, ndivyo Yesu alivyo mwanapekee wa Mungu, aliyebaki mwaminifu daima katika misheni ya Mungu Baba. Na ndio mtindo wa Haggadah Midrashi unaotumika daima na Mwinjili Mathayo. Ili kuweza kuelewa Agano la Kale hatuna budi kulisoma na kulihusianisha au kupewa mwanga wa Agano la Jipya. Agano la Kale linapata ukamilifu na utimilifu wake katika Nafsi ya Yesu Kristo. Tunaona Yesu katika majibizano yake na yule mshawishi anafanya rejea kwa kunukuu sehemu tatu kutoka katika masimulizi ya kitabu cha Kutoka. Manung’uniko na malalamiko ya wana wa Israeli wakiwa jangwani kwa kukosa chakula na Mungu kuwashushia mana. (Kutoka 16), Tukio la kukosa maji (Kutoka 17), na kuabudu ng’ombe wa dhahabu (Kutoka 32). Hivyo Yesu anatembea na kusafiri na watu wake katika historia yao.  Yesu anajaribiwa majaribu yale yale yaliyowakuta wana wa Israeli wakiwa safarini jangwani. Na ndio Mama Kanisa katika safari hii ya Kwaresima anatualika katika Dominika hii ya kwanza kukumbuka kuwa nasi si tu kwa siku hizi 40 bali siku zote za maisha yetu tutapitia majaribu kama waliyopitia wana wa Israeli na Yesu mwenyewe wakati wa maisha yake hapa duniani. Yesu anapitia majaribu matatu, ni majaribu yanayogusa hasa mambo matatu, mahusiano yetu na vitu (mali), na Mungu na wengine. Hivyo maisha yetu yote yanagusa sehemu kuu hizo tatu, aidha vitu yaani mali, Mungu mwenyewe na wenzetu. Ni kipindi cha neema kujiangalia tena ndani mwetu kila mmoja katika maisha yake ni kwa namna gani tunahusiana na vitu, Mungu na wenzetu.

Baa la Njaa linaweza kukufanya ukapoteza utu na heshima yako
Baa la Njaa linaweza kukufanya ukapoteza utu na heshima yako

Jaribu la kwanza: “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate.” Bila chakula hakuna maisha, kwani chakula kinatuwezesha kuishi maisha ya kibailojia. Kula ni moja kati ya vitenzi vinavyotumika mara nyingi katika Maandiko Matakatifu. Katika Agano la Kale tu linatumika mara 910, hivyo kuonesha ni kwa kiasi gani kula ni jambo la lazima na msingi kwa maisha ya kila mwanadamu. Wana wa Israeli wakiwa jangwani Mungu anawapa mana kutoka mbinguni. Anawaalika kila mmoja kuchukua kiasi kile tu kinachomtosha kwa siku, ndio kusema tayari Mungu anamwandaa mwanadamu kuwa na kiasi na kufikiria wengine katika mahitaji ya siku kwa siku. Tunaona wanakosa imani kwa wema na ukarimu wa Mungu na badala yake wanaanza kujilimbikizia na hivyo kwenda kinyume na maagizo ya Mungu. (Kutoka 16) Kamwe hata nasi leo hatuwezi kutosheka na mali au vitu vya ulimwengu huu kwani jinsi tutakavyozidi kujilimbikizia ndio hamu na shauku ya kupata zaidi na zaidi. Yesu leo anatuonesha kiu na njaa ya kweli haipo katika mali au vitu au vyakula au vinywaji bali kiu yetu na njaa yetu itajibiwa kwa Neno la Mungu, kwa kumsikiliza na kumtii Mungu, ni kwa kuenenda kwa kuongozwa na Neno lake la uzima. Ni kwa kukubali kuongozwa tu na Neno la Mungu hapo tunapata kweli chakula na kinywaji kwa ajili ya nafsi zetu. Kwaresima ni kipindi cha kuingia katika maisha yetu na kuangalia tena upya mahusiano yetu na mali na vitu vya ulimwengu huu. Ni kujiuliza kama maisha yangu na yako mintarafu mali za ulimwengu huu yanaongozwa na mashauri au Roho ile ya Injili, Roho ile anayotualika Yesu kuongozwa nayo si tu siku hizi 40 bali maisha yetu sote.

Jaribu la pili, kuhusu Neno la Mungu
Jaribu la pili, kuhusu Neno la Mungu

Jaribu la pili: “…Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu jitupe chini…imeandikwa usimjaribu Bwana Mungu wako” Ibilisi anamjaribu Yesu, Mwana wa Mungu kwa kunukuu Neno la Mungu, ni Ibilisi anayejipa sura isiyo yake. Lengo la Ibilisi kujaribu mahusiano ya Yesu na Mungu Baba.  Ni majaribu yanayokuja hata katika maisha yetu ya siku kwa siku kama wafuasi wa Yesu. Ni kishawishi cha kuanza kutilia mashaka upendo na uwezo wa Mungu katika maisha yetu. Kama wana wa Israeli walivyotilia mashaka wema na uwezo wa Mungu, hivyo nasi kuna nyakati tunapitia sote katika maisha yetu, yule mshawishi anatutaka tuingie nasi katika mashaka ya namna hiyo.  Mashaka ya kuona Mungu ametuacha na hayupo tena nasi katika safari ya maisha yetu kutokana na dhiki au magumu mbali mbali tunayoweza kuyapitia. Yesu alibaki mwaminifu hata katika nyakati zile ngumu kabisa katika maisha yake, na anabaki kuwa kielelezo kwetu kuwa hata nasi katika maisha yetu kuna nyakati ngumu tunapitia, lakini hatuna budi kubaki waaminifu kwa wema na uwezo wa Mungu. Yesu alibaki daima katika mahusiano mema na Mungu Baba, na ndio anatualika nasi leo kwa njia ya sala kubaki katika mahusiano na Mungu. Sala sio kwa ajili ya kumtaka Mungu atende kama tunavyotaka sisi, bali kumuomba neema na baraka zake ili tuweze kukubali mapenzi yake katika maisha yetu hata yakitutaka kutoa sadaka kubwa.

Jaribu la Tatu: Kumwabudu Ibilisi, Shetani
Jaribu la Tatu: Kumwabudu Ibilisi, Shetani

Jaribu la tatu: “…hivi vyote nitakupa kama ukipiga magoti na kuniabudu…” Ni jaribu hasa juu ya kishawishi cha kuwa wakubwa na watawala, au watu wa maana katika ulimwengu huu, na badala yake Yesu anatualika wanafunzi na rafiki zake kuwa wadogo na watumishi daima. Mara nyingi katika maisha yetu tunajikuta njia panda kati ya ukubwa/utawala na utumishi/udogo. Ni kishawishi cha kuwa watu wa maana, watu wanaotumikiwa na kuabudiwa kwa ukubwa wao bali sisi tunaalikwa kuwa watumishi wasio na faida kwani ni Mungu pekee wa kuabudiwa. Wana wa Israeli wakiwa jangwani wakamwacha Mungu na kujitengenezea mungu wa ndama wa dhahabu, ndio miungu ya mali au vitu vya ulimwengu huu, miungu tunayoitengeneza kwa mikono yetu. Hapa tunaweza kutoa msururu wa mambo au vitu tunavyovigeuza kuwa miungu yetu na kumpa kisogo Mungu wa kweli. Tunapogeukia viumbe na kumwacha Mungu hapo nasi tunageuka kumpigia magoti yule mwovu na kumwasi Mungu wetu Yesu kamwe hakupigia magoti miungu ya dunia hii, iwe watawala wa kisiasa wa nyakati zake, pesa, utumiaji wa silaha na mabavu kwa kujilinda na kujitetea, kusaka urafiki na watu wanaoonekana na kuitwa wa maana katika ulimwengu huu, hata fikra na falsafa za mafanikio kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu bali daima aliongozwa na kuishi Neno la Mungu Baba.

Yesu akabaki imara katika maisha yake hadi kifo cha Msalaba.
Yesu akabaki imara katika maisha yake hadi kifo cha Msalaba.

Katika safari ya siku hizi 40 ni fursa nyingine tunajaliwa tena mwaka huu ili kuangalia maisha yetu ya siku kwa siku mintarafu mahusiano yetu na mali, Mungu na wengine. Ni kipindi cha sala ili tutimize mapenzi ya Mungu, kufunga na matendo ya huruma. Yote lengo na shabaha yake ni ili tuweze kuwa na mahusiano mema zaidi na Mungu na jirani, ni mazoezi ya kiroho yanayotuweka karibu na Mungu na jirani. Kwaresma ni kipindi cha neema kwani kinatuleta tena karibu na Mungu na jirani, Pasaka ni kilele kwani kila anayekula kalamu ile ya Pasaka ni yule anayekuwa na mahusiano mapya na Mungu na jirani. Nawatakia Dominika na tafakari njema! Shavua tov!

23 February 2023, 17:02