Injili inatupa kama kielelezo majaribu ambayo Kristo Yesu mwenyewe aliyapitia na akayashinda na hivi kutuonesha nasi njia ya kuyashinda majaribu tunayokabiliana nayo Injili inatupa kama kielelezo majaribu ambayo Kristo Yesu mwenyewe aliyapitia na akayashinda na hivi kutuonesha nasi njia ya kuyashinda majaribu tunayokabiliana nayo  

Tafakari Neno la Mungu Dominika ya Kwanza Kwaresima Mwaka A: Silaha za Mapambano

Masomo ya dominika hii ya kwanza ya Kwaresima yanaleta mbele yetu dhamira ya vishawishi au majaribu katika maisha. Kwa namna ya pekee, Injili inatupa kama kielelezo majaribu ambayo Yesu mwenyewe aliyapitia na akayashinda na hivi kutuonesha nasi njia ya kuyashinda majaribu tunayokabiliana nayo kila siku katika maisha yetu ya ufuasi: Majaribu: Mali, Sifa na Madaraka.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Tumekianza kipindi cha Kwaresima, kipindi cha toba, wongofu, sala na matendo ya huruma kama njia ya kutuandaa kuliingia fumbo la Mateso ya Kristo ili tuweze kushiriki neema ya ukombozi wake. Masomo ya dominika hii ya kwanza ya Kwaresima yanaleta mbele yetu dhamira ya vishawishi au majaribu katika maisha. Kwa namna ya pekee, Injili inatupa kama kielelezo majaribu ambayo Yesu mwenyewe aliyapitia na akayashinda na hivi kutuonesha nasi njia ya kuyashinda majaribu tunayokabiliana nayo kila siku katika maisha yetu ya ufuasi. UFAFANUZI WA MASOMO KWA UFUPI: Kabla hatujaingia katika tafakari pana juu ya majaribu ya Yesu katika injili, tuyapitie kwa kifupi masomo yanayotangulia, yaani somo la kwanza na somo la pili. Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha Mwanzo (Mwa. 2:7-9, 3:1-7). Mungu amemuumba mwanadamu akamweka katika bustani nzuri ya Edeni. Hapo katikati kinatokea kitu ambacho matokeo yake ni kwamba kinabadilisha kabisa hali ya binadamu na mahusiano yake na Mungu na vitu vyote. Kilichotoea ni ushawishi au majaribu ya nyoka, ushawishi uliomsababishia mwanadamu kumuasi Mungu na kumletea matokeo hayo mabaya katika maisha yake. Somo la pili kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum 5:12-19) linakuja kuonesha kitu kikubwa kilichotokea ili kuzuia mwendelezo wa matokeo mabaya ya kosa la Adamu katika maisha ya mwanadamu. Kilichotokea ni sadaka au kifo cha Kristo Msalabani. Tunaoneshwa kuwa kwa jinsi ile ile ambavyo kosa la mtu mmoja, Adamu, liliharibu uhusiano wa mwanadamu na Mungu na si kwa Adamu tu bali kwa wanadamu wote, basi kwa sadaka ya mtu mmoja, Kristo, ndivyo uhusiano wa mwanadamu na Mungu wake unarejeshwa. Kosa la kutokutii la mtu mmoja Adamu linaondolewa na neema ya kutii ya mtu mmoja – Kristo.

Jangwani ni majali pa mapambano ya maisha
Jangwani ni majali pa mapambano ya maisha

UCHAMBUZI WA INJILI: Tukiingia sasa katika Injili, tunasoma kutoka kwa mwinjili Mathayo (4:1-11) habari za vishawishi au majaribu ya Yesu. Katika Injili hii, ninawaalika tuviangalie vipengele vitatu tu kati ya vingi vilivyopo. Kipengele cha kwanza ni ule wakati ambapo mjaribu alimjia Yesu. Na wakati huo ni pale ambapo Yesu alipatwa na njaa. Wakati wa njaa ni wakati wa udhaifu wa kimwili, ni wakati mtu anapohitaji kitu anachokoswa, yupo katika kutafuta (anatafuta nini? Amani, usalama, utulivu maishani, afya n.k). Huo ndio wakati wa vishawishi na ndio mwanya ambao mjaribu anautumia kuingia. Mjaribu anatumia kwa mfano mwanya wa migogoro iliyopo kuongeza mpasuko katika familia na jamii, anatumia mwanya wa matatizo yanayokukabili: magonjwa, ugumba, vifo n.k kukuingiza katika ushirikina, kukutenganisha na Mungu wako na kuiondoa hata ile imani kidogo uliyokuwa nayo. Mjaribu alimjia Yesu baada ya kufunga siku arobaini mchana na usiku akaona njaa. Kipengele cha pili tunachopenda kukiangalia ni majaribu yenyewe ambayo Yesu aliyapata. Nayo ni matatu: kubadili mawe kuwa mkate, kujirusha kutoka juu ili Malaika wamdake; na kumsujudia Ibilisi ili apewe milki na enzi zote za ulimwengu. Haya ni majaribu yanayogusa maeneo makubwa matatu yanayohangaisha maisha ya mwanadamu: mali, sifa na mamlaka. Katika kishawishi cha kwanza Yesu anajibu “mtu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu”. Mwana wa Mungu ni yule anayetambua kuwa mali (chakula, malazi na mavazi) si vitu vinavyomfanya asione umuhimu wa Mungu katika maisha yake. Awe navyo, asiwe navyo, yeye ni mwana na Mungu ni Baba.

Tunahitaji kuingia katika majangwa yetu ili kupambana na Ibilisi
Tunahitaji kuingia katika majangwa yetu ili kupambana na Ibilisi

Katika kishawishi cha pili kuhusu sifa (Kujimwambafai, kujitafutia heshima au jina kati ya watu) Yesu anajibu usimjaribu Bwana Mungu wako. Mpe Yeye kwanza sifa, heshima na utukufu. Tafuta heshima na sifa katika kutimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yako. Na katika kishawishi cha tatu, Yesu anatambua kuwa mamlaka yatoka kwa Mungu na asili yake ni kutumikia katika uhuru wa wana wa Mungu. Mamlaka yanayohitaji kutoa gharama ya kumsujudia Ibilisi yanaweka rehani uhuru wa wana Mungu na yanawageuza watumwa. Mali, heshima na mamlaka pamoja na matamanio yake yote mema, yatafutwe ndani ya mapenzi yake Mungu. Katika kipengele cha tatu na cha mwisho, tunakwenda kujiuliza, majaribu ya Yesu yalidumu kwa muda gani? Baada ya kuchambua vipengele vya majaribu ya Yesu ambayo ndani yake tumeona majaribu ya ubinadamu mzima, tunaweza kusema kuwa majaribu ya Yesu yalidumu katika maisha yake yote ya hapa duniani. Haya ni majaribu aliyopambana nayo tangu mwanzo hadi mwisho kwa maana hata alipokuwa msalabani aliendelea kujaribiwa ajishushe msalabani ajiokoe. Hata wakati huo wa mateso makali aliendelea kumtii Baba akaikamilisha sadaka ya ukombozi wetu pasipo kuanguka katika dhambi.

Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushindi wa Yesu
Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushindi wa Yesu

Kumbe hizo siku arobaini alizofunga mchana na usiku sio tu kidokezo cha miaka 40 ambayo Waisraeli walijaribiwa jangwani bali ni kiashirio pia cha kuwa alishiriki kikamilifu majaribio yao na majaribu ya ubinadamu mzima. Kwetu sisi ni mwaliko pia wa kuwa macho wakati wote kwa sababu majaribu na vishawishi maishani mwetu havikomi. Huambatana nasi kila siku. Neema tunazozichota katika kipindi hiki cha Kwaresima zitufae kuamsha dhamiri zetu na kutuimarisha ili tuweze kuyashinda majaribu na hatimaye, tuweze kusherehekea vyema Fumbo la Pasaka.

Liturujia D 1 Kwaresima
25 February 2023, 09:41