Tafakari Dominika ya Kwanza ya Kwaresima Mwaka A: Vishawishi Vikuu Katika Maisha
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli (Napoli), Italia
Mwanadamu katika maisha yake ya kila siku anaandamwa na vishawishi vikubwa vitatu: kishawishi cha kutimiza tamaa za mwili, kishawishi cha kumiliki vitu na kishawishi cha kuonesha nguvu, madaraka na uwezo wake ili kujimwambafai mbele ya wengine. Vishawishi hivi, visipotawaliwa na kudhibitiwa, huwa chanzo cha anguko la mwanadamu ambalo humweka mbali na Mungu. Kwaresima ni kipindi cha kujiweka karibu na Mungu kwa kushinda vishawishi. Yesu katika Injili anatupatia njia ya kushinda vishawishi: kufunga, kujikatalia na kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yetu ya kila siku. Tunapaswa kumshinda Ibilisi, baba wa uongo wote. SOMO LA INJILI: Mt. 4:1-11. Injili ya leo inasimulia tukio la Yesu kwenda nyikani na kujaribiwa na Shetani kwa siku arobaini. Waisraeli waliamini kuwa makazi ya Shetani na pepo wengine waovu yalikuwa ni nyikani/jangwani au baharini. Hivyo Yesu anapokwenda nyikani ni ishara ya wazi kuwa anaanza kazi ya kupambana na nguvu za uovu ambazo mkuu wake ni Ibilisi. Injili inatuambia kuwa Yesu alikuwa jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani. Kwenye Maandiko Matakatifu namba zina maana kubwa: namba 40 inaashiria “kipindi kirefu” (longevity). Hivyo tunafunuliwa kuwa majaribu ya Shetani kwa mwanadamu siyo ya siku moja au mbili (siyo ya kipindi kifupi) bali ni ya kipindi kirefu (maisha yetu yote ni mapambano dhidi ya Shetani).
Somo la Injili linatufundisha kuwa “uaminifu kwa mpango wa Mungu na kuishi Neno lake ni mbinu za kushinda vishawishi”. Baada ya Yesu kupokea Roho Mtakatifu wakati wa kubatizwa anaongozwa na Roho huyo huyo kwenda jangwani/nyikani kujaribiwa na Ibilisi. Majaribu ambayo Ibilisi anampatia Yesu yalilenga kumwondoa Yesu katika njia sahihi ya ukombozi wa mwanadamu. Akiwa jangwani/nyikani anapata majaribu matatu: (1) anashawishiwa ageuze mawe kuwa mikate ili kutuliza njaa kali ya kimwili aliyokuwa nayo baada ya kufunga kwa siku 40. Kishawishi hiki kinawakilisha vishawishi vinavyolenga kuridhisha/kutuliza tamaa za mwili- yaani vishawishi vya “kuridhisha na kutuliza haja za mwili” (satisfactions of the body). Baada ya Yesu kuona njaa ndipo Ibilisi anamshawishi Yesu ageuze mawe kuwa mikate. Kwa maneno mengine ni kama Ibilisi alikuwa anamwambia Yesu, “Kwa nini uteseke kwa njaa wakati una uwezo wa kugeuza mawe kuwa mikate. Usiutaabishe mwili wako bure, ondokana na njaa ya mwili pamoja na mateso na mahangaiko yake kwa kuyafanya mawe yawe mikate”. Ibilisi analenga kumshawishi Yesu akwepe mateso kama njia ya kumkomboa mwanadamu- yaani asiwakomboe binadamu kwa mateso msalabani bali kwa njia rahisi ya kuwavuta kwa kuwatendea miujiza, hasa ya vyakula/vitu (material things). (2) anashawishiwa ajitupe chini kutoka kwenye kinara cha hekalu ili adhihirishe tumaini lake kwa Mungu na Mungu aoneshe nguvu yake ya kumwokoa.
Hapa ni kama Ibilisi anamwambia Yesu, “Wewe ni mwana wa Mungu, una nguvu/uwezo wa kujitupa chini na usidhurike maana imeandikwa kuwa [Mungu] atakuagizia malaika wake wakulinde na kukudaka mikononi mwao [hapa Ibilisi ananukuhu Zab. 91:11-12].” Ibilisi ana maneno matamu kweli kweli. Kishawishi hiki kinawakilisha kishawishi cha mwanadamu cha kutaka kuonesha uwezo/nguvu zetu na kutaka kumjaribu Mungu kwa kudai miujiza (desires for showing powers and miracles). (3) anashawishiwa amsujudu Ibilisi ili apate ulimwengu wote na milki zake. Ibilisi ni mwongo mkubwa. Ibilisi anaahidi kumpa Yesu milki zote za ulimwengu na fahari zake kana kwamba ulimwengu ni mali yake. Ulimwengu na fahari zake zote ni mali ya Mungu, siyo mali ya Ibilisi. Mungu ndiye aliyeumba ulimwengu. Kishawishi hiki kinawakilisha vishawishi vya tamaa za kumiliki mali (possessions) kiasi cha kuacha kumsujudu na kumtumikia Mungu. Ibilisi, katika kishawishi cha kwanza na cha pili, anataka Yesu adhihirishe kuwa Yeye ni mwana wa Mungu kwa kutenda miujiza. Ingawa Yesu alikuwa na uwezo wa kutenda hiyo miujiza, hata hivyo hakuitenda hiyo miujiza ili kuonesha kuwa “kuwa kwake Mwana wa Mungu hakutokani na kutenda miujiza bali kuwa kwake Mwana wa Mungu ni asili yake ya milele.”
Kadhalika, kuwa kwake Mwana wa Mungu kunaendelea kudhihirishwa kwa Yeye kubaki mwaminifu katika kutimiza matakwa ya Mungu wala si matwaka na matamanio yake mwenyewe au matakwa ya Ibilisi. Kadhalika, Yesu anapokabiliana na vishawishi vya Ibilisi hajengi hoja kutoka hewani bali anatumia Neno la Mungu akisema “Imeandikwa” - yaani imeandikwa katika Torati: Jibu la Yesu kwa kishawishi cha kwanza linatoka Kumb. 8:3, ya kwamba “Mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Mungu”; Jibu la Yesu kwa kishawishi cha pili linatoka Kumb. 6:16, ya kwamba “Msimjaribu Bwana, Mungu wenu…” Jibu la Yesu kwa kishawishi cha tatu linatoka Kumb. 6:13-15, ya kwamba “Mtamcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mtamtumikia yeye peke yake.” Hata sisi leo tunakabiliwa na vishawishi hivyo vitatu: tamaa za kutuliza haja za mwili, tamaa/kishawishi cha kuonesha nguvu/uwezo wetu (pamoja na kumdai Mungu miujiza) na tamaa za mali. Kwanza, katika maisha yetu Ibilisi anatuangusha kwenye kishawishi cha kutuliza “njaa” zetu za mwili: njaa za ngono, njaa vya ulevi, njaa za anasa na mahangaiko ya kuuridhisha na kuufurahisha zaidi mwili kuliko kuhangaikia zaidi mambo ya kiroho, mambo yamhusuyo Mungu. Ni vizuri kujua kuwa maisha siyo tu kupata mahitaji ya kimwili, bali kupata pia mahitaji ya kiroho. Pili, kishawishi kingine kikubwa cha binadamu ni kutaka kuonesha nguvu/uwezo/madaraka yake na pia kumjaribu Mungu kwa kudai miujiza.
Yesu alikuwa na uwezo wa kujitupa chini kutoka kwenye kinara cha hekalu bila kudhurika na tena kwa kufanya hivyo angepata umaarufu na pengine watu wangevutwa zaidi kumwamini. Hata hivyo Yesu hatumii nguvu/uwezo wake kutafuta umaarufu, utukufu au sifa. Kwa bahati mbaya wengi wetu ni kinyume kabisa cha Yesu kwani tunapenda kuonesha nguvu/madaraka/uwezo wetu ili watu wengine watutambue, watusifu na hata wavutiwe kwetu. Jambo hili limetufanya kutumia kila njia kutafuta uwezo/madaraka/nguvu: tunakwenda Nigeria kununua nguvu za giza ili tuweze kutenda miujiza; tunanyanyasa na kuonea wengine kwa sababu ya madaraka/pesa yetu; tunafanya mauaji ili tupate nguvu ya pesa; tunakwenda kwa waganga ili kupata madaraka/nguvu na vyeo ili tuwe juu ya wengine. Ibilisi pia anatuaminisha kuwa Mungu anatambulikana kwa miujiza, “Atakuagizia malaika wake… mikononi mwao watakuchukua”. Mungu ni Mungu tu hata bila miujiza. Wengi wetu tunadai miujiza ili tumwamini Mungu: tuponywe magonjwa, tufaulu mitihani hata bila kusoma, tupate utajiri bila hata kuusotea, nk. Tatu, watu wengi leo tunahangaika kutafuta kumiliki mali/vitu kwa gharama yoyote (possessions by any cost) kiasi cha kujikuta tunatawaliwa na mali pamoja na nguvu za giza na hivyo kumweka Mungu kando. Katika ulimwengu wa sasa Ibilisi anawaambia watu wengi “Niabudu/nisujudu, nami nitakupa mali”. Kutokana na ahadi hii ya uongo ya Ibilisi, watu wengi wamemuacha Mungu na kuwa watumwa wa mali na mawakala wa shetani kwa kujiambatanisha na nguvu za giza, mizimu na vikundi vya kishetani. Mali siyo kiini cha maisha yetu- kiini cha maisha yetu ni Mungu, hivyo tujitahidi kumjua, kumpenda, kumtumikia na mwisho kufika kwake mbinguni.
Injili yetu ya leo inatufundisha mambo makubwa yafuatayo: (1) Kristo amekuja kuleta ushindi juu ya nguvu zote za giza. Waisraeli waliamini kuwa “nyikani/jangwani” ni makao ya mapepo (demons) ambayo ni kiashiria cha nguvu zote za giza. Yesu amekwenda jangwani na kupata ushindi dhidi ya Ibilisi. Ushindi wa Yesu dhidi ya vishawishi vya Ibilisi (mkuu wa nguvu za giza) ni kiashiria cha ushindi wa Yesu dhidi ya nguvu za uovu, hasa dhambi na mauti. Tukimwamini Kristo tutapata ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Katika Injili Yesu amemshinda Ibilisi ambaye katika somo letu la kwanza amemshinda wanadamu. Yule Ibilisi aliyejifanya mshindi sana ameshindwa. (2) Ili kushinda vishawishi tunahitaji kuongozwa na Roho Mtakatifu na kuishi Neno la Mungu. Yesu, wakati wa kujaribiwa, hakuwa peke yake- alikuwa anaongozwa na Roho Mtakatifu. Hivyo nasi maisha yetu yanahitaji kuongozwa na Roho Mtakatifu ili tushinde vishawishi vya Ibilisi. Roho Mtakatifu anapatikana kwa namna ya pekee katika kushiriki maisha ya sakramenti. Kadhalika kila tusalipo na kutenda mema tunapata neema za Roho Mtakatifu. Yesu pia ametufundisha kuwa tukiishi Neno la Mungu tutapata nguvu ya kushinda vishawishi. Majibu yote ya Yesu kwa Ibilisi yalitoka katika Neno la Mungu (Torati).
Hii ni kuonesha kuwa Yesu alijua na kuliishi Neno la Mungu. Neno la Mungu ni silaha dhidi ya Ibilisi na hila zake. Neno la Mungu ni upanga tunaopewa na Roho Mtakatifu (rejea Waefeso 6:17). Mara nyingi tunaanguka katika vishawishi kwa sababu hatusomi wala kuishi Neno la Mungu. (3) Neno la Mungu linaweza kupotoshwa na kuwa sababu ya sisi kunaswa na Ibilisi. Ibilisi, anapomjaribu Yesu mara ya pili, anatumia pia Neno la Mungu akisema, “kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.” (hapa Ibilisi ananukuhu Zab. 91:11-12). Hapa kuna fundisho kubwa kuwa Ibilisi (na mawakala wake) wanaweza kutumia Neno la Mungu kutuingiza katika vishawishi na dhambi. Mara ngapi mmesikia watu wakitumia Neno la Mungu kuhalalisha uovu wao wa kuoa wake wawili ati kwa kuwa kuna watu kwenye Biblia walikuwa na wake wawili au zaidi? Wangapi wanafanya ukahaba huku wakijitetea mbona Rahabu alikuwa kahaba na bado Mungu alimwokoa? Hata kwenye somo la kwanza nyoka (Ibilisi) anaanza kwa kupotosha maagizo/Neno la Mungu: “Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? (Je, ni kweli Mungu aliwakataza Adamu na Eva kula matunda ya miti yote ya bustani? Hapana. Walikatazwa kula tu matunda ya mti wa katikati). Tena nyoka anaendelea kupotosha Neno la Mungu: Mungu alisema wakila matunda ya mti wa katikati watakufa, lakini nyoka (Ibilisi) anawaambia hawatakufa. Ibilisi ni mpotoshaji mkubwa. Hata Eva naye anapotosha Neno la Mungu kwa kusema kuwa Mungu aliwakataza kuyala na kugusa matunda ya mti wa katikati. Huu ni uwongo. Mungu aliwakataza kuyala lakini hakuwakataza kuyagusa (yaani wangeweza kuyagusa lakini chondechonde wasiyale). Dhambi huanza pale tunapopotosha Neno/maagizo ya Mungu. Hata leo manabii wengi wa uwongo wanatumia Neno la Mungu kupotosha watu na kuwatumbukiza dhambini. Kaa chonjo, saa mbaya!