Tafakari Dominika VII Mwaka A: Nguvu ya Upendo na Msamaha Katika Maisha
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Dominika ya Saba ya Mwaka A wa Kanisa inahitimisha sehemu ya kwanza ya Mwaka A wa Kanisa ambamo tumetafakari kuhusu: Heri za Mlimani, Muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Hii ni Katiba ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Waamini wanahimizwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu ili kuyachachua malimwengu kwa utakatifu wa maisha. Kanisa kama Mama, Mwalimu na Mlezi. Mababa wa Kanisa wanasema Mkristo hutekeleza wito wake ndani ya Kanisa katika ushirika pamoja na wabatizwa wote, anapokea Neno la Mungu, neema ya Sakramenti na kujifunza mfano wa utakatifu na ushuhuda wa tunu msingi za Kikristo; anajifunza maisha adili na ibada ya kiroho na kwamba, maisha adili hupata chemchemi na kilele chake katika sadaka ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Rej. KKK 2030 – 2051. Kristo Yesu ameedelea zaidi katika kufundisha na kufafanua kuhusu utimilifu wa Amri za Mungu katika maisha na utume wake na kukazia kwamba, hakuja kuitangua Torati au Manabii bali kutimiliza na hivyo Kristo Yesu anakuwa ni chemchemi ya Katekesi ya maisha mapya katika Roho Mtakatifu, neema, Heri za Mlimani; dhambi na msamaha, fadhila za Kimungu na kibinadamu, Amri kuu ya upendo na katekesi kuhusu Kanisa kwa sababu Kristo Yesu ni njia, ukweli na uzima. Rej. KKK 1697-1698.
Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya VII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa, Kristo Yesu anatangaza sheria mpya ya upendo, huruma, msamaha na upatanisho inayoleta mapinduzi makubwa ya Kiinjili, chachu ya wema na utakatifu wa maisha na hivyo kuwawezesha waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa Ufunuo wa Uso wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu uliotundikwa pale juu la Msalaba. Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu, katika Injili ya Mathayo 5: 38-48 anawaalika wafuasi wake kumwilisha fadhila ya upendo katika maisha yao mintarafu mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani, kwa kutoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya sheria: Jicho kwa jicho na jino kwa jino. Hii ni sheria inayokita mizizi yake katika Agano la Kale, maarufu kama “Talion” yaani Sheria ya Kulipiza Kisasi. Sheria hii ilikuza na kudumisha uhasama, chuki, hasira na uadui na matokeo yake ni Vita ya Dunia ya Tatu inayopiganwa vipande vipande sehemu mbalimbali za dunia hadi hivi leo, ikiambatana na vitendo vya kigaidi. Kristo Yesu anataka wafuasi kuongozwa na Heri za Mlimani; wawe chumvi ya dunia na nuru ya Mataifa, daima wakijitahidi kuwa ni vyombo na ufunuo wa huruma ya Mungu, kwa kuwapenda, kusamehe na kuwaombea adui zao, ili wapate kutubu na kuwa watu wema zaidi, tayari kushiriki ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ndio mchakato wa ujenzi wa umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika ujirani mwema, kwa sababu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Hii ni changamoto inayowataka waamini kuwa ni waaminifu kwa mpango wa Mungu, kwa kuhakikisha kwamba, wanamwilisha haki inayopita ile ya Mafarisayo, kwa kuachana na kiburi, majivuno na majigambo, mizizi ya dhambi. Yesu analeta mageuzi ya Kiinjili kwa kuwataka wafuasi wake kuwapenda, kuwasamamehe na kuwaombea adui zao, ili kuendeleza mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaopata utimilifu wake katika: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu pale Mlimani Kalvari, aliposema: “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Lk 23:34. Kifo cha Stefano shuhuda wa Injili: “wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli. Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake.” Mdo 7: 58-60. Baba Mtakatifu Francisko anasema, sheria ya jicho kwa jicho; na jino kwa jino ilikuwa na madhara makubwa katika jamii. Kristo Yesu katika mafundisho yake anatoa mwelekeo mpya unaopaswa kufuatwa kwa kutoshindana na mtu mwovu wala kulipiza kisasi kwa kuwa umetendewa maovu. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo kwa watoto wake wote bila ubaguzi. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeeshea mvua wenye haki na wasio haki. Mwenyezi Mungu anawataka watoto wake wote wawe watakatifu kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mtakatifu.
Kwa maneno mengine, Mwenyezi Mungu anawaalika watoto wake kuishi vyema na kutafuta kila ambacho Kristo Yesu katika maisha na utume wake alikuja kufanya. Hata akiwa pale juu Msalabani hakuwanyooshea watesi wake kidole kuwahukumu bali aliwafungulia mikono yake, akawasamehe na kuwaachia waigongomelee Msalabani. Hii ndiyo njia, dira na mwongozo kwa Wakristo. Mwenyezi Mungu amewapenda upeo, na wao wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo; wamesamehewa dhambi zao, wawe pia wepesi wa kusamehe! Wameonja upendo, wawe wa kwanza kuwaonjesha wengine huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wakristo wawe na ujasiri hata wa kuwapenda na kuwaombea adui na wale wote wanao wadhulumu na kuwatesa! Haya ni maneno aliyoyachagua Kristo Yesu mwenyewe kwa makusudi mazima! Huu ndio utofauti mkubwa unaopaswa kuoneshwa na Wakristo kwa kuwaombea na kuwapenda adui zao kwa kutambua kwamba, upendo wa Mungu hauna mipaka: Hiki ni kiini cha Injili na wala hakuna “cha salia Mtume”. Hiki ni kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa. Wapendeni na kuwaombea adui zenu ni mwaliko kwa waamini kujitahidi kuyamwilisha maneno haya machungu katika uhalisia wa maisha yao, kwa kuwapenda na kuwaombea adui zao. Kwa mwamini anayempenda Mungu kwa hakika hana adui moyoni mwake. Hii ni ibada ya kuondokana na utamaduni wa chuki na hali ya kutaka kulipizana kisasi. Utamaduni huu unaweza kufyekelewa mbali kwa kwenda kinyume na litania ya malalamiko kwa kupenda na kusali.
Haya ni mapinduzi makubwa ambayo yameletwa na Kristo Yesu katika historia ya maisha ya binadamu kwa kuwapenda na kuwaombea adui. Huu ndio mwelekeo sahihi wa maisha. Baba Mtakatifu anasema, kwa mtu anayependa, anatambua pia umuhimu wa kusamehe na kupenda. Hii inatokana na ukweli kwamba, hekima ya dunia hii ni upuuzi mbele ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anaona mbali zaidi na anafahamu jinsi ya kushinda katika mapambano haya kwa sababu amemkomboa mwanadamu si kwa ncha ya upanga bali kwa njia ya Msalaba. Huku ndiko kupenda, kusamehe na kuishi kama mtu mwenye ushindi. Imani inaenezwa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na wala si kwa ncha ya upanga! Bustanini Getsemani, Mitume walitumia upanga, lakini wakawa wa kwanza “kuchanja mbuga na kutokomea kusikojulikana”. Maisha na utume wa Kristo Yesu ni mfano bora wa kuigwa: kwa kupenda kwa dhati kabisa katika hali ya unyenyekevu na kupenda upeo! Ni kweli kwa nguvu za mtu binafsi si rahisi sana, kumbe, wanapaswa kuomba neema ya kujifunza kupenda na kusamehe. Waamini waombe neema ya kuwaona jirani zao kuwa ni watu wanaopaswa kupendwa na kusamehewa na wala si vikwazo na vizingiti vya maisha. Nguvu ya msamaha ni chemchemi ya maondoleo ya dhambi, ni mwaliko wa kujifahamu, kujikubali na kujipokea jinsi ulivyo na mwelekeo unaoakisi tabia ya Kimungu, tayari kujenga na kudumisha msingi wa haki, amani na maridhiano. Nguvu ya msamaha inaokoa, inaganga na kuponya majeraha ya mahusiano na mafungamano ya watu: katika ndoa, familia na jamii katika ujumla wake.
Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa katika Somo la Pili: 1Kor 3: 16-23, anawaalika Wakristo kuwa ni wajenzi wa msingi wa haki, amani na maridhiano. Wakristo watambue kwamba, kwa Sakramenti ya Ubatizo wamekuwa ni Mahekalu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, kumbe watafute na kuambata hekima ya Kimungu, ili kuwasaidia kujenga ushirika na mafungamano ya kiimani. Kristo Yesu anatangaza sheria mpya ya upendo, huruma, msamaha na upatanisho inayoleta mapinduzi makubwa ya Kiinjili, chachu ya wema na utakatifu wa maisha na hivyo kuwawezesha waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa Ufunuo wa Uso wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu uliotundikwa pale juu la Msalaba.