Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 5 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Wajibu wa Wakristo ni kuyatakatifuza malimwengu kwa ushuhuda wa maisha yao adili. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 5 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Wajibu wa Wakristo ni kuyatakatifuza malimwengu kwa ushuhuda wa maisha yao adili.  (Vatican Media)

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Tano Mwaka A : Kutakatifuza Malimwengu

Masomo ya dominika hii yanasisitiza umuhimu na thamani ya matendo ya huruma katika maisha ya kikristo ambayo kwayo yanamfanya Mkristo kuwa chumvi na mwanga kwa wengine katika maisha ya kiroho, kimwili na kijamii ili nao waweze kumtambua Mungu aliyefunuliwa na Yesu Kristo, aliyeumba vitu vyote vinavyoonekana na visivyooneka. Ndiye anayetuita tuishi kitakatifu.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 5 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanasisitiza umuhimu na thamani ya matendo ya huruma katika maisha ya kikristo ambayo kwayo yanamfanya Mkristo kuwa chumvi na mwanga kwa wengine katika maisha ya kiroho, kimwili na kijamii ili nao waweze kumtambua Mungu aliyefunuliwa na Yesu Kristo, aliyeumba vitu vyote vinavyoonekana na visivyooneka. Ndiye anayetuita tuishi kitakatifu kama yeye alivyo ili mwisho wa maisha yetu hapa duniani ukifika atustahilishe kuishi naye milele yote mbinguni. Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa 58:7-10). Katika somo hili Mungu kwa kinywa cha Nabii Isaya anawaonya Wayahudi waliorudi toka utumwani Babeli, kwamba kufunga na kusali kwao ni kazi bure kama hawatendi haki kwa ndugu zao, kuwagawia wenye njaa chakula, kuwakaribisha maskini na kuwavika nguo walio uchi. Matendo haya ya huruma ndiyo yanayofanya nuru ya Mungu iwapambazukia kama asubuhi, kuwafanye wawe na afya njema kwani utukufu wa Bwana utawafuata na kuwalinda. Ndiyo maana mzaburi katika wimbo wa katikati anaimba akisema; “Nuru huwazukia wenye adili gizani…naye mwenye haki atakumbukwa milele” (Zab. 111:4-9). Kwa kutenda matendo ya huruma kwa wengine wanapata kibali machoni pa Mungu nao wakatapo mwita ataitika, watakapomlilia naye atasema; Mimi hapa.

Ninyi ni chumvi ya dunia na nuru ya mataifa
Ninyi ni chumvi ya dunia na nuru ya mataifa

Hata kwetu sisi, mahusiano mema na wenzetu ndiyo hasa yanayodhihirisha kuwa Kristo yu kati yetu. Kusali sala ndefu na kufunga kwa mda mrefu hakutufai chochote kama hatuwajali wenzetu. Kwanza matendo ya huruma yanayoongwa na amri kuu ya mapendo, kisha zifuate sala na mafungo. Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 2:1-5). Katika somo hili Mtume Paulo anatukumbusha kuwa msalaba wa Yesu Kristo ndio kiini cha habari njema ya wokovu wetu. Pia Mungu anachagua viumbe dhaifu kama vyombo vya kulihubiri neno lake ili kuonyesha kwamba nguvu ya Injili si katika ufasaha wa maneno au hekima ya mhubiri bali katika nguvu ya Mungu inayojidhihirisha katika msalaba wa Kristo ndiyo inayofungua mioyo ya watu ili wasadiki. Mtume Paulo anafikia ufahamu huu baada ya mda mrefu. Itakumbukwa kuwa akiwa Athene Ugiriki, Mtume Paulo alijaribu kutumia hekima ya kibinadamu kuwahubiria wagiriki. Hii ni kwasababu Wagiriki, watu wasomi, walipenda kujadili hoja mbalimbali katika lugha ya kisomi wakitafuta ufasaha wa mambo kifalsafa zaidi. Mtume Paulo alitumia mfumo huo wa hoja na akawavutia kwa hoja nzuri, nao wakatamani kuendelea kumsikiliza. Lakini alipoongelea habari za ufufuko wa wafu hawakuona hoja ya kisomi. Ndiyo maana walimwambia tutakusikiliza tena kesho kuhusu habari hiyo, wakimaanisha, hoja haina mantiki ya kisomi.

Mkristo ni kama chumvi na nuru ya ulimwengu
Mkristo ni kama chumvi na nuru ya ulimwengu

Katika safari yake ya pili ya kimisionari akiwa Troa, Paulo alitambua kuwa sio hoja za kifalsafa ndizo zinazowavutia watu. Katika kuhubiri kwake watu wengine walisinzia na kulala. Hili linajionesha baada ya mtu mmoja kuanguka kutoka ghorofani na kufa sababu ya kulala wakati wa mahubiri (Mdo 20:9). Lakini Paulo alishangaa kuona kuwa Injili iliendelea kuenea kwa wakristo wa Korintho bila ya kutumia ufasaha wa kifalsafa katika kuhubiri kwake. Ndipo akatambua kuwa neno la Mungu halitegemei hekima ya kibinadamu wala ufasaha wa lugha. Ndiyo maana katika somo hili anawaambia; “Nilipokuja kwenu, sikuja kuwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno, wala kwa hekima zangu. Neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa nguvu ya Roho wa Mungu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.” Tumekombolewa kwa msalaba wa Kristo. Msalaba ndiyo nuru na mwanga wa maisha yetu ya kiroho. Kila mkristo anapaswa kuunyanyua msalaba juu kwa matendo ya mwanga ili awamulikie wengine waone njia ya kwenda kwa Mungu nao watambue upendo wa Kristo kwao waweze nao kuongoka na kumfuata. Ndiyo maana Yesu alisema; “Anayetaka kunifuata sharti ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake kila siku na anifuate”. Tukumbuke kuwa katika mahubiri kinachowaongoa watu siyo ufasaha wa lugha wala hekima ya kibinadamu bali nguvu ya Roho wa Mungu iliyo katika neno lake linapohubiriwa nao watu wakalipokea na kuliishi kwa kutenda matendo mema. Mama Kanisa analitambua hili ndiyo maana katika sala ya Koleta, Padre kwa niaba ya waamini anasali akisema; “Ee Bwana, tunakuomba utulinde sisi watoto wako kwa pendo lisilo na mwisho. Na kwa kuwa twategemea tu neema yako ya mbinguni utuhifadhi daima kwa ulinzi wako.”

Waamini wayatakatifuze malimwengu kwa chachu ya maadili na utu
Waamini wayatakatifuze malimwengu kwa chachu ya maadili na utu

Injili ni ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 5:13-16). Katika Injili ya dominika 4 mwaka A Yesu alitupa mwongozo wa maisha ya kikristo unaosimikwa katika heri nane za mlimani kuwa; maskini wa kiroho, wapole, wenye huruma, wanyofu na watu wa amani kama tukitaka kuingia ufalme wa Mungu. Katika Injili ya dominika 5 mwaka A, Yesu anatufundisha kuwa maisha ya kila mkristo ni kama chumvi na nuru. Umuhimu wa chumvi na nuru/mwanga katika maisha ya kila siku uko wazi sio tu kwa mwanadamu bali hata kwa viumbe wengine.  Kile ambacho chumvi inafanya katika chakula na kile ambacho mwanga unafanya katika maisha yetu ndicho ambacho wakristo tunapaswa kuwa kwa maneno na matendo yetu kwa watu wengine. Kazi ya chumvi ni kukoleza na kuongeza ladha ya chakula. Chumvi ni kikolezo cha chakula na ni dawa. Mwandamu anatumia chumvi apate kuweka ladha katika chakula, anaitumia chumvi kutunza na kuhifadhi chakula kisioze, pia anatumia chumvi kama dawa. Chumvi ni alama ya hekima na busara kwa uzoefu wa kuishi mda mrefu, ndiyo maana tunasema mtu amekula chumvi nyingi tukimaanisha ameishi miaka mingi. Hivi ndivyo inavyotupasa wakristo kuwa hapa duniani. Matendo yetu mema yawe kama chumvi, yakoleze na kuleta ladha ya maisha kwa wengine.

Waamini wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za kiinjili
Waamini wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za kiinjili

Tusipotimiza huu wajibu mwisho wetu ni kuukosa uzima wa milele. Mwanga hutumika kuondoa giza ili watu wapate kuona au kitu chochote kipate kuonekana. Kumbe kazi ya mwanga ni kuwaonyesha watu njia. Kukiwa na giza hatuoni. Mwanga unatuwezesha kuona uzuri na thamani halisi ya vitu vilivyoumbwa na Mungu na kuvitumia kwa mpango wake. Mwanga unawezesha mimea kukua. Wana sayansi wanatuambia kwamba kama mwanga wa jua ungetoweka maisha yangetoweka duniani; viumbe hai vyote vingekufa. Kile ambacho mwanga unafanya ndicho tunachopaswa kufanya sisi wakristo katika maisha yetu. Kama mwanga unavyoviwezesha viumbe hai kama mimea kukua, ndivyo mwanga wa imani unavyotusaidia kukua na kukomaa katika maisha ya Kikristo nasi tunapaswa kuwasaidia wengine wauone mwanga wa imani kwa Kristo katika maisha yao. Mwanga wa imani unatusaidia kuku ana kukomaa katika ut una wema ndani mwetu. Hivyo tuna wajibu wa kuwasaidia pia watu wengine wakue katika wema. Katika Biblia giza ni hali ya kuwa na dhambi ni hali ya kukosa uwepo wa Mungu ni hali ya kutokuwepo na neema ya Utakaso.

Wawe ni wajenzi na wasanii wa ufalme wa Mungu
Wawe ni wajenzi na wasanii wa ufalme wa Mungu

Mwanga ni ishara ya uwepo wa Mungu, ni ishara ya uwepo wa neema ya utakaso. Mwanga huu unaweza kuelezwa kuwa ni Neno la Mungu kama Mzaburi anavyosema; “Neno lako ni taa ya kuniongoza na mwanga katika njia yangu” (Zab. 119:105). Hivyo, mtu anapojua neno la Mungu na amri zake anakuwa na mwanga na anaweza kufuata njia nzuri ya kuishi. Yeyote yule anayewajulisha watu neno la Mungu na Amri zake anaeleweka kuwa analeta mwanga kwa watu. Watu wamuone Mungu na waone njia ya kuweza kumfikia. Anawatoa watu gizani. Hivyo, basi kuwa mwanga ni kuishi maisha ya mfano. Ili watu wayaone matendo yetu wamtukuze Mungu. Kwa matendo yetu watu waone wanavyopaswa kuishi. Kila mmoja katika nafasi yake anapaswa kuhakikisha kuwa anakuwa mfano wa kuigwa na wengine. Basi tumwombe Mungu atujalie ujasiri na moyo wa kujisadaka ili tuweze kuwa kweli nuru/mwanga na chumvi kwa mataifa tukiwa tumeungana na Kristo Nuru na Mwanga wa kweli kama anavyosali Padre katika sala baada ya Komunyo akisema; “Ee Mungu, umependa tushiriki mkate mmoja na kikombe kimoja. Tunakuomba utujalie kuishi tumeungana na Kristo, tupate kuzaa matunda kwa furaha kwa manufaa ya wokovu wa ulimwengu.”

Dominika 5 Mwaka A wa Kanisa
04 February 2023, 17:51