Tafakari Dominika ya VI ya Mwaka A: Kanisa ni Mama, Mlezi na Mwalimu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Heri za Mlimani, Muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Hii ni Katiba ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Mama Kanisa anawakumbusha watoto wake kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani ufunuo wa Kristo Yesu, Bwana wa uzima wa milele. Kristo Yesu anawakumbusha wafuasi wake akisema, “Ninyi ni chumvi ya dunia… Ninyi ni nuru ya ulimwengu.” Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakiri kwa kusema, Kristo Yesu ndiye “Mwanga wa Mataifa, Lumen Gentium.” Ni matumaini ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuona kwamba mng’ao wa nuru ya Kristo ung’aao juu ya uso wa Kanisa kwa njia ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inawaangaza walimwengu wote, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya umoja, Ishara na Chombo cha kuwaunganisha wanadamu wote. Rej. Lumen gentium, 1. Mtakatifu Yohane wa XXIII anasema, Kanisa ni Mama na Mwalimu wa Mataifa yote, katika muktadha wa Muasisi wake, Kristo Yesu, anaalika kuukumbatia ulimwengu katika upendo, ili wanadamu waweze kupata utimilifu na wokovu katika Kristo Yesu, kwa kuzingatia nguzo msingi za ukweli.
Mama Kanisa amekabidhiwa dhamana ya kurithisha uhai kwa watoto wake, kuwafundisha na kuwaongoza, ili utu, heshima na haki zao msingi ziweze kulindwa, kuthaminiwa na kudumishwa. Ukristo ni daraja inayokutanisha dunia na mbingu. Hii ni huduma inayotolewa kwa mwanadamu mzima: mwili na roho, akili na utashi, ikimfanya ainue akili yake juu ya mabadiliko ya hali ya maisha hapa duniani, ili hatimaye, aweze kufikia juu kwa uzima wa milele, huko juu mbinguni, ambako atapata furaha na amani isiyokuwa na kikomo! Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya VI ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa inakazia kuhusu: Kanisa kama Mama, Mwalimu na Mlezi. Mababa wa Kanisa wanasema Mkristo hutekeleza wito wake ndani ya Kanisa katika ushirika pamoja na wabatizwa wote, anapokea Neno la Mungu, neema ya Sakramenti na kujifunza mfano wa utakatifu na ushuhuda wa tunu msingi za Kikristo; anajifunza maisha adili na ibada ya kiroho na kwamba, maisha adili hupata chemchemi na kilele chake katika sadaka ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Rej. KKK 2030 – 2051. Kristo Yesu katika Injili Mt 5:17-37 anajipambanua kuwa ni utimilifu wa Torati na Manabii. Anachukua fursa hii kufafanua Amri za Mungu, Neno, Dekalojia yanayopata utimilifu wake katika Agano Jipya na muhtasari wake ni Amri ya upendo kwa Mungu na jirani na kwa njia ya imani wanadamu wote wapate kuokoka kwa imani, Ubatizo na kuzishika Amri za Mungu na kwa kuongozwa na dhamiri nyofu, Sheria ya Mungu inayozungumza na mwanadamu kutoka katika undani wake. Rej. KKK 1052-2082.
Kristo Yesu anajielekeza zaidi katika kufundisha na kufafanua kuhusu utimilifu wa Amri za Mungu katika maisha na utume wake na kukazia kwamba, hakuja kuitangua Torati au Manabii bali kutimiliza na hivyo Kristo Yesu anakuwa ni chemchemi ya Katekesi ya maisha mapya katika Roho Mtakatifu, neema, Heri za Mlimani; dhambi na msamaha, fadhila za Kimungu na kibinadamu, Amri kuu ya upendo na katekesi kuhusu Kanisa kwa sababu Kristo Yesu ni njia, ukweli na uzima. Rej. KKK 1697-1698. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kristo Yesu ni utimilifu wa Torati na Unabii. Maana Injili inahubiri na kutangaza uhuru wa watoto wa Mungu, inakataa utumwa dhambi, inaheshimu hadhi ya dhamiri nyofu, inawahamasisha waamini kujiongezea talanta, kwa ajili ya huduma na mafao ya wengi. Rej. Gaudium et spes. Kristo Yesu anatangaza jinsi ya kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu kwa njia ya uchaji wa Mungu, Ibada, Maisha adili na Matakatifu. “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.” Mt 5:23-24. Liturujia inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha. Hii ni sehemu ambayo Kristo Yesu ameifafanua kwa kina mapana, kama Mwalimu, ili kuwawezesha wafuasi wake kufikia ukomavu wa uhuru unaoongozwa na dhamiri nyofu.
Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa katika Somo la Pili katika Waraka wake wa Kwanza kwa Wakorintho 2: 6-10, anawaalika waamini kujivika hekima itokayo juu kama ilivyoandikwa “Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.” 1Kor 2:9-10. Huu ni mwaliko wa kujenga Kanisa la Kisinodi kwa kuongozwa na hekima ya Roho Mtakatifu ili kusoma alama za nyakati, kwa kutoa upendeleo wa pekee kwa maskini, ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu. Kwa kuwasaidia waamini kujenga dhamiri nyofu ili kutambua mema na mabaya. Ni mwaliko wa kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa kujikita zaidi katika upendo, uaminifu, udumifu, msamaha na upatanisho wa kweli sanjari na kuzingatia viapo vyetu katika ukweli na uwazi. Ninawatakia kila la kheri katika kuzingatia Heri za Mlimani kama muhtasari, dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo, zinazowasaidia waamini kuyatakatifuza malimwengu kwa chumvi na nuru ya Kristo Yesu, ili kuishi maisha adili na matakatifu yanayoongozwa na Amri za Mungu na kuendelea kutambua kwamba, kwa hakika, Kanisa ni Mama, Mlezi na Mwalimu hasa wa maisha adili na Matakatifu.