Tafakari ya Dominika ya VII ya Mwaka A wa Kanisa: Iweni watakatifu kama Baba yenu wa Mbinguni alivyo Mtakatifu. Tafakari ya Dominika ya VII ya Mwaka A wa Kanisa: Iweni watakatifu kama Baba yenu wa Mbinguni alivyo Mtakatifu.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika VII ya Mwaka A wa Kanisa: Wapendeni Adui Zenu Na kuwaombea!

Muhimu: Ikiwa tutamkazia macho Kristo hatutaweza kupoteza hamu ya kuwa watakatifu. Mwito ni kuwa watakatifu kama Baba yetu wa mbinguni: Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu. Ukamilifu katika maisha ya kiroho ni matokeo ya upendo usio na mipaka, upendo usiotofautisha rafiki na adui, upendo ambao hushinda uovu kwa wema!

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, - Pozzuoli (Napoli), Italia

Askofu Guido Marini wa Jimbo la Tortona nchini Italia katika mahubiri yake ya Misa ya Krisma ya Alhamisi Kuu Aprili 21, 2022 aligusia kishawishi cha kuridhika na umaskini wa kiroho tulionao “mediocrity” kiasi kwamba hatuhisi uwepo wa pengo lililopo katika maisha yetu ya kiroho kwa sababu hatuhisi tena shauku ya kuwa watakatifu. Anasema ikiwa tutamkazia macho Kristo hatutaweza kupoteza hamu ya kuwa watakatifu kwa katika mioyo yetu tutasikia tena kila mara shauku na kiu ya kumfuata kwa utakatifu wa maisha yetu. Mwito wetu ni kuwa watakatifu kama Baba yetu wa mbinguni: Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu. Ukamilifu katika maisha ya kiroho ni matokeo ya upendo usio na mipaka, upendo usiotofautisha rafiki na adui, upendo ambao hushinda uovu kwa wema! SOMO LA KWANZA: Law. 19:1-2, 19-18: Katika somo letu la kwanza Mungu anawapa mwongozo wana wa Israeli wa namna ya kuishi na kudumisha mapendo kati yao watakapoingia katika nchi ya ahadi. Mungu, katika mwongozo anaoutoa kupitia Musa, anawataka wana wa Israeli “kushinda chuki, vinyongo na visasi kati yao.” Na njia pekee ya kushinda chuki na visasi kati yao ni kila mmoja kumpenda mwenzake kama anavyoipenda nafsi yake mwenyewe. Kwa maneno mengine kama wewe hupendi kuchukiwa, basi nawe usimchukie mwingine; kama wewe hupendi kulipwa kisasi, basi na wewe usilipize kisasi. Tukiwapenda wengine kama tunavyozipenda nafsi zetu, hapo tutakuwa watakatifu kama Mungu alivyo Mtakatifu. Kwa hulka yetu ya kibinadamu kuna nyakati tunakoseana, kuhitilafiana na hata kuwa na migogoro kati yetu. Hali hii ya kibinadamu isitufanye kuwekeana vinyongo, kujenga chuki kati yetu na kulipa visasi. Visasi, vinyongo na chuki dhidi ya mwingine siyo namna ya kupata amani au utulivu. Vinyongo, visasi na chuki humsababishia mtu kuwa na dhambi zaidi maana mambo haya hupelekea kutendeka kwa dhambi kubwa zaidi kama vile uuaji. Mungu anatutaka kuziba vinyongo, visasi na chuki kwa kuwapenda hata wale wanaotukosea. Fundisho hili ndilo ambalo Yesu analisisitiza katika Injili: wapendeni adui zenu.

Upendo ni chachu ya utakatifu wa maisha
Upendo ni chachu ya utakatifu wa maisha

SOMO LA PILI: 1Kor. 3:16-23: Moja kati ya matatizo yaliyowakabili Wakristo wa Korintho ni mafarakano yaliyotokana na “majigambo ya kujibainisha na wale waliowahubiria Injili.” Mtume Paulo alifika Korintho na kuhubiri Injili na baadaye aliondoka na kwenda maeneo mengine. Baada ya Paulo kuondoka Korintho, mtu mwingine aitwaye Apolo aliendelea kuhubiri Injili hapo Korintho ili kuimarisha imani. Inaonekana Apolo alikuwa na uwezo mkubwa katika kuhubiri na kushawishi watu kuipokea imani, pengine kuliko Paulo. Kadhalika, inaonekana pia Mtume Petro naye aliwahi kufika Korintho na kuhubiri Injili. Baada ya muda kuliibuka mafarakano katika kanisa la Korintho. Wakristo wa Korintho walianza kuulizana kwa majivuno: hivi nani kati yetu ni mkristo bora kuliko mwingine? Je, ni sisi tuliopokea Injili kutoka kwa Paulo ambaye alitokewa kabisa na Yesu? Je, ni sisi tuliopokea Injili kutoka kwa Apolo mtu mashuhuri katika kuongea na kuhubiri? Je, ni sisi tuliopokea Injili kutoka kwa Petro, mmoja wa mitume 12 wa Yesu? Hivyo, kila kundi lilianza kujigamba na kujibainisha na yule aliyewahubiria Injili: Sisi ni wa Paulo; Sisi ni wa Apolo; Sisi ni wa Kefa (Petro). Hali hii iliathiri sana umoja katika kanisa la Koritho ambalo Paulo analielezea kama Hekalu ya Mungu. Kutokana na majigambo haya ya kujibainisha na waliowahubiria Injili (akina Paulo, Apolo na Kefa), Wakristo wa Korintho walianza kugawanyika na kuzozana wao kwa wao.

Wakristo wanapaswa kujikita katika uekumene wa maisha
Wakristo wanapaswa kujikita katika uekumene wa maisha

Mparanganyiko huu ulisababisha hali ya imani kuzorota katika Kanisa la Korintho. Hivyo Paulo anawaonya wasijisifu kwa sababu ya watu/wanadamu waliowahubiria Injili bali wakumbuke kuwa wao ni mali ya Kristo wala siyo mali ya Paulo au Apolo au Kefa: “mtu ye yote na asijisifie wanadamu.” Kujisifu kwa ajili ya watu ni upuuzi. Wakijitambua kuwa wao ni mali ya Kristo basi hawatajisifu bali watakuwa na umoja na kukua kiimani. Hata leo miongoni mwa matatizo yanayotukumba sisi Wakristo ni majivuno na kujiambatanisha na watu fulani badala ya kujiambatanisha na Mungu. Kuna watu hawaendi kanisani mpaka wasikie Misa inaongozwa na Padre fulani na huyo Padre akihama na wao wanaacha kwenda kanisani. Hawa hawana tofauti na waamini wa Korintho waliosema, “Mimi ni wa Paulo.” Wengine wanafikiri ya kwamba wao ni wakristo bora kuliko wengine eti kwa kuwa walibatizwa au kufungishwa ndoa na Askofu; na hata kwetu sisi Mapadre wapo wanaojiona wao ni mapadre bora zaidi kwa sababu walipadrishwa na Askofu fulani. Na wengine wanafikiri wao ni bora zaidi kwa sababu ya uwezo wao kiakili au kiuchumi. La hasha! Sisi sote ni sawa mbele ya Mungu. Tukiendekeza mambo kama haya tutaharibu hekalu la Mungu (yaani Kanisa).

Heri za Mlimani ni Mwongozo adili wa maisha ya Kikristo
Heri za Mlimani ni Mwongozo adili wa maisha ya Kikristo

SOMO LA INJILI: Mt. 5:38-48: Injili ya Mathayo kuanzia Mt. 5:1-7:28 hujulikana kama Hotuba ya Mlimani kwa kuwa Yesu anafundisha akiwa mlimani. Sehemu hii ya mafundisho ya Yesu (Hotuba ya Mlimani) huitwa pia “Katiba ya Wakristo” kwani inatoa mwongozo na dira ya namna Mkristo anavyopaswa kuishi ili afike mbinguni. Kwangu mimi sehemu hii ya Injili ya Matayo naiita “Tiketi ya Mbinguni” maana tukiyashika haya anayofundisha Yesu tutakuwa tayari tumepata tiketi ya kuingia mbinguni. Katika Injili ya leo Yesu anafundisha mambo makubwa mawili: (i) Kutolipiza kisasi na (ii) kuwapenda adui. Kwanza, tuanze na fundisho la kwanza la kutolipiza kisasi. Yesu anafundisha juu ya kutolipiza kisasi maana kwa Wayahudi kulikuwa na sheria inayotaka mtu atendewe sawasawa na kile alichotenda yeye, yaani sheria ya kulipa kisasi: mtu akitenda ubaya, basi na yeye atendewe ubaya huo huo (rejea Walawi 24:20). Kwa kadiri ya Yesu sheria hii inazidisha zaidi uhasama na chuki kuliko kuleta amani. Hivyo, Yesu hataki watu walipe visasi wanapotendewa mabaya. Katika kufundisha jambo hili Yesu anatoa mifano kadhaa: (i) ukipigwa shavu moja, geuza na jingine, (ii) mtu akiwa anakudai (na umeshindwa kulipa) hadi kufikia hatua ya kukunyang’anya shati lako (vazi lako), wewe mpe na koti na (iii) ukilazimishwa kubeba mzigo wa mtu [hasa Askari wa Kirumi] kwa umbali fulani, wewe beba kwa umbali mrefu zaidi.

Shindeni ubaya kwa kutenda mema
Shindeni ubaya kwa kutenda mema

Mifano hii ya Yesu tunaweza kushindwa kuielewa vizuri. Hebu tuone ufafanuzi wake kwa kifupi. Mfano wa kwanza: kwa kawaida mtu akikupiga kofi huwa anatarajia kuwa na wewe utampiga kofi ili kulipiza kisasi. Sasa mtu huyo atastaajabu akiona unageuza na upande mwingine ili akupige. Wewe unayegeuza shavu la pili utakuwa umeonesha upole mkubwa na pengine unyenyekevu wa hali ya juu. Yeye aliyekupiga atajiona mpumbavu na mwenye hatia. Tendo hilo litamuumiza zaidi yeye kuliko ulivyoumia wewe. Mfano wa pili: kwa Wayahudi mtu akivua shati na koti alihesabika yu uchi. Hivyo, kama mdeni wako amefikia hatua ya kukaa uchi kwa sababu ya deni unalomdai, wewe unayemdai utaonekana huna utu wala ubinadamu. Hivyo, watu watakudharau sana wewe uliyesababisha mwenzako kuwa uchi kisa deni. Hali hii, kama dhamiri yako ni safi, itakuuma sana na hata kukuaibisha. Mfano wa tatu unahusiana na Maaskari wa Kirumi: Kulikuwa na sheria inayomruhusu Askari wa Kirumi kuamuru raia wa Kiyahudi (au mwingine yeyote asiye Myahudi) kumbebea kwa lazima mzigo/furushi lake au la Mrumi mwingine. Hata hivyo, sheria ilisema mtu anayeamriwa kubeba mzigo huu asibebe umbali usiozidi hatua elfu moja (maili moja). Leo Yesu anasema mtu (akilenga Askari wa Kirumi) akikulazimisha kubeba mzigo kwa umbali wa maili moja, wewe mbebee kwa maili mbili (kwa hatua elfu mbili). Yesu anataka yule aliyelazimishwa kubeba azidishe umbali.

Msilipize kisasi hamna vigezo
Msilipize kisasi hamna vigezo

 

Hali ya kuzidisha umbali itamfanya yule aliyembebesha aonekane mwonevu na hivyo angeweza kupewa adhabu kwa sababu ya kuzidisha umbali uliotakiwa kisheria kwa mwanajeshi wa kirumi kubebewa furushi. Kwa mifano hii Yesu anataka kufundisha nini? Fundisho la Yesu ni hili: ukitendewa jambo baya, basi wewe jibu kwa kufanya jambo la ziada linaloonesha upole, upendo na ukarimu badala ya kulipiza kisasi. Kwa maneno mengine Yesu anafundisha kuwa tukitendewa jambo baya na mtu, tujitahidi kumtendea huyo mtu jambo jema ambalo ni kinyume kabisa na mategemeo au mawazo yake. Kimsingi Yesu anafundisha kuwa tusihangaike kupambana na wanaotutendea mabaya, bali tujitahidi kuwatendea wema ambao utakuwa chachu ya wao kuacha ubaya wao. Pili, tuangalie agizo la Yesu la kuwapenda adui zetu. Kwa kigiriki (lugha ya Agano Jipya) kuna maneno matatu yanayomaanisha upendo: kuna neno “eran” (eros) linalomaanisha upendo wa mwanaume kwa mwanamke (upendo wa kimapenzi); kuna neno “philein” (philia) ambalo linamaanisha upendo tunaoonesha kwa watu wetu wa karibu au wapendwa wetu ama marafiki; kuna neno “agapan” (agape) linalomaanisha upendo wa kikristo ambao msingi wake ni kuwatendea wengine ukarimu/wema na kumtakia mwingine mafanikio. Yesu anaposema “wapendeni adui zenu” anatumia neno “agapan” (neno linalomaanisha upendo wa agape) kuonesha kuwa tunapaswa kuwatendea wengine wema/ukarimu na kuwatakia mema hata kama wao wanatutendea mabaya, kututukana au kutufedhehesha.

Acheni chuki na uhasama, jengeni haki, amani na maridhiano
Acheni chuki na uhasama, jengeni haki, amani na maridhiano

Hoja ya Yesu ni hii: tunapaswa kuwapenda adui zetu kwani hata Mungu naye ni mwema (ana upendo) kwa wote wema na wabaya- kwa wanaomfurahisha na kwa wanaomchukiza. Mungu habagui. Hivyo nasi tusiwapende tu wale wanaotutendea mema (marafiki zetu na wapendwa wetu tu), bali tuwapende hata wale ambao kwa vipimo vyetu vya kibinadamu wanaonekana kuwa ni maadui zetu (yaani ni waovu kwetu). Na kwa kadiri ya Yesu namna kubwa ya kuonesha upendo kwa adui zetu ni kuwaombea.  Kutokana na Injili ya leo tunafundishwa mambo makubwa mawili: (1) Tusiwe watu wa kulipiza visasi kwani visasi huzidisha zaidi chuki na uhasama badala ya kuleta amani na utulivu. Kwa bahati mbaya wengi wetu tunapenda sana kulipiza visasi pale tunapotendewa ubaya. Mara nyingi tunafikiri kuwa tutapata amani tukilipiza visasi au tutawakomesha waliotufanyia ubaya. Tunajidanganya sana. Visasi huzidisha chuki, uhasama na migogoro. Ndoa nyingi hazina amani na nyingine zimevunjika kwa sababu ya kulipiza visasi; ndugu wameuana na wengine wapo jela kwa sababu ya kulipiza visasi. Mbaya zaidi visasi vinatuua sisi wenyewe kiroho na kimwili taratibu. Tunapolipiza kisasi tunajikomesha wenyewe kwani tunateseka sana moyoni, tunakosa amani ya moyo. Kwetu sisi tunapaswa kujinyenyekesha (kuwa wapole) na kuwa watu wa kusamehe. Mwanafalsafa mmoja alisema, “Njia nzuri ya kulipiza kisasi ni kusamehe.” Kusamehe ni nini?

Jipatanisheni na Mungu pamoja na jirani
Jipatanisheni na Mungu pamoja na jirani

Kusamehe ni kutokutumia kumbukumbu ya ubaya uliotendewa kulipiza kisasi- yaani unafahamu wazi mabaya uliyotendewa na mtu fulani lakini hutumii ufahamu/kumbukumbu ya hayo mabaya kulipiza kisasi. (2) Tunapaswa kuwapenda adui zetu na kuwaombea. Ukristo wa kweli unatudai kufanya jambo la ziada ambalo kwa hali ya kawaida ni gumu kufanywa. Kwa hali ya kawaida ni vigumu sana kumpenda adui yako: adui ni mtu anayekutendea au kunuia uovu juu yako, adui ni anayepingana na wewe, adui ni mtu ambaye hakutakii mema, adui ni mtu ambaye anapenda kuona unaangamia au hufanikiwi, adui ni mtu mwenye chuki na wewe. Kwa kadiri ya vipimo vyetu adui ni mtu mwovu, hafai kabisa. Je, mtu mwenye sifa hizi unaweza kumpenda? Wengi wetu hatuwapendi adui zetu bali tunakazana kuwalaani, kuwaombea mabaya, kulipiza visasi na hata kuwaangamiza. Yesu anataka tuwapende adui zetu kwa kuwatendea mema/ukarimu na kuwatakia mema. Yesu anafundisha jambo gumu kwa hulka ya binadamu: jambo hili ni gumu sana lakini siyo kwamba haliwezekani. Kwa nini Yesu anataka tuwapende adui zetu? Kwa sababu hakuna faida yoyote tunayopata kwa kuwachukia adui zetu. Tunapojenga uadui na mtu tunateseka sana ndani ya nafsi zetu. Leo Yesu anatupa namna bora ya kuwapenda adui- nayo si nyingine bali ni kuwaombea na kuwatakia matashi mema. Je, ni wangapi kati yetu huwa tunawaombea adui zetu katika sala zetu? Na kwa nini tunahitaji kuwaombea? Ili waongoke na kuwa watu wema zaidi na hivyo kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.  Dominika Njema.

16 February 2023, 11:35