2020.03.13 Dominika ya III ya Kwaresima (A):Kipindi hiki cha kwaresma kila mmoja ajitafiti na kujiuliza kiu yangu ni ipi na wanaume hawa watano kwangu ni wepi. 2020.03.13 Dominika ya III ya Kwaresima (A):Kipindi hiki cha kwaresma kila mmoja ajitafiti na kujiuliza kiu yangu ni ipi na wanaume hawa watano kwangu ni wepi. 

Dominika ya III ya Kwaresima Mwaka A:Yesu ni maji ya Uzima!

Kristo ana nguvu ya kumbadili mdhambi apate kuokoka na kuwa mwema,mwana wa Mungu.Yule mwanamke alipopata maji ya uzima,hakufungamana tena na Hekalu la Yerusalemu au Gerezimu ila alimwabudu Mungu katika Roho na Kweli.Ujumbe huu ni wetu sisi pia:Kipindi hiki cha kwaresma kila mmoja wetu inafaa kujitafiti na kujiuliza kiu yangu ni ipi na wanaume hawa watano kwangu ni wepi au ni nini?

Na Padre Paschal Ighondo – Radio Vatican. 

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima mwaka A wa Kanisa. Masomo ya dominika hii yanatuongoza katika kujua na kutambua kuwa Yesu Kristo ni maji ya uzima na heri yule anayeamini na kuyatafuta maji haya maana atakuwa na uzima wa milele maana; “Bwana asema, atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi, yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji yakibubujikia uzima wa milele (Yn. 4: 13-14). Kadiri ya mapokeo ya mama Kanisa, katika dominika hii linafanyika takaso la kwanza la wakatekumeni watakao batizwa katika mkesha wa Pasaka.

Somo la kwanza ni la Kitabu cha kutoka (Kut 17: 3-7). Somo hili linatueleza jinsi wana wa Israeli walivyomnung’unikia Musa na Mungu na kumjaribu kwa kukosa maji walipokuwa jangwani licha ya kuona jinsi walivyokombolewa kutoka utumwani Misri kwa maajabu mengi. Hata hivi Mungu aliwavumilia na kuwapa maji, ingawa hawakustahili. Nasi tulipobatizwa tulivushwa kutoka vilindi ya bahari ya dhambi, kutoka utumwa wa shetani kama waisraeli kutoka mikono ya Farao. Tunapoendelea kusafiri katika jangwa la ulimwengu huu, Kristo ni Musa mpya anayetuongoza katika nchi ya ahadi, yaani mbingu, anatuliza njaa yetu kwa chakula cha mbingu (Ekaristi Takatifu) na kiu yetu kwa neno la Mungu. Tunaalikwa tusiwe kama waisraeli, tusimjaribu Mungu kama Yesu alivyomjibu shetani katika jaribu la pili kuwa imeandikwa usimjaribu Bwana Mungu wako. Hivyo tunaitwa kusikiliza sauti yake kama wimbo wa katikati unavyoimba; “Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu mioyo yenu” (Zab. 95:1-2, 6-9).

Somo la pili ni la waraka wa Mtume Paulo kwa warumi (Rum 1-2, 5-8). Katika somo hili Mtume Paulo anatueleza kuwa Mungu alianza kutupenda sisi akatuletea wokovu ambao ni zawadi bila stahili zetu kwa njia Yesu Kristo Mwanae wa pekee. Zawadi kubwa pia ni Roho Mtakatifu tunayempokea kwa njia ya ubatizo na Kipaimara akaaye ndani mwetu ambaye anatuwezesha kumpenda Mungu na kumwita Baba. Mtume Paulo anatueleze kina cha upendo wa Yesu alipoyatoa maisha yake kwa ajili yetu wakati sisi tulipokuwa bado wadhambi. Ni kwa gharama ya maisha yake na kwa kifo chake ametuletea uzima wa kweli na Roho Mtakatifu ambaye mitume walimpokea siku ya pentekoste na ambaye kila mmoja wetu alimpokea alipobatizwa na tunaendelea kumpokea katika sala, sakramenti za Kanisa na pia tunapojitoa kwa ajili ya wengine.

Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 4:5-42). Kabla ya kuitafakari sehemu hii ya injili ni vyema tukajua mpangilio wa Injili tunazosoma kuanzia domenika ya 3 ya kwaresma hadi domenika ya 5 katika mwaka A. Mpangilio huu ni wa kiustadi mno. Domenika ya 3A tunasoma simulizi la mwanamke Msamaria aliyeenda kuchota maji katika kisima cha Yakobo (Yn. 4:5-42). Katika simulizi hili tunafundishwa kuwa kwa ubatizo Kristo anakuwa chemchem ya Uzima wa milele. Domenika ya 4A tunasoma simulizi la kuponywa mtu aliyezaliwa kipofu (Yn. 9:1-41). Simulizi hili linatufundisha kuwa kwa ubatizo, Yesu anakuwa Mwanga wa Maisha yetu. Na domenika ya 5A tunasoma simulizi la kufufuliwa kwa Lazaro (Yn. 11:1-45). Sehemu hii ya Injili inatufundisha kuwa katika ubatizo, Kristo anatufufua kutoka mauti ya dhambi na kutupatia uzima wa kiroho ndani mwetu.

Mpangilio huu unalenga kuwaandaa wakatekumeni watakaobatizwa usiku wa Pasaka baada ya maandalizi ya miaka mitatu. Zamani kadiri ya mapokeo ya kanisa, katika dominika ya kwanza ya kwaresima, wakatekumeni walioonesha ukomavu wa kiimani walichaguliwa na majina yao kuandikwa kwenye kitabu cha watakaobatizwa usiku wa Pasaka na dominika ya 2 walitambulisha kwa jumuiya wa waamini. Katika domenika tatu za mwisho za kwaresima, yaani dominika ya 3, 4, na 5 yalifanyika matakaso matatu ya wakatekumeni. Kumbe katika domenika ya 3 linafanyika takaso lao la kwanza na kutolewa fundisho la umuhimu wa maji ya ubatizo kwa maondoleo ya dhambi.

Dhambi ni kujitenga na Mungu. Matokeo ya kujitenga na Mungu ni kukosa amani ndani ya nafsi zetu mpaka pale tunapojuta na kuomba msamaha. Mdhambi anapokiri ubaya wake na kutambua ufinyu wa uwezo wake, anakuwa na kiu ya Mungu. Maandiko matakatifu yanamlinganisha Mungu na chemchemi ya maji ya uzima, anayekaa karibu naye anapata uhai, anapata utakaso, anaapata nguvu na maisha yake yanafanikiwa. “Ee Mungu wewe ni Mungu wangu, nakutafuta kwa moyo. Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu, nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji” (Zaburi 63). “Nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote; nitawanyunyizia maji safi, nitawatakasa na uchafu wenu wote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, asema Bwana” (Ezekieli 36:23-26). Mungu kupitia kinywa cha nabii Yeremia anasema; “Watu wangu wametenda maovu mawili, wameniacha mimi chemchemi ya uzima na kujichimbia visima vinavyovuja ambavyo maji yake hayakai ndani yake” (Yer. 2:13). Na ni kweli tukiangalia matukio ya wanaoangamia kwa kuwategemea wanadamu wapate mafanikio, si haba kusikia habari za kufa kwao.

Tukirudi katika Injili, mazingira ya simulizi la Yesu na mwanamke Msamaria ni katika kisima cha Yakobo kilichopo katika barabara ya Yudea kuelekea Galilaya katika mji wa Shekem. Kisima hiki masimulizi yanasema kuwa kina urefu wa mita 32, bado kipo na kinatoa maji safi tena kwa wingi. Itakumbukwa kuwa katika siku za kale, Kisimani ilikuwa ni mahali pa makutano ya watu mbalimbali; Wachungaji kunywesha mifugo yao, Wafanyabiashara kutangaza na kuuza bidhaa zao, vijana kutafuta na kukutana wachumba wao, na akina mama kuchota maji na kupata habari mpya za mtaani (rejea Mwa 26:15-25, 29:1-14, Kut 2:15-21). Tukichukulia kama mahali pa kukutana wachumba wanaonuia kuoana na kutilia maanani kuwa katika lugha ya kibibilia, Israeli alijulikana kama mwanamke aliyeposwa na Mungu na tukikumbuka jinsi Israeli alivyomsaliti Mungu kama inavyoelezwa katika kitabu cha Nabii Hosea kuwa Israeli alikuwa kama kahaba kwa kuabudu miungu mingine na alijikahabisha mwenyewe huko Misri, baadaye kwa Waashuru, Wababilonia, Wapersia, Wagiriki na mwisho kwa Warumi. Na kila wakati aliiba miungu yao, tunaona kuwa kitaalimungu Mwanamke Msamaria anasimama badala ya Taifa la Israeli na jamii yote ya wanadamu iliyomwasi Mungu kwa ukahaba wa kuabudu miungu mingine. Yesu anakuja kutupatanisha na Mungu wa kweli na anafanya hivyo hatua kwa hatua.

Katika simulizi hili la mwanamke msamaria, tunaona pedagojia ya Yesu inavyotuongoza tuweze kujitambua jinsi tulivyo ndani ya nafsi zetu na kumrudia Mungu. Ni pedagojia ya mazungumzo, majadiliano na kusikilizana inayosimikwa na kujengwa katika heshima ya utu wa mtu, uvumilivu, ukweli na uwazi kwa kila mmoja. Kuambiana ukweli na kuukubali ni hatua muhimu sana katika wongofu. Inahitaji ujasiri na msaada wa Roho Mtakatifu tunaoupata kwa njia ya sala, kufunga na kutenda matendo ya huruma. Yesu alimwongoa mwanamke msamaria hatua kwa hatua kumtambua na kumfahamu kwa kutambua na kufahamu udhaifu na dhambi zake na kuzikiri wazi. Mwanamke msamaria alimtambua Yesu kwanza kama Myahudi; “Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kutoka kwangu Msamaria” (Yn 4:9). Pili kama Bwana: “Bwana huna kitu cha kuchota maji, na kisima ni kirefu” (Yn 4:11). Baada ya mahojiano na mwanamke kutaka kuyapata maji ya uzima Yesu alimwambia; “Nenda kamleta mume wako” naye anakiri kuwa udhaifu wake akisema; “Sina mume”. Hapa Yesu anaanza kujifunua kwake na kumwambia; “umejibu vyema maana; umekuwa na wanaume watano naye uliye naye sio wako”. Tano hapa inawakilisha vitabu vitano vya mwanzo katika Biblia, yaani Torati ya Musa. Hapa sasa ni hatua ya tatu anamtambua Yesu kama Nabii akisema; “Bwana naona ya kuwa u-nabii” (Yn 4:19). Baada ya mazungumzo kuendelea inafika hatua ya nne ambapo anamtambua Yesu kama Masiha; “Najua ya kuwa yu aja Masiha aitwaye Kristo”. Hatua ya mwisho Yesu anajifunua kwake na kusema: “Mimi ninayesema nawe ndiye” (Yn 4:25-26).

Kristo ana nguvu ya kumbadili mdhambi apate kuokoka na kuwa mwema – mwana wa Mungu. Yule mwanamke alipopata maji ya uzima, hakufungamana tena na Hekalu la Yerusalemu au Gerezimu ila alimwabudu Mungu katika Roho na Kweli. Ujumbe huu ni wetu sisi pia: “Mungu ni Roho na wamwabuduo halisi watamwabudu katika roho na kweli” (Yn. 4, 24). Kipindi hiki cha kwaresma kila mmoja wetu inafaa kujitafiti na kujiuliza kiu yangu ni ipi na wanaume hawa watano kwangu ni wepi au ni nini? Ukiwatambua, utamtambua Kristo na kumuomba akupe maji ya uzima wa milele, naye atakuponya na uovu wako wote na kukujaza Roho Mtakatifu atakayekata kiu yako yote nawe utaacha mtungi wako na kwenda mbio kwa furaha kuwaambia watu kuwa nimekutana na Kristo njooni nanyi mkamwone yuko katika Sakramenti ya Kitubio anawasubiri kuwapokea, kuwatakasa na kuwasafisha na uovu wenu wote na kisha kuwatakasa, atawalisha na kuwashibisha kwa Mwili wake katika Ekaristi Takatifu na kuwakata kiu yenu kwa Damu yake. Baada ya hayo yote wataweza kusema; “Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu” (Yn 4:42).

Tafakari ya Dominika ya III ya kwaresima
10 March 2023, 18:42