Dominika ya Matawi Kanisa linaadhimisha siku ile Yesu Kristo alipoingia kwa shangwe mjini Yerusalemu kama Mfalme na Mkombozi (Mt. 21:1-11), mwanzo wa maadhimisho ya Juma Kuu la Ukombozi wa mwanadamu. Dominika ya Matawi Kanisa linaadhimisha siku ile Yesu Kristo alipoingia kwa shangwe mjini Yerusalemu kama Mfalme na Mkombozi (Mt. 21:1-11), mwanzo wa maadhimisho ya Juma Kuu la Ukombozi wa mwanadamu.  (Vatican Media)

Dominika ya Matawi: Kristo Yesu Anaingia Yerusalemu Kwa Shangwe: Mfalme na Masiha

Dominika ya Matawi Kanisa linaadhimisha siku ile Yesu Kristo alipoingia kwa shangwe mjini Yerusalemu kama Mfalme na Mkombozi (Mt. 21:1-11), watoto walimlaki; nao walichukua matawi ya mitende mikononi, wakapaza sauti wakisema: Hosana juu mbinguni: Mbarikiwa wewe uliyekuja na wingi wa rehema yako”. Pili ni Mateso ya Yesu Kristo (Mt. 26:14-27,66), yanayotuingiza katika Jumaa Kuu la kuadhimisha fumbo la ukombozi wetu, mateso, kifo na ufufuko wake – Pasaka.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Utangulizi: Injili ya Mathayo 21:1-11: Kumbukumbu ya Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo: I. Isa 50:4-1, II. Phil 2:6-11, III. Mt. 26:14-27,66. Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya Matawi mwaka A wa kanisa. Katika Dominika hii Kanisa linaadhimisha matukio makuu mawili: Kwanza, Bwana wetu Yesu Kristo kuingia kwa shangwe mjini Yerusalemu kama Mfalme na Mkombozi (Mt. 21:1-11). Ndiyo maana maneno ya moja kati ya nyimbo za mwanzo katika dominika hii yanasema; “Siku sita kabla ya Pasaka, wakati Bwana alipoingia mjini Yerusalemu, watoto walimlaki; nao walichukua matawi ya mitende mikononi, wakapaza sauti wakisema: Hosana juu mbinguni: Mbarikiwa wewe uliyekuja na wingi wa rehema yako”. Pili ni Mateso ya Yesu Kristo (Mt. 26:14-27,66), yanayotuingiza katika Jumaa Kuu la kuadhimisha fumbo la ukombozi wetu, mateso, kifo na ufufuko wake – Pasaka. Hili ni adhimisho kuu moja linalodumu kwa muda wa siku tatu mfululizo: Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na Jumamosi Takatifu. Itakumbukwa kuwa Alhamisi Kuu, tunaadhimisha Karamu ya mwisho, mlo wa mwisho aliokula Kristo Yesu na wanafunzi wake muda mfupi kabla ya kukamatwa na kuanza kuteswa hadi kufa Msalabani. Ni siku aliyoweka Sakramenti za Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu na Amri ya mapendo inayomwilishwa katika huduma na hasa kwa maskini. Ijumaa Kuu tunaadhimisha: mateso na kifo cha Kristo Msalabani na Jumamosi Kuu tunaomboleza kwa masikitiko makuu tukingojea ufufuko wake tunaoanza kuusherehekea kwa vijilia vya pasaka kwa ibada ya Mwanga na kupigwa kwa mbiu ya kumshangilia Kristo mfufuka. Maadhimisho haya yanakuwa na maana kwa walioziishi vyema siku arobaini za kwaresima, siku za mfungo mtakatifu uliojikita katika kusali, kufunga, kutafakari neno la Mungu na kutenda matendo ya huruma kama sehemu ya kujihuisha katika maisha ya kiroho na kujipatanisha na Mungu.

Dominika ya Matawi: Matawi ya Mitendo kielelezo cha ushindi
Dominika ya Matawi: Matawi ya Mitendo kielelezo cha ushindi

Masomo yote kwa ujumla wake (I. Isa 50:4-1, II. Phil 2:6-11, III. Mt. 26:14-27,66), yanamwonesha Yesu Kristo kuwa ni mfalme wa amani, mpole, mnyenyekevu, mvumilivu na hana makuu. Hivyo anaingia Yerusalemu kwa shangwe na furaha akiwa juu ya mwanapunda – mnyama aliyetumiwa na watu duni, maskini na wanyonge kwa safari na kazi. Kadiri ya mapokeo, mwanapunda ambaye hajatumiwa bado kwa kazi yoyote, alitumika kwa mambo matakatifu. Yesu kupanda mwanapunda ni ishara wazi kuwa yeye ni Mtakatifu na yote anayoenda kuyafanya ni Matakatifu. Tukio hili linatimiza utabiri wa nabii Zekaria usemao; “Furahi sana Ee binti Sayuni, piga kelele ee binti Yerusalemu! Tazama Mfalme wako anakuja kwako. Ni mwenye haki, naye ana wokovu, ni mnyenyekevu amepanda punda, naam, mwana punda, mtoto wa punda” (Zek.9:9). Watu waliochukua matawi kama ishara ya ushindi na matumaini, walitandika nguo zao huku wakiimba nyimbo za furaha. Hili ni kundi la watu wanyonge, wenye kipato cha chini, watu toka mashambani, nao wanafanya mji wa Yerusalemu utikisike kwa kelele za shangwe. Hivyo kuamsha hasira za wakuu wa Makuhani, Mafarisayo na Waandishi, hata wakaanza mikakati ya kumkamata Yesu tena usiku, wakati wa giza, wakiwa na taa na mienge, marungu na mikuki na silaha za kivita huku wamejaa hofu na mashaka. Yesu anakamatwa akiwa bustanini Gethsemane akisali. Naye bila ubishi anaanza safari ya ukombozi kuelekea Golgota kusulubiwa.

Matawi ni ishara ya ushindi wa Kristo, Mfalme na Masiha
Matawi ni ishara ya ushindi wa Kristo, Mfalme na Masiha

Ni safari yenye mateso makali: Anabebeshwa msalaba mzito, anafanyiwa dhihaka njiani, anapigwa mijeledi, anatemewa mate, anatukanwa na pale Msalabani anapigiliwa misumari mikononi na miguuni. Hatimaye anakufa kwa sababu ya dhambi zetu kama mtu aliyelaaniwa na Mungu kama tunavyosoma katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati: “Ikiwa mtu ametenda dhambi ipasayo kufa, nawe ukamtundika juu ya mti, mzoga wake usikae usiku kucha juu ya mti; lazima utazikwa siku hiyohiyo. Kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu, asije akatia unajisi katika nchi yako akupayo Bwana Mungu wako iwe urithi wako” (Kum.21:22-23). Lakini kwa kifo chake kilivyokuwa cha pekee, dunia ilitetemeka, jua lilififia, kukawa giza, pazia la hekalu likapasuka mara mbili, nao walioshuhudia walisadiki uaguzi wa manabii na kusema; “Hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu”. Haya yote aliyotendewa Yesu, yanatufundisha kuwa hakuna utukufu pasipo mateso na hakuna Pasaka bila Ijumaa kuu. Mateso na mahangaiko ya maisha yetu hapa duniani yanaakisi tu mateso ya Kristo kwa ajili ya dhambi zetu. Kwa kujua ukweli huu Kanisa linatuhimiza kuvumilia mateso na magumu yanayotupata katika kumfuata Kristo ili tuufikie utukufu wa milele. Mateso tuyapatayo katika kuikiri na kuishuhudia imani yetu yanatustahilisha kuingia katika ufalme wa mbinguni, kama tukiyapokea kwa imani na bila kunung`unika. Lakini tutambue kuwa majukumu yanayotukabili katika maisha ya kila siku sio mateso. Mfano ili kuleta mafanikio, maendeleo katika maisha lazima kufanya kazi kwa bidii na kwa uvumilivu mkubwa, kutumia nguvu, kujinyima au kuacha starehe zingine na wakati mwingine kuumia. Haya ni majukumu na sio mateso ndiyo maana Mtume Paulo anatuambia “asiyefanya kazi na asile”, kwani kazi ni agizo la Mungu kwa Mwanadamu la kuutiisha ulimwengu.

Maandamano na Matawi ni kumshangilia Kristo Mfalme na Maisha
Maandamano na Matawi ni kumshangilia Kristo Mfalme na Maisha

Lakini pia, yapo mateso na mahangaiko yatokanayo na dhambi na makosa yetu wenyewe. Mfano wa matendo yanayotusababishia mateso yasiyotulea wokovu: kukamatwa na kupigwa kwa sababu ya ziwi, uasherati na uzinzi, hivyo kubaki na maumivu na makovu kama vile kutolewa meno yote ya sebuleni au kufanywa chongo. Kuendesha vyombo vya usafiri kama gari, pikipiki au baiskeli kwa mwendo kasi ukasababisha ajali, ukaanguka, ukavunjika. Kutumia dawa za kuzuia au kutoa mimba, kukakuharibia mfumo wa uzazi, ukashindwa kupata watoto unapowahitaji, ulevi, uvivu, uzembe kazini unaokusababishia kufukuzwa kazi, ukala rushwa na kufungwa genezani. Matendo haya yanatusababishia matatizo na masumbuko mengi na watu wajanja wanaoongozwa na Ibilisi wanayatumia ili kujinufaisha, wakidai kutusaidia kwa kimiujiza. Haya ni mateso ya kujitakia wala Mungu hahusiki na wala hayatuletei wokovu bali yatatupeleka katika “moto wa milele aliyetayarishiwa ibilisi na malaika zake tangu awali”. Tunapotafakari juu ya mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo yaletayo wokovu, kila mmoja anapaswa kujiuliza juu ya mateso anayosababisha kwa wengine anaoishi nao. Tukishayatambua basi tuweke nia ya dhati ya kujuta na kujirekebisha ili Pasaka itukute wenye furaha kwa kuwa imani yetu kwa Yesu imeongezeka, tufufuke na Kristo tusibaki ndani ya kaburi la dhambi. Kujua thamani ya mateso kutupe uvumilivu, ustahimilivu na ujasiri wa kuyapokea ili yatuimarishe zaidi kiimani. Tukiwa na mtazamo huo kamwe mateso hayatakuwa kikwazo kwa imani yetu. Tukumbuke kuwa Mungu hatuletei mateso bali huweza kuyaruhusu yatupate ili atupatie mazuri zaidi iwapo tutakuwa na imani na kumtegemea yeye. Uvumilivu na kumtegemea kwa imani ndiyo dawa ya kuyakabiliana na mateso.

Juma kuu Kanisa linatafakari mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu
Juma kuu Kanisa linatafakari mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu

Katika simulizi la mateso ya Yesu, umati wa watu walipiga makelele wakisema asulubishwe, asulubishwe. Kwetu sisi kwa mawazo yetu, kwa maneno yetu, kwa matendo yetu maovu, kwa kutokutimiza nyajibu zetu za kikristo, kwa dhambi zetu tunatoa mlio na makelele hayo hayo, msulubishe, msulubishe. Petro alijaribu kupambana na nguvu za giza kwa upanga. Kristo alipambana na kumshinda shetani si kwa mapanga na vitisho bali kwa uvumilivu wake, kwa unyenyekevu wake, kwa upole wake na kwa utii wake kwa Mungu Baba. Kumbe tunapswa kujitafakari na kujiuliza, je hatuna fikra kama za Petro za kupambana na nguvu za shetani na Ibilisi kwa upanga wa giza, maseng’enyo, malumbano, mapigano, visasi na fitina. Je, hatusemi kila siku katika makundi ya watu msulubishe, msulubishe, mwondoshe, mwondoshe. Tukumbuke ufalme wa Kristo si wa Dunia hii hivyo hatupaswi kumpigania kwa nguvu za kimwili, kisiasa, kijeshi, bali kwa ushuhuda wa maisha yetu mema. Mtakatifu Petro hakuishia hapo bali mara tatu amemkana Kristo akisema; “Mimi si mfuasi wa mtu huyu”, akasisitiza; “mimi simjui mtu huyu”. Sisi pia tunafanya jambo hili hili katika maisha yetu pale tunapoionea aibu Injili, tunaporudi nyuma kiimani sababu ya matatizo na magonjwa mbalimbali, tunapokosa imani na matumaini kwa nguvu na uweza wa Kristo, tunapotafuta suluhu ya matatizo katika dhambi.

Dominika ya Matawi: Kristo Yesu Mfalme na Masiha wa Bwana
Dominika ya Matawi: Kristo Yesu Mfalme na Masiha wa Bwana

Jogoo amekwisha kuwika mara ya tatu, tunaalikwa kujirudi, tujiweke chini ya msalaba kwani hatuna tumaini lingine, “Japo kwao wanaopotea Msalaba ni kikwazo na upuuzi”, kwetu ni nguvu ya Mungu, kwetu ni nguvu ya Kristo, kwetu ni alama ya ushindi, tuutazame msalaba kwa imani kuu na moyo wa toba. Tumwombe Mungu atujalie moyo thabiti na wa ujasiri wa kuyapokea mateso na mahangaiko kwa uvumilivu na imani kuu kama Kristo alivyoyapokea na hata pale tunaposikia hatumjui mtu huyu! Mwondoshe! Mwondoshe! Msulubishe! Msulubishe! Tusikatishwe tamaa au kukwazika na kurudi nyuma, tuutazame msalaba, utupe nguvu na ujasiri, utuimarishe na kutuunganisha zaidi na Kristo ili mwisho wa yote tukamsifu Mungu pamoja na malaika zake huko mbinguni milele yote. Isaya anasema; “Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi…huniamsha sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao”. Tuombe neema ya kuwa wasikivu na watii. Tukubali kufundishwa na kuelekezwa. Tuingie juma kuu kwa moyo wa majuto. Tujipatanishe na Mungu, ndipo tutakapokuwa na sababu ya kufurahia siku ya Pasaka na tunuie kutorudi nyuma tena mpaka tutakapomaliza safari yetu na kufurahi milele katika Pasaka ya Mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.

Matawi 2023

 

31 March 2023, 11:37