Tafakari ya Dominika ya II ya Kwaresima Mwaka A:Kufanya mabadiliko ya kweli-Metamorphosis
Na Padre Philemon Anthony Chacha wa Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vaticani katika Dominika hii ya pili ya kwaresima ambapo tunaendelea na kile kipindi ambacho Mama Kanisa ametupatia cha siku arobaini za mapambano ya kiroho. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Fransisko katika Kipindi cha Kwaresima mwaka huu unaojikita katika kauli mbiu isemayo “Toba ya Kwaresima na Mchakato wa Sinodi” unaendelea kutusindikiza katika kipindi hiki. Ujumbe huu unaochota utajiri wake kutoka katika tukio la Kugeuka Sura kwa Bwana wetu Yesu Kristo mbele ya wanafunzi wake Petro, Yakobo na Yohane nduguye. Ni ujumbe unaotukumbusha kupanda juu ya mlima kumsikiliza na kumsindikiza Kristo katika kupata mambo muhimu katika maisha yetu ya kiroho. Ni katika muktadha huu masomo yetu ya dominika hii yanatualika kubadilisha Maisha yetu na kuyafanya yawe mapya, kuuvua ule utu wa kale na kuuvaa ule utu mpya (rej. Ujumbe wa Kwaresima Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania 2023). Yanatualika pia kujikita katika kutafakari kukutana kwetu na Mwenyezi Mungu.
Somo la kwanza kutoka kitabu cha Mwanzo (Mwz 12:1-4a) linatuambia jinsi Abramu alivyokutana na Mungu na kuamini katika ule wito aliousikia. Abramu anaalikwa na Mungu kuacha nchi yake, kuacha jamaa zake na nyumba ya baba yake, kwenda katika nchi ambayo haijatajwa kwa ajili ya kufanywa kuwa taifa kubwa. Abramu anakubali mwaliko huu na anaenda, anaacha vyote na anaaanza safari iliyojaa imani na matumaini kwa kuwa karibu yake yupo Mungu anayemuongoza. Abramu hajui nini kilicho mbele yake, hajui ni nini kitakachomkuta, hajui ni wapi anaelekea lakini anatembea kwa imani.
Ndugu msikilizaji wa Radio Vaticani, somo hili linaweza kuwa ni mfano mzuri hata katika maisha yetu ya kila siku, pale tunaposema “Ndio” kwa Mungu katika kufuata mwaliko wake: watu wa ndoa wanaacha familia zao, ardhi yao, watu wao wa karibu, ili kwenda kwenye mpango mpya wa familia; kijana ambaye anachagua njia ya utawa au ya upadre anaacha nyumba yao kwa ajili ya kwenda kujenga nyumba kubwa zaidi yaani ile ya Jumuiya ya Kikristo. Hivyo basi pale ambapo Bwana anatuita hatuna budi nasi kuwa na uwezo wa kusema “Ndio” kama alivyotuonyesha baba yetu Abramu. Tunapaswa kutembea kwa imani, hasa katika kipindi hiki cha Kwaresima, tukiweka mipango yetu, maazimio yetu, mawazo yetu kwa Mungu, Yeye atatulinda na kutuongoza na hatimae kubadilisha maisha yetu na kuona si kwa macho ya kibinadamu bali kwa macho ya kiMungu. Imani na utii aliokuwa nao Abramu ni matokeo ya kukutana na Mungu. Kumbe hata na sisi tukiamini kuwa Mungu yupo tutakutana naye. Lakini swali ni Je tunakutana na Mungu wapi?
Ni katika sala, kufunga, tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma ambazo ndizo nguzo kuu nne za kipindi hiki cha Kwaresima. Katika somo la pili Mtakatifu Paulo Mtume kwenye waraka wake kwa Timotheo (2Tim 1:8b-10) anatukumbusha kuwa Mungu “anatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake”. Katika somo hili tunaalikwa kuwa tayari katika kuvumilia mateso na mahangaiko kwa ajili ya Injili, na kumshukuru Mungu kwa ajili ya wito wa utakatifu, sio katika kuamini nguvu zetu, akili zetu lakini katika ile neema ya Mungu. Somo letu la Injili linatoka katika injili ya Mathayo (Mt 17:1-9), inasimulia jinsi Petro, Yakobo na Yohane walivyokuwa mashahidi wa tukio la kugeuka sura kwa Yesu pale mlimani. Yesu aliwachukua na kuwaleta katika mlima mrefu faraghani (Mt 17,1).
Tukumbuke kuwa wanafunzi wa Yesu walipoambiwa na Yesu kuwa atakwenda kuteswa, walihuzunika na wakamkataza kuwa haitatokea hivyo, Yesu anapowapeleka mlimani na kugeuka sura anataka kuwaonesha kuwa baada ya mateso kuna utukufu wa milele. Wakati huu unakuwa ni wa muhimu sana kwa wanafunzi hawa wa Yesu, mpaka sasa walikuwa wanamtambua Kristo katika muonekano wake wa nje tu, mtu ambae hana tofauti na wengine, yule ambae walijua anapoishi na anapotokea. Baada ya kugeuka sura kwa Yesu pale mlimani sasa wanamfahamu kuwa ni tofauti na yule waliokuwa wakimfahamu kabla. Wanamtambua sasa kuwa ni Yesu wa kweli, ambae si rahisi kumuona kwa macho ya kawaida tu, lakini ni tunda la ufunuo.
Kumbe Yesu anataka kuwaonesha kuwa pamoja na kwamba wanamuona katika hali yake ya kibinadamu, bado ana hali nyingine, hali ya Utukufu wa kimungu. Kung’aa kwa sura kwa Bwana wetu Yesu Kristo pale mlimani inatukumbusha kuwa njia ya Msalaba inapelekea katika ufufuo na Maisha ya umilele na hiyo ndio maana halisi ya Kwaresima, kutusaidia sisi kuingia katika mafumbo hayo. Njia ya msalaba ni wakati ambao upendo wa Mwenyezi Mungu unalipuka ndani ya uovu wa mwanadamu na kuanza ile safari mpya, safari ya ukombozi, safari ya maisha mapya, safari ile ya utu upya. Ni katika nguvu ya msalaba ndipo kunatokea kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume; ni katika nguvu ya msalaba ndipo wafia dini wengi wanapata ule ushujaa wa kukiri Imani ya Kristo; ndipo wamisionari wengi ambao wanayatoa maisha yao kwa ajili ya maskini, wagonjwa na wale waliodharauliwa katika jamii.
Ni katika nguvu ya Msalaba, Mtakatifu Fransisko wa Assisi anakataa kuendelea kuishi maisha ya kifahari na kuamua kuyatoa maisha yake kwa ajili ya maskini, kukataa kuwa mtoto wa tajiri na mfanyabiashara maarufu na kuwa mtoto wa Mwenyezi Mungu. Ni katika nguvu ya msalaba ambapo Mt Yohane Bosco aliamua kuyatoa maisha yake kwa ajili ya vijana maskini na wasiojiweza, kuwaletea habari njema ili waweze kuwa “Raia Wema na Wakristo Hodari”. Ndugu msikilizaji wa Radio Vaticani, kumbe nasi pia tunaalikwa kujifunua zaidi katika upendo wa Kristo ili tuweze kuwa daima viumbe wapya wenye kung’arisha ule wema wa Mungu katika ulimwengu wetu wa leo. Tutiwe moyo kuwa baada ya vishawishi vya hapa duniani, baada ya mateso ya hapa duniani, pamoja na misalaba yetu ya kila siku kama tunavoambiwa kwenye kituo cha pili cha Njia ya Msalaba, kuna utukufu wa milele, tusikate tamaa hata mara moja tukamsahau Mungu kuwa ni muweza wa yote.
Kugeuka Sura kwa Yesu kutukumbushe tena kuyageuza maisha yetu, kuuvua utu wa kale kuuvaa utu upya, utu wa ndani wenye utakatifu. Tuachane na mambo ya dhambi, mambo ya kiulimwengu yanayotuweka mbali na Kristo, tupande mlimani pamoja na Bwana, tukamsikilize, tukamtafakari Kristo katika ukimya unaotokana na kusoma Maandiko Matakatifu na kuuona utukufu wake. Tumuombe Mama yetu Maria atusaidie katika kusikiliza ile sauti ya mwanae, akiwa yeye ni mfano bora wa yule anayesikiliza Neno la Mungu na kulikaribisha moyoni mwake. Ili kwa maombezi yake, Kristo azidi kuwa mwanga na kiongozi katika maisha yetu.