Tafuta

Tukio la kutabaruku upya Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Geita, Jumamosi tarehe 18 Machi 2023 baada ya toba na malipizi ya dhambi pamoja na kurejesha tena Ekaristi Takatifu ndani ya Kanisa kuu la Bikira Maria Malkia wa Amani: Ushuhuda! Tukio la kutabaruku upya Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Geita, Jumamosi tarehe 18 Machi 2023 baada ya toba na malipizi ya dhambi pamoja na kurejesha tena Ekaristi Takatifu ndani ya Kanisa kuu la Bikira Maria Malkia wa Amani: Ushuhuda! 

Jimbo Katoliki la Geita: Kutabarukiwa kwa Kanisa Kuu Bikira Maria Malkia wa Amani

Tukio la kutabaruku upya Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Geita, baada ya toba na malipizi ya dhambi pamoja na kurejesha tena Ekaristi Takatifu ndani ya Kanisa kuu la Bikira Maria Malkia wa Amani, iwe fursa ya pekee kwa watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Geita, kupyaishwa na kurejea tena katika ahadi yao ya kuwa "kama mawe yaliyo hai ... iliyojengwa katika nyumba ya kiroho, kuwa ukuhani mtakatifu, kutoa sadaka dhabihu zinazokubalika mbele ya Mungu: Ushuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utakatifu na utukufu wa Mama Kanisa anasema Mtakatifu Yohane Paulo II ni Kristo Bwana: Kuhani, Sadaka, na Hekalu la Agano Jipya. Tukio la kutabaruku upya Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Geita, Jumamosi tarehe 18 Machi 2023 baada ya toba na malipizi ya dhambi pamoja na kurejesha tena Ekaristi Takatifu ndani ya Kanisa kuu la Bikira Maria Malkia wa Amani, iwe fursa ya pekee kwa watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Geita na Tanzania katika ujumla wake, kupyaishwa na kurejea tena katika ahadi yao ya kuwa "kama mawe yaliyo hai ... iliyojengwa katika nyumba ya kiroho, kuwa ukuhani mtakatifu, kutoa sadaka dhabihu zinazokubalika kwa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo” (1 Pt 2:5.) Tukio hili liwakumbushe watu wa Mungu kuhusu: maana, wito na utume wao ndani ya Kanisa. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni ishara thabiti na sababu ya hali ya juu kabisa ya ushirika katika uzima wa kimungu na umoja wa Taifa la Mungu ambalo hulifanya Kanisa liwepo. Ekaristi Takatifu ni kilele cha tendo la Mungu la kuutakatifuza ulimwengu katika Kristo Yesu na kilele cha tendo la waamini kuliabudu Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa ni mahali patakatifu panapowawezesha waamini kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, Kuabudu, Kusali na Kutafakari Matendo makuu ya Mungu katika maisha yao. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, liturujia ni chemchemi ya kwanza na ya lazima ambayo toka kwake waamini wanaweza kuchota roho ya kweli ya Kikristo kwa Mwenyezi Mungu kuabudiwa na mwanadamu kutakaswa.

Unajisi wa Kanisa na kufuru dhidi ya Ekaristi Takatifu ni hatari sana.
Unajisi wa Kanisa na kufuru dhidi ya Ekaristi Takatifu ni hatari sana.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafafanua kwamba, Altare, ambayo Kanisa lililounganika katika kusanyiko huizunguka katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, yanaonesha mambo mawili ya fumbo moja. Altare inaonesha: sadaka na meza ya Bwana. Altare ni alama ya Kristo mwenyewe aliye kati ya kusanyiko la waamini wake, papo hapo akiwa kafara iliyotolewa kwa ajili ya upatanisho kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Kristo alijitoa kwa ajili ya ukombozi wa binadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Altare ni sura ya mwili wa Kristo anasema Mtakatifu Ambrosi na kwamba, mwili wa Kristo uko juu ya Altare. Kumbe, Kanisa linafundisha kuhusu umoja kamili kati ya Sadaka na Altare. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walileta mageuzi makubwa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kuonesha umuhimu wa kuzunguka Altare katika maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa. Rej. KKK 1382, 1672 na 1372. Bikira Maria, Mama wa Mungu, sura na kielelezo cha Kanisa, Nyota ya Uinjilishaji mpya na chachu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi awe ni dira na mwongozo kwa watu wa Mungu ili waweze kuitikia kikamilifu mpango wa Kimungu kwa ari ya imani, matumaini na mapendo, kwa ajili ya kuwajenga na kuwafariji watu wote wenye mapenzi mema, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, daima wakiendelea kujiaminisha chini ya huruma ya Mungu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Katika Kristo Yesu, Kanisa ni kama Sakramenti au ishara na chombo cha kuwaunganisha watu kiundani na Mwenyezi Mungu na hivyo kuleta umoja kati ya wanadamu wote.

Altare ni kielelezo cha sadaka na meza ya Bwana, alama ya Kristo Yesu.
Altare ni kielelezo cha sadaka na meza ya Bwana, alama ya Kristo Yesu.

Roho Mtakatifu hulitakatifuza na kuliongoza Kanisa kwenye kweli zote na kulipamba kwa karama na mapaji yake na hivyo kuwawezesha waamini kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani, Ufalme unaosimikwa katika: Ukweli, Uzima, Utakatifu, Neema, Haki, Mapendo na Amani. Ni katika muktadha huu, waamini wanahimizwa kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu, haki na amani; tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Hatima na mustakabali wa maisha ya mwanadamu uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, Uso wa huruma ya Baba wa milele mwaliko kwa waamini ni kuendelea kuwa ni mashuhuda wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu na Kanisa ambalo kimsingi ni mwili wa Kristo Yesu katika Fumbo na wanaunganishwa pamoja kwa njia ya Sakramenti za Kanisa. Hili ndilo Kanisa: Moja, takatifu, katoliki na la Mitume. Kanisa katika hija ya maisha na utume wake hapa duniani linaendelea kusonga mbele katikati ya madhulumu ya ulimwengu na faraja za Mungu likitangaza Fumbo la Msalaba hadi Bwana atakapo kuja tena. Re. 1Kor 11:10:35. Kwa uwepo wa Kristo Yesu Mfufuka, Kanisa linapata nguvu ya kuzishinda, kwa saburi na upendo, taabu na shida za ndani na za nje na kuufunulia ulimwengu; kwa uaminifu fumbo la Bwana, ingawa bado liko katika kivuli, mpaka mwisho wa nyakati litakapodhihirishwa katika utimilifu wa mwanga wake. Rej. Lumen gentium 1- 14.

Utakatifu ni ukuu wa Kanisa ni Kristo: Bwana, Kuhani, Sadaka na Hekalu
Utakatifu ni ukuu wa Kanisa ni Kristo: Bwana, Kuhani, Sadaka na Hekalu

Waamini watambue na kukumbuka kwamba, Kristo Yesu ndiye Jiwe kuu la pembeni na kila mwamini anapaswa kujengeka na kuwa ni jiwe hai, ili waamini wote waweze kutembea kwa pamoja katika umoja, ushirika na utume, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Bila uwepo wa Kristo Yesu kati yao, Kanisa kama Jengo litageuka na kuwa ni uwanja wa fujo, “patashika nguo kuchanika.” Waamini wajitahidi kuwa mawe hai katika Kanisa kwa kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha, kwa kumsikiliza Mwenyezi Mungu anayezungumza pamoja nao kutoka katika undani wa nyoyo zao, yaani dhamiri nyofu. Waamini wamwachie nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza katika kufikiri na kutenda! Waamini wenyewe wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakizwa kwa ajili ya Mungu na jirani zao, kwa kuwa ni sadaka safi inayompendeza Mungu pamoja na jirani zao. Kanisa, Nyumba ya Mungu na Hekalu la Roho Mtakatifu ni mahali ambapo Kristo Yesu anaendelea kujitoa sadaka katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Na waamini wanaompokea Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai wanapaswa na wao kugeuka na kuwa ni “Ekaristi” Mkate uliomegwa na kutolewa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini wajenge utamaduni wa kusali na kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Sakramenti za Kanisa na hasa zaidi Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upanisho kwani hizi ni Sakramenti Pacha.

Kanisa ni Sakramenti ya umoja na wokovu wa watu wote.
Kanisa ni Sakramenti ya umoja na wokovu wa watu wote.

Waamini waache ubinafsi na tabia ya kujitafuta wenyewe na badala yake, Kristo Yesu apewe kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa. Wajitahidi kuufia ubinafsi wao! Waamini wahakikishe kwamba, wanakuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huduma na upendo; kwa kujitahidi kumwilisha Neno la Mungu na neema ya Sakramenti za Kanisa katika matendo, kielelezo makini cha imani tendaji. Waamini katika ujenzi wa Jumuiya kama Kanisa, wajitahidi kushirikisha karama na mapaji yao waliokirimiwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini wawe ni vyombo vya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kujenga na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika sheria ya upendo kwa Mungu na jirani. Waamini waendelee kujifunza kutoka katika shuke ya Bikira Maria, Mwanafunzi wa kwanza wa Kristo Yesu. Kufuru kubwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na unajisi wa utakatifu wa Kanisa na vifaa mbalimbali vya Ibada iwe ni fursa ya kuendeleza moyo wa toba, wongofu wa ndani na malipizi ya dhambi, tayari kuambata na kukumbatia utakatifu wa maisha, kielelezo cha imani tendaji. Kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Jimbo la Geita na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam ni baada ya kukamilika kwa ukarabati wa: Altare, kwa kununua tena Tabernakulo mpya pamoja na vifaa vya Ibada na Visakramenti.

Kardinali Pengo na baadhi ya Maaskofu wakisali mbele ya kaburi la Rais Magufuli
Kardinali Pengo na baadhi ya Maaskofu wakisali mbele ya kaburi la Rais Magufuli

Lengo ni kurejesha tena utakatifu wa Kanisa hili, tukio ambalo pia linaonesha urika wa Maaskofu Katoliki Tanzania kwa kuhudhuria kwa wingi. Watu wachache ndani ya jamii, wasiruhusiwe kuchezea uhuru wa kuabudu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitangaza “declarat” kwamba binadamu anayo haki ya uhuru wa dini. Uhuru huo ndio huu, kwamba, kila binadamu lazima akingiwe na shurutisho la mtu mmoja mmoja, la makundi ya kijamii, au la mamlaka yoyote ya kibinadamu. Hivyo kwamba, katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubalika kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine. Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili. Haki hii ya binadamu ya uhuru wa dini yatakiwa kuzingatiwa katika sheria za jamii ili iwe haki ya raia. Rej. DH 2. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulizingatia hasa: mema ya kiroho kwa kila mtu; ukweli na haki; Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa. Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya wokovu wa mwanadamu. Kanisa linawajibu wa kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, linahimiza umuhimu wa kulinda dhamiri nyofu pamoja na wajibu wa kimaadili. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipania pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba: wanaendeleza Mafundisho ya Kanisa kuhusu haki msingi za binadamu zisizoondosheka na katika sheria za muundo wa jamii. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kufunda dhamiri za watu, ili kutambua utu, heshima na haki msingi za binadamu. Rej. DH.1. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la uvunjwaji wa haki ya uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; hali inayojikita katika: vita, chuki na uhasama; misimamo mikali ya kidini na kiimani; pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyotishia misingi ya haki, amani, umoja na mafungamano ya kijamii.

Jimbo Katoliki Geita

 

 

17 March 2023, 17:13