Sinodi ya bara la Afrika huko Addis Ababa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Addis Ababa.
Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu: Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume. Jumatano, Mosi Machi 2023, Kamati Kuu ya SECAM imefanya kikao chake cha kwanza Addis Ababa nchini Ethiopia, chini ya Kardinali Fridolin Ambongo, Askofu Mkuu wa Kinshasa (DRC). Kikao hiki kilitanguliwa na Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Makamu wa Rais wa SECAM kutoka Msumbiji, Askofu Lucio Andrice Muandula wa Jimbo Katoliki la Xai Xai.
Nia ilikuwa ni kuombea ufanisi wa maadhimisho hayo ya Sinodi Barani Afrika. Pili kuombea amani, utulivu na maridhiano nchini Nigeria wakati huu wa uchaguzi mkuu ingawa Tume ya Uchaguzi Nigeria imetangaza mteule Bola Ahmed Tinubu kuwa mshindi kwa kupata kura milioni 8. 79 kati ya kura milioni 93.5 za wapiga kura wote waliojiandikisha.
Zaidi ya wajumbe 200 kwa hiyo wanashiriski na wengi wao ni waamini walei. Wanaume na wanawake pamoja na vijana ambao mara nyingi wamesahauliwa katika vikao vya Kanisa. Kimsingi, hawa ni baadhi ya mapadre, masista, vijana, baadhi ya waseminari na wanovisi, pamoja na maaskofu 15 na makadinali 7. Na ufunguzi rasmi wa awamu ya bara la Sinodi ya Afrika utakuwa Alhamisi tarehe 2 na hitimisho lake ni tarehe 6 Machi 2023.