Tafakari Dominika IV ya Kwaresima Mwaka A wa Kanisa: Yesu Ni Mwanga Unaofukuza Giza la Dhambi na Mauti
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya nne ya Kipindi cha Kwaresima mwaka A wa Kanisa. Dominika hii inajulikana kama dominika ya furaha kama maneno ya wimbo wa mwanzo yanavyosema; “Furahi Yerusalemu, shangilieni ninyi nyote mpendao. Furahini, ninyi nyote mliao kwa ajili yake, mpate kunyonya na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake (Isa. 66:10-11). Tunaalikwa kufurahi kwa kuwa tumekaribia kuadhimisha siku ya wokovu wetu – mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo – Pasaka. Katika domenika hii linafanyika takaso la pili la wakatekumeni watakao batizwa usiku wa Pasaka. Ujumbe wa masomo ya Dominika hii umejikita katika kweli hii: Yesu ni mwanga unaofukuza giza la dhambi na kifo. Somo la kwanza ni la Kitabu cha kwanza cha Samweli (1Sam. 16:1b, 6-7, 10-13a). Somo hili linaeleza kuwa licha ya Daudi kuwa mdogo kati ya watoto wa Yese, Mungu alimchagua na kumpaka mafuta kupitia mikono ya Samweli ili awe mfalme, aanzishe kipindi kipya katika historia ya wokovu. Samweli alipotumwa na Mungu kwenda kumpaka Daudi mafuta awe mfalme wa Israeli alishangaa kwa nini Mungu amemchagua Daudi kuwa mfalme. Yeye alifikiri kuwa Eliabu angefaa kuwa mfalme kwasababu alikuwa ni mtoto wa kwanza na zaidi sana alikuwa na sura nzuri na kimo kirefu. Katika jamii ya Waisraeli hata katika jamii zetu mtoto wa kwanza anapewa upendeleo wa pekee katika mambo mengi kama urithi na baraka ya wazee. Samweli alikuwa na mtazamo huo. Lakini Mungu alimwambia; “Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo”. Mungu alimchangua Daudi mchunga kondoo kuwa mfalme sababu moyo wake ulikuwa na hofu ya Mungu. Huyu ndiye Bwana aliyemteua na kumtia mafuta kwa kuwa alimtegemea Mungu kama kiitikio cha wimbo wa katikati kinavyosema; “Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu” (Zaburi 23:1).
Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (Efe. 5:8-14). Katika somo hili Mtume Paulo anatukumbusha na kutufahamisha kuwa mkristo ameingia katika mwanga wa Kristo kwa njia ya ubatizo hivyo hatupaswi kuchanganya mienendo yetu ya kikristo na matendo ya giza bali tuyakemee kwani ni ya aibu. Mtume Paulo anawaambia wakristo wa Efeso kuwa “wakati fulani mlikuwa gizani lakini sasa ninyi ni mwanga katika Kristo, kuweni kama watoto wa mwanga katika wema na katika kuishi vema katika kweli” (Efe. 5:9). Itakumbukwa kuwa Mtume Paulo aliandika barua hii kwa wakristo wa Efeso, wakati akiwa gerezani Roma. Mtume Paulo anapoongelea kuhusu mwanga na giza ni kutaka kuwaonesha Waefeso tofauti iliyopo kati ya maisha ya kipagani na maisha ya kikristo na ibada ya kikristo na ibada ya kipagani. Masimuliza na makala ya kihistoria yanashuhudia kuwa ibada ya kuabudu katika mahekalu ya kipagani ya wakati ule ilikamilishwa kwa vitendo vya zinaa vilivyofanyika hekaluni na vitendo hivi vilikuwa sehemu ya ibada. Katika mji wa Efeso kulikuwa na hekalu la mungu wa kike Diana, (Mdo 19:23-41). Baadhi ya wakristo kabla ya kuongokea Ukristo, wakiwa wapagani walishiriki ibada hizo. Hivyo Paulo anawakumbusha jinsi maisha yao na ibada yao ilivyokuwa zamani kabla ya kuongokea ukristo akisema; mlikuwa bado gizani (Ef 5:9). Ibada yetu ya Kikristo ni tofauti kabisa na ibada ya kipagani. Jumuiya ya kikristo inakusanyika kwa ibada ili kuangaziwa na Kristo. Mtume Paulo anatuambia ibada ya jumapili ni wakati tunaopaswa kutambua kile Bwana anachotaka kutoka kwetu (Ef 5:10). Kristo anatuangazia mwanga wake tunaposali, tunaposikiliza neno la Mungu na tunapoadhimisha Ekaristi Takatifu. Lakini ili ibada yetu iwe ya kweli, haipaswi kuishia kanisani, inapaswa iendelee kwa juma zima. Ni maisha yetu ya kikristo kwa wiki nzima ndiyo yanayofanya ibada ya jumapili iwe ya maana. Tunapozidi kukaribia sikukuu ya pasaka Kanisa linatualika kutambua umaana wa ubatizo wetu kwa kuchunguza dhamiri zetu na maadhimisho ya ibada za sakramenti hasa upatanisho ili tusijebaki katika giza wakati Yesu akiujaza ulimwengu mzima kwa mwanga wa Pasaka.
Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 9:1-41). Sehemu hii ya Injili inahusu simulizi la kuponywa kwa kijana aliyezaliwa kipofu. Mwinjili Yohane anatumia ishara ya mwanga na giza mara kwa mara kufafanua maandiko matakatifu. Mwanga ni ishara ya uzuri, furaha, utakatifu na uzima. Na giza ni ishara ya ubaya, masikitiko, dhambi na kifo. Mwanga na giza haviwezi kukaa mahali pamoja kwa wakati mmoja. Uwepo wa kimoja huondoa kingine. Kuchagua mwanga ni kuchagua maisha maana unakuwa upande wa Mungu na kuchagua giza ni kuchagua kifo maana unakuwa upande wa shetani (Yn. 8:44). Kuwa upande wa Mungu ni kumsikiliza na kumfuata Yesu Kristo Nuru na mwanga wa kweli. “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu; yeye anifuataye hataenda gizani kamwe bali atakuwa na nuru ya uzima wa milele” (Yn. 8:12). Yesu katika kumponya kijana aliyezaliwa kipofu amefanya tendo hilo hatua kwa hatua kama ilivyokuwa kwa mwanamke msamaria. Kwanza anamuonea huruma na kumwendea, kisha akatema mate akatengeneza tope, akampaka machoni kwa hiyo tope, akamwambia aende kunawa katika Birika-Kisima cha Siloamu. Naye akaenda, akanawa, akarudi anaona. Maana ya Sioamu ni aliyetumwa. Yesu ndiye kisima chetu, yeye ndiye aliyetumwa na Mungu. “Basi kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu”, ndiye Kristo. Kijana kipofu anapoulizwa alivyopona, anaeleza kwa ufasaha na usahihi hatua hizi alizofanya Yesu. Anashuhudia kuwa ni yeye aliyezaliwa kipofu, na anakiri kwa ushujaa na ujasiri kuwa Yesu ndiye aliyemponya naye ni Nabii, hana dhambi. “Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na kuyafanya mapenzi yake; humsikia huyo. Hajawahi sikika mtu yeyote ameyafumbua macho ya kipofu, ambaye alizaliwa hali hiyo. Kama huyo asingalitoka kwa Mungu, asingeweza kutenda neno lo lote.”
Kipofu aliyeponywa alipoulizwa Yesu ni nani, alijibu ni Nabii. Lakini Mafarisayo walimwambia, wewe umezaliwa katika dhambi tupu nawe unatufundisha sisi? Hata sisi tunaweza kufanana na mafarisayo tunawapomdharau wanaotuonya na kutushauri katika jambo linalogusa tabia na matendo yetu. Tunawadharau wale wanaotushauri kwa vile ni wadogo, maskini, walemavu au wanyonge. Kwa sababu ya kiburi na majivuno hatuwasikilizi kwa sababu kama tungewasikiliza ingetubidi kubadilisha namna yetu ya maisha. Katika kipindi hiki cha kwaresma tujishushe na kuwasikiliza wale wanaotuonya au kutushauri juu ya tabia au mienendo yetu ili tuweze kuponywa na madhaifu yetu. Tunapozidi kukaribia sikukuu ya Pasaka Kanisa linatualika kutambua umaana wa ubatizo wetu ambao Kristo alikuwa mwanga wa maisha yetu. Kanisa linatualika kuchunguza dhamiri zetu ili maneno ya mtume Paulo yasiwe; mlikuwa katika mwanga wa Kristo lakini sasa mpo gizani kwa dhambi. Kristo yupo tayari kutuwezesha tuweze kuona tena, kwa upande wetu tunapaswa tu kwenda kunawa katika bwawa la sakramenti ya upatanisho baada ya kutambua madhaifu yetu na kuyatubu ili tusijebaki katika giza wakati Yesu akiujaza ulimwengu mzima mwanga wa Pasaka. Kristo ni nuru ya ulimwengu, amekuja kutuangazia ili tuweze kuwa na mtazamo sahihi juu ya maisha yetu, mtazamo ambao utatuwezesha kuiona njia inayokwenda kwa Mungu na kutambua mapenzi yake. Kama Yesu alivyomponya kipofu akaweza kuona tena nasi katika kipindi hiki cha kwaresma tukiri upofu wetu mbele yake ili macho ya mioyo yetu yafunguke nasi tupate kuona.
Sala yetu daima iwe Bwana nipate kuona. Kama mpango wa kando/mchepuko umekufanya kipofu hata humwoni mwenzako wa ndoa, sali na kuomba; “Bwana nipate kuona”. Ubinafsi umekufanya kipofu hata huoni matatizo ya wengine, sali na kuomba, “Bwana nipate kuona”. Pombe imekufanya kipofu hata huoni mahitaji ya familia yako, sali na kuomba, “Bwana nipate kuona”. Tamaa za ujana zimekufanya kipofu hata huoni mwelekeo wa maisha yako, sali na kuomba, “Bwana nipate kuona”. Tumwombe Kristo atusaidie tujikubali tunapokosea na tukiendee kitubio ili atusamehe na kuturudishia neema zake zitakazotusaidia kuona njia ya uzima wa milele. Basi tumwombe Mungu atusaidie kuamka usingizini. Tutumie vizuri siku hizi zilizobaki katika kipindi hiki cha kwaresima tutoke katika giza na upofu wa dhambi na kuingia katika mwanga wa Kristo kwa kunawa katika kisima cha Siloamu ya Kristo na turudi tunaoona siku ya Pasaka. Tumsifu Yesu Kristo.