Tunaadhimisha tukio la Yesu kuingia Yerusalemu ili kuyakabili mateso yake, mateso ambayo yameuletea ulimwengu ukombozi kwa kifo na ufufuko wake. Tunaadhimisha tukio la Yesu kuingia Yerusalemu ili kuyakabili mateso yake, mateso ambayo yameuletea ulimwengu ukombozi kwa kifo na ufufuko wake.  (Vatican Media )

Tafakari Dominika ya Matawi: Mwanzo wa Juma Kuu: Mafumbo Makuu ya Wokovu: Pasaka!

Tunaadhimisha dominika ya Matawi. Tunaadhimisha tukio la Yesu kuingia Yerusalemu ili kuyakabili mateso ambayo yameuletea ulimwengu ukombozi kwa kifo na ufufuko wake. Kwa dominika hii Kanisa linaingia katika Juma Kuu. Linaitwa Juma Kuu kwa sababu ndani yake yanatendeka mafumbo ya wokovu wetu ambayo ni makubwa kuliko mafumbo mengine yoyote tunayoadhimisha kwa mwaka mzima wa Kiliturujia, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko uletao uzima wa milele.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, dominika hii tunaadhimisha dominika ya Matawi. Tunaadhimisha tukio la Yesu kuingia Yerusalemu ili kuyakabili mateso yake, mateso ambayo yameuletea ulimwengu ukombozi kwa kifo na ufufuko wake. Kwa dominika hii Kanisa linaingia katika Juma Kuu. Linaitwa Juma Kuu kwa sababu ndani yake yanatendeka mafumbo ya wokovu wetu ambayo ni makubwa kuliko mafumbo mengine yoyote tunayoadhimisha kwa mwaka mzima wa Kiliturujia, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko uletao uzima wa milele. UFAFANUZI WA MASOMO: Kabla hatujaanza kuyafafanua masomo ya Misa ya dominika hii, ni muhimu tukazielewa sura zake mbili, yaani maeneo mawili makubwa ambayo masomo haya yamejikita. Eneo la kwanza ni lile la utimilifu wa unabii, kwamba Yesu anaingia Yerusalemu kutimiza kile kilichokuwa kimetabiriwa. Na eneo la pili ni kudhihirisha alama za ukombozi, yaani yale anayokwenda kuyakabili Yerusalemu yanabeba alama za ukombozi aliokuja kuuleta kwa mwanadamu na kwa ulimwengu mzima.

Matawi ni ishara ya ushindi wa Kristo, Mfalme na Masiha
Matawi ni ishara ya ushindi wa Kristo, Mfalme na Masiha

Katika Agano la Kale, Mungu amezungumza mara nyingi na taifa lake na kuwafunulia kwa njia ya manabii matumaini ya ukombozi. Ni hapa ndipo tunapata unabii kuwa angekuja masiya na ni huyo ambaye angewakomboa watu wa Mungu kutoka katika utumwa waliokuwa nao. Watu wa Mungu waliupokea unabii huu na walisubiri kwa hamu ujio wa Masiya hayo aliyetabiriwa. Tatizo lilikuwa ni kwamba hawakujua huyo atakuwa ni masiya wa namna gani. Baadhi walitumaini masiya angekuwa mfalme, baadhi walitumaini angekuwa nabii kama Musa, wengine angekuwa kuhani na wapo waliotumaini kuwa angekuwa kiongozi wa kisiasa ambaye angewatoa katika ukoloni. Injili tunayoisoma kabla ya maandamano ya matawi, Injili ya Mathayo 21:1-11 inaonesha baadhi ya matumaini haya ambayo watu walikuwa nayo. Yesu anapoletewa punda na mwanapunda, mwinjili Mathayo anaongeza kusema kuwa kitendo hicho cha Yesu kupanda punda kinatokea ili kutimiza unabii unaosema “tazama mfalme wako anakuja kwako, mpole naye amepanda punda na mwanapunda, mtoto wa punda.” Ni matumaini ya Masiha aliye mfalme. Anapoingia Yerusalemu, watu wanampokea wakipaza sauti na kusema “Hosana, Mwana wa Daudi”. Hosana ni neno linalomaanisha “utuokoe”. Ni Yesu anayeambiwa utuokoe Mwana wa Daudi kwa maana ni yeye anayeonekana anakuja kutimiza unabii kuhusu ujio wa ukombozi.

Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu
Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu

Somo la kwanza tunalolisoma kutoka kitabu cha nabii Isaya (Isa 50:4-7) linatuonesha aina nyingine ya Masiha.  Somo hili halimtaji moja kwa moja masiya bali linaleta maneno au sala ya yule aliyefahamika kama mtumishi wa Bwana. Anachokizungumza mtumishi mwenyewe ni kuwa anaonesha utayari wake wa kuyakabili mateso bila kurudi nyuma. Anasema “sikuwa mkaidi wala sikurudi nyuma. Naliwatolewa wapigao mgongo wangu na wang’oao ndevu mashavu yangu, sikuficha uso wangu usipate fedheha.” Somo hili linatuonesha kuwa Yesu anapoingia Yerusalemu, pamoja na kupokelewa kama mfalme, Mwana wa Daudi anayekuja kuokoa, yeye anaingia kama yule mtumishi wa Bwana ambaye anakuja kuyakabili mateso. Yerusalemu ni mji uliosifika kwa kuwaua manabii. Sasa na yeye anaingia kama mtumishi anayejua kilicho mbele yake lakini harudi nyuma wala haogopi kwa sababu anatambua hayo ndiyo mapenzi ya Mungu. Somo la pili ambalo linatoka katika waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi (2:6-11) linakuja kuendeleza dhamira ya unabii wa Isaya. Ni somo ambalo ni kama vile linakuja kujibu swali. Kwa nini Yesu aliamua kuchagua njia ya mateso ili kuukomboa ulimwengu? Hakukuwa na njia nyingine? Jibu linalotoa somo hili ni kuwa Kristo amefanya hivyo kwa sababu ya unyenyekevu na utii wake kwa Baba. Yeye ambaye ni Mungu sawa na Baba aliamua kujishusha, akanyenyekea. Na aliponyenyekea akawa mtii hadi kupokea mateso na kufa Msalabani.

Dominika ya Matawi Mwanzo wa Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa
Dominika ya Matawi Mwanzo wa Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa

Mtume Paulo hakomei hapo tu kuonesha kuwa unyenyekevu na utii mwisho wake ni kifo. Anaendelea kuonesha kile kilichotokea baada ya kunyenyekea, baada ya kutii na baada ya kufa: Mungu alimwadhimisha mno, yaani alimwinua juu sana, akampa jina lipitalo kila jina, ili kwa jina lake kila goti lipigwe na kila ulimi ukiri kuwa Yesu Kristo ni Bwana na ana utukufu sawa na Mungu Baba. Njia ya unyenyekevu na ya utii sio njia inayoangamiza au njia inayompoteza mtu kwenye ramani. Ni njia inayomfikisha mtu kwenye utukufu kwa kuwa ndio njia inayoficha ndani yake mapenzi ya Mungu. Katika maeneo mawili yanayotusaidia kuyaelewa masomo ya dominika ya leo, eneo la utimilifu wa unabii na eneo la alama za ukombozi, ninawaalika sasa tugeukie eneo lile la pili. Tendo kubwa la ukombozi ulioletwa na Kristo ni Mateso, Kifo na Ufufuko wake. Kimsingi hayo ni matendo lakini yote kwa pamoja yanaitwa tendo kwa sababu yameungana na tena mwelekeo wake ni mmoja. Na hili ndilo fumbo la Pasaka. Sehemu kubwa ya tendo hili tutalisikia katika historia ya Mateso inayosokwa katika dominika hii na kurudiwa katika ukamilifu wake siku ya Ijumaa Kuu. Tukirudi katika somo la Injili inayosomwa mwanzo wa maandamano, Yesu anawatuma wanafunzi wawili waende kuwafungua punda na mwanapunda wampelekee. Wakati injili nyingine zote tatu (Marko, Luka na Yohane) zinaelezea tukio hili, mnayama anayefunguliwa ni mmoja tu mwanapunda. Ni Mathayo pekee anayezungumzia wanyama wawili, punda na mwanapunda. Upekee huu wa simulizi la Mathayo umetafsiriwa na Mababa wa Kanisa kama mojawapo ya alama ya ukombozi. Yesu anapoingia Yerusalemu anakwenda kukamilisha kuwafungua wanyama hawa wawili wanaowakilisha makundi mawili ya watu wa Mungu, punda anayewakilisha wayahudi na sinagogi lao, na mwanapunda anayewakilisha watu wa mataifa. Wote kwa pamoja wanahitaji kufunguliwa na kufikishwa hadi katika mlima wa Yerusalemu, mlima wa ukombozi.

Dominika ya Matawi: Fumbo la Pasaka: Mateso, kifo na ufufuko.
Dominika ya Matawi: Fumbo la Pasaka: Mateso, kifo na ufufuko.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, dominika ya Matawi inayo historia yake na ukuu wake katika maisha ya imani yetu. Kihistoria, tangu karne ya 5, huko Israeli katika dominika hii wakristo walikusanyika  katika mlima wa Mizeituni na kufanya maandamano hadi Yerusalemu wakiwa na matawi ya mizeituni. Ibada hii ilisambaa hata nje ya Israeli na maandamano yakaanza kufanyika kukumbuka tukio hilo la Yesu kuingia Yerusalem. Utamaduni huu umeingia katika liturujia, na sasa sio tu tendo la kumbukumbu ya kihistoria bali ni tendo la kukiri hadharani imani na utayari wetu wa kumfuata Kristo ambaye kwa mateso yake sisi tumepona. Matawi yanayobarikiwa ni kisakramenti. Tangu mwanzo wakristo wamekuwa wakiyapeleka nyumbani na kuyatunza kwa uchaji kama alama ya kupokea baraka ya Mungu kwa wakati huu wa Pasaka. Ni baraka inayozikinga nyumba, mashamba na mifugo dhidi ya mashambulizi ya pepo wabaya. Wasafiri katika vyombo vya maji wamekuwa wanatunza pia matawi katika vyombo vyao wakiamini katika nguvu ya Mungu kuwakinga dhidi ya dhoruba na machafuko yanayoweza kuvizamisha vyombo na kuleta mauti. Mwaliko tunaoupokea tangu mwanzo wa dominika hii ya Matawi pamoja na Juma lote Kuu ni kuyashiriki kikamilifu maadhimisho yake ili kuipokea ndani yetu neema ya ukombozi. Tujitahidi kujiandaa kiroho hasa kwa kupokea Sakramenti ya Upatanisho, kuhudhuria na kushiriki kikamilifu Ibada ya Misa ya Alhamisi Kuu, adhimisho la Ijumaa Kuu na Pasaka kwa kuwa haya ndiyo maadhimisho ambayo ni kitovu cha maadhimisho ya mwaka mzima wa kiliturujia.

Liturujia Matawi
31 March 2023, 17:05