Tafakari Dominika ya Matawi: Mwanzo wa Maadhimisho ya Juma Kuu: Fumbo la Ukombozi
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Dominika ya Matawi, Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu, alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme na Masiha na kushangiliwa kama Mwana wa Daudi anayeleta wokovu, ndiye Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana. Hii ndiyo maana ya wimbo wa Hosana. Ni Mfalme wa utukufu anayeingia Yerusalemu akiwa amepanda Mwana punda na kushangiliwa na Watoto wa Wayahudi wakiwa wamebeba matawi ya mitende mikononi mwao kama kielelezo cha amani na unyenyekevu wake. Matawi yatakayobarikiwa yatatunzwa na waamini kama visakramenti majumbani mwao, kuwakumbusha ushindi wa Kristo Yesu wanaouadhimisha kwa kuandamana, huku wakiwa wamebeba matawi ya mitende mikononi mwao. “Hili litimie andiko; Maisha ya kila mwamini ni kutimiza mapenzi ya Mungu!” Wainjili wote wanatenga nafasi ya kutosha kutuelezea masimulizi juu ya mateso na kifo chake Bwana wetu Yesu Kristo. Kimsingi kweli za imani zinabaki kuwa ni zilezile ingawa zinawakilishwa kila mmoja kwa mtindo wake. Kila mwinjili kwa namna yake kwa kutegemea aina ya uandishi, lakini pia aina ya jumuiya aliyokuwa anaiandikia, na lengo au makusudi yake ya kufikisha katekesi kusudiwa. Mwaka huu, Mama Kanisa anatualika katika Dominika ya leo ya Matawi kutafakari sehemu ya Injili ya Mathayo: 26:14-27:66. Dominika ya matawi inatuingiza katika Juma Kuu, Juma Takatifu, Juma la Wokovu wetu, ndilo Juma la kutafakari Wokovu wetu yaani mateso, kifo na ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo.
Mwinjili Mathayo, katika masimulizi yake anatumia maneno “…Ili litimie andiko”. (Mathayo 25:24) “Naam, Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yasemavyo”. (Mathayo 26:56) “Lakini haya yote yametendeka ili maandiko na manabii yatimie…”. Ndio kusema tunaposoma sehemu kubwa ya Injili ya Matayo hatuna budi kukumbuka kuwa alikuwa anawaandikia Jumuiya ya Wakristo wenye asili ya Kiyahudi, hivyo daima kwa kuwaonesha na kuwakumbusha kuwa Yesu ndiye Kristo, ndiye Masiya aliyetabiriwa na Manabii wa Agano la Kale. Hadhira yake ilielewa mara moja na kupata ujumbe kwani walikuwa tayari wanajua Maandiko Matakatifu hasa Agano la Kale. Yesu Kristo ndio ukamilifu wa Maandiko Matakatifu, unabii wote unakamilika na kutimia katika nafsi ya Yesu Kristo. Mwinjili Mathayo pia anatupa hata kiasi gani cha pesa alichopewa Yuda Iskariote ili amsaliti Yesu, na pia anatuonesha jinsi hatima na mwisho wake ulivyokuwa wa kusikitisha na kuhuzunisha. (Mathayo 27:9-10) Si kwa ajali anatupa kila taarifu kumhusu ili kila mmoja wetu kama mfuasi wa Yesu ajichunguze na kuangalia maisha yake na hasa mahusiano yetu na Yesu Kristo. Katika kutualika kumwona Yesu, tayari akiwa anazungumziwa katika Agano la Kale, tunaona jinsi simulizi lake linavyoendana na Zaburi ile ya 22 juu ya mateso ya mtu mwenye haki. Yesu ni ukamilifu wa ufunuo wote, ndio ukamilifu wa kile kilichonenwa na kutabiriwa katika Agano la Kale. Hapa chini nitajaribu kuonesha mfanano wa karibu kabisa wa Zaburi ile ya 22 na Yesu Kristo katika masimulizi ya Mateso na Kifo chake kadiri ya Mwinjili Mathayo.
Kadiri ya Mwinjili Mathayo, mtu huyu mwenye haki anayezungumziwa katika Zaburi ni Yesu Kristo. Kama Yesu alipokuwa pale juu msalabani alivyolia, (Mathayo 27:46) ndivyo pia anavyoanza mtu mwenye haki. “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Mtu mwenye haki katika Zaburi tunasoma; “Husema: Alimtegemea Mwenyezi-Mungu, basi, Mungu na amkomboe! Lakini ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu…” (Zaburi 22:8-9) Ndio maneno na kashfa alizozipata Yesu kwa wale waliomwona akiwa pale juu msalabani. (Matayo 27:39,41-43). “Koo langu limekauka kama kigae…” Ndivyo na Yesu anaona kiu akiwa pale juu msalabani. (Zaburi 22:16). Mtu wa haki akiwa amezungukwa na watesi wake; “Nimebaki mifupa mitupu; adui zangu waniangalia na kunisimanga. Wanagawana nguo zangu, na kulipigia kura vazi langu.” (Zaburi 22:17) Ndicho ambacho wanafanya pia wale maaskari wa kirumi waliomsulubisha Yesu wakiwa chini ya msalaba. (Mathayo 27:35). Kama Yesu alivyolia kwa sauti kubwa na kuisalimu roho yake (Mathayo 27:50) ndivyo pia Mtu wa haki afanyavyo. (Zaburi 22:25).
Mwinjili Mathayo anatumia Zaburi hiyo ya 22 ili kutuelezea masimulizi ya mateso yake Yesu Kristo, kuwa ndiye mtu wa haki, mtu wa Mungu aliyeteseka bila kuwa na kosa wala dhambi yeyote ile. Ni lengo lake kutualika nasi kutafakari kwa kina mateso na kifo chake Bwana wetu Yesu Kristo ili tusiishie tu kuona kama ni kweli ya kihistoria bali nyuma yake kuna ujumbe mkubwa na mzito wa Kitaalimungu. Ingawa hata Wainjili wengine nao wanafanya marejeo kwa Maandiko Matakatifu ila sio kwa kiasi kile anachofanya Mwinjili Mathayo. Na sababu kubwa kama nilivyosema hapo juu kuwa alikuwa anawaandikia jumuiya ya waamini wenye asili ya Kiyahudi, hivyo walikuwa ni watu waliokua na kulelewa wakisoma Maandiko Matakatifu. Wayahudi walikuwa daima wanamtarajia Masiha anayekuja kama mshindi, mtawala mwenye nguvu na mabavu. Ni katika hatima ya Yesu anaonekana kuwa dhaifu na mnyonge na aliyeshindwa, ni katika mazingira haya Wayahudi wanakwazika na kushindwa kumwona Yesu kama Masiha.
Ni pale chini Msalabani tunaona makuhani, waandishi na wazee wa Kiyahudi wakimrushia maneno ya kejeli Yesu msalubiwa: (Mathayo 27:40) “Wewe! Si ulijidai kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu? Sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi, shuka msalabani!” Huo ndio ulikuwa mtazamo wao wa Masiha anayeshinda na sio anayeshindwa na kuishia kufa kifo cha aibu pale Msalabani. Ni katika mazingira haya tunaona Mwinjili Matayo anamzungumzia Yesu kama Masiha yule anayezungumziwa kutoka Kitabu cha Zaburi sura ile ya 22, juu ya mtu wa haki anayeteseka na kutaabika bila hatia, anamfananisha huyu na Yesu. Mungu hakumuokoa Yesu kutoka pale juu msalabani kwani angeweza kufanya hilo kwa uwezo wake wa Kimungu. Mungu hakuzuia Mwana wake wa pekee asipitie hukumu ile na hata mateso yake bila kustahili. Mzaburi na pia Yesu anapokuwa pale msalabani anasali na kulia; “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha”, labda ndio kishawishi kikubwa na sala ya wengi wetu leo ulimwenguni kote. Ni haki kabisa kumlilia na kumuomba Mungu awe nasi daima kila nyakati katika maisha yetu. Kama vile Kristo anavyosali daima awe na Baba yake nasi tunaalikwa pia kutambua kuwa bila Mungu hatuwezi kumshinda yule muovu na hila zake.
Mungu alibadili kushindwa kwake na kuwa ushindi, kifo chake kuwa ni kuzaliwa katika maisha mapya, kaburi lake kuwa ni tumbo kutoka kwake sisi sote tumepata uzima wa milele. Ni mwaliko wangu leo kuwa na jicho jipya na hasa tukumbuke kuwa maisha ya duniani ni ya muda tu kwani sisi ni raia wa MAISHA YA UMILELE, MAISHA YASIO NA MWISHO, MAISHA PAMOJA NA MUNGU.Hivyo, kifo hakina neno au kauli ya mwisho, kwani kinabaki kuwa ni njia na lango la kuingia katika maisha ya umilele. Uzushi mkubwa katika nyakati zetu ndiyo ule wa “secularization”. nikiri kukosa neno la kufaa kwa Kiswahili lakini mzizi wa neno hilo ni “saeculum”, neno la Kilatini lenye kumaanisha, ya ulimwengu huu, ni kuishi kwa kuongozwa na kuona kila kitu kinaanza na kuishia hapa ulimwenguni, kuona sasa na kusahau kuwa kuna umilele. Sisi hata kama tunapitia nyakati ngumu kiasi gani hatuna budi kuongozwa na ukweli kuwa sisi ni wa milele, sisi maisha yetu hayaishi kwa kuwa tunakufa leo hata kwa wingi, kwa maradhi, ajali, njaa, kiu au kuuawa kama anavyouawa Yesu pale juu Msalabani.
Na uzushi huu ndio unaotufanya nasi kurudia kosa lilelile la Yuda Iskariote, badala ya kumgeukia na kumfuasa Kristo tunajikuta kugeukia viumbe, mara nyingi tunakuwa watumwa wa fedha, vitu na mali. Maisha yetu yanapokosa kuelekea umilele na kuona kana kwamba hapa duniani tunabaki milele. Yuda Iskariote ni mimi na wewe kila mara tunamfuasa Yesu Kristo huku tukisukumwa na tamaa zetu nyingine za kibinadamu. Yuda Iskariote anakosa kuona thamani kwa Yesu Kristo aliye Bwana na rafiki yake wa kweli na kugeukia vipande vile vya fedha, anaona thamani katika kubaki na kuongozwa na maisha ya kale, kadiri ya mafundisho ya makuu wa makuhani. Yuda Iskariote anapotambua kosa lake anakwenda kwa makuhani wakuu na huko kwa kweli anakosa huruma na msamaha ambao kwa hakika alipaswa kuupata kwa Bwana wake tu, Yesu Kristo. Yuda Iskariote anakosea njia, anakosa mwelekeo sahihi, kila mara hatuna budi kutambua kuwa ni kwa kumkimbilia Yesu tu pale msalabani hapo kwa hakika tunapokea huruma yake ya milele, huruma isiyo na mipaka. Yuda Iskariote alikosea njia pale mwanzoni na kujikuta anamsaliti Bwana na Mwalimu wake na hata baada ya kutambua kosa lake bado anakosea tena njia. Yuda Iskariote anabaki kutualika nasi kujitafakari maisha yetu iwe kabla ya kutenda makosa na baada ya kutenda, ni wapi nakimbilia mimi na weye?
Mwinjili Mathayo pia leo anatualika kuwa sisi wanafunzi wa Yesu hatunabudi kuepuka kila aina ya dhulma na utumiaji wa mabavu. Petro anaalikwa na Yesu kurudisha upanga wake alani, sisi Wakristo hatuna hata nafasi moja inayohalalisha kutumia upanga, bali daima sisi tunaalikwa kuwa wajumbe wa amani, iwe katika familia zetu, katika jamii zetu, katika nafasi zetu za kazi na popote pale. Leo Baba Mtakatifu Francisko anaualika ulimwengu mzima kujitafakari tena hasa nyakati hizi za leo, mataifa makubwa leo wanatumia sehemu kubwa ya bajeti zao kwa silaha za kivita za kila aina na za kisasa na za bei ghali, lakini hakuna uwekezaji mkubwa katika elimu, afya, na hata wengi wanakufa leo kwa kukosa chakula na maji safi na salama na makazi bora ya kuishi. Labda mimi na weye tunaweza kusema tupo mbali na mfano huo, itoshe tu kuona mara ngapi tumekuwa na mambo mengi hata tusiyoyahitaji na pembeni yangu kuna mtu anakosa chakula, dawa au hata elimu? Basi, ni mwaliko kwa kila mmoja wetu kuingia ndani mwake na kujitathmini mintarafu upendo wetu kwa Mungu na jirani. Nawatakia tafakari njema na Maadhimisho matakatifu ya Mateso, Kifo na Ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Juma Kuu lirejeshe tena: Imani, matumaini na amani ulimwenguni kote. Kristo ameshinda mateso na kifo kwa ufufuko wake nasi tu watu wa ufufuko, daima tumkimbilie Yesu Kristo aliye Bwana na Mwokozi wetu.