Tafuta

Utukufu wa Kristo Yesu umetundikwa juu ya Msalaba, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu. Utukufu wa Kristo Yesu umetundikwa juu ya Msalaba, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu. 

Tafakari Dominika ya Pili Kipindi cha Kwaresima: Imani, Upendo na Ushuhuda

Kuishi na kuutazama daima utukufu wa Kristo ndiyo shauku ya kila mkristo! Hata hivyo, kushiriki katika utukufu wa Kristo kunatudai: imani thabiti katika majaribu, mateso pamoja na kusikiliza sauti ya Kristo katika maisha yetu ya kila siku. Abramu, Petro, Yohane na Yakobo wawe mifano kwetu ya: imani thabiti na upendo zaidi kwa Kristo, upendo ambao unafumbatwa katika kujikatalia na kujisadaka wenyewe kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.: Imani, upendo na ushuhuda!

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli (Napoli), Italia.

Kuishi na Kristo na kuutazama daima utukufu wake wa kimungu ndiyo hamu na shauku ya kila mmoja wetu aliyeikumbatia imani ya kikristo. Hata hivyo, kushiriki katika utukufu wa Kristo kunatudai: imani thabiti katika majaribu, mateso pamoja na kusikiliza sauti ya Kristo katika maisha yetu ya kila siku. Abramu, Petro, Yohane na Yakobo wawe mifano kwetu ya: imani thabiti na upendo zaidi kwa Kristo, upendo ambao unafumbatwa katika kujikatalia na kujisadaka wenyewe kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. SOMO LA KWANZA: Mwa. 12:1-4°: Katika somo letu la kwanza tunasikia juu ya “mwito wa Abramu- mwito ambao unamfanya Abramu/Ibrahimu atambulikane kama baba wa imani.” Mungu anamwamuru Abramu aondoke katika nchi yake anayoishi, aache na jamaa zake na familia nzima ya baba yake na kisha kwenda katika nchi asiyoijua (ambayo Mungu atamuonesha). Ibrahimu anatii agizo la Mungu bila kusita wala bila kuuliza maswali. Tusifikiri kana kwamba kutii jambo hili ilikuwa suala jepesi: Abramu ameishi katika nchi yake ya Harani kwa muda mrefu, ameishi na ndugu na jamaa zake kwa miaka 75, sasa leo anaambiwa (tena na asiyemwona/asiyemjua) aondoke na kwenda kwingine kusikojulikana na aache ndugu na jamaa zake ambao ameishi nao kwa miaka mingi. Je, unafikiri jambo hili lilikuwa jepesi? La hasha! Jambo hili halikuwa jepesi hata kidogo. Ni imani tu inayomfanya Abramu atii agizo hili la Mungu licha ya ugumu uliokuwemo: Abramu hajui aendako, Abramu anaacha ndugu zake na kwenda mahali ambapo hana hata ndugu. Tena Abramu haulizi “Nakwenda wapi? Kuna nini huko? Nitafaidika nini? Nitafanya nini huko? Nitaishi vipi huko na uzee wangu huu?” Kutii agizo la Mungu bila kuuliza maswali haya yote ni miongoni mwa mambo yanayomfanya Abramu aitwe “baba wa imani” kwani “imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (Ebr. 11:1): hajawahi kuiona hiyo nchi anayokwenda, lakini anakwenda; anaamini ahadi ya Mungu kuwa atafanywa taifa kubwa licha ya kwamba mke wake ni tasa (rejea Mwa. 11:30); hajawahi kumuona Mungu lakini anamwamini na kumtii; Abramu mpaka dakika hii hajaona muujiza wowote wa Mungu lakini anamwamini (imani ya kweli haihitaji miujiza ili mtu aamini); Abramu anatii maagizo/amri ya Mungu bila kuuliza maswali. Hii ndiyo imani ya kweli. Imani hii ya Abramu inasifiwa pia na mwandishi wa Waraka kwa Waebrania (rejea Ebr. 11:8).

Kung'ara kwa Kristo Yesu ni kielelezo cha utukufu na ukuu wake wa daima
Kung'ara kwa Kristo Yesu ni kielelezo cha utukufu na ukuu wake wa daima

Kutoka somo letu la kwanza tunajifunza mambo makubwa mawili: (1) Imani ya kweli inajidhihirisha katika kutii maagizo ya Mungu na kujiaminisha kwa Mungu pasipo kusita (total obedience and total surrender to God). Abramu anadhihirisha imani yake kwa Mungu katika hali ambayo wengi wetu tungeonesha mashaka mashaka na kujiulizauliza maswali mengi moyoni. Abramu hajaona muujiza wowote kutoka kwa Mungu ili kushawishika kutii agizo la Mungu. Abramu amemwamini Mungu na kujiaminisha kabisa kwake. Wengi wetu imani yetu ni imani ya juu juu tu, yenye mashaka mashaka na maswali mengi yasiyo na tija: tunamwamini Mungu mguu mmoja ndani, mwingine nje- hatujajiaminisha kwa Mungu mazima mazima. Ni kama tuna imani ya “kubeep” (kupiga na kukata). Ni wangapi tunatii maagizo ya Mungu, hasa amri zake? Ni wangapi tunajiaminisha mazima mazima kwa Mungu nyakati tunapokabiliwa na magumu ya maisha? Tuombe Mungu aimarishe imani yetu. (2) Tunapaswa kuacha “tunayoyapenda” ili kufika nchi ya ahadi [mbinguni]. Mungu anamwambia Abramu awaache “jamaa zake” na “nyumba ya baba yake” [yaani wote wa familia yake]. Jamaa na wanafamilia ni watu ambao tuna muungano nao wa damu au wa urafiki- ni watu ambao tuna mapenzi ya dhati kwao ya asili kabisa. Hao ndio Abramu anaambiwa awaache. Kwa maneno mengine Mungu anamtaka Abramu aachane na wapendwa wake. Hata sisi leo tunaalikwa “kuachana na yale tunayoyapenda” kwa ajili ya kutimiza mpango wa Mungu. Sisi tunapaswa kuachana na dhambi ambayo kwa asili tunaipenda sana na ambayo inajifanya kuwa ni jamaa/rafiki/ndugu yetu. Ni lazima kuacha dhambi ili kufika nchi ya ahadi ambayo tumeahidiwa na Mungu (yaani mbingu). (3) Baraka huambatana na watu wenye imani na wanaotii maagizo ya Mungu. Katika simulizi hili neno “baraka/bariki” limejitokeza mara 5. Hii ni kuonesha kuwa mtu mwenye imani na mtii kwa Mungu hupewa baraka kama tuzo. Baraka anazopewa mtu huyo, kwa maana ya kwanza, ni baraka za kiroho: kukua na kustawi kiroho akiwa na mahusiano mazuri na Mungu. Mtu mwenye imani na mtii kwa neno la Mungu huwa chanzo cha baraka kwa wengine. Kama Abramu anavyoahidiwa kuwa “baraka,” nasi pia tunapaswa kuwa “baraka” kwa wengine: tuwe chanzo cha amani, furaha, faraja na mafanikio kwa wengine.

Waamini wanapaswa kumsikiliza Kristo Yesu: Neno. Dhamiri, Sala na Tafakari
Waamini wanapaswa kumsikiliza Kristo Yesu: Neno. Dhamiri, Sala na Tafakari

SOMO LA PILI: 2 Tim. 1:8b-10: Timotheo alikuwa mshirika wa karibu wa Mtume Paulo katika utume wa kuhubiri Injili. Sasa Paulo anatambua kuwa karibu utume wake unafikia mwisho kwa kuwa yu karibu kuuawa kwa sababu ya kuhubiri Injili (na sasa yu kifungoni). Mtume Paulo, akifahamu fika kuwa ni lazima kazi ya kuhubiri Habari Njema isonge mbele hata baada ya yeye kuuawa, anamuandaa Timotheo kuendeleza kazi hiyo. Paulo anamuandaa Timotheo kisaikolojia ya kuwa katika kuhubiri kwake Injili atakutana na mabaya na hivyo hana budi kuyavumilia: “Uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili…” Mtume Paulo anapotumia neno “mabaya” anamaanisha mateso, dhuluma, magumu, taabu, shida na adha atakazozipata kama matokeo ya kuhubiri Injili. Kwa maneno mengine Paulo anamtahadharisha Timotheo kuwa hakuna ukristo rahisi- hakuna ukristo bila mateso, taabu, adha na mengineyo. Hivyo, ni lazima kuvumilia mateso kwa ajili ya Injili/Ukristo na wala siyo kukata tamaa na kuacha kuhubiri Habari Njema. Ushauri wa Paulo kwa Timotheo unatulenga pia sisi Wakristo wa nyakati hizi. Kumtangaza Kristo na kuishi ukristo wetu si jambo rahisi. Injili/Ukristo una madai na gharama zake- ukristo unaambatana na mateso/magumu. Mtakatifu Mama Teresa wa Kalkuta alitambua hili na ndiyo maana alisema, “Kama mtu anatafuta dini nzuri na ya starehe, basi asije kwenye ukristo.” Wapo watu wengi wanaoteseka kwa sababu ya imani na upendo wao kwa Kristo/Injili: Wakristo wengi wanatekwa na hata kuuawa kwa ajili ya imani maeneo mbalimbali, wapo Wakristo wengi wametengwa na ndugu zao kwa sababu wamechagua kuwa Wakristo ilihali ndugu zao wengine ni wa dini tofauti; wapo Wakristo wengi wanateseka kwa sababu wameamua kusimamia na kuishi mafundisho ya kanisa; wapo Wakristo wengi wanaoteseka kwa sababu tu wameamua kusema ukweli na kukemea maovu katika jamii, n.k. Mateso/magumu haya yasiwe chanzo cha sisi kulegea kiimani, kuiasi imani au kutafuta suluhisho la mkato. Tukivumilia mabaya/mateso haya na kuyapokea kwa jicho lamani tutapata tuzo: “Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka” (Mt. 24:13).  Fadhila hii ya uvumilivu nyakati za mateso tutaipata ikiwa tunategemea nguvu ya Mungu itokayo katika mazoezi ya kiroho: sala, kufunga, kutenda matendo mema, utii kwa mapenzi ya Mungu, unyenyekevu, kupokea Sakramenti, kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, kusoma vitabu vya maisha ya kiroho, na mengineyo.

Waamini wajenge utamaduni wa kusikiliza na kusali na Neno la Mungu.
Waamini wajenge utamaduni wa kusikiliza na kusali na Neno la Mungu.

SOMO LA INJILI: Mt. 17:1-9: Katika somo letu la Injili tunasikia simulizi la “Yesu kugeuka sura, tukio ambalo kwalo Yesu anafunua umungu wake ili kuimarisha imani ya wanafunzi wake watakapomwona akiteswa msalabani.” Tukio la Yesu kupanda mlimani na kugeuka sura linatokea wakati Yesu akiwa safarini kwenda Yerusalemu ambako atakamatwa, atateswa, atasulibishwa na kisha kuuawa kwa ajili ya wokovu wa wanadamu. Hivyo Yesu anapanda mlimani kuomba/kusali ili kuchota nguvu ya kukabiliana na mateso na kifo chake. Yesu anapanda mlimani na wanafunzi wake watatu: Petro, Yohane na Yakobo. Hawa ndiyo ambao Yesu alisema “hawataonja mauti kabisa, hata watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika ufalme wake” (rejea Mt. 16:28). Wanafunzi hawa watatu wamekuwa na nafasi ya pekee katika matukio fulani maalum yaliyofanywa na Yesu (rejea pia Mk. 14:33, 5:37, Lk. 8:51, 9:28). Swali la msingi ni hili: kwa nini Yesu anawachukua wafuasi hawa watatu tu? Kuna sababu kuu mbili: (i) mitume hawa watatu wana sifa za pekee kila mmoja na (ii) ushahidi wa tukio/jambo lolote ulipaswa kuthibitishwa na watu wawili au watatu ili ukubalike miongoni mwa Wayahudi. Ushahidi wa mtu mmoja kamwe ulikuwa haukubaliki (rejea Kumb. 19:15; 2 Kor. 13:1). Hivyo Yesu anawachukua mitume watatu ili baada ya ufufuko wake watoe ushahidi wa kuaminika wa tukio hili la Yeye kugeuka sura. Labda tuangalie sifa ya pekee aliyonayo kila mmoja wa wafuasi hawa watatu wanaopanda mlimani pamoja na Yesu: Petro ndiye mtume aliyempenda zaidi Yesu kuliko mitume wengine na hivyo anaandaliwa kuwa kiongozi wa Kanisa na kiongozi wa mitume wote (rejea Yn. 21:15-17); Yohane ni mwanafunzi aliyependwa zaidi na Yesu. Wataalam wa Maandiko Matakatifu wanasema sababu ya Yohane kupendwa zaidi na Yesu ni uamuzi wake wa kutokuoa (kuishi useja) ili aweze kumtumikia na kuambatana na Yesu kikamilifu (kwa kadiri ya mapokeo Yohane ndiye mtume pekee ambaye hakuoa). Kwa maneno mengine Yohane aliacha kuoa ili amtumikie Yesu bila kujibakiza; Yakobo wa Zebedayo anachukuliwa na Yesu kwenye matukio makubwa ili kuimarishwa zaidi kiimani kwani ndiye atakuwa mtume wa kwanza kuuawa (kumwaga damu yake) kwa ajili ya kumshuhudia Kristo (rejea Mdo. 12:2).

Waamini wawe ni mashuhuda wa Kristo katika kutangaza Injili ya huruma
Waamini wawe ni mashuhuda wa Kristo katika kutangaza Injili ya huruma

Tukio la Yesu kugeuka sura linatufunulia na kutufundisha mambo mengi: (1) Yesu Kristo ni Mungu kweli na ni Mwana wa Mungu. Mitume walizoea kumwona Yesu katika mwonekano wake wa kibinadamu na hivyo walizoea kumwona katika asili ya kibinadamu. Leo Yesu anageuka sura kuonesha upande wa pili wa asili yake- asili ya umungu. Lengo kubwa la kufunua umungu wake ni nini? Yesu alifunua umungu wake ili kuwafanya wanafunzi wake wasibaki kumtazama katika ubinadamu wake tu pindi atakapoteswa na kufa msalabani, bali wamwone pia katika umungu wake, yaani Yeye ni Mungu na hivyo atashinda dhambi na mauti na hivyo kudhihirisha utukufu wake wa kimungu. Kadhalika, katika tukio hili Mungu anadhihirisha kwa Yesu ni Mwanae: “Huyu ni Mwanangu.” (2) Yesu Kristo ni utimilifu wa Torati na Manabii. Yesu anapogeuka sura wanatokea Musa na Eliya na kuzungumza naye. Musa anawakilisha Torati/Sheria na Eliya anawakilisha mafundisho ya Manabii. Hivyo Yesu ni utimilifu wa kile kilichonenwa katika Torati na kile kilichofundishwa na manabii. Kwa maneno mengine, yote yaliyonenwa katika Torati na Manabii yanapata utimilifu wake katika Kristo. Yesu mwenyewe anasema “Msidhani kuwa nimekuja kutangua sheria na mafundisho ya manabii. Sikuja kutangua bali kukamilisha” (Mt. 5:17). Yote waliyofundishwa Wayahudi katika Torati na Manabii yanapata ukamilifu wake katika Kristo Yesu. (3) Mungu yu pamoja na wateule wake, hasa nyakati za mahangaiko, shida na mateso. Yesu anapanda mlimani kusali akijua wazi kuwa muda si mrefu atauawa. Yesu tayari ameishaanza kuteseka sana moyoni kwa kuwa anajua wazi aina ya kifo anachokwenda kuuawa. Hivyo, anapanda mlimani kwenda kukutana na Mungu ili amtie nguvu ya kukabiliana na mateso na kifo chake (Mlimani, kwa kadiri ya Wayahudi, ni mahali ambapo Mungu huwepo kuzungumza na watu). Mungu anashuka katika wingu (wingu ni ishara ya uwepo wa Mungu, rejea Kut. 13:21) na kuonesha kuwa yupo pamoja na Yesu katika safari yake ya mateso. Hata sisi tunapaswa kutambua kuwa Mungu hakai kimya katika mateso yetu wala hatuachi bali yupo pamoja nasi kututia nguvu. Wengi wetu huwa tuna desturi ya kukata tamaa nyakati za shida na kufikiri Mungu hayuko nasi na hivyo kuanza kukimbilia miungu mingine: waganga wa kupiga ramli, wahubiri wanaotenda miujiza, mizimu, n.k.

Imani, upendo na udugu nguzo ya ushuhuda wenye mvuto
Imani, upendo na udugu nguzo ya ushuhuda wenye mvuto

Hata hivyo, Mungu yupo pamoja na wote wanaosali wakati wa shida, mahangaiko na mateso. (4) Tupende kukaa katika utukufu wa Mungu kama Petro. Kukaa na Mungu na kuona/kuonja utukufu wake kunapaswa kuwa tamanio letu la kwanza. Petro, baada ya kuona utukufu wa ajabu wa Yesu, anashauri kujenga vibanda vitatu (cha Yesu, cha Musa na cha Eliya) ili azidi kuona utukufu wa Mungu. Je, mimi na wewe tunatamani kuona utukufu wa Mungu? Je, tunatamani kukaa na Mungu/Yesu? Ni watu wangapi tunatamani kukaa mbele ya Yesu wa Ekaristi na kuona/kuonja utukufu wake? Wengi wetu tunapenda kutumia muda mwingi kukaa na malimwengu badala ya kukaa mbele ya Mungu na kuonja utukufu wake katika maisha yetu.  (5) Tunapaswa kuwa watii kwa Kristo. Katika tukio la Yesu kugeuka sura tunasikia ya kuwa sauti ya Mungu Baba ilisikika ikisema, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye.” Huu ni mwaliko kwetu sisi sote kumsikiliza Kristo. Kristo anazungumza nasi katika mahubiri, anazungumza nasi kila tusomapo na kutafakari Neno la Mungu, anazungumza nasi katika sala, anazungumza nasi katika Sakramenti kama vile Kitubio, anazungumza nasi katika dhamiri zetu na anazungumza nasi katika matukio ya maisha (magonjwa, misiba, majanga ya asili, n.k). Je, tunamsikiliza? (6) Tunapaswa kuwa na sifa kama za akina Petro, Yohane na Yakobo ili tuweze kufunuliwa na kuona utukufu wa Mungu. Hatima ya maisha yetu ni siku moja tuweze kuona utukufu wa Mungu huko mbinguni. Ili tuweze kufikia hatima hiyo ni lazima kujitahidi kuwa na sifa kama za wanafunzi watatu ambao Yesu anapanda nao mlimani: kwanza, kumpenda sana Kristo kuliko vyote kama Petro alivyompenda sana Kristo; pili, kujitahidi kupendwa sana na Kristo kama Yohane alivyopendwa sana na Kristo, hasa kwa kumtumikia pasipo kujibakiza; tatu, kuwa tayari kufa kwa ajili ya Kristo kama Yakobo alivyokuwa wa kwanza kufa kwa ajili ya Kristo. Tukio zima la Yesu kugeuka sura lina maana sana katika maisha yetu ya kiroho hasa wakati huu wa Kwaresima. Tukio la Yesu kugeuka sura ni mwaliko kwetu kugeuza mwenendo wetu mbaya wa dhambi na kuanza kuishi mwenendo mzuri wa maisha. Wakati wa mabadiliko ni sasa.

 

12 March 2023, 15:00