Tafakari Dominika ya Pili Kipindi cha Kwaresima: Tafakari ya Kina!
Na Padre Gaston George Mkude, Roma.
Kipindi cha Kwaresima kinasimikwa katika nguzo kuu nne: yaani; Sala, Kufunga, Neno la Mungu na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Toba ya Kwaresima na Mchakato wa Sinodi.” Ni ujumbe unaochota amana na utajiri wake kutoka katika tukio la Kristo Yesu kugeuka sura mbele ya wanafunzi wake Petro, Yakobo na Yohane nduguye, baada ya kuwa ametangaza Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, jambo ambalo lilionekana kuwa ni kashfa kwa Mtume Petro, kiasi cha kuambiwa na Kristo Yesu, alikuwa ni Shetani, kikwazo kwake kwani alikuwa hawazi yaliyo ya Mungu bali ya wanadamu. Rej Mt 16:23. Kumbe, Kwaresima ni mwaliko wa kupanda mlimani pamoja na Yesu kama tukio la Kisinodi! Amani na Salama!Sehemu ya Injili ya Dominika ya leo tunasikia juu ya simulizi la Yesu kugeuka sura juu ya mlima mrefu akiwa pamoja na wanafunzi wake watatu nao ni Petro, Yakobo na Yohane. Yafaa tangu mwanzo kuwa makini tunapokutana na masimulizi yanayohitaji maelezo ya kina ili kuweza kupata ujumbe kusudiwa kwani kinyume chake tunaweza kuishia kudhani kuwa Mwinjili Mathayo anajaribu kutupa simulizi tu na jinsi lilivyojiri. Simulizi la kugeuka sura Yesu juu mlimani karibu linasimuliwa na wainjili wa Injili zote pacha karibu katika mtindo na namna inayofanana sana. Na ndio pia Baba Mtakatifu Francisko anatualika kutafakari tukio la Yesu kupanda mlimani na kugeuka sura akiwa na wanafunzi wale watatu kuwa wazo kuu kwa kipindi chote cha Kwaresima mwaka huu 2023.
Leo tunasikia kutoka Mwinjili Mathayo. Mwinjili anaanza kwa kutueleza “Baada ya siku sita”, na hapo tunakuwa na maswali ni siku sita baada ya nini? Kwa kweli hasemi waziwazi ila yawezekana kabisa ni siku sita baada ya tukio la Yesu kuwapa mtihani wanafunzi wake wakiwa katika mji wa Kaisaria Filipo juu ya utambulisho wake. Ni katika mji ule wa kipagani, Yesu anawauliza wanafunzi wake watu wanamsema Yeye kuwa ni nani na mwishoni anawageukia pia wanafunzi wake kutaka kusikia nao wanamtambua Yesu kama nani? (Mathayo 16:13-20) Lakini swali lingine kwa nini Yesu anaamua kwenda juu mlimani na wanafunzi wale watatu tu? Katika Injili ya Mathayo tunaona kila mara Yesu anapotaka kutenda au kufundisha jambo lenye umuhimu mkubwa tunaona anapanda juu mlimani. Katika jaribu la mwisho la Somo la Injili ya Dominika ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A tunaona Yesu anajaribiwa akiwa juu ya mlima mrefu. (Mathayo 4:8). Mafundisho ya Heri yanatolewa juu mlimani. (Mathayo 5:1). Muujiza wa kulisha watu mikate unafanyika pia mlimani. (Mathayo 15:29). Na mwisho wa Injili ya Matayo tunaona Yesu Mfufuka anakutana na wanafunzi wake na kuwatuma kwenda ulimwenguni kote wakiwa juu ya mlima ule walioagizwa. (Mathayo 27:16). Mlimani kadiri ya Agano la Kale daima ni sehemu inayoonesha ujumbe wa kiteolojia, kuwa ni mahali pakukutana na Mungu. Juu ya mlima Sinai, Musa anapokea maagizo au amri zile za Mungu na pia Elia juu ya mlima Horebu anakutana na Mungu. Hivyo, mlimani ni zaidi ya sehemu ya kijiografia kwani inaonesha tukio la kukutana na Mungu.
Lakini tukizidi kusoma Agano la Kale tunaona hata Musa ilikuwa ni baada ya siku sita alipanda mlimani (Kutoka 24:16), na hapandi peke yake bali pamoja naye ni Haruni, Nadabu na Abihu na wakafunikwa na wingu (Kutoka 24: 1,9). Na wakiwa juu mlimani uso wa Musa ukageuka na kung’aa. (Kutoka 34:30) “Haruni na watu Waisraeli wote walipomwona waliogopa kumkaribia, kwani uso wake ulikuwa unang’aa.” Natumaini sasa tumepata mwanga kuwa Mwinjili Matayo anamtambulisha Yesu kama Musa mpya anayekwenda mlimani ili kuwaletea watu wake sheria mpya akiwa na wanafunzi wake watatu kama alivyofanya Musa. “…Uso wake ukang’aa kama jua na mavazi yake yakawa meupe kama mwanga”. (Matayo 17:2) Hata ishara hizi pia tunakutana nazo katika Maandiko Matakatifu hasa Agano la Kale. (Zaburi 104:1-2) “Umsifu Mwenyezi Mungu ee nafsi yangu! Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, wewe ni mkuu mno! Umejivika utukufu wa fahari. Umejizungushia mwanga kama vazi…” Hivyo ni ishara zinazotumika kuonesha uwepo na hasa ukuu wa Mungu na ndio Mwinjili Matayo anazitumia pia kutuonesha kuwa ni katika Nafsi ya Yesu tunakutana na Mungu katika ukuu na utukufu wake. Wingu jeupe lililowafunika tunaweza kufanya rejea (Kutoka 13:21) ambapo Mungu aliwaongoza watu wake mchana na usiku katika ishara hiyo ya wingu. Musa akiwa mlimani tunaona pia mlima ulifunikwa na wingu, (Kutoka 24:15-16) na hata wakati anashuka kutoka mlimani sura ya Musa iling’aa (Kutoka 39:29-35). Hivyo ishara za wingu na kung’aa sura nazo ni ishara zenye kuonesha uwepo wa Mungu. Ndio kusema mitume wale watatu Petro, Yakobo na Yohane wanaambiwa juu ya utambulisho halisi wa Yesu “His true identity” lakini hasa lengo la ujio wake ulimwenguni.
Siyo Masiha kwa jinsi walivyokuwa wanafikiri wao, bali baaada ya kukataliwa na wakuu wa dini alipaswa kupitia mateso na kifo na mwisho kufufuka. Na hata wao kama wanafunzi wake hawana budi kupitia njia ile ile kama ya Bwana na Mwalimu wao. Sauti kutoka mbinguni (Mathayo 17:5), ilikuwa ni aina ya uandishi iliyotumiwa pia na Marabi katika kufanya hitimisho la kuonesha kuwa ni mawazo ya Mungu mwenyewe. Sura iliyotangulia ile ya 16 ilikuwa ni juu ya utambulisho wa Yesu. Yesu alianza kuwauliza wanafunzi wake watu wanamnena kuwa ni nani? Baada ya kusikia majibu au mitazamo ya watu wengine mwishoni anawauliza pia wanafunzi wake na Simoni Petro anajibu kuwa ni Masiha. Sauti kutoka mbinguni leo inamtambulisha Yesu kuwa; “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye, msikilizeni”. Ni Mwana mpendwa aliyependezwa na Baba kama tunavyoweza kusoma katika Kitabu cha Nabii (Isaya 42:1). Siku ile ya Ubatizo wa Yesu pale mtoni Yordani ilisikika pia sauti kuwa “Huyu ni Mwana wangu niliyependezwa naye”, (Mathayo 3:17), ila leo unaongezeka ujumbe zaidi wa “msikilizeni”, hata pale anapotualika kupitia njia ngumu na mateso na madhurumu bado mwaliko wa Mungu Baba kwetu ni kumsikiliza Yesu. Na ndio safari yetu ya Kwaresima kila mara ni kukaa karibu naye kwa sala na tafakari ili kila mmoja wetu aweze kutambua ni misheni gani ninayoitiwa na Bwana na Mwalimu wetu. Ni Neno wa Mungu, hivyo hatuna budi kumsikiliza. Nafasi ya Injili katika kipindi cha Kwaresima, si tu kuisoma bali tutenge muda wa kuwa rafiki daima wa Maandiko Matakatifu na tusikubali kuongozwa kwa akili zetu bali mang’amuzi tunayoyapata kutokana na sala na tafakari za kweli.
Katika Maandiko Matakatifu kitenzi kusikiliza hakimaanishi tu kusikia kwa masikio yetu bali zaidi sana kutii, kukubali kuenenda kadiri ya Neno la Mungu. (Kutoka 6:12 na Mathayo 18:15-16) Hivyo mwito wa Mungu kwa wanafunzi wale watatu ni mwito kwa kila mmoja wetu, kulisikiliza Neno na kulitii kwa maana ya kulishika, kuliweka katika maisha yangu ya kila siku. Musa na Eliya ni akina nani? Musa ndiye aliyepokea sheria na amri za Mungu kwa watu wake na Eliya alitambulika kama nabii wa kwanza, na hivyo watu hawa wawili kwa Wayahudi walitumika kama kuwakilisha Maandiko Matakatifu. Kama nilivyowaalika tangu awali kuwa ili kupata ujumbe kusudiwa hatuna budi kuelewa aina ya uandishi ya Mwinjili Matayo ambaye daima anatuonesha ili kumwelewa Yesu hatuna budi kusoma kwa kuhusianisha na Agano la Kale. Na hivyo hivyo hatuwezi kuelewa Agano la Kale kama hatutalisoma kwa kulihusianisha na Yesu. Bila Yesu, Agano la Kale linabaki bila kueleweka, na pia bila Agano la Kale, Yesu anabaki kuwa fumbo lisiloeleweka kwetu. Siku ile ya Pasaka, Kristo Mfufuka anapokutana na wafuasi wale wawili wa Emausi tunaona ili waweze kuelewe fumbo la mateso na kifo na ufufuko wake anaanza kuwaeleza Maandiko yote kuanzia Agano la Kale. (Luka 24:27) mIshara ya vibanda vitatu anayosema Petro sio rahisi sana kupata maana yake. Anayefanya kibanda ni mmoja anayetaka kubaki hapo bila kutoka kwa kufanya makazi ya kudumu, yawezekana Petro alitaka waendelee kubaki katika hali ile ya utukufu. Lakini Yesu anatuonesha kuwa daima yeye ni msafiri, daima yupo safarini, na ndio maisha ya kila Mkristo, tu wasafiri kila siku ya maisha yetu. Tunaalikwa kutoka iwe katika ubinafsi wetu ili tuweze kumwelekea jirani aliye muhitaji zaidi yangu. Na ndio lengo la mazoezi ya kiroho kwa kipindi hiki cha neema cha Kwaresima ili tutoke katika hali zetu tunazozipenda na kuzifurahia kwa kumpenda Mungu zaidi na jirani. Sala, Kufunga na Matendo ya Huruma vyote lengu na shabaha lake ni kutualika kutoka katika “comfortable zones” zetu na kuwa daima safarini. Mfungo mzuri ni ule unaoruhusu kumfungulia mwingine kutoka katika hali duni na ya uhitaji zaidi yetu. (Askofu Bagonza wa KKKT - Karagwe).
Hata baada ya kukutana na Mungu kwa namna ya pekee katika Maadhimisho yetu ya kiliturjia au sala binafsi tunaalikwa daima kutoka na kwenda kutumikia wengine, kwenda kuwashirikisha wengine mema na ukuu wa Mungu. Kishawishi cha kujenga vibanda vitatu kwa maana ya kutaka kuendelea kubaki katika comfortable zones zinampata kila mmoja wetu, Kwaresima ni mwaliko wa kushuka kutoka mlimani ili nasi tuweze kwa maisha yetu kupanda mlima ule wa Kalvari pamoja na Yesu, kwa kutumikia ndugu zetu wanaokuwa wahitaji zaidi wa upendo na huruma ya Mungu. Muda wa sala na Maadhimisho ni nafasi za kutusaidia kukutana na kumsikiliza Mungu nini na wapi anatutaka kwenda na kutumika. Kama tulivyoona kuwa hatuwezi kuelewa Agano la Kale ikiwa hatutalisoma kwa kumuhusianisha Yesu na ndio tunaona Petro anakosa bado kuelewa “Identity” ya Yesu hata kama alimkiri kuwa ni Kristo, ni Masiha. (Matayo 16:16). Kwake alibaki kumwona Yesu ni Masiha ila kwa mantiki ya dunia hii, mtu mkubwa na muhimu sawa kama walivyo Musa na Eliya. Na ndipo tunaona Mungu anaingilia kati kwa kumtambulisha Yesu. Yesu si tu nabii au mmoja wa manabii bali ni “Mwana mpendwa wa Mungu Baba”. Na hi indio inatutofautisha na wengine kwani sisi Wakristo kwetu Yesu ni Kristo, ni Mwana pekee wa Mungu tangu milele yote! Kutaka kujenga vibanda vitatu kwa Yesu, Musa na Eliya ni sawa na kusema wanafanana kwa hadhi. Mara baada ya mazungumzo yao tunaona anabaki Yesu peke yake. Mungu alinena na watu wake mwanzoni kwa njia ya Musa na manabii ila sasa anabaki Mwana pekee wa Mungu anayenena nasi. Ni Yeye pekee tunaalikwa na kupaswa kumsikiliza kwani Ni Neno wa Mungu. Musa na manabii walishamaliza misheni yao tunabaki na tunaalikwa sasa kumsikiliza Mwana pekee wa Mungu Baba. Waliyoyena Musa na manabii yanapita ukamilifu wake katika Nafsi ya Yesu Kristo, aliye kweli Mwana wa Mungu. Nawatakia Dominika na Kwaresma Takatifu! Shavua tov!