Tafakari Dominika ya tatu Kipindi cha Kwaresima Mwaka A: Mwanamke Msamaria: Maji ya Uzima wa Milele
Na Padre Gaston George Mkude, -Roma.
Amani na Salama! Mama Kanisa anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika Sakramenti ya Upatanisho kama mahali muafaka pa kuonja huruma na upendo wa Mungu, tayari kusimama tena na kuendelea na safari ya Imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani! Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha Mapadre waungamishaji kwamba, wao ni vyombo vya upatanisho, huruma na upendo wa Mungu na kamwe si wamiliki wa dhamiri za waamini. Wajenge utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa makini, ili wawasaidie waamini wao kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu maisha na wito wao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Kwaresima ni fursa ya kukutana na Yesu, ajuaye njaa na kiu yetu ili atupe maji ya uzima! Dominika ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A wa Kanisa ilikuwa ni ya kuwateua na kupokea majina ya Wakatekumeni watakaobatizwa katika Kesha la Pasaka. Dominika iliyopita yaani ya pili ya Kwaresima Kanisa limewakabidhi rasmi Kanuni ya Imani, na leo Dominika ya tatu wanapata takaso la kwanza, ndio kuwapatanisha na kuwaleta karibu na Mungu na pia Kanisa. Na ndio somo la Mwanamke Msamaria linatualika safari ile ya imani ya kila mmoja wetu na hasa kwa namna ya pekee ndugu zetu Wakatekumeni. Maisha ya kila mwamini na Mbatizwa ni kutembea katika urafiki na Mungu, ndio kuishi maisha ya neema ya utakaso, yaani utakatifu. Ni mwaliko kwao kuenenda na kutembea katika utakatifu kwani huo ndio wito wa kila mfuasi wake Yesu Kristo.
Mwinjili Yohane daima huwa hatuelezi matukio ya Yesu kwa lengo la kutupa michapo au taarifa tu ya kile kilichojiri, bali daima kufikisha ujumbe na mafundisho ya kitaalimungu. Na moja ya matukio hayo ndio mkutano wa Yesu na mwanamke Msamaria pale kisimani. Simulizi hili si tu limebeba kweli za kihistoria bali zaidi sana ujumbe wa kitaalimungu kwa lugha ile ya ishara mbali mbali kama tutakavyojaribu kuziangalia katika tafakuri yetu ya leo. Kisima katika lugha ya kibiblia ilikuwa ni mahali pa kukutania watu na hasa wachungaji walifika kunywesha mifugo yao, wafanyabiashara pia walifika kisimani pamoja na bidhaa zao kuchuuza, kwani hapo wangeweza kupata wateja, wanawake na hasa saa za asubuhi na jioni na sio mchana kama tunavyosikia leo kwa ajili ya kuteka maji, lakini haswa kisimani ilikuwa ni mahali ambapo wapenzi walikutana aidha kwa mara ya kwanza au kwa majadiliano zaidi ya urafiki wao. Kisima ni mahali pa watu kukutana, ni mathalani gulioni au masokoni au vijiweni katika mazingira yetu ya leo. Tunaweza kusoma zaidi katika Biblia sehemu mbalimbali zinazoonesha makutano ya kisimani. (Mwanzo 24:10-25; 26:15-25; 29:1-14; Kutoka 2:15-21) Simulizi la leo la makutano ya kisimani tunaona wahusika wakuu ni Yesu na mwanamke Msamaria. Kisima kinachozungumziwa na Mwinjili Yohane ni kweli kipo hadi leo, na kina umri wa zaidi ya miaka 3000 na bado hadi leo kinatoa maji safi na salama kwa kunywa kama ilivyokuwa nyakati zile za Yesu.
Kilikuwa ni kisima ambapo wasafiri hasa watokao Galilaya kuelekea Uyahudi walisimama na hapo kuweza kupata nguvu kwa mapumziko na kupooza kiu yao. Mwinjili Yohane anatuonesha hata Yesu kwa uchovu wa safari anafika mahali hapo na anapumzika na ilikuwa mchana wa saa sita. Mwinjili Yohane hataji tu muda bila kuwa na sababu ya kiteolojia. Tunasoma Yesu anahukumiwa kifo mchana wa saa sita. (Yohane 19:14,28-30) “Ilikuwa yapata saa sita mchana, siku ya maandalio ya Pasaka, … Naona kiu…yametimia! Kisha akainamisha kichwa, akatoa roho”. Saa ya kiu ya Yesu ndio saa ile ya wokovu wa ulimwengu, kiu yake ni kuona sisi tulio wadhambi tunapata wokovu. Ni kiu ya upendo kwa mwanadamu na ulimwengu mzima, ni kiu ya kumkomboa mwanadamu! Mwanamke Msamaria anashangaa kuona Yesu akimuomba maji, hakuna cha ajabu kwa mtu kuomba maji, ila ikumbukwe kwa Wayahudi na Wasamaria walikuwa ni watu wasiochangamana, na hata mbaya zaidi mazungumzo kati ya mwanamke na mwanaume na wakiwa peke yao isingeeleweka wala kukubalika katika jamii ile ya Yesu. Na hata ikibidi kumsemesha mwanamke mkiwa peke yenu basi mwanaume alipaswa kutumia maneno machache sana hivyo sio kufanya mazungumzo, bali kama ilipaswa basi ni kuuliza kitu au jambo fulani. Mfano kama mwanaume anafika Magomeni na anapotea hajui tena njia ya kuelekea Kariakoo hakupaswa hata kuuliza; Wapi njia ielekeayo Kariakoo? Kwani tayari sentensi hiyo ina maneno mengi itoshe tu kusema: Kariakoo? Na hapo mwanamke naye aidha kwa ishara au neno moja au mawili kumuonesha mwanaume njia.
Tunaona hata wanafunzi wa Yesu wanaporejea na kumkuta Bwana na Mwalimu wao akiongea na mwanamke Msamaria walibaki na mshangao mkubwa. Yesu ndio anawaalika wanafunzi kuwa na mtazamo mwingine, kubadili vichwa vyao kama kweli wanataka kuwa wanafunzi na wafuasi wake. Ni kufikiri na kutenda kama Yesu. Ni kukubali wokovu wa fikra, ni kukubali kubadili vichwa vyetu. Na hiyo ndio metanoia ya kweli. Labda kabla ya kuendelea sana tunajiuliza mwanamke yule Msamaria alikuwa nani haswa, maana Mwinjili Yohane hamtambulishi kwa jina lake, wala wapi alitokea haswa ila anamtambulisha kama mwanamke Msamaria, kwa kusema ni Msamaria ni sawa na kusema ni mpagani, asiyeamini katika Mungu wa kweli. Si tu anakuja kisimani peke yake kama tulivyoona mwanzoni kuwa kisimani ilikuwa ni makutano pia ya wapenzi, na labda ndio maana anakuja sio na akina mama wengine bali akiwa peke yake. Na si anakuja peke yake, hata Mwinjili anatuonesha kuwa Yesu alibaki kisimani peke yake kwa sababu wanafunzi wake walienda mjini kutafuta chakula. Ni saa ile ya Wokovu hakika ni Mungu mwenye huruma (Misericordia) anakutana na mdhambi (Misera).
Hapo tunabaki na swali la msingi kwa nini Mwinjili anakazia kutuonesha kuwa walikuwa wao wawili peke yao pale kisimani. Kama tulivyoona kuwa kisimani ilikuwa ni sehemu au mahali pakukutania wapenzi. Na katika Agano la Kale tunaona taifa la Israeli lilibaki daima kama mchumba aliyepaswa kubaki kuwa mwaminifu katika mahusiano na Mungu. Urafiki na mapenzi yao yalianza tangu wakiwa safarini jangwani wakiwa wanaelekea nchi ile ya ahadi. Lakini tunaona wakiwa safarini mara kadhaa wanapoteza uaminifu na ukaribu wao na Mungu, na hivyo kuamsha wivu kwa upande wa Mungu. Je, Mungu aliye mume au mchumba wake Israeli anafanya nini katika mazingira ya kukosa uaminifu kwa mke wake? Je Mungu atawaacha kwa kuwatalaki? (Isaya 54:6-7 na Hosea 2:16-17). Ni katika majadiliano ya Yesu na mwanamke Msamaria anamuuliza yupo wapi mume wake, na kumuonesha kuwa tayari ameshakuwa na waume watano na hata huyu aliye naye sasa si mume wake halali. Yesu anamuonesha hapa kisimani kurejea na kurudi kwa mume wake wa kwanza aliye kweli mpenzi wa moyo na maisha yake, ndiye Mungu wa kweli. Ni Mungu anamuonesha Israeli kurejea na kuwa mwaminifu kwa Mungu, aliye kweli upendo kwake. Njia ile kwa wanaojua jiografia ya nchi takatifu haikuwa lazima mmoja kuipitia atokapo au aendapo kati ya Galilaya na Uyahudi kwani njia rahisi zaidi ilikuwa ni ile ya bonde la mto Yordani.
Lakini Mwinjili Yohane anatuonesha ulazima kwa upande wa Yesu na wanafunzi wake kupita njia ya Samaria, ndio kusema jinsi upendo wa Mungu kwa watu wake na hasa wale wanaokuwa mbali naye. Ni jinsi Mungu anavyoshuka na kufanyika mwanadamu ili mwanadamu apate uzima wa kweli na wa milele. Mwinjili anaonesha Yesu kuchoka ndio kusema jinsi mwanadamu anavyokuwa mbali na Mungu kila mara tunapomwasi Mungu na kugeukia miungu mingine ya uongo na kuiabudu. Mungu anakuwa mbali hivi anapotufikia anatuonesha jinsi Mungu alivyo na kiu kuona nasi tunakuwa na kiu ya kumtafuta Yeye ili atupe maji yale ya uzima ili tukinywa tusione kiu kamwe. Tunaona kama vile mwanamke Msamaria alivyokuja kisimani kuchota maji ya kawaida, na hata wanafunzi wa Yesu nao wanaenda mjini kusaka chakula cha dunia hii. Ni jinsi gani sote mara nyingi tunaelekea na kupoteza muda kwa mambo ya dunia hii yasiyoweza kuwa chakula wala kinywaji chetu cha kweli. Njaa na kiu ya kweli ni katika kumtafuta Mungu, ni katika kukaa karibu na pamoja na Mungu, ni katika kusafiri pamoja na Mungu hata tukiwa katika nyakati ngumu kiasi gani. Siku hizi ambapo dunia nzima tunasafiri katika hofu kubwa ya mmomonyoko wa maadili, vita, mdororo wa kiuchumi na tena tukiwa katika wakati wa neema wa Kwaresima, tunaalikwa kujiweka karibu zaidi na Mungu. Na ndio nafasi ya kusali zaidi na ndivyo tunavyoona juhudi mbalimbali za makusudi za kutuweka karibu na Mungu. Ni tukio la kututafakarisha sio kwamba Mungu anatuadhibu na kutuangamiza wanadamu ila ni nafasi ya neema ya kutufanya nasi tuwe na kiu na njaa ya kuwa na Mungu, ya kusafiri naye siku zote za maisha yetu.
Wanawaisraeli walipokuwa njiani kule jangwani na hasa walipokosa maji walianza kulalamika na kujadiliana wao kwa wao, na hasa kwa kuanza kumlaumu Mungu aliyewatoa katika nchi ile ya utumwa. Je, nasi tuwe kama Wanawaisraeli walivyokuwa kule Masa na Meriba? Je, muda na wakati huu wa mahangahiko makubwa uwe ni muda wa kumlalamikia na kumnung’unikia Mungu? Je, uwe ni muda wa kujiona Mungu ametuadhibu na kutuacha peke yetu kati ya mateso na shida kubwa? Je tuanze kuwa na mashaka katika uaminifu na upendo wa Mungu kwetu na hivyo tuanze kujiuliza na kuhoji ikiwa Mungu yu pamoja nasi au la? Mungu anatenda muujiza kwa kuwapatia maji wana wa Israeli wakati angeliweza kuwaelekeza kuchimba kisima na kupata maji, ila anawaonesha jinsi Yeye alivyo mwaminifu daima na anavyobaki kuwa upendo usio na masharti kwa kila mmoja wetu. Masa na Meriba ni leo dunia inapotembea na kubaki katika malalamiko na manung’uniko kwa kupoteza imani kwa Mungu na ahadi zake kwetu. Tu wadhaifu lakini daima katika mikono salama ya Mungu mwenyewe. Mungu kamwe hatuachi peke yetu hata tunapokuwa mbali naye kiasi gani, daima ni kiu yake kuona nasi tunakuwa na kiu ya kurudi kwake kama tunavyotafakari somo la Injili ya Dominika ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A wa Kanisa. Mwanamke yule Msamaria kama labda wengi wetu pia katika safari hii ya Kwaresima pale mwanzoni anawaza na kufikiri juu ya maji ya kawaida, lakini tunaona taratibu anaanza naye kuelewa ujumbe kusudiwa wa Yesu kwake.
Ni safari ya kumtambua na kumjua Mungu ambaye nasi kila mmoja hana budi kuipitia katika kipindi hiki cha Kwaresima. Mwanzoni alimtambua Yesu kama msafiri wa kawaida aliyefika kisimani ili kupooza kiu yake na kupumzika, baadaye anamtambua kama mkubwa, halafu kama nabii na baadaye Masiha na mwishoni pamoja na Wasamaria wengine wanamtambua kama Mkombozi wa ulimwengu. Safari hii ya kumtambua Yesu ni ya kila mmoja wetu kwani mara nyingi pale mwanzoni Yesu ni mmoja anayepaswa kututimizia mahitaji yetu ya kila siku, na labda hata mwelekeo wa sala zetu unakuwa ni huo, tunaomba chakula, kinywaji na mahitaji mengine ya msingi ya kimwili ya siku kwa siku. Pamoja na kwamba ni kweli ni mahitaji ya msingi na labda ya lazima sana katika maisha yetu lakini hatupaswi kuishia hapo bali kufika hatua ile ya kumtambua kama Mkombozi na Mungu wetu. Hitimisho la Injili ya leo linapaswa kuwa la kila mmoja wetu baada ya kukutana na Yesu. Mwanamke Msamaria baada ya kumtambua Yesu katika mazungumzo, naye anajawa na shauku na ari kubwa na hivyo kuacha nyuma mtungi wake na kwenda kuwashuhudia wengine kuwa amekutana na Masiha, amekutana na Mkombozi. Ndio mwito kwetu baada ya kukutana na Yesu na kumtambua katika Neno lake na katika maisha ya Sakramenti na maisha ya Kanisa hatuna budi kutoka na kuwa wamisionari kwa ushuhuda wa maisha yetu na kuwashirikisha wengine furaha ile ya kukutana na kumtambua Yesu na kula na kunywa chakula na kinywaji kile cha uzima wa milele. Nawatakia tafakari njema na Dominika takatifu!