Tafakari Neno la Mungu Dominika ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A wa Kanisa: Kristo Yesu ni chemchemi ya maji yanayobubujikia maisha na uzima wa milele. Tafakari Neno la Mungu Dominika ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A wa Kanisa: Kristo Yesu ni chemchemi ya maji yanayobubujikia maisha na uzima wa milele.  (ANSA)

Tafakari Dominika Tatu Kwaresima Mwaka A: Yesu Chemchemi ya Maji ya Uzima wa Milele

Mama Kanisa anawaalika watoto wake kujibidisha kumtafuta na kumwendea Yesu katika ukweli na uwazi, ili aweze kuwaganga na kuwaponya kutoka katika undani wa maisha yao kama ilivyokuwa kwa yule Mwanamke Msamaria aliyetangatanga akitafuta upendo kwa dhati ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili! Yesu Kristo ndiye chemchemi ya maji ya uzima ambayo hukata kabisa kiu ya maisha ya roho zetu na kuwatakasa watu.

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli (Napoli), Italia

Kristo Yesu ni chemchemi ya maji yanayobubujikia maisha na uzima wa milele. Mama Kanisa anawaalika watoto wake kujibidisha kumtafuta na kumwendea Yesu katika ukweli na uwazi, ili aweze kuwaganga na kuwaponya kutoka katika undani wa maisha yao kama ilivyokuwa kwa yule Mwanamke Msamaria aliyetangatanga akitafuta upendo kwa dhati ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili! Yesu Kristo ndiye chemchemi ya maji ya uzima ambayo hukata kabisa kiu ya maisha ya roho zetu. Ni maji ya uzima wa milele ambayo yalitoka pia ubavuni mwa Kristo: na mara ikatoka damu na maji. Kristo aliye chemchemi ya maji ya uzima hujifunua kwetu hatua kwa hatua kama afanyavyo kwa mwanamke Msamaria. Kwa upande wetu tunadaiwa utulivu na uvumilivu katika kumsikiliza na kuzungumza na Kristo ambaye anajua undani wetu- hakuna lifichikalo kwake. Na zaidi ya yote tunapaswa kuacha yote ili kupata yote katika Kristo: akauacha mtungi wake! Kristo hubadili kabisa maisha yetu. SOMO LA INJILI: Yn. 4:5-42: Somo letu la Injili lina uhusiano mkubwa sana na somo letu la kwanza: katika somo la kwanza (Kut. 17:3-7) wana wa Israeli wanamlalamikia Musa na Mungu kwa sababu ya “kiu ya maji”- maji ambayo hata wakinywa watasikia tena kiu, lakini katika somo la Injili Yesu anamfunulia mwanamke Msamaria kuwa yapo “maji ya uzima”- maji ya kiroho ambayo yanabubujikia (yanatiririka) kuelekea uzima wa milele. Hivyo, badala ya kutafuta maji ya kutuliza kiu cha kimwili kama Waisraeli, Yesu anataka mwanamke msamaria atafute maji ya uzima yanayotuliza kiu ya kiroho. Kabla hatujasonga mbele ya tafakari ya Injili yetu tuone baadhi ya mambo.

Kristo Yesu ni chemchemi ya maisha ya uzima wa milele
Kristo Yesu ni chemchemi ya maisha ya uzima wa milele

Katika Injili yetu ya leo Yesu anakutana na mwanamke Msamaria kwenye kisima cha Yakobo. Yesu ni Myahudi na huyu mama ni Msamaria: kwa mapokeo ya Wayahudi ni jambo la kashfa sana kwa mwanaume Myahudi kusimama/kuongea na mwanamke, tena Msamaria (asiye Myahudi). Wasamaria ni watu gani? Baada ya taifa la Ashuru (Assyria) kuvamia ufalme/himaya ya Kaskazini (the northern kingdom of Israel) mnamo mwaka 722 B.K, watu wa taifa la Ashuru na mataita mengine ya kigeni walivamia na kuanza kuishi katika mji wa Samaria na kuoa/kuoana na Waisraeli. Jambo hili lilisababisha kuzaliwa kwa watu ambao ni matokeo ya mwingiliano kati ya Wayahudi na wasio-Wayahudi. Kizazi hiki chotara ndicho kilichoitwa Wasamaria. Kitendo cha baadhi ya Waisraeli kukubali kuoa au kuolewa na watu wa mataifa ya kigeni kiliwafanya Waisraeli wengine kuwatazama wale waliooa au kuolewa na watu wa mataifa wengine kuwa ni wasaliti na najisi kwani kizazi chao kimenajisi taifa teule la Mungu ambalo halipaswi kuchangamana na watu wengine. Hivyo, Waisraeli halisi (ambapo kizazi chao hakijaingiliana na watu wengine) waliwadharau wale Wasamaria (ambapo ni kizazi mchanganyiko). Mwisraeli halisi alikatazwa kupita eneo wanaloishi Wasamaria, kusali pamoja nao hekaluni wala kuomba msaada wowote kutoka kwa Wasamaria. Hali hii ilipelekea Wasamaria nao kuwa na sehemu yao tofauti ya kuabudia (walifanya ibada zao kwenye mlima Gerizim badala ya kwenda kwenye hekalu la Yerusalemu), Wasamaria wakawa na tafsiri yao wenyewe ya Torati (vitabu vitano vya mwanzo kwenye Bibilia) na mengineyo. Kwa ujumla Wayahudi na Waisraeli walikuwa na uadui mkubwa kati yao. Pamoja na uadui uliokuwepo kati ya Wayahudi na Wasamaria, leo Yesu anakutana na mwanamke msamaria kama rafiki na siyo kama adui.

Maji ni chemchemi ya maisha mapya katika Kristo Yesu
Maji ni chemchemi ya maisha mapya katika Kristo Yesu

Makutano na mazungumzo kati ya Yesu na mwanamke Msamaria yanatufunulia mambo mengi sana: (1) Yesu ndiye chemchemi ya uzima wa milele. Mwanamke huyu alifika kisimani kuchota maji, maji ambayo kwenye somo letu la kwanza Waisraeli wanayataka ili kutuliza kiu yao ya kimwili. Cha kushangaza mwanamke huyu ataondoka na kuacha mtungi wa maji kuonesha kuwa hitaji lake la maji ya kawaida limejazwa kwa kupatiwa maji ya uzima. Maji huleta uhai/uzima na kusafisha miili yetu. Yesu ni chemchem/kisima cha maji yaletayo uzima wa kiroho na kusafisha maisha yetu ya kiroho. (2) Yesu ni nabii, Masiha na mwokozi wa ulimwengu. Kumjua Mungu au kujua imani yetu siyo suala la dakika au siku moja. Kumjua Mungu ni hatua kwa hatua. Pole pole kadiri mwanamke Msamaria anavyozungumza na Yesu ndiyo anazidi kumtambua Yesu: mwanzoni alimwita Bwana (yaani Sir), baadaye alipoambiwa yote aliyotenda akamtambua Yesu kama nabii, baadaye kidogo anamtambua Yesu kama Masiya na baadaye akiwa na wanakijiji wengine wanamtambua Yesu kama mwokozi wa ulimwengu. Kwa ujumla kumjua Yesu/ kujua imani ni suala endelevu. Hata hivyo swali la msingi ni hili: Je, mwanamke Msamaria asingekubali kutumia muda wake kuzungumza na Yesu angemtambua Yesu kuwa ni Nabii, Masiya na Mwokozi wa ulimwengu? Hapana. Tutamtambua Yesu kama tukiwa tayari kuzungumza naye kwa utulivu na uvumilivu. (3) Yesu amekuja kuondoa uadui na utengano kati ya Mwanadamu na Mungu na kati ya mwanadamu na mwanadamu. Leo katika Injili Yesu anazungumza na mtu ambaye kwanza ni mwanamke, pili ni Msamaria (siyo Myahudi halisi), tatu mwenye namna na utaratibu wake wa kuabudu. Licha ya yote haya, bado Yesu anadiriki kuongea naye.

Watu wanazaliwa upya katika maji na Roho Mtakatifu
Watu wanazaliwa upya katika maji na Roho Mtakatifu

Hii ni kuonesha kuwa Yesu amekuja kuondoa uadui na tofauti zetu. Yeye hakuogopa kuongea naye kwa sababu ni mwanamke au kwa sababu kihistoria ni adui yake au kwa sababu wanatofautiana mahali pa kuabudia. Yesu amekuja kuondoa uadui na tofauti kati yao: tofauti zinazosababishwa na itikadi za kijinsia, tofauti zinazotokana na makabila yetu, tofauti zinazosababishwa na imani zetu. Haya yote yamevunjwa na Yesu kwa mafundisho, mateso, kifo na ufufuko wake. Cha ajabu katika karne hii ya 21 bado sisi tunabaguana kwa misingi ya udini, ukabila, ukanda, itikadi za kisiasa na hata uwezo wetu wa kiuchumi. Ni aibu sana. Tumtazame Kristo anayevunja vizingiti vyote vya utengano. (4) Mungu anajua undani wa maisha yetu dhaifu, lakini yupo tayari kutuvuta kwake. Mwanamke huyu anastaajabu kuona Yesu anajua habari za maisha yake ya kwamba aliwahi kuwa na wanaume watano na hata aliyenaye sasa si mume wake (yaani ni kama hawara au mchepuko wake ambaye wanaishi bila muungano wa ndoa- mume wa uzinzi). Hapa kuna fundisho kubwa: Mungu anajua undani wa maisha yetu- anajua hali yetu ya dhambi, anajua unyonge na udhaifu wetu. Hakuna tunaloweza kumficha Mungu. Licha ya kujua undani wa maisha ya mwanamke huyu, Yesu hatumii muda wake kumhukumu au kumtukana bali anamsaidia kwa upendo kutambua mapungufu yake na kuyarekebisha ili apate maji ya uzima wa milele (neema zitakazomfikisha kwenye uzima wa milele). Kristo yupo tayari kutuvuta kwako licha ya madhaifu yetu. Jambo kubwa ni kuwa tayari kuongoka na kujiaminisha kwake. (5) Maisha ya dhambi yanatutenga na wenzetu, yanatunyima uhuru na raha. Tubadilike. Tunaambiwa kuwa mwanamke huyu alifika kisimani “saa sita.” Kwa kawaida akina mama hufika kisimani asubuhi au jioni. Huyu mwanamke anakwenda kuteka maji saa sita mchana. Mbona hakwenda asubuhi? Inaonekana mwanamke huyu hakuwa na mwenendo mzuri wa maisha na hivyo aliogopa kwenda kisimani asubuhi ili kukwepa kusutwa na kusimangwa na wanawake wenzake. Hapa tunapata fundisho kubwa: maisha ya dhambi yanatutenga na wenzetu na yanatunyima amani. Baada ya kupata mwanga wa Kristo, mama huyu hakuogopa tena kujumuika na watu: atajiunga tena ya jamii yake na kuwaleta kwa Kristo. Mabadiliko yanawezekena kwa juhudi zetu na kwa msaada wa neema ya Mungu. Dominika njema

13 March 2023, 15:46