Tafuta

Fumbo la Pasaka ni utimilifu wa Fumbo la Umwilisho kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Fumbo la Pasaka ni utimilifu wa Fumbo la Umwilisho kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti!  

Tafakari Dominika ya V ya Kipindi cha Kwaresima: Ufufuko Wa Wafu na Matumaini ya Uzima wa Milele

Fumbo la Pasaka ni sababu na kiini cha imani, furaha na matumaini ya Wakristo hapa duniani kwani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kuwakirimia maisha ya uzima wa milele, mwaliko wa kuendelea kupyaisha imani, matumaini na mapendo. Kwa njia ya huruma na upendo wa Mungu, waamini wamepewa matumaini mapya katika Kristo Yesu! Ufufuko wa wafu, matumaini na uzima wa milele.

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, - Pozzuoli (Napoli), Italia.

Daima kifo kinawahuzunisha na kuwaogopesha wanadamu. Hata hivyo, katika Kristo kifo kinapata maana mpya kwa kuwa uzima wa waamini haundolewi, ila tu unageuzwa tu na waamini wanapata makao ya milele mbinguni, yakiisha bomolewa makao ya hapa duniani kama tunavyoelezwa na Utangulizi I wa Misa ya Wafu. Ni ukweli huu ambao Kristo anaudhihirisha kwa kumfufua Lazaro ili kuonesha kuwa Kifo siyo mwisho wa maisha ya mwanadamu maana katika Kristo kuna ufufuko kwa kuwa Yeye ni ufufuo na uzima. Fumbo la Pasaka ni utimilifu wa Fumbo la Umwilisho kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, Mwenyezi Mungu amewakirimia wanadamu dunia mpya inayoambata wokovu ulioletwa na Kristo Yesu. Huu ndio mwanga unaowaangaza watakatifu na mashuhuda wa imani walioenea sehemu mbali mbali za dunia. Fumbo la Pasaka ni sababu na kiini cha imani, furaha na matumaini ya Wakristo hapa duniani kwani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kuwakirimia maisha ya uzima wa milele, mwaliko wa kuendelea kupyaisha imani, matumaini na mapendo. Kwa njia ya huruma na upendo wa Mungu, waamini wamepewa matumaini mapya katika Kristo Yesu!

SOMO LA KWANZA: Ezek. 37:12-14: Kitabu cha Nabii Ezekieli kiliandikwa wakati Waisraeli wakiwa uhamishoni Babeli. Walichukuliwa mateka uhamishoni Babeli kama adhabu ya wao kumuasi Mungu kwa sababu ya dhambi zao: dhuluma ambayo matajiri waliwafanyia maskini, kuabudu miungu ya kigeni, rushwa, kuvunja taratibu za ibada na mengineyo. Wakiwa uhamishoni Babeli Waisraeli hawakuweza kumwabudu Mungu wao kama walivyomwabudu katika hekalu lao la Yerusalemu na mbaya zaidi walilazimishwa kuabudu miungu ya watu wa Babeli, ambayo ilikuwa ni miungu ya uongo. Katika hali hii Waisraeli walipoteza matumaini na kuona kama Mungu amewasahau. Kwa ujumla walijiona kama “taifa lililokufa,” taifa liliso la uhai tena, walijifananisha na wafu (marehemu). Ni katika muktadha huo, Mungu kupitia nabii Ezekieli anawaletea Waisraeli walioko uhamishoni Babeli ujumbe wa faraja na matumaini kuwa muda si mrefu “atalihuisha” (atawarudishia uhai) taifa la Israeli kwa kulikomboa kutoka Babeli ili lirudi tena Israeli na kujijenga upya kama taifa teule la Mungu. Mungu anatumia lugha ya picha kufikisha ujumbe huo: atalihuisha taifa la Israeli kwa kutia roho yake ndani yao kama vile anavyoweza kuwahuisha wafu- “Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu, enyi watu wangu. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi…” Huu ulikuwa ni ujumbe wa furaha na matumaini kwa Waisraeli waliokuwa wanateseka uhamishoni Babeli.

Ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele ni imani ya Kanisa.
Ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele ni imani ya Kanisa.

Ujumbe huu wa Nabii Ezekieli unaturusu na sisi pia. Sisi nasi tumekuwa mbali na Mungu kwa sababu ya dhambi zetu (yaani tupo uhamishoni). Dhambi hizi zimetufanya kuwa wafu kiroho (marehemu kiroho) - wafu ambao tupo ndani ya makaburi. Hata hivyo, Mungu aliye mwingi wa huruma yupo tayari kututoa katika hali yetu ya kufa kiroho- yaani Mungu yupo tayari kutuhuisha kiroho kwa kutia roho yake ndani yetu ili tuwe na muunganiko naye na kuenenda kama waana wa Mungu. Ni Roho yake ndiyo itakayotupatia uzima wa kiroho. Bila Roho ya Mungu ndani yetu hatuwezi kuwa hai kiroho. Roho hii ya Mungu inapatikana katika sakramenti (hasa ya kitubio), katika sala, katika Neno lake, katika kutimiza mapenzi ya Mungu na katika kushiriki mazoezi mengine ya kiroho. Hivyo hata tuwapo katika hali ya kufa katika dhambi tukumbuke kuwa Mungu anatuahidia uzima wa kiroho iwapo tutakuwa tayari kutimiza maagizo na mapenzi yake. Ni Roho hiyo hiyo ya Mungu iliyo ndani ya Kristo Yesu inayomfufua Lazaro na kumpatia uzima mpya katika somo la leo la Injili.

SOMO LA PILI: Rum. 8:8-11: Mtume Paulo katika somo letu la pili anasisitiza kuwa “maisha yetu yanapaswa kuongozwa na Roho kama tunataka kumpendeza Mungu.” Mtume Paulo katika maandiko yake anasisitiza kuwa lengo kubwa la mwanadamu linapaswa kuwa “kumpendeza Mungu”. Hata hivyo Mtume Paulo anaeleza kuwa mwanadamu hawezi kufikia lengo hilo la kumpendeza Mungu kama ataishi maisha yanayotawaliwa na mwili. “Kutawaliwa na mwili” ni kuenenda kwa kadiri ya matakwa ya mwili kwa lengo la kuuridhisha mwili (kutimiza tamaa za mwili). Kwa kadiri ya Paulo “kutawaliwa na mwili” kunasababisha mtu kutenda dhambi na hivyo kushindwa kumpendeza Mungu. Ili kumpendeza Mungu ni lazima mwanadamu akubali kuongozwa na Roho- Roho ya Kristo, Roho ya Mungu. Roho ya Mungu/Kristo ndiyo inayoongoza maisha na matendo yetu, ndiyo inayotuwezesha kushiriki maisha ya kimungu, ndiyo inayotuwezesha kupata uzima wa kimungu. Maisha ya mwanadamu yakiongozwa na Roho yanazaa matunda ya upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi (rejea Gal. 5:22-23). Maisha ya mwanadamu yakitawaliwa na mwili huzaa uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo (rejea Gal. 5:19-21). Wengi wetu maisha yetu hayampendezi Mungu kwa sababu tumekubali kutawaliwa na matendo ya mwili kwa lengo la kuufurahisha mwili (yaani kujikita zaidi katika mambo ya kimwili/kidunia zaidi ilihali tukiweka kando mambo ya kiroho: tunekuwa wazinzi na waasherati kwa sababu ya kukidhi tamaa za mwili, tumekuwa walevi na walafi kwa sababu ya kusukumwa na tamaa za mwili, tumekuwa wauaji na majambazi kwa sababu ya tamaa za mwili. Tunapaswa kumuomba Mungu ili neema yake itusaidie kuongozwa na Roho wake Mtakatifu ambaye tulimpokea wakati wa ubatizo kwani Yesu Kristo Mwenyewe alisema, “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu” (rejea Yn. 6:63).

Fumbo la kifo linatisha lakini Kristo amewaletea waja wake matumaini.
Fumbo la kifo linatisha lakini Kristo amewaletea waja wake matumaini.

SOMO LA INJILI: Yn. 11:1-45: Injili ya Yn. 10:22 inatueleza kuwa Yesu amefika Yerusalemu wakati wa sikukuu ya Kutabaruku (katika sikukuu hii Wayahudi walikuwa wanakumbuka tukio la kutabarukiwa kwa hekalu la Yerusalemu). Akiwa hekaluni Yesu anawaambia Wayahudi kuwa Yeye na Mungu Baba ni wamoja: “Mimi na Baba tu umoja” (rejea Yn. 10:30). Ukweli huu unawakasirisha Wayahudi ambao wanaokota mawe ili wampige maana amejilinganisha na Mungu. Na tena baadaye atawaeleza kuwa Yeye ni Mwana wa Mungu (rejea Yn. 10:36). Ukweli huu ulisababisha pia Wayahudi kutaka kumkamata lakini Yeye aliondoka mikononi mwao na kwenda ng’ambo ya Yordani, mahali pale alipokuwa Yohane Mbatizaji akibatiza hapo kwanza.  Mji huu aliokuwa akibatiza Yohane umetajwa kwa jina Bethania (rejea Yn. 1:28). Ni katika mji huu wa Bethania huko Perea, ng’ambo ya Yordani ndiko habari za ugonjwa wa Lazaro zinamfikia Yesu (ikumbukwe kuwa mji huu wa Bethania ni tofauti na mji wa Bethania karibu na Yerusalemu  walipoishi Martha na Mariamu na Lazaro kaka yao ambako Yesu atafika na kumfufua Lazaro). Anapokaribia Bethania Yesu anapokelewa na Martha na katika mazungumzo yake na Martha kabla ya kumfufua Lazaro Yesu anajifunua kwa kusema, “Mimi ndimi huo ufufuo na uzima.” Yesu anadhihirisha ukweli huo kwa kumfufua na kumrudishia uzima Lazaro na hivyo kuthibitisha kuwa Yeye kweli ni ufufuo na uzima. Muujiza huu pia unathibitisha kile alichosema Yesu katika Yn. 5:21, 25, 28): “Maana kama Baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, vivyo hivyo na Mwana awahuisha wale awatakao” (aya ya 21).

Kutoka katika Injili yetu ya leo (Yn. 11:1-45) tunafunuliwa kuwa: (1) Kristo ni Mungu, Bwana wa ufufuo na mleta uzima. Kwa Wayahudi (na kwetu pia) inafahamika kuwa Mungu ndiye chanzo cha uzima wa mwanadamu. Mungu pekee ndiye atoaye na atwaaye uzima wa mwanadamu. Hakuna mwingine mwenye uwezo na mamlaka hayo. Kitendo cha Yesu kurudisha uhai/uzima wa Lazaro aliyekuwa amekufa kililenga kuwafunulia Wayahudi kuwa Yeye ni Mungu kwani Mungu pekee ndiye atoaye uzima (Mungu pekee ndiye chanzo cha uzima). Kadhalika kwa tendo la kumfufua Lazaro, Yesu alilenga kufundisha juu ya ufufuo wa watu baada ya kifo cha kimwili hapa duniani. Pia Yesu alilenga kuwafundisha kuwa Yeye ana uwezo wa kumpata mwanadamu uzima, siyo tu uzima wa kimwili, bali uzima wa kiroho- yaani kumfanya yoyote aaminiye kuwa na muungano usio na kikomo na Mungu aliye Muumba wake. Hata tukifa kimwili, Yeye aweza kutupa uzima wa kiroho unaotuwezesha kuishi milele pamoja na Mungu: “Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi.” Kifo cha kimwili ni hatima ya kila binadamu lakini imani kwa Kristo itamfanya yeye aliyekufa kimwili kuwa tena na uzima wa kiroho baada ya maisha ya hapa duniani.  Kadhalika Yesu kwa kumfufua Lazaro anadokeza pia ufufuko wake mwenyewe maana uweza wa kurudisha uzima anao Yeye mwenyewe na hivyo hata wanadamu watakapouondoa kwa kumsulubisha na kumuua msalabani ataurudisha uzima huu baada ya siku tatu. (2) Sisi sote “tumekufa kiroho kutokana na dhambi” na hivyo Yesu yupo tayari kutufufua. Lazaro anatuwakilisha sisi wanadamu wote.

Bethania nyumba ya mateso inageuka kuwa ni nyumba ya matumaini
Bethania nyumba ya mateso inageuka kuwa ni nyumba ya matumaini

Kama Lazaro alivyokuwa amekufa na kisha anafufuliwa na Yesu, hata sisi ni “wafu kwa sababu ya dhambi zetu”: dhambi inaua mahusiano yetu na Mungu, dhambi inaua mahusiano yetu na wenzetu na pia dhambi inaua nafsi na dhamiri zetu wenyewe. Dhambi inatufanya kuwa marehemu. Hata hivyo Yesu yupo tayari kutufufua kiroho. Kama moja ya njia za kutufufua kiroho, Yesu anatutaka “tutoke katika makaburi yetu” kama anavyomwita Lazaro kutoka kaburini: “Lazaro, njoo huku nje”. Yesu anatuita tutoke katika kaburi la dhambi: kaburi la uzinzi, kaburi la ubinafsi, kaburi la umbea, kaburi la fitina na wivu, kaburi la utapeli na dhuluma, kaburi la uvivu wa sala na mengineyo. Tena Yesu hatuiti kwa ujumla, bali anatuita kila mmoja kwa jina lake kama alivyomuita Lazaro kwa jina. Neema ya Mungu ipo tayari kutuhuisha kiroho na kututoa katika kaburi la dhambi ikiwa tupo tayari kuitafuta na kuipokea katika Sakramenti, sala na ibada mbalimbali. (3) Tuwe tayari kufa pamoja na Kristo. Kabla ya Yesu kwenda Bethania iliyopo ng’ambo ya Yordani, Wayahudi walitaka kumuua Yesu kwa mawe baada ya kusema kuwa Yeye na Baba ni umoja (yaani Yeye na Baba ni sawa). Tena walitoa agizo kuwa yeyote atakayemuona Yesu mahala popote atoe taarifa ili wamkamate na kumuua. Yesu anapoamua kurudi tena Uyahudi (mahali anapotafutwa ili auawe) na kwenda mpaka mji wa Bethania kumfufua Lazaro, Tomaso anawambia wanafunzi wenziwe, “Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye.” Tomaso ni kama anasema, “twendeni tu huko Uyahudi pamoja na Yesu ili kama watamkamata na kumuua basi na sisi tukamatwe pamoja naye na kuuawa pamoja naye.” Tomaso anaonesha utayari wa kufa pamoja na Kirsto huko Uyahudi.

Tomaso anatuwakilisha sisi sote ambao ni wanafunzi wa Yesu. Sisi nasi tunapaswa kuwa tayari kufa pamoja na Kristo: kuteseka pamoja na Kristo, kuteseka na kufa kwa ajili ya imani yetu kwa Kristo. Tukumbuke kuwa kila aliyebatizwa (aliyekubali kuwa Mkristo) anabatizwa katika mauti ya Bwana kama mtume Paulo asemavyo: “Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?” (Rum. 6:3). Kila Mkristo anapaswa kuwa tayari kufa pamoja na Kristo. Wengi wetu hatuna huu utayari. Wengi wengi ni waoga kuteseka pamoja na Kristo. Wengi wetu tunafanya kila njia kukwepa mateso na tunatumia kila namna kuzipenda sana nafsi zetu badala ya kumpenda Kristo. Kuna hata baadhi ya Mapadre na Watawa hawataki kwenda kuhudumu kwenye nchi zenye changamoto za kiimani kwa hofu ya kuuawa. Kristo Mwenyewe alisema, “Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha” (Mk. 8:35). (4) Mungu anaruhusu muda utipe ili baadaye aoneshe utukufu wake. Yesu anapoambiwa kuwa Lazaro ni mgonjwa, haendi haraka Bethania kwa akina Martha na Mariamu. Tunaambiwa kuwa baada ya kupewa habari ya ugonjwa wa Lazaro, Yesu aliendelea kukaa huko alipokuwa kwa siku nyingine mbili. Kwa nini alifanya hivyo? Kwa sababu alitaka kuonesha utukufu wa Mungu kupitia kifo cha Lazaro. Yesu aliruhusu muda upite akijua kuwa baadaye ataonesha utukufu wake kwa kumfufua Lazaro. Pengine sisi nasi tungetaka Mungu/Kristo ajibu mahitaji yetu haraka haraka bila kuchelewa. Tungependa kesho tu ombi letu la kupata ajira lijibiwe, tungependa Mungu atuponye magonjwa yetu mara moja. Hata hivyo, Mungu anaacha muda utipe akijua wazi kuwa upo muda mwafaka wa Yeye kuonesha utukufu wake.

Imani: Ufufuko wa wafu, maisha na uzima wa milele
Imani: Ufufuko wa wafu, maisha na uzima wa milele

Mungu hakawii kujibu mahitaji yetu, bali ana muda wake wa kujibu mahitaji yetu ambayo kwayo tutaoneshwa utukufu wa Mungu. (5) Magonjwa na misiba ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu na kuimarisha imani. Yesu alipoambiwa kuwa Lazaro ni mgonjwa alijibu kwa kusema, “Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu.” Mara nyingi sisi binadamu tunapopatwa na magonjwa, misiba ya wapendwa wetu na mengineyo yenye kuleta uchungu huwa tunadhani kuwa ni laani, adhabu au ya kwamba Mungu ametuacha. Hapa Yesu anatufundisha kuwa Mungu anaweza kuruhusu tupatwe na magonjwa, misiba na mengineyo yenye kuleta uchungu ili kupitia hayo utukufu wa Mungu upate kudhihirishwa. Tunapaswa kuyapokea hayo yote kwa jicho la imani kwani Mungu huyatumia hayo kiimarisha imani yetu. Ni kutokana na msiba/kifo cha Lazaro watu wengine waliimarika kiimani baada ya Yesu kumfufua Lazaro. (6) Mungu anaguswa na mahangaiko, huzuni na changamoto zetu. Injili inatueleza kuwa Yesu alipoona maiti ya Lazaro “alilia machozi”. Kitendo hiki kinaonesha kuwa Yesu aliguswa na maumivu kama yale yaliyowagusa Martha na Mariamu kwa msiba wa kaka yao. Yesu ambaye ni Mungu-mtu anaguswa na mateso, uchungu na huzuni za mwanadamu. Tuwapo katika mahangaiko, mateso na taabu zetu tutambue kuwa Mungu hajaziba masikio wala hajafumba macho bali yupo pamoja nasi akiguswa na mahangaiko yetu na hivyo anatupatia nguvu na suluhisho la changamoto zetu za maisha. Jambo moja ni hili tunapaswa kujiaminisha mazima mazima kwa Mungu na kuitumainia nguvu yake. Tutambue kuwa hata tuwapo katika mateso Mungu anatupenda sana kama alivyowapenda Martha, Mariamu na Lazaro kaka yao. Dominika njema.

23 March 2023, 16:49