Tafakari Dominika V Kwaresima Mwaka A wa Kanisa: Matumaini ya Uzima wa Milele
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Dominika ya 5 ya Kwaresima ni dominika inayotangulia Juma Kuu. Kabla ya marekebisho ya Kiliturjia, hii ilijulikana kama dominika ya kwanza ya Mateso na ile ya Matawi kama dominika ya Pili ya Mateso. Alama iliyobaki kuonesha upekee wa dominika hii katika kipindi cha Kwaresima ni ile alama ya kufunika Misalaba na sanamu za watakatifu kwa kitambaa cha rangi zambarau. Masomo yote matatu ya dominika hii yanazungumzia ufufuko. Katika somo la kwanza, kwa kinywa cha Nabii Ezekieli Mungu anasema “tazama nitayafunua makaburi yenu na kuwatoa katika makaburi yenu enyi watu wangu.” Katika somo la pili tunasikia “yeye aliyemfufua Yesu kutoka wafu, ataihuisha miili yenu iliyo katika hali ya kufa.” Na katika Injili tunapokea Habari Njema ya Yesu kumfufua Lazaro. Nawaalika tuyapitie kwa undani kidogo masomo haya ili tuone ujumbe ule ambao Mungu anatupatia katika dominika hii. UFAFANUZI WA MASOMO: Anachokizungumza Mungu kupitia kinywa cha nabii Ezekieli katika somo la kwanza (Eze. 37:12-14) ni ujumbe katika lugha ya alama. Na hii ni mojawapo ya tabia ya ujumbe wa kinabii. Tunaliona hilo kwa sababu Ezekieli anauota ujumbe huo kwa taifa ambalo liko utumwani, taifa lililo katika mahangaiko na mateso ya kulazimika kuishi uhamishoni. Ni kipindi ambacho taifa teule lilikuwa kama limekufa. Nabii anawatangazia habari njema kuwa utumwa wao utaisha na watarudi katika nchi yao, nchi ya ahadi. Ni matumaini haya makubwa ambayo Nabii anayazungumza kama kuwafufua, kuwatoa katika kaburi la utumwa na kuwarudisha salama nyumbani. Na anayefanya kazi hiyo ni Mungu mwenyewe.
Tukiingia katika somo la pili, Mtume Paulo anasimika mafundisho yake katika msingi kuwa binadamu ni mwili na roho. Mwanadamu aliyekombolewa na Kristo kwa njia ya ubatizo na anayeishi maisha yake akiongozwa na Neno la Mungu, huyo anaye Roho wa Mungu ndani yake. Kutokana na msingi huu, Paulo anatoa mafundisho mawili. Fundisho la kwanza ni kuwa yule aliye na Roho wa Mungu ndani yake asiruhusu kutawaliwa na matendo ya mwili. Asikubali kuwa mateka wake. Fundisho la pili ni kuwa ni katika Roho huyo huyo wa Kristo akaaye ndani yake ndipo ilipo nguvu ya ufufuko. Katika mafundisho haya ya Paulo ufufuko ni maisha yasiyo na mwisho. Sasa ni vigumu kuyapata maisha haya yasiyo na mwisho kama mtu hana Roho wa Kristo ndani yake. Ujumbe wa somo la kwanza na huu wa somo la pili vinaunganishwa katika somo la Injili ambapo tunapokea habari ya ufufuko wa Lazaro. Tunasoma kutoka injili ya Yohane (Yn. 11:1-45) muujiza mkubwa Yesu anaoufanya kumfufua mtu ambaye tayari zilikuwa zimepita siku 4 tangu afariki. Huu ni muujiza unaoonesha uwezo wa Mungu wa kutenda yale ambayo kwa binadamu hayawezekani, kama kumrudishia uhai aliyekufa. Yesu anapoambiwa Lazaro ni mgonjwa haendi haraka ili kumponya bali anasubiri. Anaendelea na kazi zake nyingine na anaenda wakati Lazaro amekufa ili tu kuonesha ukubwa wa tendo ambalo Mungu anaweza kulitenda kwa mwanadamu.
Ni muujiza ambao hauzungumzii kifo tu bali hali unazungumzia pia uwezo wa Mungu kubadilisha hali ya wanaomwamini. Hili tunaliona katika maana za majina anazotumia mwinjili Yohane. Jina Lazaro kwa kiebrania maana yake ni “Mungu ni msaada wangu”. Linamwakilisha mtu anayetegemea msaada wa Mungu katika maisha yake. Huyu mtu aliishi kijiji kilichoitwa Betania. Jina Betania nalo maanda yake ni “nyumba ya mateso”. Lazaro mtu anayetegemea msaada wa Mungu aliishi katika nyumba ya mateso. Muujiza anaoufanya Yesu uaitikia kilio chake na unabadilisha hali ya nyumba ya mateso, Betania, kuwa nyumba sala na nyumba ya kumtukuza Mungu. Ndicho anachokisema Yesu anapowajibu wanafunzi wake akisema “ugonjwa huu si wa mauti bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu”. Ni muujiza pia ambao unadokeza ufufuko wa Yesu mwenyewe. Yesu anapomfufua Lazazo anaonesha kuwa anayo nguvu pia ya kujifufua na ndicho atakachokifanya siku chache baadae. Ni muujiza pia ambao unadokeza ufufuko wa wafu utakaotokea wakati wa ujio wa pili wa Yesu. Dokezo hili tunaliona pale ambapo Yesu anapoambiwa kuwa Lazaro amekufa, haendi mara moja kumfufua bali ni kama anasubiri muda upite. Kitendo hiki cha Yesu kusubiri kimetafsiriwa na wengi kama muda wa kuthibitisha kuwa aliyekufa amekufa kweli ili isionekane kama alikuwa amezimia tu. Lakini pia kitendo cha Yesu kusubiri kinaashiria pia ile subira ya ujio wake wa pili atakapowafufua wafu.
TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya dominika hii ambayo yanazungumza juu ya ufufuko yanatuachia ujumbe unaoamsha matumaini ndani yetu. Ni Mungu mwenyewe anayetangaza kwa maneno mengine kuwa kwake hakuna lisilowezekana. Kama ambavyo ana uwezo wa kufufua wafu vivyo hivyo anao uwezo wa kufufua hali zilizokufa katika maisha yetu. Tukiangalia kwa undani, huu ndio mwaliko wa kipindi cha Kwaresima ambao kila mwaka kanisa linatupatia. Kwaresima ni kipindi kinachoamsha matumaini ndani yetu. Sio kipindi cha kutukumbusha kuwa sisi ni wadhambi au kuwa sisi tumemchukiza Mwenyezi Mungu kwa sababu ya maisha yetu mabaya au kwamba hatufai mbele yake na kwamba tusipotubu Mungu atatuangamiza. Ni kweli kwamba tumetenda dhambi na tunastahili kuipokea ghadhabu ya Mungu tusipotubu na kuongoka lakini msingi wa toba na wongofu wetu umejijenga katika matumaini ambayo Mungu mwenyewe anatupatia. Matumaini ya kusamehewa, matumaini ya kupokelewa, matumaini ya kubadilika, matumaini ya kusaidiwa na matumaini ya kuanza upya. Kama Mwenyezi Mungu si Mungu wa kutupa matumaini haya basi juhudi zetu za toba na wongofu hazitatufaidia chochote. Mungu anatualika tumrudie kwa sababu ni yeye wa kwanza kutugeukia na kutunyooshea mkono akiashiria utayari wake wa kutupokea. Ujumbe wa ufufuko tunaupokea leo ni ujumbe basi unatuhimiza tusikate tamaa katika maisha, tusikate tamaa katika safari yetu ya imani na matumaini tusikate tamaa katika wito na utume mbalimbali ambao Mungu ametupatia. Tuzidi kumtumainia Yeye aliye na uwezo wa kufufua yaliyokufa kwani ni kwa njia hiyo hiyo anaweza kuyapa uzima yale ambayo katika maisha yetu ni kama yamekufa.