2020.03.13 Domenika ya II ya Kwaresima: Yesu na Msamaria. 2020.03.13 Domenika ya II ya Kwaresima: Yesu na Msamaria. 

Tafakari ya Dominika ya III ya Kwaresima Mwaka A:Uhai wa kweli

Masomo yetu ya leo yanabeba ujumbe usemao Uhai wa Kweli,kupitia ile ishara ya maji,ambayo ni alama muhimu katika Ubatizo.Sakramenti ambayo inatufanya kushiriki maisha ya kimungu kupitia kwa Mwanae Yesu Kristo.

Na Pd. Philemon Anthony Chacha wa Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican kutafakari pamoja masomo ya dominika ya tatu ya kipindi cha kwaresima mwaka A. Masomo yetu ya leo yanabeba ujumbe usemao Uhai wa Kweli, kupitia ile ishara ya maji, ambayo ni alama muhimu katika Ubatizo. Sakramenti ambayo inatufanya kushiriki maisha ya kimungu kupitia kwa Mwanae Yesu Kristo. Manung’uniko na malalamiko ya wana wa Israeli kule jangwani katika somo la kwanza, yanaamsha Imani ya Musa na Huruma ya Mungu, kama ilivyo kwenye Injili yule Mwanamke Msamaria kupitia kiu yake ya Imani na ukweli, inapelekea katika ufunuo wa Yesu kwenye kisima cha Yakobo kule Sikari. Kumbe Kristo ndiye anayetoa maji ya uzima, ambayo yanatoka ubavuni mwake pale msalabani na anatoa zawadi ya Roho Mtakatifu inavyomfikia kila muumini, kama tunavyosikia kwenye somo la pili.

Tuyaangalie kwa undani masomo yetu ya leo. Katika somo la kwanza kutoka kitabu cha kutoka (Kut 17:3-7), linaeleza juu ya ule muujiza wa maji: maji yanayomwagika kutoka kawenye mwamba au jabali, pasipokuwa na chanzo chochote, ni mahali ambapo wana wa Israeli kwa kiu yao walimnung’unukia Mungu pamoja na Musa. Mahali pale Musa alipaita Masa na Meriba kukumbuka sehemu ambayo wana wa Israeli walimjaribu Mungu. Mwenyezi Mungu anawavumilia na kuwahurumia na anawapa maji ingawa hawakustahili. Zawadi ya uhai ambayo Mungu anatujalia ni zawadi ya bure kabisa inayotoka kwake hata kama mwanandamu hana shukrani, ni mdhambi lakini yeye daima hatuachi tukimtegemea. Ni mwaliko kwa kila mmoja wetu kurudisha ile imani na matumaini yetu kwa Mungu na kumtambua yeye kuwa ni mwenye upendo na ni Baba ambaye daima hawezi kuwaacha watoto wake. Kama ile Zaburi ya 95 inavyotuambia: “kwa maana ndiye Mungu wetu, na sisi tu watu wa malisho yake, na kondoo za mkono wake.”

Mtakatifu Paulo katika ule waraka wake kwa Warumi (Rum 5:1-2,5-8), anakumbusha umuhimu wa maisha ya kikristu: tunaishi na tu wazima kwasababu Kristo alikufa na akafufuka kwa ajili yetu “wakati ulipotimia Kristo alikufa kwa ajili ya waovu”. Mungu ni uhai na anataka kushirikisha uhai huu na viumbe wake, kwa kila mmoja wetu, anatuletea wokovu ambao ni zawadi tupu bila mastahili yetu. Uhai haupatikani kama sio kwa Kristo, ambaye alishinda mauti na ni Bwana wa historia. Wakati tunaoishi sio wa bahati mbaya, bali ni zawadi, ni wakati muafaka, ni wakati sahihi Kairos. Kumbe hata kwenye magumu na changamoto za maisha tunazokutana nazo kila siku ni wakati mzuri wa uhai, wa mabadiliko na wokovu kwasababu tunaye Roho Mtakatifu ndani mwetu ambaye daima anatufanya tumpende Mungu na kumtumikia yeye.

INJILI

Injili yetu ya leo inatoka kwa Mwinjili Yohane (Yn 4:5-42), inayosimulia makutano kati ya Yesu na Mwanamke Msamaria katika kisima cha Yakobo. Ndugu msikilizaji na msomaji wa Radio Vatikani, Kisima katika Maandiko Matakatifu kilikuwa hakina maana ya kuchota maji tu pekee yake bali kilikuwa na maana nyingine zaidi: ilikuwa ni sehemu ya kukutania kwa watu mbalimbali, kuanzia wachungaji waliokuwa wanapeleka mifugo yao kunywa maji, wafanyabiashara, akina mama waliokuwa wanachota maji na kupiga soga kidogo. Sehemu ya kisimani pia walikutana wote ambao walikuwa wanapendana na wanaotarajia kuoana. Hapa tunakumbuka wakati Abramu anamtuma mtumishi wake kwenda kumchagulia kwa atakayekuwa mchumba wa Isaka, na anamchukua Rebecca (Mwa 24,11). Ni katika kisima pia ambapo Musa anakutana na atakayekuwa mke wake Zipora (Kut 2,15-22). Kisima kilikuwa ni sehemu pia ya Torah, sehemu ya Neno la Mungu, maji ya uhai yanayotoka kwa Mungu. Kama anavyotueleza Nabii Yeremia anaposema kupitia maneno ya Mungu mwenyewe “maana watu wangu wametenda maovu mawili: wameniacha mimi niliye chemchemi ya maji ya uhai wakajichimbia visima vyao wenyewe” (Yer 2,13).

Kumbe Maji ni alama au ishara ya Uhai, ya upendo wa Mungu, ishara ya Neno lake ambayo inaleta Uhai. Na ndio maana katika makutano ya Yesu na mwanamke msamaria tunaona Yesu anajifunua kuwa yeye ni yule anayetoa maji ya uzima, Uhai wa kweli ambao hautakwisha kamwe. Ndugu msikilizaji wa Radio Vaticani, tunaweza kujiuliza ni kwanini Yesu aliamua kupita katika ardhi ya Samaria huku tukitambua kuwa mji wa Samaria ulikuwa na watu walioishi maisha ya dhambi, maisha ya kutomuamini Mungu? Jibu ni kuwa Mwenyezi Mungu anataka kumkomboa mwanadamu, anapata furaha katika kusaidia, anakuwa na huruma kwa wote wanaoanguka dhambini na anafanya sherehe pale mmoja anapotoka katika lile wimbi la dhambi, na kurudi kwake kwa moyo wa toba. Mara nyingi hata katika maisha yetu tunaalikwa nasi kuwa na hali kama hii ya kutokuwa mbali na wale waliopatwa na dhambi na kuwa watu wenye huruma.

Na hivyo ndivyo tunaona kwa Yesu kuwa hataki kumuhukumu yule mwanamke msamaria badala yake anajiweka katika hali ile ile kama ya yule mwanamke ya kutaka kukata kiu yake, hamwambii kuwa “wewe ni mtu mbaya, hauna uzuri wowote, wewe ni mdhambi”. Yesu angeweza kumwambia maneno yote haya kwasababu anamfahamu kuwa ni mwanamke mdhambi. Lakini hafanyi hivyo badala yake anatafuta njia ya kugusa moyo wake kwa hali ya unyenyekevu mkubwa. Kumbe katika Mungu hakuna hali yeyote ya majivuno, na ndio maana Mahatma Gandhi aliwahi kusema: “mtu yeyote anayetaka kukutana na Mungu, lazima ajifanye kuwa mnyenyekevu … majivuno husababisha kutokukutana na Mungu

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican Mwenyezi Mungu ni mwenye huruma na ni mwingi wa rehema lakini kamwe huchukizwa na dhambi. Ndio maana Yesu anataka kumuonyesha yule mwanamke msamaria kuwa maisha anayoishi sio mazuri, na hayatampatia furaha, anataka kumuonyesha kuwa maisha anayoishi hayana mpangilio. Huu ndio upendo wa kweli. Mwanamke yule anatoka kukutana na Yesu akiwa na mabadiliko makubwa, bila kupokea baya lolote. Nasi pia tunaalikwa kufuata njia hii ya kusema daima ukweli, kama kuna tabia ambayo haiendi sawa tunaitwa kuikemea mara moja. Lakini daima kwa upendo.

Mwanamke msamaria baada ya kukutana na Yesu anakwenda kuwa shahidi wa kile alichokiona na kukisikia, na matokeo yake tunaambiwa katika Injili kuwa Wasamaria wengi walimwamini Yesu kwamba ndiye mwokozi wa ulimwengu. Na sisi je tumekutana na Yesu? Tunajua kushuhudia kule kukutana kwetu na Yesu ambako kumebadilisha maisha yetu na kutupatia uhai mpya? Tumuombe Kristo hasa katika kipindi hiki cha kwaresima akae nasi daima maana ni kupitia yeye ndipo tunapata uhai na uzima wa kweli, tunapata maji yanayoshibisha moyo na kuufanya uwe na furaha na kuondokana na ubinafsi kwa kuishi katika kujitoa sisi wenyewe kwa wengine.

TAFAKARI DOMINIKA
10 March 2023, 17:56