Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Jimbo Katoliki Geita:Kufuru na Unajisi wa Kanisa!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa Huruma” anasema, huruma haipingani na haki, bali inaonesha msimamo wa Mungu dhidi ya mwenye dhambi, yaani Mungu anampa nafasi nyingine ya kujirekebisha, kutubu, kuongoka na kuamini. Kumbe, huruma, haki na masamaha ni chanda na pete, ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana. Kutabarukiwa kwa Kanisa maana yake ni kulitenga Jengo la Kanisa kwa ajili ya maadhimisho ya Mafumbo Matakatifu ya Kanisa, kwa ajili ya sifa, utukufu na ukuu wa Mungu. Na ni katika mantiki hii, Kanisa linaitwa Nyumba ya Mungu, Makao ya watu wa Mungu, mahali ambapo waamini wanakutanika kusali, kuabudu, kumtukuza, kumwomba na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa: upendo, wema, huruma na ukarimu wake wa daima. Hapa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anasubiri kukutana na waja wake. Kumbe, huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha Jumuiya ya waamini inayoimarishwa kwa: Kusoma, Kutafakari na Kumwilisha Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma kama sehemu ya mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.
Kijana mmoja aliyetambulikana kwa jina la Elipidius Edward mwenye umri wa miaka 22, mkazi wa Kata ya Buhalala Wilyani Geita, Mkoani Geita nchini Tanzania hivi karibubni amefikishwa Mahakamani na kusomewa mashtaka mawili: Kosa la kuvunja na kuingia kwenye nyumba ya Ibada. Pili kuharibu mali za Kanisa, kunako tarehe 26 Februari 2023 majira ya saa 8 usiku wa manane. Hiki ni kitendo ambacho kimepelekea kufuru kwa Mambo Matakatifu sanjari na kulinajisi Kanisa na hivyo kugusa na kutikisa imani ya waamini wa Kanisa Katoliki ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Geita. Waamini watambue na kukumbuka kwamba, Kristo Yesu ndiye Jiwe kuu la pembeni na kila mwamini anapaswa kujengeka na kuwa ni jiwe hai na wote waweze kutembea kwa pamoja katika umoja, ushirika na utume, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.
Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki Geita nchini Tanzania anasema, kufuru kubwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na unajisi wa utakatifu wa Kanisa na vifaa mbalimbali vya Ibada imekuwa ni fursa ya kujenga: Moyo wa toba, wongofu wa ndani na malipizi ya dhambi, tayari kuambata na kukumbatia utakatifu wa maisha, kielelezo cha imani tendaji. Kutabarukiwa na kutakaswa kwa Kanisa kuu la Bikira Maria Malkia wa Amani, Jimbo la Geita na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jumamosi tarehe 18 Machi 2023 ni baada ya kukamilika kwa ukarabati wa: Altare, kwa kununua tena Tabernakulo mpya pamoja na vifaa vya Ibada na Visakramenti sanjari na kulipaka upya rangi ndani na nje ya Kanisa.
Kardinali Pengo katika mahubiri yake, alifafanua maana ya kutenga “Jengo” kwa ajili ya Ibada; umuhimu wa toba na kuomba msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama tendo la kibinadamu, changamoto na mwaliko wa kufanya tafakari ya kina, ili kutambua ujumbe wa Mungu kutokana na alama hii ya kufuru kwa Kanisa kuu la Bikira Maria Malkia wa Amani kwa watu wa Mungu Jimbo Katoliki Geita na Tanzania katika ujumla wake. Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, ametoa “Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania” Mintarafu kufuru iliyotendeka kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Malkia wa Amani, Jimbo Katoliki Geita: Huruma ya Mungu, Msamaha, Toba na Wongofu wa Ndani. Kwa upande wake Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki Geita amekazia kuhusu huruma, haki na msamaha sanjari na kuendelea kusoma alama za nyakati, ili kutambua katika tukio hili, Mwenyezi Mungu anataka kuwaambia nini watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Geita.