Tafuta

2022.04.23 Gesu Mwingi wa Huruma 2022.04.23 Gesu Mwingi wa Huruma  

Dominika II Kwaresima:Imani na mateso,tumaini la utukufu ujao

Kipindi hiki cha Kwaresima,anasema Baba Mtakatifu ni mwaliko wa kupanda juu Mlimani ili kupata mang’amuzi ya maisha ya kiroho,ili kuzama zaidi katika Fumbo la maisha ya Kristo Yesu kama utimilifu wa Sheria na Unabii.Ni mwaliko wa kumsikiliza Kristo Yesu kwa umakini mkubwa kama mtindo wa maisha ya Kanisa la Kisinodi.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya pili ya Kipindi cha Kwaresima mwaka A wa Kanisa. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Toba ya Kwaresima na Mchakato wa Sinodi.” Ni ujumbe unaochota amana na utajiri wake kutoka katika tukio la Kristo Yesu kugeuka sura mbele ya wanafunzi wake Petro, Yakobo na Yohane nduguye, baada ya kuwa ametangaza Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, jambo ambalo lilionekana kuwa ni kashfa kwa Mtume Petro, kiasi cha kuambiwa na Kristo Yesu, alikuwa ni Shetani, kikwazo kwake kwani alikuwa hawazi yaliyo ya Mungu bali ya wanadamu. (Rej. Mt 16:23) Kipindi hiki cha Kwaresima, anasema Baba Mtakatifu ni mwaliko wa kupanda juu Mlimani ili kupata mang’amuzi ya maisha ya kiroho, ili kuzama zaidi katika Fumbo la maisha ya Kristo Yesu kama utimilifu wa Sheria na Unabii. Ni mwaliko wa kumsikiliza Kristo Yesu kwa umakini mkubwa kama mtindo wa maisha ya Kanisa la Kisinodi.

Ni siku ya kumi na mbili tangu tuanze kipindi cha majiundo ya kiroho kwa kusali, kufunga, kujikatalia na kujinyima tuyapendayo kwa ajili ya wahitaji ili tujipatanishe na Mungu. Masomo ya domenika ya kwanza ya kwaresima yalitupeleka nyikani/jangwani ili kutupa nguvu ya kuyashida majaribu. Masomo ya domenika ya pili yanatutoa nyikani kwenye majaribu na kutupeleka juu ya mlima ili kukutana na Mungu katika utukufu wake na kutuonyesha uzuri wa kuyashida majaribu. Ujumbe huu umejikita katika wito wa Ibrahimu Baba wa Imani ambao ni mwangwi wa kuitwa kwa kila mmoja wetu kutoka katika dhambi na kuingia katika utukufu baada ya kuvumilia taabu na mateso ya kupambana na dhambi na utukufu wenyewe unajidhihirisha wazi kwa Yesu kwa kugeuka sura.

Somo la kwanza ni la kitabu cha mwanzo (Mwa.12:1- 4a). Somo hili linahusu wito wa Abrahimu baba wa Imani. Mwinjili Mathayo ameanza injili yake akisema; Habari za ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Abrahamu (Mt.1:1). Yesu Kristo kwa jinsi ya mwili ni mzao wa Abrahamu. Mama Kanisa anamtambua Abrahamu kama Baba wa Imani. Lakini kwanini Yesu kwa jinsi ya mwili ni wa uzao wa Abrahimu na sio wa Adamu? Katika Biblia sura mbili za mwanzo zinatuonesha uzuri wa kazi ya uumbaji wa Mungu. Kuumbwa kwa ulimwengu, dunia na viumbe vyote vinavyoonekana na visivyoonekana na mwanadamu (Mw. 1:1-2:25). Sura ya tatu hadi ya kumi na moja zinasimulia jinsi mwanadamu alivyojitenga na Mungu kwa kutenda dhambi: Anguko la mwanadamu na matokeo ya dhambi (Mw. 3:1-5:32), habari za Noa na gharika kuu (Mw. 6:1-9:29) na kutawanywa kwa mataifa kwa kile kinachofahamika kama mnara wa Babeli (Mw. 10:1-11:32). Masimulizi haya yalikuwa ni sehemu ya somo la kwanza kuanzia jumatatu ya wiki ya 5 kipindi cha kawaida mpaka ijumaa ya wiki ya sita. Katika sura hizi tunaona kuwa mwanadamu baada ya kutenda dhambi hakuweza tena kurudi kwa Mungu kwa jitihada yake mwenyewe, hakuwa na nguvu ya kujiokoa mwenyewe.

Sura ya kumi na mbili inafuangua ukurasa mpya wa mabadiliko makubwa katika uhusiano kati ya Mungu na mwanadamu yanayoanza kwa Mungu kumwita Abrahamu kuwa baba wa taifa teule, watu wa Israeli kwa maisha ya Abrahamu (12:1-25:18). Mungu alimwita Abrahimu na kumwambia; “Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa”. Hii ni hatua muhimu katika historia ya wokovu wa mwanadamu. Katika huruma yake Mungu anashuka na kukaa na mwanadamu, anaongea naye, anamwongoza ili aweze kurudi tena kwake. Abrahamu kuitikia sauti ya Mungu ni kitendo cha kishujaa na cha kujitoa sadaka.  Abrahimu aliitika na kutii, kwa imani akaondoka, akaacha yote, akajikabidhi mikononi mwa Mungu, akawa Baba wa Imani na chanzo cha baraka kwa mataifa yote. Nasi tunaitwa tutoke katika maisha ya ukale tuingie katika maisha mapya. Tutokea katika maisha tuliyoyazoea, maisha ya dhambi, twende tukamsikilize Yesu, Mwana wa Mungu ili tukawe warithi wa ufalme wake. Kila mmoja anaitwa kwa jina lake na kuambiwa, toka wewe katika tamaa zako, toka wewe katika dhambi zako, nenda ukapate neno la uzima wa milele. Na hii inawezekana kwa imani dhabiti, kwa kufunga, kusali na kutenda matendo ya huruma.

Somo la pili ni la Waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Timotheo (2Tim.  1:8b-10). Mtume Paulo akiwa gerezani Roma, anamhimiza Timotheo mhubiri chipukizi, Askofu kijana wa Efeso, aliyeitwa na kupewa neema ya Mungu kwa kuwekewa mikono na Paulo mwenyewe, asikatishwe tamaa katika utume wake sababu ya mateso na mahangaiko bali avumilie akizitumia nguvu alizojaliwa na Mungu kushiriki mateso kwa ajili ya Injili. Na sisi tuliokombolewa, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi na neema zake Mungu, tunaitwa ili kwa neema hiyo tuliyoipewa katika Kristo Yesu kwa njia ya ubatizo, na umauti wetu ukabatilishwa na kufunuliwa uzima usioharibika hata milele yote tuishuhudie hii imani kama Abrahimu Baba yetu.

Injili ni ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 17:1-9). Sehemu hii ya Injili inasimulia kugeuka sura kwa Yesu. Tukio hili ni la muhimu sana kwa sababu lilifunua umungu wa Yesu na kuonyesha kuwa yeye ni ukamilifu wa sheria na manabii kwa kuonekana na kutoweka kwa Musa na Eliya. Ndiyo maana Mama Kanisa ametenga siku maalumu ya kusherehekea tukio hili la Yesu kugeuka sura siku ya tarehe 6 Agosti ya kila mwaka kwa sababu ya umuhimu wake. Lengo la kukumbuka tukio hili katika maisha ya Yesu ni kutukumbusha asili ya wito wetu wa kuwa watakatifu. Hitimisho la tukio hili ni sauti ya Mungu Baba iliyosikika na kudhibitisha kuwa Yesu Kristo ni nafsi ya pili ya Mungu na ni mwana wa Mungu: “Huyu ni Mwanangu, mteule; Msikilizeni yeye.” Tukio hili la kugeuka Sura kwa Yesu linatokea wakati Yesu anasali akiwa pamoja na wanafunzi wake watatu; Petro, Yohane na Yakobo mlimani Tabor. Hii inatuonesha dhamani na nguvu ya sala. Sala ina nguvu ya kuzifungua mbingu na kumfanya Mungu ashuke na kusema nasi. Ndiyo maana tunasema, sala ni kuongea na Mungu. Sala ni kuinua akili na roho mbele za Mungu. Sala ni mawasiliano kati ya Mungu na Mwanadamu. Moja ya nguzo kuu ya kipindi cha kwaresima na kusali kwa bidii tena bila unafiki.

Katika tukio hili wanatokea Musa na Eliya. Itakumbukwa kuwa Musa alikaa mlimani siku 40 kupokea amri 10 za Mungu na (Kut. 24,16-18), Elia alitembea mwendo wa siku 40 mpaka mlima wa Mungu (1Waf. 19,3-8), na Yesu anafunga siku 40 akiwa ndio utimilifu wa yote (Mt. 4:2). Mwinjili Luka anasema kuwa hawa walizungumza na Yesu juu ya kifo ambacho kingekamilishwa Yerusalemu (Lk.9:31). Baada ya mazungumzo hayo, Musa na Elia walitoweka na hapo Mungu anatoa agizo la kumsikiliza Yesu, mwanaye mteule. Kuonekana kwa hawa wawakilishi wawili wa Agano la Kale kutoa ushuhuda kuwa sheria na manabii vinapata utimilifu katika Yesu Kristo kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Ndiyo maana Mungu anatuita tuwe wasikivu kwake. Nyakati zetu Yesu anaongea nasi Injili inaposomwa na kufafanuliwa tunaambiwa tulisikilize.

Kitu kingine kinachoambatana na tukio la Yesu kugeuka sura ni sauti kutoka katika wingu. Kwa Wayahudi wingu lilikuwa ni ishara ya uwepo wa Mungu na utukufu wake. Tunasoma katika Maandiko Matakatifu kuwa: “Waisraeli waliongozwa na wingu jangwani” (Kut.13:21). “Wingu liliifunika hema ya kukutania” (Kut. 40:34). Pia Musa alipokea amri za Mungu juu ya mlima uliofunikwa na wingu (Kut. 24:16-18). Kwa jinsi hii Yesu alionesha bayana ni utukufu wa namna gani aliokuwa nao kama Masiha na ni njia ipi anayopaswa kuifuata kila anayekusudia kumfuata yeye. Sauti hiyo iliyosikika kutoka katika wingu jeupe ndiyo hasa sauti ya Mungu Baba iliyomtambulisha na kumshuhudia Yesu kuwa ni Mwanae pekee na kuwataka wafuasi wake wamsikilize yeye.

Kugeuka sura kwa Yesu kunakuja baada ya Petro kukiri kuwa Yesu ndiye Masiha, Mwana wa Mungu aliye hai (Mt. 16:13-15), tena baada ya Yesu kuwatabiria juu ya mateso, kifo na ufufuko wake (Mt. 16:21-22) na kuwapa masharti ya kumfuata ambayo yamejikita katika kuuchukua msalaba, kuubeba na kumfuata (Mt.16:24). Matukio haya yalikuwa kikwazo kwa wafuasi wake hata wengine wakarudi nyuma. Mtume Petro alimwambia Yesu; “Bwana hili halitakupata”, na Yesu akamkemea na kumwambia; “Rudi nyuma yangu shetani wewe”. Hata sisi tunapopingana na mpango wa Mungu kwa namna yoyote ili Yesu anatuambia; “Rudi nyuma yangu shetani wewe”. Kumbe tukio hili la kugeuka sura kwa Yesu ni kielelezo wazi kwa wafuasi wake kwamba mateso na utukufu vinaambatana. Nasi tukishiriki mateso pamoja na Kristo, tutashirikishwa pia utukufu wake.

Mitume Petro, Yohane na Yakobo walichukuliwa wakashuhudie utukufu huu ili wakija kuwasimuliwa wengine waweze kuamini na kukubali kuwa ni kweli kwani kwa Wayahudi ili jambo zito kama hilo liweze kukubalika lilihitaji mashahidi watatu tena wanaume. Kwa tukio la kugeuka sura, Yesu aliwaonesha wazi wafuasi wake utukufu atakaoupata kwa njia ya mateso na kifo. Hali hiyo ya utukufu iliwavutia Petro, Yohane na Yakobo na kuwafanya wayapokee mateso ya Kristo kadiri ya mpango wa Mungu Baba. Wakawa tayari kumfuata Yesu katika njia hiyo ya mateso hata kukubali nao kufa kifo dini, kama mashahidi wa imani. Nasi tunakumbushwa kuwa tayari kuyapokea mateso tunayopata katika kutekeleza wajibu wetu wa kumfuata Kristo ili mwisho wa maisha ya hapa duniani tukaufurahie utukufu wa Mungu mbinguni milele yote.

Tafakari ya II ya Kwaresima
04 March 2023, 18:44